Serikali Inapuuza Kilimo. Ukuaji wa Sekta ya Kilimo Unaendelea Kushuka

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA
WIZARA YA KILIMO, MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI

HOTUBA YA NAIBU MSEMAJI WA SEKTA YA KILIMO, MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI NDG. SELEMANI MISANGO KUHUSU BAJETI YA WIZARA YA KILIMO KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.

Utangulizi.
Ndugu Waandishi wa Habari
Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo iliwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 17 Mei 2022, Chama cha ACT Wazalendo kimefuatilia kwa kuisoma na kuichambua hotuba hiyo kwa lengo la kubainisha ni kwa kiasi gani inakidhi matarajio na matamanio ya wananchi wanaojishughulisha na sekta ya kilimo hapa nchini.

Kupitia uchambuzi huo, Chama Cha ACT Wazalendo kupitia Naibu Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi tunatoa maoni yetu kutokana na hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Kwa kufanya hivyo, tumekuja na hoja tisa (9) kuhusu bajeti ya mwaka huu, zifuatazo ni hoja zenyewe;
1. Serikali inapuuza Kilimo, Ukuaji wa sekta ya kilimo unaendelea kushuka.
Tanzania imeendelea kutegemea Sekta ya Kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake kwa kutoa ajira kwa asilimia 61.1 ya nguvu kazi za watanzania wote na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye miaka yenye mvua za kutosha. Katika mwaka 2021 Sekta ya Kilimo ilichangia asilimia 23.1 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 27.7 mwaka 2020. Mchango mkubwa katika Pato la Taifa ulitokana na Sekta ya Kilimo, ikifuatiwa na Sekta nyingine za kiuchumi.
Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Kilimo wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2021/22, kwa miaka hii mitatu mfululizo ukuaji wa Kilimo umekuwa ukishuka na kupanda huku mwaka 2021 takwimu zikionyesha ukuaji umeshuka zaidi. Mwaka 2019 sekta ya Kilimo ilikua kwa wastani wa 4.4%, Mwaka 2020 kwa 5.3% na Mwaka 2021 kwa 4.2 %.
Kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanashiriki katika shughuli za kilimo, ni wazi kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato na kupunguza umasikini. Hii inamaanisha, unapowekeza kwenye sekta ya kilimo unakuwa umewekeza kwa theluthi mbili ya Watanzania. Unapokuza kilimo unakuza uchumi wa theluthi mbili ya Watanzania, na unapoacha kilimo kishuke maana yake umewafukarisha theluthi mbili ya Watanzania.
Kiuhalisia Sekta ya Kilimo inapaswa kukua kwa asilimia zaidi ya 8% angalau kwa miaka mitatu mfululizo, na ukuaji huo uendelee kukua kwa wastani wa 6% kwa muda miaka kumi mfululizo.
Bajeti iliyoombwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni Shilingi 751,123,280,000 kwa kulinganisha na bajeti kuu (kama ilivyowasilishwa ukomo wa bajeti), kiasi hiki hakizidi asilimia 3 ya bajeti kuu ya Serikali, ni kiwango cha chini zaidi kwa kulinganisha na makubaliano ya mataifa ya Afrika kupitia Azimio la Maputo la kutenga kiasi cha asilimia 10 ya bajeti kuu kwenye Sekta ya Kilimo.
Sisi ACT Wazalendo kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020 4.4(i) tulisema tutatenga 20% ya bajeti ya maendeleo kwenye Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, mara mbili zaidi ya makubaliano yaliyoazimiwa na Umoja wa Afrika (CAADAP).
2. Kilimo kijibu mahitaji yetu ya ndani.
Mwenendo wa kupanda kwa bei za bidhaa hususani zinazotokana na mazao yenye mahitaji makubwa hapa nchini, umezua taharuki kwa takribani miezi saba (7) sasa. Miongoni mwa bidhaa/mazao hayo ni pamoja na ngano, sukari na mafuta ya kula. Moja ya sababu ya kupaa kwa bei za bidhaa/mazao hayo ni kutokana kuwepo kwa utegemezi mkubwa kutoka nje.
Kwa mujibu wa takwimu za wizara katika mwaka 2021/2022, uzalishaji wa ngano umefikia tani 70,288 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya zaidi ya tani 1,000,000 za ngano kwa mwaka sawa na upungufu wa tani 929,712, uzalishaji wa mafuta ya kula ni tani 300,000 wakati mahitaji halisi ni tani 650,000 sawa na upungufu wa tani 350,000 na sukari mahitaji ni tani 710,000 huku zinazozalishwa ni tani 378,449, sawa na 67.7% ya mahitaji ya sukari
Katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2022/23 tulitarajia kuona mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa mazao yenye mahitaji makubwa (Import substitution crops) ili kupunguza uagizaji wa bidhaa/mazao hayo kutoka nje ya nchi, ambayo ni changamoto ya muda mrefu.

Kinyume chake Serikali imekuja na maneno matupu ya kila mwaka tunapokuwa katika hali kama tunayoipitia hivi sasa. Jambo la kushangaza tunazalisha arizeti, ufuta, korosho, chikichi, karanga za kutosha lakini zinasafirishwa kwenda nje kulisha viwanda vya ughaibuni, wenyewe tukishuhudia upungufu mkubwa. Tumebinafsisha mashamba ya ngano na sasa yamekuwa mapori, mbuga ya wanyama binafsi (private concession). Kuchelewa kwa kiwanda cha sukari kwa miaka mitatu, kwa ubadhirifu tu wa Serikali.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali irudishe na kugawa kwa wananchi mashamba yote iliyobinafsisha na ambayo hayafanyi uzalishaji ili yatumike kuzalisha kama vile NAFCO Hanang (mashamba saba yenye ukubwa wa hekta 100,000).
Pili, Serikali iwatumie wazalishaji wadogo wadogo kwa kuiga Modeli ya Bangladesh ya “Hub and Spoke” ili kuongeza uzalishaji wa ngano. Serikali inasema inataka kutumia wakulima wakubwa kutoka ughaibuni kuja kuwekeza nchini ili kumaliza tatizo la mafuta ya kula, ngano na sukuri, hii haitokuja kutokea kwa kuwa msingi wa wakulima wakubwa sio kukidhi mahitaji yetu ndani bali kupata faida.
Tatu, Serikali iwekeze na kuwezesha Viwanda vya Alizeti na Mawese.
3. Bodi za mazao zimeshindwa kumkomboa mkulima na kuendeleza kilimo.
Serikali ilianzisha Bodi ya Mazao na baadaye Benki ya Kilimo, ili kuwezesha kilimo, pamoja na kuundwa kwa bodi hizo, kilimo kimeendelea kukumbwa na changamoto kadhaa kama vile; bei kubwa za mbolea na viuwatilifu, masoko duni ya mazao, bei kubwa ya nyenzo za kilimo, huduma ya fedha yenye mlolongo na mzunguko mrefu, huduma dhaifu ya ugani na kilimo cha kutegemea mvua. Licha ya fedha nyingi za umma kuangamizwa, kilimo bado kimekuwa duni na ukweli juu ya kauli hii unathibitishwa na idadi kubwa ya vijana wanaoachana na kilimo na kukimbilia mijini kutengeneza jeshi jipya la WAMACHINGA.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka 2020/21 zinaonyesha utendaji wa bodi kama ifuatavyo;
 Bodi ya Korosho ilijiwekea Mpango Mkakati wa miaka 5 (2021/22 - 2025/26) ya kuzalisha korosho ghafi kiasi cha tani 700,000 ifikapo mwaka 2025/26. Hata hivyo, Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Maendeleo ya Kilimo, uzalishaji wa zao hilo ulishuka Kwa miaka 4 mfululizo kwa 33% kutoka tani 313,826.39 zilizozalishwa mwaka 2017/18 hadi tani 210,785.85 mwaka 2020/21.
 Ripoti ya CAG pia imeonyesha Mkoa wa Pwani umeshuka sana kwa uzalishaji wa zao la korosho na ubora wake. Ripoti imeonyesha kwa mwaka 2020/21 Mkoa wa Pwani ulizalisha Tani 10,551, ni 12% tu ya tani hizo zilikiwa za daraja la kwanza.

 Bodi ya Chai; zao hilo limeporomoka kutoka Tani 2,510 mwaka 2020/21 hadi Tani 2,412 2022
 Bodi ya Kahawa; Kwenye mpangokazi wake wa miaka 5 (2020/21 - 2024/25 ilijiwekea lengo la kuzalisha miche ya Kahawa Milioni 20 lakini mpaka kufikia Juni 2021 taasisi zilizoingia mikataba hiyo ya JKT ITENDE iliyopewa jukumu la kuzalisha miche milioni moja ilikuwa imezalisha miche 223,841 huku TACRI MBOZI waliopewa jukumu la kuzalisha miche milioni 3 ilikuwa imezalisha miche 350,000 tu mpaka wakati huo.

 Ukichukua kasi hii ya taasisi hizi mbili ni wazi kabisa dhamira ya kuwa na miche ya kahawa milioni 20 ifikapo 2024/25 haitakuwa imefikiwa.

 Bodi ya Pareto; iliingia makubaliano na Taasisi ya TARI Naliendele kusambaza mbegu Tani 71.9 zenye uwezo wa kuzalisha miche milioni 9.2. Bodi imeshindwa kubainisha ni miche mingapi imezalishwa.

 Bodi ya Pamba; kwa mujibu wa Ripoti ya CAG, Serikali imeshindwa kuisimamia Bodi ya Pamba ambayo imeisababishia Taifa hasara kubwa ya fedha Shs Milioni 847.24 kutokana na kuagiza viuatilifu vilivyobakiza muda mfupi kwisha muda wake. Bodi imekuwa na mwendelezo wa tabia ya kuagiza viuatilifu vilivyobakiza muda mfupi kwisha ubora wake, kwa mfano; Mwaka wa fedha 2019/20 kulikuwa na mlundikano wa viuatilifu vyenye thamani ya ShT Milioni 198.84 na mwaka uliofuatia June 2021 kulikuwa na ongezeko la viuatilifu vya thamani ya ShT Milioni 648.40 na kufanya jumla ya ShT Milioni 847.40.

Kwa kuwa fedha zilizoripotiwa na CAG kuwa zimeangamia ni nyingi sana, Chama Cha ACT Wazalendo kinaitaka TAKUKURU kuchunguza Kwa kina suala hili na kuchukuwa hatuwa stahiki.

4. Upatikanaji wa mbolea na matumizi ya zana za kisasa
Katika msimu wa kilimo 2021/22 tumeshuhudia kupaa kwa bei ya mbolea na kwa namna fulani upatikanaji wake ulikuwa unasumbua sana. Pamoja na sababu zingine, sababu kuu ni uzalishaji mdogo wa mbolea ndani ya nchi, jambo linalofanya kuwa na utegemezi wa mbolea kutoka nje kwa asilimia zaidi ya 95%, ambapo bei zake hatuna uthibiti wake wa moja kwa moja. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara 2021/22 mahitaji ya mbolea nchini kwa mwaka ni Tani 718,051 huku mbolea inayozalishwa nchini ni Tani 32,239 tu.
Hali hii ya kutojitosheleza kwa mbolea, imepaisha bei za mbolea kwa asilimia hadi 220 ikilinganishwa na bei za mbolea kwa msimu uliopita. Kwa hiyo, tunaitaka Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji na kujitosheleza kwa mbolea kwa kufufua na kuharakisha mazungumzo na mwekezaji wa kiwanda cha UREA Kilwa Masoko, Lindi. Pia, kusimamia uzalishaji wa kiwanda cha mbolea cha Dodoma na Minjingu.

Aidha, Serikali irejeshe mfumo wa ununuzi wa pamoja wa mbolea kupitia vyama vya ushirika na kupitia shirika la Mbolea (TFC) isimamie uagizaji wa mbolea kutoka kwa wazalishaji moja kwa moja ili kunusuru wakulima.
Kuhusu zana za kilimo; kwa mujibu wa hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Kilimo ya mwaka 2020/21, matumizi ya matrekta ni 25.7% na wakulima wanaolima kwa jembe la mkono ni 50%. Kwa takwimu hizo, nchi haitaweza kuleta Kilimo cha Kimapinduzi.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali, kupitia taasisi zake, kuingiza matrekta (imara) na kuyauza kwa ruzuku pia kwa mkopo wa masharti nafuu.
5. Msururu wa Kodi na tozo kwenye mazao
Serikali kwa miaka kadhaa imekuwa ikifumbia macho kilio cha wakulima kutokana na tozo kubwa na nyingi wanazotozwa wakati wa kuuza mazao yao. Hali hii inawakatisha tamaa ya kuongeza jitihada kwenye Sekta ya Kilimo.
Kwa mfano, kwenye zao la tumbaku, mrundikano wa kodi nyingi na zisizo na umuhimu zimesababisha kuchochea wakulima wengi kupunguza uzalishaji kwa sababu wamekuwa wakipata hasara badala ya faida.
Kwenye zao la korosho nako makato ni mengi yanayodidimiza faida ya mkulima. Kwa kutumia mfano halisi wa makato yanayotokana na tozo na kodi kwenye zao la Korosho kwa msimu wa 2021/22 unaonyesha kama ifuatavyo kwa kila kilo moja;
• Tozo ya Bodi ya korosho ShT 30/-
• Tozo ya Halmashauri ShT 65/-
• Tozo ya Chuo Cha Naliendele ShT 15/-
• Tozo ya chama Kikuu Cha Ushirika ShT 30/-
• Tozo ya chama Cha Msingi Cha Ushirika ShT 25/-
• Tozo ya kuchangia Elimu Halmashauri ShT 30/-
• Tozo ya usafirishaji korosho Toka ghala la AMCOS hadi ghala la Chama Kikuu Cha Ushirika (inategemea na umbali).
Utitiri wa tozo kwa mazao ya wakulima yanashusha tija kwa kiasi kikubwa sana na hatimaye kushusha ari ya kujihusisha na kilimo. Hii ni moja miongoni mwa sababu zinazopelekea vijana na wananchi wengine kufanya shughuli nyingine tofauti na kilimo.
6. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ni kitanzi kwa wakulima.
Tunatambua kuwa Mfumo wa stakabadhi ghalani unasimamiwa chini ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kupitia Bodi ya Leseni ya Maghala (Tanzania Warehouse Licensing Board - TWLB) kwa mujibu wa Sheria Na. 10 ya mwaka 2005 na kutekelezwa kwa kanuni za mfumo za mwaka 2006, lakini ni wazi kuwa athari zake zinagusa moja kwa moja sekta ya kilimo.
Kwa uzoefu, utekelezaji wa mfumo huu umekuwa ukiacha maumivu makubwa sana kwa wakulima wetu badala ya kuwa msaada—tofauti na ilivyotarajiwa. Changamoto ya mfumo huu ni kuwa hakuna ushirikishwa wa moja kwa moja kuhusu kuamua bei ya mazao ya wakulima. Pili, ucheleweshwaji wa malipo kwa wakulima (wakulima wanakopwa) jambo ambalo wakulima wengi hawawezi kumudu, hatimaye wanauza kwa watu wa kati (Kangomba) kwa bei ya chini zaidi (wananyonywa). Lakini kutokana na shida alizokuwa nazo mkulima anajikuta anaingia kwenye mtego huo.
Aidha, Serikali na vyama vya ushirika wamekuwa madalali wa mazao badala ya kuwatafuta wateja wa bei yenye tija kwa wakulima. Mfumo huu wa masoko unawanufaisha zaidi watumishi wa vyama vya ushirika, watumishi wa Serikali na Wafanyabiashara wanaonunuwa mazao kwa mtindo wa kangomba. Mazao yaliyoathirika zaidi na sheria hii ni korosho, ufuta, mbaazi na tumbaku.
Tumetazama bajeti na vipaumble vya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2022/23 hatujaona mkakati wa kuboresha mfumo huo ili kuwezesha na kuwanufaisha wakulima; na kutokana na changamoto hizo za mfumo, sisi ACT Wazalendo tunapendekeza mfumo wa malipo wa stakabadhi ghalani uimarishwe uwe wa kieletroniki na uwe wa papo kwa papo. Pia, utumike mfumo wa soko la bidhaa (commodities exchange) kwa kuwashirikisha moja kwa moja wakulima wenyewe.
7. Kilimo cha kutegemea mvua
Pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji (Irrigation Development Fund (IDF)) Kupitia Tume ya Taifa ya umwagiliaji(NIRC), bado sekta hii ya umwagiliaji haiwanufaishi wakulima. Tanzania ina mabonde mengi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, hivyo ni mhimu kwa nchi kuwekeza katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji ili sekta hii iwe na tija kwa taifa.
Chama cha ACT Wazalendo tunaiagiza Serikali kuwekeza nguvu zaidi kwenye mabonde ya Mto Ruvu, Rufiji, Pangani, Kilombero, Ruvuma, Mbwenkuru, Ruaha, Kihansi, Mara, na mabonde ya ziwa Tanganyika na Victoria. Kama Taifa litawekeza nguvu na maarifa ya kutosha maeneo hayo Taifa litajihakikishia akiba ya chakula cha kutosha na ziada kujipatia pesa za kigeni.
8. Safari ya kufungamanisha Kilimo na viwanda bado ni ndefu.
Kwa kutazama sifa ya uchumi wa nchi yetu, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika unatawaliwa kwa sehemu kubwa na sekta ya uzalishaji wa malighafi (Extractive industry) hususani kilimo, uvuvi, misitu na madini. Kwa upande wa kilimo sehemu kubwa ya mazao yanayoingiza au changia pato la taifa ni mazao ambayo huwa ni malighafi inayotegemea soko la nje.
Uzalishaji wa mazao unaofanywa na wakulima hauna uhusiano mkubwa na sekta ya viwanda iliyopo nchini, jambo ambalo linaathiri Maendeleo ya kilimo chetu kwa namna mbalimbali. Kwanza, bidhaa zinazozalishwa viwandani hazijibu changamoto zinazokikabili kilimo Chetu, tumeona uhalisia kuwa asilimia 95 ya mbolea inayotumiwa na wakulima nchini haizalishwi ndani, pia viuatilifu na zana za kazi nazo zinaagizwa kutoka nje. Hivyo hivyo, kwa upande wa kilimo malighafi zinazozalishwa zinasafirishwa nje kwa ajili ya viwanda vya ughaibuni.
Katika mipango ya Serikali hakuna dhamira ya dhati ya kumaliza muundo huu wa uzalishaji wa uchumi wetu ili kukisaidia kilimo na wakulima wetu.
ACT Wazalendo, tunaendelea kusisitiza kuwa ni wakati sasa wa kuunganisha Maendeleo ya viwanda na ukuaji wa kilimo. Pia, Serikali iweke mkazo kwenye viwanda vidogo maeneo ya vijijini vinavyoendeshwa, kumilikiwa na kusimamiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vyao vya ushirika ambavyo vitaweza kuzalisha ajira na kuchakata mazao.

9. Miundombinu mibovu vijijini
Umasikini kwa Tanzania ni suala lenye uhusiano wa karibu na maisha ya vijijini ambako ndiko watu wengi masikini wanaishi. Maeneo ya vijijini Tanzania ndiko kwenye miundombinu mibovu ya kiuchumi na kijamii kiasi cha kuathiri maisha ya jamii inayoishi huko. Hali hii mbaya inajumuisha miundombinu ya Elimu, Afya, Maji, Barabara, Umeme na hata huduma za kijamii na ugani.
Asilimia zaidi ya 70% ya masikini huishi vijijini wakitegemea kilimo. Zaidi ya 32% ya wakazi wa vijijini huishi chini ya kiwango cha umasikini, 24% huishi maeneo ya mijini na 16% tu ya wakazi wa Dar es salaam ndio masikini hivi. Zaidi ya 80% ya uzalishaji mazao ya chakula hufanywa na wazalishaji wadogo vijijini wenye mashamba kati ya nusu eka na eka moja tu. Zaidi ya 60% ya wazalishaji hawa wadogo ni wanawake.
Kutoa kipaumbele kwenye kilimo ni kuwekeza kwenye miundombinu inayohudumia kilimo na wakulima vijijini.
Hitimisho
Kilimo kimechangia 23.1% ya Pato la Taifa kwenye robo ya nne ya mwaka 2021 ingawa ilipata bajeti ya chini ya 4% na ambayo kiwango chake huathiriwa zaidi kwa ajili ya mdororo wa thamani ya Shilingi. Mchango wa Sekta ya kilimo kwenye pato la Taifa (GDP) linapungua huku ukuaji wa sekta wenyewe ukibaki bila tija na kukwama. Hii husababishwa na hoja kuwa ziko changamoto kadhaa katika sekta ya kilimo ambazo hazijafanyiwa kazi kabisa kwa miaka nenda rudi.

Imetolewa na:
Ndugu Selemani Misango,
[email protected]
Naibu Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
ACT Wazalendo.
18 Mei, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK