Seif Sharif Hamad

Mwenyekiti

Maalim Seif Sharif Hamad alichaguliwa kwa kishindo na shauku kubwa kuwa Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika kati ya tarehe 14 na 15 mwezi wa tatu, 2019. Maalim anatambulika kama gwiji la mapambano ya demokrasia na haki za binadamu visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.


Seif Sharif Hamad alizaliwa mnamo tarehe 22/10/1943, Wete, Pemba. Alihudhuria Uondwe na Wete Boys kwa ajili ya elimu yake ya msingi na baadaye kujiunga na George VI Memorial Grammar Secondary School kisiwani Unguja kwa miaka miwili kati ya 1958 na 1961 kwa ajili ya elimu ya juu ambayo alimaliza Disemba 1963.


Mnamo mwaka 1964, Serikali mpya ya Mapinduzi ilimuomba Maalim afundishe kwenye shule za sekondari kabla hajajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 na 1975. Maalim alihitimu chuoni hapo na Shahada ya Sayansi ya Siasa, Utawala wa Umma na Mahusiano ya Kimataifa.


Maalim amewahi kufanya kazi kama mjumbe wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Waziri wa Elimu wa Zanzibar (1977 -1980). Maalim pia ni mjumbe mwanzilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (1980-1981) na Mbunge wa Bunge la Tanzania (1977). Pia amewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) (1977-1987), Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya CCM (1982-1987) na aliwahi kuteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kutoka 1984 hadi 1988.


Kutokana msimamo wake usioyumba juu ya umuhimu wa mabadiliko ya kisiasa nchini, Maalim alifukuzwa kazi kama Waziri Kiongozi 22/1/1988 na pia akafukuzwa kwenye Baraza la Mapinduzi. Punde baada ya hapo, akafukuzwa kutoka CCM, ambapo kipindi hicho kilikuwa ni chama pekee cha siasa nchini. Kutokana na kufukuzwa, Maalim pia alipoteza nafasi yake kwenye Baraza la Wawakilishi.


Mnamo Mei, 1989, Maalim alikamatwa na kufikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka ya kupikwa ya kukutwa na nyaraka za siri za Serikali. Kutoka mwaka 1989 hadi 1991, Maalim alifungwa kwenye Gereza Kuu la Zanzibar. Mnamo April, 2000, alikamatwa tena na kupikiwa mashtaka mapya. Mahakama ya Zanzibar hatimaye ilitupilia mbali mashtaka hayo mnamo Novemba 2003.


Akiwa gerezani na nje ya gereza, Maalim alikuwa ni sauti kuu ya vuguvugu la kudai demokrasia visiwani Zanzibar, maarufu kwa jina lake la kifupisho kama KAMAHURU (Kamati ya Kupigania Vyama Vingi).
Siasa za vyama vingi zilipoanzishwa tena Tanzania mwaka 1992, KAMAHURU ilijiunga na vuguvugu jingine linalofanya shughuli zake Tanzania Bara kuunda chama cha the Civic United Front (CUF) - au Chama cha Wananchi - CUF. Mwanzoni, Maalim alikuwa kama Makamo wa Raisi wa chama hicho na baadaye kuwa Katibu Mkuu, nafasi aliyoendelea kuishikilia hadi Machi 2019.


Maalim amekuwa mgombea wa uraisi kwa kupitia tiketi ya CUF kuwakabili wagombea wa CCM kwenye chaguzi tatu zilizofanyika 1995, 2000 na 2005 na inaaminika na jamii ya Kitanzania na ile ya Kimataifa kwamba Maalim amekuwa akishinda chaguzi hizo lakini amekuwa akinyimwa ushindi huo na Tume ya Uchaguzi inayodhibitiwa na CCM.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2010, Maalim aligombea tena, mara hii dhidi ya mgombea wa CCM Dk Ali Mohamed Shein ambaye alipata asilimia 50.1 dhidi ya asilimia 49.1 alizopata Maalim. Lakini chini ya Makubaliano ya Maridhiano na kura ya maoni ambayo iliiweka dhana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwenye Katiba ya Zanzibar, CUF ilikuwa sehemu ya Serikali na Maalim akiwa Makamo wa Kwanza wa Raisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Maalim alishinda uchaguzi wa uraisi wa Oktoba 2015 kwa asilimia 53 kabla ya matokeo hayo hayajabatilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), hatua ambayo iliididimiza Zanzibar kwenye kipindi kirefu cha mgogoro wa kikatiba.


Kufuatia hujuma zilizodhaminiwa na dola za kuitumia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mahakama ya kuipora CUF na kuikabidhi kwa Mwenyekiti wake wa zamani, mnamo Machi 18, 2019, Maalim aliuongoza uongozi wote na wanachama wa CUF kukihama chama hicho na kuhamia chama cha ACT-Wazalendo. Maalim bado anaendelea kupigania mabadiliko ya kidemokrasia na haki za binadamu nchini.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK