SEMU:Tujenge Muafaka wa Kitaifa kupata Katiba Mpya

MAELEZO YA NDUGU DOROTHY MANKA SEMU, WAZIRI MKUU KIVULI ACT WAZALENDO KUFUATIA HOTUBA YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU KUHUSU MAPITIO YA KAZI NA MWELEKEO WA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA WA 2022/2023

Ndugu Wanahabari,
Mtakumbuka kuwa Bunge linaendelea kujadili mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa Fedha wa 2022/2023 jijini Dodoma. Mtakumbuka pia kuwa Chama cha ACT Wazalendo kiliunda Kamati ya Kuisimamia Serikali na kuteua Wasemaji wa Kisekta wa kila Wizara ya Serikali ili kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa wananchi. Kwa muktadha huo, nikiwa Msemaji wa Kisekta kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na kwa niaba ya Kamati ya Kuisimamia Serikali ya ACT Wazalendo tunatoa kwenu maoni machache kuhusu Hotuba ya Waziri Mkuu aliyeitoa Bungeni.
Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi yetu Waziri Mkuu ndiye Msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali. Kwa hiyo tulitegemea kuwa hotuba ya Waziri Mkuu ingejaribu kueleza majawabu ambayo yangesaidia kutatua changamoto mbalimbali ambazo nchi yetu inakabiliana nazo kwa sasa zikiwemo changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hata hivyo hotuba hiyo haijatoa matumaini kwa wananchi hususan kuhusu masuala yanayohusu maisha yao ya kila siku.
Ndugu wanahabari,
Ofisi ya Waziri Mkuu ndio yenye kusimamia Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa. Katika Ibara ya 28-29 Waziri Mkuu amezungumzia hali ya Siasa nchini na matumaini yaliyopo ya mchakato wa kuboresha mazingira ya kufanya siasa nchini. ACT Wazalendo INATAMBUA juhudi mbalimbali zinazofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluh Hassan ili kuboresha hali ya siasa na demokrasia nchini. Kuundwa kwa Kikosi Kazi kilichotokana na Mkutano wa Wadau wa Demokrasia Jijini Dodoma mwezi Desemba 2021 ni hatua mojawapo ambayo inatoa nafasi kwa wadau kutoa maoni ya maeneo ya maboresho katika mfumo wa Katiba yetu na sheria zinazosimamia shughuli za siasa na uchaguzi. Hotuba ya Waziri Mkuu haijaonyesha jitihada za makusudi za Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha kazi inayofanywa na Kikosi Kazi hicho inakuwa jumuifu na kuzingatia maoni ya wadau wengi. Kwa mfano mchakato wa kukamilisha kupatikana kwa Katiba Mpya nchini unapaswa kuanza sasa kwani tumaanini hautakuwa mchakato rahisi na utachukua muda mrefu. Kazi ya kwanza ya kufanywa katika eneo hili mazungumzo baina ya vyama na viongozi ya kujenga kwanza mwafaka wa kitaifa ili mchakato uweze kuongozwa na maslahi mapana ya Taifa. Kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndio Ofisi kiongozi katika masuala ya kisiasa tulitarajia kuona ‘roadmap’ ya kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kuwa mchakato wa kukamilisha kuandikwa kwa Katiba Mpya unaweza kuchukua muda mrefu na hivyo tukafika kwenye uchaguzi mkuu kabla ya kuukamilisha chama chetu kimekuwa kikipendekeza kuendelea na mchakato huo sambamba na mchakato wa kupata Tume Huru ya Uchaguzi ambayo inapaswa sasa hivi kuanza kuandaa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Hotuba ya Waziri Mkuu hajazungumzia mahala popote mpango wowote wa Serikali wa kufanya mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi ili kuifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa huru kwa kuajiri wafanyakazi wake yenyewe na kusimamia chaguzi zote nchini ikiwemo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Tunaendelea kushuhudia chaguzi ndogo zinazoendelea nchini zikiwa bado zimegubikwa na changamoto zile zile zilizotokea katika kilichoitwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Ni muhimu na lazima kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na Sheria mpya ya uchaguzi mapema iwezekanavyo. ACT Wazalendo tunafahamu kuwa ili kuifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa huru kutakuwa na haja ya mabadiliko madogo ya Katiba ya nchi yetu kuwezesha hilo. Baadhi ya maeneo yatakayohitaji mabadiliko ya Katiba ni kama vile;
1. Ibara ya 74(1) ya Katiba inayompa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuteua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume. Marekebisho hapa yawezeshe mchakato wa uteuzi kuwa wa wazi kupitia Kamati ya Uteuzi itakayotajwa kwenye sheria ya uchaguzi.
2. Ibara ya 74(5) inayompa Rais mamlaka ya kumwondoa madarakani mjumbe yeyote wa Tume kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake, ama kutokana na ugonjwa au kwa sababu yoyote au kwa tabia mbaya au kwa kupoteza sifa za kuwa mjumbe.
3. Ibara ya 74(12) inayonyang'anya Mahakama mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililofanywa na Tume katika kutekeleza madaraka yake. Marekebisho hapa yatawezesha matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa mahakamani.
4. Ibara ya 75 (1) na (2) inayoizuia Tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kuweka mipaka yake bila kupata kibali cha Rais.
5. Ibara ya 75 (6) inayokataza Mahakama kuchunguza jambo lolote lililofanywa na Tume katika kutekeleza madaraka yake ya kugawa majimbo ya uchaguzi na kuweka mipaka yake.
6. Ibara ya 74(7) ikisomwa pamoja na kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Uchaguzi inayompa Rais mamlaka ya kuteua Mkurugenzi wa Uchaguzi, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Tume. Marekebisho hapa ni kuifanya Tume iajiri yenyewe Mtendaji Mkuu na watumishi wengine wa Tume.
Ndugu wanahabari,
Pamoja na mapendekezo haya ACT Wazalendo inaonelea kwamba ni muhimu na lazima kuwepo kwa maridhiano ya kitaifa kwanza kabla ya kupiga hatua yeyote, Kwani bila kuwepo na mazungumzo miongoni mwa wadau muhimu na kukubaliana mambo ya msingi na kujenga mwafaka kwa mambo hayo mchakato wa Katiba utakwama tena. Ni rai yetu kwa Ofisi ya waziri Mkuu kusimamia kwa ukamilifu jitihada ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano amezianza katika kuelekea kuweka mazingira bora ya kufanya siasa nchini.

Ndugu Wanahabari,
Ofisi ya Waziri Mkuu pia inasimamia kukabili majanga nchini. Siku za hivi karibuni tumeshuhudia masoko yakiungua moto na kamati za uchunguzi kuundwa bila ya taarifa zake kuwekwa wazi na matukio yamekuwa yakiendelea. Kuna minong’ono kuwa masoko haya yanachomwa makusudi ili operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara wadogo ikamilike. Minong’ono hii inaweza kuondoka kwa kupitia tu uchunguzi huru kuhusu matukio mbalimbali ya kuungua kwa masoko na kuharibu mali za wananchi wetu. Katika Hotuba yake Waziri Mkuu hajaonyesha matumaini yeyote ya kuipa nguvu Idara ya Maafa ili kuweza kuzuia masoko kuungua n ahata majanga mengine nchini. ACT Wazalendo inataka kuundwa kwa Tume Huru itakayohusisha wafanyabiashara wadogo wenyewe kuchunguza vyanzo vya masoko kuungua sehemu mbalimbali za nchi na hatua mahususi za kuchukua kudhibiti hali hiyo.

Ndugu wanahabari,
Eneo la Mwisho ambalo Kamati ya Kuismamia Serikali ya ACT Wazalendo inapenda kutolea maoni ni suala la hali ya maisha ya wananchi (mfumuko wa bei na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu). Vilio kutoka kila kona ya nchi yetu vinaonyesha kuwa maisha yamekuwa magumu sana kwa wananchi wengi. Gharama za maisha zimekuwa kubwa kutokana na kupanda bei kwa bidhaa zote muhimu hususan chakula na mafuta ya petroli na dizeli. Tumeona bidhaa za chakula kama vile ngano, mchele, mafuta ya kula vimepanda kwa wastani wa asilimia 60 hadi asilimia 180 nchi nzima. Vilevile kwa pembejeo za kilimo na Mbolea, vifaa vya ujenzi mwenendo wa bei upo juu zaidi. Katika hotuba ya Waziri Mkuu Bungeni suala hili halijapewa uzito unaostahiki.
Tunawapongeza wabunge wote ambao wamepaza sauti kuhusu suala hili kwani wananchi wanaumia sana. Katika mazingira kama haya ambayo wananchi wanateseka Serikali imetangaza kuwa imelipia ndege zingine tano mpya. Hii imeongeza chumvi kwenye vidonda na inaonyesha kuwa Serikali ipo ‘out of touch’ na kutojali. Unawezaje kutoa mabilioni ya fedha kununua ndege katika mazingira haya ambayo wananchi hawawezi kukabili bei ya Sukari, Mafuta ya kula, Mchele, maharage, ngano nk.
ACT Wazalendo inaelekeza kwa Serikali kuwa ni lazima ifunge mkanda wa matumizi yake na vile vile itoe nafuu kwa wananchi kwa kupunguza kodi zake katika mafuta ya dizeli kwa angalau shilingi 500 kwa kila lita ya Dizeli ili kuwahami wananchi. Serikali pia ichukue hatua za kupunguza ushuru wa forodha kwa mafuta ya kula na sukari ili kupunguza bei za bidhaa hizo kwenye masoko na kuwahami wananchi.

Asanteni kwa kunisikiliza
Ndg. Dorothy Jonas Semu
Waziri Mkuu Kivuli, ACT Wazalendo
11 April 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK