Serikali iondoe shilingi 500 ya kodi kwenye kila lita ya Mafuta (Petroli, Diseli na mafuta ya taa), kuhami maisha ya watanzania.

Wananchi hawawezi tena kuhimili gharama: Serikali iondoe shilingi 500 ya kodi kwenye kila lita ya Mafuta (Petroli, Diseli na mafuta ya taa), kuhami maisha ya watanzania.


Utangulizi:

Jana tarehe 3 Mei 2022 Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta ya petroli, diseli na mafuta ya taa huku tukiona ongezeko la bei za rejareja za petroli kwa shilingi 287 (sawa na asilimia 10), Diseli shilingi 566 kwa kila lita (sawa na asilimia 21) na Mafuta ya taa shilingi 430 (sawa na asilimia 16.03) kwa kulionganisha na bei za mwezi April. Na kufanya bei mpya ya petroli 3,148 kutoka 2,861 kwa Dar es Salaam na bei ya juu zaidi kuwa 3,495 Kagera kwa Tanzania Bara. Bei ya Diseli ni shilingi 3,258 kutoka shilingi 2692 na bei ya mafuta ya taa shilingi 3112 kutoka shilingi 2682. Bei hizi zimetangazwa kuanza kutumika leo tarehe 4 Mei 2022.
Tozo na kodi za Serikali zinavyoongeza maumivu:
ACT Wazalendo tumefanya uchambuzi wa gharama halisi ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa katika soko la dunia, kwa mwezi April (ambapo mafuta yanayoenda kutumika yaliagizwa) baada ya gharama za usafiri, bima na forodha, (CIF) na kabla ya kodi na tozo za Serikali na kulingalisha gharama iliyotangazwa mwezi huu. Pia, tumetazama utaratibu wa udhibiti na usimamizi wa bei na namna biashara inavyoendeshwa.


Moja, Serikali inaongeza mzigo kwa wananchi. Kwa utafiti tulioufanya bei ya mafuta sokoni (soko la dunia, mwezi April 2022) kwa lita ya petroli ni Sh1,438.80, dizeli Sh 1401.28. Gharama za usafiri, forodha na bima (CIF) mpaka Bandari ya Dar es Salaam kwa petroli ni Sh100.71, dizeli Sh 61.65 kwa kila lita moja. Hivyobasi, kabla ya serikali haijaongeza kodi na tozo zake zote gharama ya petroli ikiwa bandarini, Dar es Salaam itakuwa ni shilingi 1539.51 na gharama za diseli itakuwa ni shilingi 1462.93. Serikali imeongeza shilingi 1321 kwenye lita ya petroli sawa na asilimia 46.1 na shilingi 1229.07 kwenye diseli ambayo ni sawa na asilimia 45.6.
Kutona na hali halisi ya bei za mafuta na athari zilizopo mtaani, ACT Wazalendo inaona ukimya wa serikali juu ya kupanda kwa bei za mafuta na kupanda kwa gharama za maisha ni kutowajali wananchi wake ambao ndio waathirika wakubwa wa jambo hili. Tunaendelea kuisisitiza Serikali kuchukua hatua ili kuinusuru nchi yetu kutoka kwenye hali tete zaidi.
Mapendekezo ya ACT wazalendo ili kukabiliana na tatizo hili:
1. Serikali isimamishe kwa muda angalau tozo ya Shilingi 500 kwenye mafuta.
Katika kila lita ya petroli, diseli na Mafuta ya taa serikali isimamishe kuchukua shilingi 500 ili kukabiliana kupaa kwa bei. Mahitaji na matumizi ya mafuta kwa mwezi ni wastani lita milioni mia nne (Petroli, Diseli na Mafuta ya taa) Tunafahamu kusimamishwa kwa tozo hiyo, kutaathiri bajeti ya serikali. Kiasi ambacho serikali itapoteza kwa kuondosha shilingi 500 kwa kila mwezi itakuwa ni wastani wa Shilingi Bilioni 200, ambayo tunapendekeza kusimamisha kwa muda ununuzi wa ndege na Serikali ibane matumizi yake (safari za nje, semina na Warsha, bunge la bajeti lifupishwe) kufidia kuondolewa kwa kodi ya shilingi 500.

2. Pia, kutumia fedha za akiba zilizopo kwenye Mfuko wa fedha wa kimatiafa (IMF) kufidia kodi iliyoondolewa kwenye kodi ya mafuta (Petrol, Diseli na mafuta ya taa).

3. Serikali iongeze uwezo wa kuagiza mafuta ili kuwa na akiba ya mafuta (reserve):
Ni wazi kuwa Serikali haina utamaduni wa kuwa na akiba ya mafuta (Reserve). Hii ni miongoni mwa mambo yanayopelekea bei ya mafuta kupanda kila mwezi hivyo ni wakati wa serikali kupitia shirika la Mafuta (TPDC) kujenga utamaduni wa kuwa na akiba ya mafuta ya kutosha kwa angalau miezi sita ili kukabili dharura ya namna hii.

4. Tuwekeze kwenye nishati mbadala kulinda uhuru, kuleta unafuu bei na nishati endelevu:
Ni wazi kuwa mpango wa kuitumia gesi kama nishati mbadala umechelewa sana kuliko matarajio ambayo wananchi wamepewa. Katika hali iliyopo sasa nchini, ni muhimu kufikiria namna ya kutumia rasilimali za nchi kujikwamua kutoka kwenye majanga ya kinishati ambayo hatuwezi kuyakabili moja kwa moja kutokana na kutozalisha wenyewe nchini.

Hivyobasi, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuharakisha mradi wa kusindika wa Gesi asilia gas kuwa kimiminika, kwa kuweka wazi mazungumzo na makubaliano, pamoja na mikataba kwa wananchi, kuwashirikisha wananchi.
Hitimisho:
ACT Wazalendo inaitaka Serikali itimize wajibu wake wa kuhami wananchi katika majanga na kuhakikisha panakuwa na ustawi wa wananchi katika nyakati kama hizi. Ni wakati sasa, Serikali itangaze dharula ya kitaifa juu ya hali ya uchumi (national crisis) na hatua za dharura zichukuliwe na wananchi, wadau wote wa maendeleo ili kuzuia hali isiendelee kuwa mbaya kwenye janga hili la kitaifa.

Imeandaliwa na:
Ndg. Is-haka Rashid Mchinjita,
Msemaji wa Sekta ya Nishati,

Ndg. Immanuel R. Mvula
Msemaji wa sekta ya Fedha na Uchumi

Ndg. Ally Saleh
Msemaji wa sekta ya Habari, Teknoloji ya Habari na Uchukuzi

ACT Wazalendo.
04 Mei 2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK