Serikali iwajibike kudhibiti mfumko wa bei bidhaa muhimu za mahitaji ya Wananchi

ACT kuishauri Serikali mbinu za kukabiliana na kupanda bei za bidhaa nchini:
Serikali itoe unafuu wa kodi, ibane matumizi yake na kuwezesha uzalishaji wa ndani ili kudhibiti kupanda kwa bei za bidhaa nchini.

Ndugu Waandishi Wa Habari,
Kumekuwa na mwenendo wa kupanda kwa bei za bidhaa nchini Tanzania kusiko kwa kawaida ndani ya Miezi sita (6) mfululizo kati ya Septemba 2021 mpaka Machi 2022.
Bidhaa zilizo panda bei ni zile zinazotokana na mazao ya chakula na vinywaji, na bidhaa za viwandani ambazo siyo chakula. Kwa taarifa hizi, ni sahihi na kweli bidhaa zimepanda bei nchi nzima.
Chama cha ACT Wazalendo kimethibitisha upandaji wa bei katika mikoa kadhaa ikiwemo, Mwanza, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Iringa, Mbeya, Lindi, Tabora, Ruvuma na Dar es Salaam. Taarifa za kitafiti tulizokusanywa katika mikoa tajwa inaonyesha ongezeko la bei ya bidhaa za mazao ya chakula kwa wastani ufuatao ndani ya miezi sita:
1. Unga wa Ngano kutoka Shilingi 1,200 mpaka shilingi 2,000 kwa kilo ongezeko la shilingi 800 kwa miezi sita sawa na asilimia 67
2. Mafuta ya kula kutoka shilingi 3,000 mpaka shilingi 8,500 kwa lita ambayo ni ongezeko la shilingi 5,500 sawa na ongezeko la asilimia 183.
3. Sukari kutoka Shilingi 2,500 mpaka 3,000 kwa kilo ni ongezeko la Tsh. 500 ambayo ni sawa na 20%
4. Mchele kutoka wastani wa shilingi 1,200 mpaka shilling 2,200 ambayo ni wastani ongezeko la Shilingi 1,000 sawa na asilimia 83
5. Vitunguu kutoka shilingi 90,000 mpaka shilingi 200,000 kwa gunia sawa na ongezeko la shilingi 110,000 sawa na asilimia 122
Ndugu waandishi wa habari, pamoja na bei hizi za mazao, utafiti wetu umebaini mwenendo wa bei ya mafuta ya kula, mchele na ngano upandaji wake umekuwa na athari kubwa katika kupaisha mfumuko wa bei na hivyo kufanya wananchi walio wengi kutomudu gharama za maisha.
Mbali na bidhaa za vyakula, tumeshuhudia pia kupanda kwa bidhaa zisizo za chakula kama vile vifaa vya ujenzi (mabati na saruji), pembejeo za kilimo (Mbolea) nazo upandaji wake umepaa kwa wastani wa asilimia 90 hadi 150 kwa mbolea za UREA, CAN, DAP, SA na NPK. Pia, bidhaa za matumizi ya nyumbani kama vile sabuni.
Pia, tumeshuhudia kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol, diseli na Mafuta ya taa kwa miezi sita linafanyo wastani wa ongezeko la asilimia 18 hadi 26. Katika kipindi cha hii miezi mitatu bei hizi zimekuwa zikipanda kila uchao na hivyo kuathiri sana wananchi. Taarifa za Benki Kuu ya Tanzania za kila Mwezi zinaonyesha kumekuwa na kuongezeka kwa bei ya bidhaa kuanzia nusu ya pili ya mwaka 2021 ingawa sio kwa ukubwa huu wa miezi 3 ya mwanzo ya 2022.

Ndugu Waandishi,
Kushindwa kuzalisha mahitaji yetu ya baadhi ya bidhaa muhimu za ndani ni sababu kubwa inayopelekea kama taifa, tushindwe kudhibiti upandaji wa bei za vitu mara kwa mara. Uwezo wetu wa kuzalisha bidhaa kwa matumizi yetu ya wananchi bado ni mdogo. Kwa mfano;
• Matumizi yetu ya ngano ni metriki tani milioni moja, lakini uwezo wetu wa kuzalisha ndani ya nchi ni metric tani 93,000 tu. Tunategemea kuagiza tani karibia laki 990,000.
• Mafuta ya kula matumizi yetu ni tani 570,000 lakini uwezo wetu wa ndani ni tani 205,000 kiasi kinachobaki chote tani 365,000 tunaagiza nje ya nchi ambako hatuna udhibiti wa bei.
Pili, utitiri wa kodi za serikali kwenye bidhaa zinazoingizwa nchini, zinachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la gharama za bidhaa hususan zile zinazoingizwa nchini kama vile; mafuta, mbolea na ngano. Mfano mchanganuo wa bei ya mafuta ya petrol, diseli na mafuta ya taa baada ya gharama ya usafiri, forodha na bima mpaka yanapofika bandarini kwa mwezi septemba 2021 ilikuwa shilingi 1,162 kwa petrol, dizeli Shs.1,098/ na mafuta ya taa Shs1,062/. Tozo na kodi mbalimbali zilizoongezwa na serikali pamoja na mamlaka zake ilikuwa shilingi 1,113.48 kwa petrol na kufanya bei kuwa 2,405 rejareja huku kodi na tozo za serikali ziliongeza gharama kwa asilimia 51 katika kila lita moja. Hivyo hivyo kwa diseli na mafuta ya taa ongezeko kutokana na kodi na tozi lilikuwa ni zadi ya asilimia 50.
Tatu, upandaji wa mafuta ya kula na mbolea hutokana na uholela wa serikali katika kusimamia bei za bidhaa hizo. Mfano; tunashuhudia mafuta ya kula yanapanda kila siku, jambo ambalo haliendani na utaratibu wa kawaida wa soko. Utaratibu unaotumika kuingiza mafuta nchini sio wa kila siku, hivyo hauwezi kutarajia bei kupanda kila uchao.
Mapendekezo ya ACT:
Chama cha ACT Wazalendo kinatoa mapendekezo ya muda mfupi na muda mrefu yafuatayo kwa Serikali kwa ajili ya kukabiliana na hali hii:
Kwanza, serikali ipunguze au kuondoa kodi kwenye bidhaa zote muhimu zilizoathirika na bei hususani ngano, mafuta ya kula na sukari ili kuwapa ahueni wananchi. Hii itasaidia kupunguza bei na makali ya maisha kwa wananchi. Mathalani, ushuru wa bidhaa kwa uagizaji wa mafuta ya kula ushuke mpaka 10% tu kutoka 35% ya sasa, hivyo hivyo kwa Ngano na Sukari. Kwa upande wa mafuta ya petroli Serikali isimamishe kwa muda ushuru wenye thamani ya angalau Shilingi 500 kwa lita ya Mafuta.
Tunaelewa kwamba upunguzaji au uondoaji huu wa kodi utaathiri sana ukusanyaji wa mapato kwa serikali kwa mwaka huu wa fedha hivyo tuanshauri katika pendekezo letu jingine kuwa;
Pili, ili kukabili pengo la Kodi katika pendekezo la kwanza, Serikali ibane matumizi yake kufidia kufutwa kwa kodi au punguzo la kodi katika bidhaa tajwa hapo juu. Haiwezekani Wananchi wajifunge mikanda kiuchumi kukabiliana na mfumuko wa bei huku serikali ikiendelea na matumizi kana kwamba hakuna tatizo.
Yapo maeneo ambayo serikali inaweza kupunguza na kubana matumizi kama Safari za nje za Viongozi wa Nchi na Maafisa wa Serikali, Matumizi ya Magari, Sherehe na dhifa mbalimbali, Makongamano na Semina na kupunguza urefu wa Bunge lijalo la bajeti. Pia serikali yenyewe iangalie maeneo mengine ambayo inaweza kujifunga mkanda kufidia Mapato ambayo yatapotea kwa kuondoa au kupunguza Kodi za bidhaa muhimu ili kunusuru Kasi ya upandaji wa Bei na gharama za Maisha.
Tatu, mkakati wa kuongeza uwezo wa uzalishaji kujitosheleza mahitaji yetu ya ndani. Kwa bidhaa kama ngano ambayo ina mnyororo mrefu hasa katika biashara ndogo ndogo ni muhimu tukajijengea uwezo wa kuongeza uzalishaji. Nchi yetu imejaliwa ardhi yenye rutuba yenye uwezo wa kuzalisha ngano kwa wingi. Eneo lote la nyanda za juu kusini mikoa ya Mbeya, Rukwa/Sumbawanga na Iringa. Nyanda za Juu Kaskazini maeneo ya Hanang, Babati, Karatu, Loliondo,Monduli, Loliondo na West Kilimanjaro yanafaa sana kwa uzalishaji wa Ngano.
Serikali inatakiwa kuwa na mkakati kwanza wa Soko ili wakulima wawe na soko la uhakika kuweza kulima, pili upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu (agrochemicals) na tatu kuwa na maofisa ugani ili kuweza kuzalisha kwa ubora (Quality) na uwingi (quantity). Kwa sasa wakulima hawana motisha ya soko kwani wahitaji wakubwa (Millers na Brewers) wanaagiza nje, lakini serikali ikiwa na mkakati basi hawa Watumiaji wakubwa wataingia mikataba na wakulima ili wazalishe. Tanzania Breweries imewahi kufanya hivyo huko nyuma.
Lakini pia Serikali inaweza ikaongeza uzalishaji kwa kutumia wazalishaji wadogo kwa kuiga modeli ya Bangladesh ya “Hub and Spoke” Muundo huu unasaidia kuwa na centre ya uzalishaji ambapo kuna Wataalamu, maafisa ugani na watenegeneza mipango na upande wapili kuna wazalishaji wadogo na wanavijiji. Kwa pamoja hawa wawili wanasaidiana katika kuzalisha ngano kwa wingi na ubora. Kwa sasa uzalishaji kwa ekari moja ni chini ya nusu tani (kilo 300 kwa ekari) wakati wastani ni Tani 1.5 kwa ekari 1.
Ndugu waandishi wa Habari, Kinachopendekezwa kwenye ngano ndicho hicho hicho tunapendekeza kifanyike kwenye mafuta ya kula kwa kuongeza uzalishaji wa Mawese na Alizeti. Mazao haya mawili yanauwezo mkubwa wa kukidhi mahitaji yetu ya ndani. Kinachotakiwa ni serikali kuwa na mkakati Mahususi wa kukuza uzalishaji wa Mazao haya.
Nne, Serikali irudishe na kugawa kwa wananchi mashamba yote iliyobinafsisha na ambayo hayafanyi uzalishaji ili yatumike kuzalisha. Mashamba hayo ni kama yale ya NAFCO Hanang ambayo yalibinafsishwa na sasa hayazalishi ngano kwa kiwango kinachopaswa, na mengine yameachwa kugeuka mapori. Kabla ya ubinafsishaji Mashamba haya yalikuwa yanazalisha tani 50,000 kwa mwaka kabla ya kubinfsishwa. Sasa hivi mashamba haya hayazalishi kwa kiwango na mengine yanakodishwa na Halmashauri ya wilaya kwa wananchi kama wapangaji.
Mashamba haya 7 yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 100,000 yakiwekwa katika uzalishaji kwa kutumia model tuliyopendekeza hapo juu yanaweza kuzalisha tani 150,0000 kwa mwaka.
Mashamba mengine ni lile la Sukenya Farm (12,000 ekari) huko Loliondo ambalo limebinafsishwa na badala ya kuzalisha limegeuzwa kuwa mbuga binafsi ya Wanyama. Pori (Private Concession). Mbali ya hayo kuna mashamba mengi ya iliyokuwa Kampuni ya Bia Tanzania kabla ya ubinafsishaji ambayo kwa sasa hayazalishi. Ni vema mashamba haya yakachukuliwa na serikali na kugawiwa kwa wazalishaji wadogo wadogo ili waweze kuzalisha.

HITIMISHO:
Tangu tuliposhuhudia kupanda kwa bei kuliko kawaida kwa bidhaa muhimu kwa maisha ya wananchi, serikali imekuwa inakuja na sababu za kukwepa kuwajibika. Sisi ACT Wazalendo tumeona visababu vyovyote vile haviwezi kuwa na maana ikiwa wananchi wanaendelea kuumizwa na bei hizi. Tunatumai mapendekezo haya yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kunusuru mkwamo wa Maisha ya watanzania. Pia, tunatoa rai kwa wadau wengine kuungana kuhakikisha kuwa hali ya Maisha ya watanzania walio wengi ambao wanaguswa na mfumuko huu wa bei inanawiri na kustawi.

Imeandaliwa na:
Ndugu. Emmanuel Mvula
Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi,
ACT Wazalendo.
02.04.2022

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK