Serikali Ishughulikie Zao la Korosho Kuepusha Kuporomoka kwa Uchumi wa Wakulima.

STAKABADHI GHALANI, KUPOROMOKA BEI YA KOROSHO; SERIKALI ISIRUHUSU KUUA UCHUMI WA WAKULIMA WA KOROSHO

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kujielekeza kushughulikia tatizo la kuporomoka kwa bei ya korosho kutokana na uhalisia wa umuhimu wa zao hilo kwenye uchumi wa kusini, hususani Mikoa ya Lindi, Mtwara na Tunduru. Minada iliyotangazwa ilileta bei ya juu ya Shilingi 2,011 na bei ya chini Shilingi 1,480 jambo lililopelekea wakulima kugomea kuuza korosho zao kwa kuwa zinaenda kuwakandamiza na kuwanyonya zaidi.
Katika kuelezea kadhia hiyo Kiongozi wa Chama Ndg. Zitto Zuberi Kabwe akiongea na wananchi, wanachama na Viongozi wa ACT Wazalendo katika kata ya Mahuta wilaya ya Tandahimba, Mtwara amesema: “Licha ya bei ya korosho kushuka sana na wananchi kuonyesha hazitowafaidisha kwa kuigomea minanda hiyo kutokana na gharama za uzalishaji, kupanda kwa gharama za maisha na mwenendo wa soko la Dunia hakuna hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwanusuru wakulima. Badala yake imeiachia Bodi ya Korosho kutumia nguvu kuwalazimisha wakulima wauze hivyo hivyo, hii haikubaliki.”

Kiongozi amesisitiza kuwa, “Serikali haijajielekeza kushughulikia changamoto ya bei na namna ya kuwasaidia wakulima hao kwa sababu inafaidika kupitia utitiri wa kodi na ushuru walizoweka zinazofikia shilingi 950 kwa kila kilo moja.”

Katika hatua nyingine Kiongozi wa Chama ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka, muda wa kati na kumaliza kabisa kero hizo;
“Kwanza, tunaitaka Serikali ichukue hatua za haraka kwa kupunguza ushuru, kodi na tozo hadi Shilingi 650 ili kupandisha bei na kuwanuifaisha wakulima. Pili, ni wakati sasa kuhakikisha wakulima wanaunganishwa na hifadhi ya jamii ili kuwalinda na anguko la bei za mazao, bima ya afya, kuanguka kwa uzalishaji kutokana na ukame, mikopo ya kuongeza uzalishaji na pensheni kwa wakulima wazee.” Alisema Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe

Aliendelea kuwa “Hatua nyingine, ni kuweka msisitizo wa kubangua korosho yetu, Serikali ione aibu tumekuwa tunasafirisha korosho ghafi kwa muda mrefu sana, tufufue viwanda vya korosho, tuweke vivutio vya kujengwa viwanda vipya ili tusisafirishe ajira, tusiwe watumwa wa bei kila uchao. Tuwawezeshe wakulima kupitia vyama vyao kutumia teknolojia rahisi ili kuweza kubangua korosho zao.”

Katika hatua nyingine Ndugu Zitto alisema kilio cha wakulima katika maeneo mengi ni stakabadhi ghalani na kwamba uzoefu wa miaka takribani 15 sasa tangu uanze kutumika inaonekana wazi mfumo huo umepoteza malengo na unatumika kumkandamiza mkulima badala ya kumsadia kama ilivyotarajiwa.

Wananchi wanaulalamikia na kuukataa kwa sababu za kucheleweshewa malipo yao. Kupitia mfumo huo Serikali inaanzisha tozo na ushuru mbalimbali usiozingatia maslahi ya wakulima na bila kuwashirikisha wakulima wenyewe.

"Serikali inapaswa kujua kwamba uamuzi wowote unaogusa maisha ya watu, watu wenyewe ndio wanapaswa kuamua, sio kuburuzwa kama mifugo. Hivyo, tunamtaka Waziri wa Kilimo Ndg. Hussein Bashe kushughulikia matatizo haya kwa haraka. Pili, Serikali iende kidigitali kwenye mfumo wa malipo ya mazao ya Korosho ili iwe papo kwa papo, unauza korosho zako unapata fedha yako. Mifumo ya kukopana ni ya kizamani na ya kinyonyaji." alisema.

Imetolewa na;

Janeth Joel Rithe
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma.
17 Novemba, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK