Serikali isitishe tozo
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
Tunaitaka Serikali kusitisha tozo na kuweka wazi fedha za tozo zilizokusanywa.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa takribani miezi mitatu sasa, kumekuwa na mjadala mzito nchini kwetu kuhusu maisha ya wananchi. Mjadala huu umetawaliwa na hisia nzito juu ya ugumu wa maisha unaosababishwa na mambo kadhaa ikiwemo kupanda kwa bei ya bidhaa hususani bidhaa za chakula (mchele, unga wa sembe na dona, ngano na maharagwe), kwa upande mwingine mafuta ya petroli, diseli na mafuta ya taa licha ya mwezi huu kupungua kidogo bado bei yake inawapa maumivu watanzania.
Pamoja na mijadala hii, hivi karibuni pamekuwa na kilio cha wananchi juu ya mzigo mkubwa wa makato (tozo) yaliyoanzishwa kwenye miamala ya kibenki na kuendelezwa kwa tozo kwenye mitandao ya simu. Utekelezaji wa tozo ya miamala ya fedha kupitia benki ilianza rasmi tarehe 1 Julai 2022 kufuatiwa na tangazo la Serikali kupitia Waziri wa Fedha Ndg. Mwigulu. Lameck Nchemba. Kuanzishwa kwa tozo za kibenki kumeenda kuunganisha maumivu ya wananchi yanayotokana na tozo za miamala ya simu iliyoanzishwa mwaka jana.
ACT Wazalendo tuliungana na wananchi kupinga kwa nguvu zote utitiri huu wa tozo na tuliweka wazi kuwa, tozo hizi zina athari kubwa kwa uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi wenzetu.
Pia, tulieleza kuwa tozo hizi zinakiuka utaratibu wa uanzishwa wa vyanzo vya mapato vya Serikali kwa kuwa haipanui wigo wa walipa kodi (tax base) badala yake inaweka makato mara nyingi zaidi kwenye chanzo kile kile.
Aidha, ACT Wazalendo tulieleza kuwa tozo hizi zitaenda kushusha ari na hamasa ya wananchi kutumia mifumo rasmi ya kifedha jambo ambalo linaenda kinyume na jitihada zilizofanywa huko nyuma za kuwaunganisha wananchi kwenye mifumo hii.
Vilevile, tulieleza kuwa tozo zinaenda kuwa kikwazo katika uchumi wa kidigitali na kurejesha utamaduni wa kuhifadhi fedha majumbani ambao unaweza kurejesha uvamizi na uhalifu wa kinyang’anyi.
Tumesikiliza hoja na utetezi wa Serikali kuhusu tozo ni wazi kuwa wameamua kupuuza ukweli kuwa wananchi wanaumia zaidi na haiweki bidii kutatua changamoto zinazoleta ugumu wa maisha badala yake inawaongezea ugumu.
Kubwa ya yote, utitiri huu wa kodi siyo njia ya kujenga uzalendo kwa wananchi kama Serikali inavyosema. Wala hizi siyo mbinu rafiki za kupanua wigo wa mapato ya Serikali.
Ni aibu kwamba Serikali inatumia nguvu kuwanyamazisha wananchi na kupuuza maoni ya wadau wa maendeleo kwa kutumia mbinu na kauli mbalimbali.
Ni vyema tukarejea, siku za nyuma Serikali ilikataa kushauriwa juu ya uanzishwaji wa tozo kwenye miamala ya mitandao ya simu hadi pale wananchi walipoamua kusitisha au kupunguza matumizi ya mitandao hiyo kama njia za kufanya miamala mbalimbali. Baada ya kukwama, ndipo, Serikali ilijitokeza na kusema imepunguza makato lakini hata hivyo wananchi wengi bado hawaoni kama wamepata nafuu yoyote kutokana na punguzo hilo.
ACT Wazalendo na Wadau wa Maendeleo tulitarajia Serikali ingeweza kujifunza kutokana na anguko la miamala yenye thamani ya trilioni 1.2 kwenye huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi, na anguko la makusanyo zaidi ya asilimia 74.4 kwa kuwa Serikali ilikusanya chini ya asilimia 25.6 ya malengo iliyojiwekea wakati wa bajeti.
Kutokana na mwenendo huu, ACT Wazalendo tunarudia wito kuwa Serikali isitishe utaratibu huu wa kuwatoza wananchi kwa kuwa tayari wananchi wanalipa kodi mbalimbali ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuwahudumia na kuboresha huduma zote za msingi (Elimu, Afya, Maji na Umeme).
Fedha za tozo zinaenda wapi?
Kutokana na hoja, maoni na malalamiko ya wananchi kupinga mfumo huu wa tozo, Serikali kupitia mkutano wa Waandishi wa habari uliojumuisha mawaziri wanne (4) ilijitokeza kutetea tozo kwa kusema kuwa fedha hizo ndio mkombozi wa wananchi kwa kuwa zinajenga vituo vya afya, inajenga shule na madarasa, inajenga miundombinu ya barabara. Kauli na utetezi wa namna hii umeacha maswali mengi kwa wadau mbalimbali.
Mwaka 2021, Serikali ilitueleza kwamba fedha za mkopo wa UVIKO-19, zilitumika kujenga madarasa, shule mpya, vituo vya afya na kuimarisha miundombinu.
Serikali inaacha maswali mengi inapojitokeza tena na kutueleza kwamba fedha za tozo za miamala ndio zinatumika kwa malengo yaleyale kama ya mkopo wa UVIKO-19.
Licha ya sisi ACT Wazalendo tangu hapo awali kupinga utitiri huu wa tozo zinazoongeza mzigo kwa wananchi, tunaitaka Serikali iweke wazi makusanyo ya fedha zote zinazotokana na miamala ya simu na benki. Pia, iweke wazi matumizi ya fedha hizo ili kuondoa mkanganyiko uliopo wa matumizi mahususi ya fedha zilizokusanywa kupitia tozo za miamala ya kieletroniki na fedha za mkopo wa UVIKO-19 uliochukuliwa na Serikali kutoka shirika la fedha duniani (IMF).
Aidha, tunamshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum wa mapato yaliyokusanywa na matumizi ya fedha zote zilizopatikana kutokana na tozo za miamala za simu. Ukaguzi huu ni muhimu sana kwani kuna mkanganyiko kuhusu matumizi ya fedha zilizopaswa kukusanywa kupitia miamala ya simu na fedha za Mkopo wa Serikali wa kuimarisha uchumi kutokana athari za Ugonjwa wa Uviko-19 kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Mwisho, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iache kupuuza vilio vya wananchi nchini kote kwa visingizo vyovyote. Athari zitakazotokana na kulazimisha utekelezaji wa mfumo wa tozo ni kubwa kuliko malengo ya kifedha yanayotarajiwa kuvunwa na Serikali. Serikali iwafute machozi wananchi kwa kusitisha kabisa tozo hizi na pengo lake lifidiwe kwenye vyanzo vingine ambavyo havitaleta athari.
Imetolewa na:
Ndugu Emmanuel L. Mvula
[email protected]
Twitter: @Immamvula
Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi
ACT Wazalendo
12 Septemba, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter