RISALA YA NGOME YA VIJANA ACT WAZALENDO KWA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN - RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA HITIMISHO LA MAANDAMANO YA AMANI LEO 18 APRILI, 2023.

RISALA YA NGOME YA VIJANA ACT WAZALENDO KWA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN - RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA HITIMISHO LA MAANDAMANO YA AMANI YA KUDAI UWAJIBISHWAJI KWA WABADHIRIFU WA FEDHA ZA UMMA LEO TAREHE 18 APRILI, 2023.


Mhe. Rais,
Awali ya yote kwa niaba ya Vijana wote wa Chama cha ACT Wazalendo na Watanzania wengine wote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa mahali hapa muda huu. Lakini jambo lingine la msingi na kubwa ni kukushukuru wewe kwa kukubali kupokea Risala yetu yenye madai na madhumuni mahususi ya kuonesha hisia zetu dhidi ya ubadhirifu kupitia maandamano ya amani. Hii ni hatua kubwa sana kwetu na kwa nchi yetu.

Mhe. Rais,
Lengo la maandamano yetu ni kukuomba uchukue hatua dhidi ya wabadhilifu wote wa fedha za umma kwa mujibu wa mamlaka uliyo nayo na kwa mujibu wa sheria zetu za nchi na kwamba tupo pamoja na wewe na tunakuunga mkono kwa hatua za makusudi na muhimu utakazochukua dhidi ya wabadhilifu hawa. Kwani ubadhilifu wa fedha za umma umekuwa ukijirudiarudia kila mwaka katika taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali huku watumishi na viongozi wa umma wanaofanya ubadhilifu huo wakiendelea kusalia madarakani bila hatua zozote kali za kiuwajibikaji dhidi yao.

Mhe. Rais,
Nchi yetu bado ni maskini na huduma za kijamii kama elimu, afya na miundombinu bado ni duni sana. Fedha ambazo zingelisaidia katika utoaji wa huduma za kijamii zinaliwa na viongozi wachache ambao hadi sasa bado wapo ofisini bila uwajibikaji wowote wala hatua kali zaidi dhidi yao. Wananchi pamoja na kipato chetu duni tunalipa kodi chungu nzima ili kuchangia maendeleo ya nchi yetu, badala yake kodi zetu zinatafunwa na watu wachache na hawawajibiki wala kuwajibishwa kutokana na ubadhilifu mkubwa wanaoufanya.

Mhe. Rais unahangaika kila mahali duniani kutafuta mikopo na misaada kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, lakini unapofanikiwa na kuleta fedha hizo, takribani zote zinaishia kwenye mifuko ya wajanja wachache.
Tumekuwa taifa la kusomewa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kila mwaka bila hatua zozote za uwajibikaji kuchukuliwa na hivyo kila mwaka tumeendelea kushuhudia ubadhilifu mkubwa ukijirudia na kujirudia kwa kiwango kikubwa. SASA TUMECHOKA TUNAHITAJI HATUA KALI ZAIDI DHIDI YA WOTE WALIOFANYA UBADHILIFU.

Mhe. Rais,
Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT Wazalendo tumeona hatua ulizochukua tarehe 09 Aprili, 2023 kwa kuvunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na kuagiza Watendaji wa Taasisi kupitia na kujibu hoja za CAG katika maeneo yao na watakaobainika wachukuliwe hatua kwamba bado hazitoshi.
Hatujaridhishwa na hatua hizi za ujumla ulizochukua Mh. Rais kwani mara zote watendaji wa serikali wana tabia na mtindo wa kulindana. Na mara zote hawatilii maanani maagizo ya namna hii yanayotolewa na viongozi.

MADAI YETU
1. Wahusika Waondolewe Ofisini, Wakamatwe, Wachukuliwa Hatua Kali za Kisheria na Wafilisiwe Mali.

Mh. Rais, tunataka hatua kali zaidi zichukuliwe dhidi ya wote waliofanya ubadhilifu wa fedha za umma katika ripoti ya CAG. Katika maeneo tofauti tofauti ambapo ubadhilifu umetokea kuanzia Serikali za Mitaa, Idara za Serikali, Mashirika ya Umma, Serikali Kuu na katika Miradi ya Serikali hatua kali zichukuliwe kwa wote walio husika na ubadhilifu huo.
Mfano, Malipo hewa ya NHIF shilingi bililioni 14.5, Upotevu usiokwisha wa mabilioni ya fedha za mikopo asilimia 10 kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu, matumizi mabaya fedha za mkopo wa Uviko-19 shilingi bilioni 212, Uzembe katika sakata la Vishikwambi na katika maeneo mengine, wote wachukuliwe hatua kali.
Tunapaswa kuchora mstari utakaobainisha wazi kuwa sasa mali za umma ni moto wa kuotea mbali. Wabadhirifu wafukuzwe kazi mara moja, wafikishwe mahakamani, na wafilisiwe mali zao.

2. Tunaomba Uunde Tume Huru ya Kijaji kwa ajili ya Uchunguzi wa Matumizi Mabaya ya Ofisi na Maadili Dhidi ya Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Bwana Biswalo Mganga.

Mh. Rais, Ni muhimu Tume kuundwa ili kuchunguza madai ya washtakiwa kutishwa na kulazimishwa kukiri makosa ili kupewa uhuru wao na ukiukaji wa kanuni za mwenendo wa mashtaka ya jinai katika kile kilichoitwa Plea Bargain.

3. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Ajiuzulu (Individual Ministerial responsibility) au Awajibishwe na Mamlaka ya Uteuzi.

Mh. Rais, kufuatia ubadhilifu mkubwa uliotokea katika wizara yake ikiwemo upotevu wa shilingi Trilioni 2.9 fedha zilizotengwa na Bunge 2021/2022 kwa TANROADS kutekeleza miradi 88 ya barabara ikiwa kwa mujibu wa CAG miradi hiyo haikutekelezwa na haifahamiki fedha hizo ziko wapi, tunataka Waziri mwenye dhamana ajiuzulu mara moja na asipofanya hivyo wewe ukiwa mamlaka ya uteuzi wake, basi umuondoe kazini.

4. Uwazi wa Mikataba.
Mhe. Rais, usiri wa mikataba kwa muda mrefu kimekuwa ni kichaka kikubwa cha ubadhirifu wa fedha za umma. Tunaomba mikataba yetu iwe wazi na tuondokane na utamaduni usiofaa wa usiri katika mikataba na upatikanaji wa tenda mbalimbali za serikali. Tubadili sheria zetu kuhakikisha kwamba hakuna mkataba ambao serikali itaingia bila kuidhinishwa na Bunge.

5. Taasisi Zilizowekwa Awali Chini ya Ofisi ya Rais Ziondolewe.

Mh. Rais, ili kuleta uwajibikaji na ili ziweze kukaguliwa na CAG kwa mujibu wa sheria. Tunaomba taasisi zilizowekwa chini ya ofisi ya Raisi zioendolewe. Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na TAKUKURU. Kwa mujibu wa sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya 2007 kifungu cha 47(1 na 2) kinaeleza kuhusu TAKUKURU kufanyiwa ukaguzi kwani inatengewa fedha na Bunge, lakini haijawahi kukaguliwa.
Tumeelezwa na wewe mwenyewe Mh. Rais jinsi ambavyo kuna ufisadi unaofanyika kwenye taasisi hizi. Mathalani malipo ya ununuzi wa ndege uliyobainisha kuwa yamezidishwa kiwango cha malipo kufikia dola za kimarekani milioni 86 badala ya dola milioni 37. Tunawezaje kujua ufanisi wa matumizi ya fedha za taasisi hizo katika utendaji wao ikiwa hatujui fedha walizotengewa na Bunge hazikaguliwi na hatujui zimetumika namna gani? Tunaomba kupata mageuzi katika eneo hilo.

Mwisho,

Mh. Rais dhima ya ulinzi wa rasilimali za umma iko mikononi mwako. Una uwezo na nafasi kubwa ya kuzuia na kukomesha utamaduni na vitendo vya ubadhirifu ambao umeota mizizi katika serikali yako. Tunaomba, pamoja na kuchukua hatua za makusudi tulizoanisha, tunaamini kuna haja na umuhimu mkubwa wa kufanya mageuzi ya kimfumo na kisheria ili kuimarisha taasisi za kiuwajibikaji. Kwa kuzingatia hilo, tunakuomba uharakishe mchakato wa uandikaji wa Katiba Mpya ya nchi yetu ili kukamilisha dhamira yako ya kuleta mageuzi ya kimfumo ndani ya nchi yetu. Kwa kuimarisha mifumo, fedha na rasilimali za nchi yetu zitakuwa salama.

 

Abdul Omar Nondo
Mwenyekiti Ngome ya Vijana
ACT Wazalendo
18 Aprili, 2023.
Dar es Salaam.

Showing 2 reactions

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK