Serikali Iondoe Tozo ya Sh 500 kwenye mafuta. Ruzuku iliyowekwa bado haitoshi.
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
Ruzuku ya Serikali kwenye Mafuta; Bado haitoshi, Serikali iondoe tozo ya sh.500.
Utangulizi:
Tumefuatilia leo tarehe 10 Mei 2022 Waziri wa Nishati Januari Makamba ametoa kauli ya Serikali Bungeni kuhusu Ongezeko kubwa na kupaa kwa bei ya Mafuta. Waziri ametaja hatua kadhaa ili kupunguza bei ya mafuta nchini, ACT Wazalendo kupitia tamko la pamoja wasemaji wa sekta ya Nishati, sekta ya Fedha na Mipango na Sekta ya Uchukuzi la tarehe 04 Mei 2022, tulitoa mapendekezo yetu na kuitaka Serikali kuingilia kati haraka. Katika mapendekezo yetu tuliitaka Serikali kufanya mambo yafuatayo; Serikali kuondoa tozo ya shilingi 500, kuanzisha utaratibu wa kuhifadhi mafuta, Kutumia akiba ya nchi ya shirika la fedha kutoa ruzuku, Serikali kubana matumizi na kuweka mkakati wa nishati mbadala.
Kupitia kauli ya Waziri wa nishati, Serikali imechukua baadhi ya mapendekezo tuliyoyatoa lakini bado hazitoshi na zinahitaji zitekelezwe kwa haraka zaidi, kama tunavyoelezea hapo chini.
Moja, Serikali kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 102 kwa ajili ya kushusha bei za mafuta. Hatua hii ina ahueni, lakini bado haitoshi kuleta unafaa na kutua mzigo mzito kwa wananchi. Kwasababu kwa ruzuku hii ya Serikali itaenda kupunguza gharama zenye thamani ya shilingi 250 hadi 320 kwa kila lita moja ya mafuta (Petroli, Diseli na Mafuta ya taa). ACT Wazalendo tunaona haitoshi kutoa ruzuku kwa kiasi kilichotolewa, ingefaa kwenda sambamba na hatua za kuondoa kodi na tozo za Serikali kwenye kila lita moja ya mafuta yenye thamani ya shilingi 500 sawa na bilioni 150 kwa mwezi. Tunaendelea kusisitiza Serikali ifanye zaidi kwa kuondosha tozo hizo ili unafuu upatikane.
Pili, Serikali ianze utekelezaji, kusbiri hadi mwezi Juni ni kuendelea kuwaumiza wananchi. Nafuu iliyosemwa na Serikali inapaswa kuanza sasa mpaka hapo mwaka wa fedha utakapoanza, Sababu zilizotolewa na Serikali kuendelea kusubiri hadi tarehe 1 Juni, hazina mashiko kwani hali ya wananchi ni mbaya hawawezi kumudu ugumu wa maisha.
Tatu, kuanzishwa kwa hifadhi ya mafuta ya kimkakati ni hatua nzuri ambayo tuliipekendeza bado tunaendelea kusisitiza kuwa hatua ianze haraka hatuwezi kuendelea kusubiri. Sambamba ni hili ushirika wa Shirika la mafuta la taifa (TPDC) kuagiza mafuta nje ili kupata bei ya mafuta yenye punguzo zaidi ni muhimu kupewa kipaumbele. Jambo hili nalo lilipaswa kuanza tangu mwaka jana kuendelea kusubiri zaidi ni kutojali maslahi ya wananchi.
Hitimisho:
ACT Wazalendo inaitaka Serikali ichukue jitihada za makusudi kutekeleza hatua za dharura na kuhakikisha inajipanga kwa hatua za kati, isiishie kwenye kutoa kauli tupu.
Imeandaliwa na:
Ndg. Is-haka Rashid Mchinjita,
Msemaji wa Sekta ya Nishati,- ACT Wazalendo.
10 Mei, 2022
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter