Rais Samia, Rejesha Miswada hii Bungeni: Msemaji Sekta ya Sheria na Katiba ACT Wazalendo atoa wito.

MAONI YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO KATIKA MUSWADA WA MABADILIKO YA SHERIA MBALIMBALI NAMBA 7 WA MWAKA 2021 ULIYOPITISHWA NA BUNGE.


1.0. UTANGULIZI

Serikali ilipitisha Muswada wa mabadiliko ya Sheria mbalimbali Namba 7 wa mwaka 2021 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 7) Act, 2021) ambao umefanya mabadiliko katika sheria mbalimbali ambazo ni; Sheria ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (Sura ya 209), Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki (Sura ya 218), Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Sura ya 20), Sheria ya Kuzuia Makosa ya Uhujumu Uchumi (Sura ya 200), Sheria ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (Sura ya 430), Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (Sura ya 49), Sheria ya Kanuni za Adhabu (Sura ya 16), Sheria ya Upatikanaji wa Huduma ya Mawasiliano kwa Wote (Sura ya 422) na Sheria ya Veterinari (Sura ya 319).

Maoni haya yamejikita Zaidi katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Sura ya 20)

2.0. MABADILIKO YA SHERIA YA MWENENDO WA MAKOSA YA JINAI (SURA YA 20)

2.1. Utatuzi wa mashtaka yenye sura ya jinai, madai au kiutawala kwa njia za kiutawala na madai (Kifungu cha 4 (3))

Bunge limepitisha mabadiliko ya kifungu cha 4 (3) kinachosema kwamba mashitaka yote yenye sura mbili (Jinai, Madai au Kiutawala) yatalazimika kwanza kutatuliwa kwa njia za madai au kiutawala kabla ya kuanzisha taratibu za mashtaka ya jinai.

UDHAIFU
a) Kifungu hiki kinaondoa dhana ya mashtaka ya jinai kwa kutaka kufunika makosa ya jinai kumalizwa kwa njia ya kiutawala au madai.
b) Hakuna utaratibu ambao umewekwa kwa njia zinazopendekezwa na kifungu hicho ili kuweza kuharakisha mashtaka hayo kutatuliwa kwa njia ya kiutawala. Utatuzi huo unaweza kuchukua muda mrefu bila usuluhishi kupatikana.
c) Kifungu kinaondoa uhuru wa mtu kuchagua njia ya kupata haki yake.
d) Njia ya madai huchukua muda mrefu kabla ya kesi kuamuliwa kulingana na idadi ya mashauri mahakamani.
e) Kifungu hakijaonyesha haki za dharura ambazo zinaweza kuchukuliwa na mtendewa au mtu aliyeathirika na makosa au mashtaka (there is no temporary remedies proposed by the proposed amendment).

MAPENDEKEZO
a) Kifungu kiondolewe kabisa, au
b) Kifungu kionyeshe haki za dharura ambazo muathirika wa makosa anaweza kuchukua, au
c) Kifungu kibainishe makosa ambayo yatalazimika kusuluhishwa kwa njia za kiutawala au madai.

2.2. Kuzuia kukamatwa tena kwa mtuhumiwa aliyeachiwa kufuatia uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka kuondoa mashtaka kwa nolle prosequi (Kifungu 91 (3))

Mabadiliko haya yamezuia kukamatwa tena kwa mtuhumiwa aliyeachiwa kufuatia uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka kuondoa mashtaka kwa nolle prosequi. Kwa mujibu wa kifungu hicho cha 91, isipokuwa kama kuna ushahidi wa kutosha.

UDHAIFU
a) Hakuna ushirikishwaji wa moja kwa moja kwa mahakama ili kuweza kujiridhisha kama kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa kabla ya kukamatwa tena.
b) Kifungu hiki bado kinapendelea ukamatwaji wa watuhumiwa mara baada ya kuachiwa.

MAPENDEKEZO
a) Kifungu kibadilishwe kwa kukataza watuhumiwa walioachiwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuondoa mashtaka kukamatwa tena.
b) Kibali cha mahakama kihusishwe kwa DPP kufanya maombi mahakamani ili mahakama ijiridhishe uwepo wa ushahidi wa kutosha utakaomuwezesha mtuhumiwa aliyeachiwa kukamatwa tena.

2.3. Kutofungua mashtaka mpaka upelelezi utakapokamilika, isipokuwa kwa makosa makubwa (Kifungu 131A)

Mabadiliko haya yanakataza kufungua mashtaka mpaka upelelezi utakapokamilika, isipokuwa kwa makosa makubwa. Zaidi mabadiliko haya yametoa haki mtuhumiwa kupewa dhamana ya polisi kwa makosa ambayo sio makubwa au ambayo hayasikilizwi Mahakama Kuu.

UDHAIFU
a) Kifungu hiki hakijabainisha muda wa kumaliza upelelezi kwa makosa yote.
b) Kifungu hiki hakijabainisha muda wa kumaliza upelelezi kwa makosa makubwa ambayo hayana dhamana.
c) Hakuna muongozo wa utoaji dhamana ili kuepusha usumbufu kwa watuhumiwa wakiwa polisi.

MAPENDEKEZO
a) Kifungu kibainishe muda wa kufanya upelelezi kwa makosa yote.
b) Kifungu kitoe mamlaka kwa Waziri mwenye dhamana kutengeneza kanuni au miongozo ya utoaji dhamana kwa watuhumiwa wanaoachiwa kwa dhamana ya polisi.
c) Mahakama Kuu ipewe jukumu la kufatilia muda wa upelelezi kwa makosa ambayo yanaanzia mahakama za chini (Committal proceedings)

 


MAONI YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO KATIKA MUSWADA YA MABADILIKO YA KUDHIBITI UTAKATISHAJI WA FEDHA HARAMU, SURA YA 423 (THE ANTI-MONEY LAUNDERING (AMENDMENT) ACT, 2022).

1.0. UTANGULIZI
Bunge limepitisha Muswada wa mabadiliko ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu, Sura ya 423 (The Anti-Money Laundering (Amendment) Act, 2022) na kufanya marekebisho yatokanayo katika sheria nyingine tano ili kukabiliana na changamoto katika udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi. Marekebisho ya sheria nyingine yatokanayo na marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu, ni Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (Sura ya 197), Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, (Sura ya 79), Sheria ya Bima, (Sura ya 394), Sheria ya Ushirikiano Katika Masuala ya Jinai (Sura ya 254), Sheria ya Kuzuia Ugaidi (Sura ya 19) na Sheria ya Mapato ya Uhalifu, (Sura ya 256).

Maoni haya yamejikita katika sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu, Sura ya 423 na Sheria ya Kuzuia Ugaidi (Sura ya 19).

2.0. MABADILIKO YA SHERIA YA KUDHIBITI UTAKATISHAJI WA FEDHA HARAMU, SURA YA 423

2.1. Tafsiri ya neno Mnufaika Manufaa (Beneficial Owner)
Mabadiliko haya yamependekeza Direct beneficial owner (Mnufaika Manufaa wa moja kwa moja) kujumuisha wamiliki wa hisa kwa kwa asilimia 5 au zaidi, wamiliki wa riba kwa asilimia 5 au zaidi. Aidha, mabadiliko haya yamependekeza indirect beneficial owner (Mnufaika Manufaa kwa njia isiyo ya moja kwa moja) kujumuisha wamiliki wa hisa kwa asilimia 5 au zaidi, wamiliki wa riba kwa asilimia tano au zaidi ambao watakuwa ni makampuni au taasisi au mashirika ambayo yanaendeshwa na watu halisi.

UDHAIFU
a) Tafsiri hii inakinzana na tafsiri ambayo ipo katika Kanuni ya 2 ya Kanuni za Mmiliki Manufaa ambazo zimetungwa chini ya Sheria ya Makampuni.
b) Marekebisho haya hayajabadilisha maana ya beneficial ownership (Mmiliki Manufaa) katika Kanuni za Mmiliki manufaa ambazo zimetungwa chini ya Sheria ya Makampuni.

MAPENDEKEZO
a) Mabadiliko haya yarekebishe maana ya mmiliki manufaa katika Kanuni za Mmiliki Manufaa ili kuondoa maana zinazokinzana au maana tofauti kwa jambo linalofanana na kuwa na maana moja.

2.2. Mtoa taarifa za utakatishaji fedha kumchunguza mteja (Kifungu 15A)
Mabadiliko haya yamependekeza mtoa taarifa au mtu anayewasilisha taarifa za utakatishaji fedha kuendelea au kumchunguza mteja juu ya biashara zake katika hatari ambazo zimeainishwa au ambazo zitakuwa zinapelekea utakatishaji fedha kabla ya kuanzisha mahusiano ya kibiashara, kabla ya kufanya miamala, endapo utakatishaji fedha au kufadhili ugaidi unapohisiwa kufanyika.

UDHAIFU
a) Kifungu cha 15A hakitekelezeki kwa urahisi kwasababu mtoa taarifa anaweza kushindwa kufikia baadhi ya taarifa kwa kuhofia kuvunjwa kwa usiri wa biashara za wahusika. Aidha sio rahisi kwa mtoa taarifa kupewa ushirikiano pale ambapo anataka kufahamu taarifa za biashara ambayo haihusiani na mtoa taarifa.
b) Kifungu hicho kinaweza kutumika kama mtego kuweka wajibu ambao hautekelezeki kirahisi na kupelekea kuweka makosa kwa mtoa taarifa ikiwa atakiuka au atashindwa kufanya jukumu hilo.

MAPENDEKEZO
a) Kifungu cha 15A kiondolewe na mamlaka ya kuchunguza yabaki kwa mamlaka zenye mamlaka ya kufanya uchunguzi au kujiridhisha juu ya uwepo wa viashiria vya utakatishaji fedha au ufadhili wa ugaidi.

2.3. Mtoa Taarifa kutunza kumbukumbu za mteja (Kifungu 16 (1) (a))
Kifungu hiki kinamtaka mtoa taarifa kutunza kumbukumbu za mteja katika miamala yote ya ndani na nje ya nchi, kujua faili za mteja, kujiridhisha mienendo ya mteja, tathimini katika utakatishaji fedha, vitendo vya kufadhili ugaidi na kutunza taarifa za mashaka katika miamala inayofanyika.

UDHAIFU
a) Bado sheria inamtaka mtoa taarifa kujikita katika tathimini ya vitendo vya utakatishaji fedha na ugaidi bila kujali ugumu wa kutekeleza jukumu hilo katika ufanyaji wa tathimini ya vitendo vya utakatishaji fedha na kufadhili ugaidi.

MAPENDEKEZO
a) Kifungu kibadilishwe kwa kubakiza wajibu wa mtoa taarifa kutunza kumbukumbu za miamala, taarifa za mteja anayejihusisha naye (majina, namba ya vitambulisho / pasi ya kusafiria, anwani ya makazi) tu kwa kipindi ambacho sheria imeainisha. Uwezo wa kufanya tathimini bado itakuwa ni vigumu kwa mtoa taarifa kutekeleza zoezi hilo kulingana na changamoto nilizozitaja katika udhaifu wa kifungu cha 15A.

2.4. Wajibu wa mtoa taarifa kutengeneza kanuni za ndani kwa ajili ya kutoa taarifa ya vitendo vya utakatishaji fedha (Kifungu 18)
Kifungu hiki kinawataka watoa taarifa kuwa na kanuni za ndani ya ofisi ambazo zitawasaidia kutoa taarifa ya vitendo vya utakatishaji fedha kwa wateja wao.

UDHAIFU
a) Kifungu hiki kitasababisha kutokuwa na ufanano wa kanuni za ndani. Hili ni jambo kubwa linalopaswa kuwa na uwiano wa kanuni ili kuepuka kuwa na utofauti katika maamuzi.
b) Kifungu hiki kinaweza kusababisha wengine kuonekana hawachukulii uzito jambo hili kwa kuwa na miongozo au kanuni dhaifu.

MAPENDEKEZO
a) Kifungu hiki kiweke wajibu wa kutengeneza kanuni kwa Waziri mwenye dhamana. Na mchakato huu ushirikishe watoa tarifa wote waliotajwa na sheria hii au wawakilishi katika kila sekta ya watoa taarifa.
b) Mara baada ya kuunda kanuni hizo, watoa taarifa wote wapewe nafasi ya kutoa maoni (awamu hii iwajumuishe wale ambao hawakuhudhuria katika mchakato wa kwanza kwa sababu ya uwakilishi).

2.5. Watoa Taarifa kuandaa programu za kuzuia na kudhibiti vitendo vya utakatishaji (Kifungu 19(1))

Mabadiliko haya yanamtaka mtoa taarifa ambaye ana kikundi kipana katika muudo wa kampuni au ushirika kuhakikisha kwamba anatoa programu za kuzuia na kudhibiti vitendo vya utakatishaji fedha ndani ya kikundi hicho.

UDHAIFU
a) Sheria inaweka wajibu wa moja kwa moja kwa mtoa taarifa bila kuhusisha serikali kutoa mafunzo kwanza kwa watu wa ndani ya nchi ili baadaye waweze kuwafundisha wenzao ukizingatia suala la utakatishaji fedha ni suala la kitaalamu ukizingatia bado kuna changamoto ya wataalamu katika taasisi wanaoweza kutoa mafunzo mazuri.

MAPENDEKEZO
a) Serikali ihusike kwa mara ya kwanza kabla ya kuachia jukumu la kutoa program kwa watu wa ndani ya taasisi.

SEHEMU YA PILI: MAREKEBISHO YA SHERIA YA KUZUIA UGAIDI (SURA YA 19)

2.6. Maana ya Ugaidi (Kifungu cha 4 (2) (a))
Mabadiliko haya yametafsiri mtu atahesabika kuwa amefanya ugaidi endapo atatishia au atasababisha hofu kwa umma au sehemu ya umma.

UDHAIFU
a) Maana hiyo bado inaleta utata kwasababu mtu anaweza kusababisha hofu kwa umma na sehemu ya umma bila kuwa gaidi.
b) Maana hiyo inaweza kuwaweka watu hatiani kwa kosa la ugaidi bila uhakika kutokana na utata uliyopo katika maana hiyo.
c) Bado sheria haijachambua kwa kiasi gani hofu au vitisho hivyo vitajumuishwa kuwa ni viashiria vya ugaidi.

MAPENDEKEZO
a) Kifungu hicho kisomeke kwamba; “Mtu atahesabika kuwa amefanya ugaidi endapo atatishia au atasababisha hofu kwa umma au sehemu ya umma kwa lengo la kuteka kikundi cha watu au jengo, kujilipua, kulipua jengo au eneo lolote au kulenga kikundi fulani cha watu kwa kutumia silaha au milipuko ya aina yoyote.” (Kwasababu vitendo vya ugaidi huwa vinawalenga kundi fulani la watu au sehemu ya kundi la watu kwa takwa la kisiasa au mzozo wa serikali na magaidi (there must be a target of a specified people or place, (mostly are civilians and buildings)).

2.7. Vitendo vya ugaidi (Kifungu cha 4 (3))
Mabadiliko ya kifungu hiki yanataja moja ya vitendo vya ugaidi katika kifungu cha 4 (3) (a) ni kufanya shambulizi katika uhai wa mtu amabalo litasababisha kifo au maumivu makubwa katika mwili wa mtu.

UDHAIFU
a) Kifungu hiki kimejikita zaidi katika uhai wa mtu tu.
b) Kifungu hakielezi vitu vingine kama majengo, makundi ya watu, au makundi maalumu.

MAPENDEKEZO
a) Kifungu hicho kijumuishe mashambulizi katika eneo, majengo, makundi maalumu, au makundi ya watu. Kisiishie kutaja uhai wa mtu kwa sababu ugaidi haulengi kutoa uhai wa mtu peke yake hujumuisha vitu vingi kwa lengo la kutishia au kushurutisha jambo fulani lifanyike.

2.8. Kutajwa kama Gaidi wa ndani (Kifungu 12A)
Mabadiliko ya kifungu hiki yanampa haki Waziri kumtaja mtu yeyote kama Gaidi wa ndani ya nchi kwa kuzingatia vigezo ambavyo vimetajwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

UDHAIFU
a) Sheria imempa Waziri mamlaka ya moja kwa moja bila kuweka uangalizi wa nguvu yake.
b) Sheria haijatoa nafasi kwa mtu aliyetajwa kama gaidi na Waziri kupinga maamuzi hayo mahakamani.

MAPENDEKEZO
a) Mahakama ihusishwe katika uangalizi wa nguvu hii ya kiutawala ambayo Waziri amepewa.
b) Mhusika apewe haki ya kukata rufaa kulingana na maamuzi ya Waziri.


HITIMISHO

Mabadiliko haya yamelenga kuleta sura mpya katika sheria hizi. Isipokuwa chama kinaona bado kuna udhaifu katika baadhi ya maeneo ambayo tumeyaainisha katika maoni yetu.

Chama kinaitaka Serikali na Bunge kwa ujumla kuzingatia maoni haya kwani lengo la sheria ni kuongoza watu katika mizani ya haki, usawa, utu na udilifu na sio kumkomoa mtu yeyote. Hakuna haja ya kuharakisha mabadiliko ambayo bado ni dhaifu katika mifumo ya utoaji haki.

Aidha, Chama kinamsihi Mheshimiwa Rais kutokusaini mabadiliko haya ya sheria ambayo yamepitishwa na Bunge. Tunamsihi Rais kuurudisha muswada huu uliopitishwa na Bunge kwa mabadiliko zaidi katika vifungu tulivyovianinisha katika maoni yetu.

Aidha, tunatoa wito kwa AZAKI, Wanazuoni, na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kupinga marekebisho haya kwa njia mbalimbali zilizoanishwa katika sheria zetu ikiwemo kuangalia uwezekano wa kutumia njia ya Mahakama kupinga marekebisho haya yaliyofanywa na Serikali kupitia Bunge. Sisi tunaamini marekebisho haya yatakuwa na athari mbaya kwa wananchi, hivyo yanapaswa kubadilishwa kama tulivyoshauri.

Imeandaliwa na:
Wakili Victor Kweka,
Msemaji Sekta ya Katiba na Sheria,
ACT WAZALENDO.

14 Februari, 2022.
Dar es salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK