Serikali ichukue hatua kulinda usalama wa raia na mali zao

SERIKALI ICHUKUE HATUA KULINDA USALAMA WA RAIA NA MALI ZAO 

Hivi karibuni miji yetu nchini imekumbwa na vitendo vya uvamizi kwa wananchi na mali zao, kujeruhiwa na kuporwa. Matukio haya yameripotiwa na Wananchi katika jiji la Dar es Salaam wakazi wa maeneo ya Wilaya za Ilala, Temeke na Kawe kwa nyakati tofauti. Vitendo hivi vimedaiwa kufanywa na vijana wanaoitwa Panya Road. Mpaka sasa, waathirika wakuu wa matukio hayo ni Wakazi wa kata za Chanika, Zingiziwa na Mtaa wa Mtongani kata ya Kunduchi.

Vijana hao wamekuwa na desturi ya kuvamia nyumba moja baada ya nyingine wanaiba, wanajeruhi na kubaka. Matukio hayo yamekuwa yakifanyika kati ya majira ya saa nne hadi saa tano mpaka sasa zaidi ya watu 89, wamejeruhiwa kwa mtindo wa kuingia nyumba moja baada ya nyingine.

Wahalifu hao inasemekana wanafanya shughuli zao kwa uhuru mkubwa na huwa inawachukua hadi masaa mawili kufanya vitendo vyao huku vituo vikubwa vya polisi vikiwa karibu na maeneo ya matukio.

Juzi wamevamia nyumba ya mtaa wa Gogo jirani na kituo cha polisi na wamefanya vitendo vya kinyama na kuondoka salama. Usiku wa majuzi pia, wamejeruhi watu 19 wa Kata ya Kunduchi.

ACT Wazalendo inalaani vikali vitendo hivyo vinavyofanywa na makundi ya vijana wahuni na kulitaka Jeshi la Polisi nchini kuchukua HATUA stahiki za kulinda Raia na Mali zao.

Zifuatazo ni hatua za haraka ambazo ACT Wazalendo inazitaka mamlaka kuchukua:

1. Ufanyike msako mkali wa wahalifu hawa ili kuwabaini na kuwakamata na kuchukuliwa hatua za kisheria kwani wahalifu hawa wanaishi miongoni mwa jamii zetu.

2. Vikundi vya Ulinzi Shirikishi viimarishe usimamizi wake ili viweze kutekeleza kazi na wajibu wake kwa ufanisi.

3. Jeshi la Polisi liwe na operesheni Maalum ya kudhibiti vitendo hivi vinavyohatarisha amani ya wananchi na mali zao kwa kutumia za kiusalama kubaini mitandao hii ya kihalifu.

4. Serikali itekeleze mipango ya uchumi ambayo ACT Wazalendo imekuwa ikiitaka kutekeleza ili kuijengea nchi uwezo wa kuhimili hali ngumu ya kiuchumi na maisha magumu miongoni mwa wananchi. Mipango hiyo itawezesha kuzalishwa kwa ajira, kuboresha hali za maisha ya Wananchi kwa kupunguza ugumu wa gharama za maisha.

Imetolewa na:
Mbarala Maharagande
[email protected]
Msemaji wa Kisekta Wizara ya Mambo ya Ndani
ACT Wazalendo

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK