Sheria kandamizi za Habari, zinaminya uhuru na haki ya kupata Habari.
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI NDG. ALLY SALEH KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.
Utangulizi:
Tukiwa tunafuatilia mwendelezo wa uwasilishaji na mijadala ya bajeti katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jana tarehe 20 Mei 2022, Ndg. Nape Moses Nnauye amewasilisha vipaumbele, taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka uliopita na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Wananchi na wadau wengine wa sekta ya Habari na mawasiliano wana kiu kubwa kusikia hotuba na vipaumbele vya wizara hii kutokana na ukweli kwamba katika zama tulizopo sekta ya Habari na mawasiliano ina mchango mkubwa sana katika Maisha ya mwananchi wa kawaida. Pia, wizara hii ndio yenye dhamana ya Usimamizi wa taasisi zinazoshughulikia masuala ya udhibiti, upatikanaji, biashara, uwezeshaji na usalama wa habari na mawasiliano. Majukumu haya yote kwa sehemu kubwa, yanategemea mpango wa bajeti ili kufanikishwa kwake.
Kutokana na umuhimu huo, Sisi ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Habari Ndg. Ally Saleh tumefuatilia hotuba ya bajeti neno kwa neno na kufanya uchambuzi ili kuona kwa kiasi gani inaweza kubeba matarajio na matamanio ya wadau na wananchi kwa ujumla wake. Katika hotuba hii, tumeonyesha hoja nane (8) kuhusu vipaumbe, utekelezaji wa bajeti na mpango wa makadirio ya mapato na matumizi kutoka kwenye hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Hoja nane (8) za ACT Wazalendo kuhusu Hotuba ya Bajeti ya wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
1. Sheria kandamizi za Habari, zinaminya uhuru na haki ya kupata Habari.
Kwa muda mrefu tasnia ya Habari imekuwa ikikabiriwa na udhibiti, lakini kiwango cha udhibiti na ubinywaji wa tasnia kwa miaka sita (6) katika awamu ya tano ya Serikali, ulikuwa wa kiwango cha juu zaidi. Uhuru wa kupata Habari ulikumbana na vikwazo vya kisheria, uhuru wa utoaji na upatikanaji wa Habari nao ulikuwa mashakani. Kwa wastani kudorora kwa ustawi na uhuru wa Habari, vyombo vya Habari, wanahabari na wananchi kulichangiwa kwa kiasi na sheria kandamizi zilizokuwepo kabla ya Serikali ya awamu ya tano na zile zilizotungwa au kufanyiwa marekebisho chini ya uongozi wa awamu ya tano. Mifano ya sheria hizo ni sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015 (Cybercrimes Act 2015), Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni (2018), Sheria ya Vyombo vya Habari (2016), Sheria ya Magazeti 1976, Sheria ya Utangazaji 1993.
Licha ya kupungua kwa matukio yanayohusiana na kinachoitwa ukiukwaji wa sheria ya makosa ya kimtandao, kufungiwa kwa vyombo vya habari, kutishiwa kwa wanahabari na kubinywa uhuru wa kupata habari. Bado hali ya uhuru wa habari haijaimarika na haitabiriki, hivyo basi mazingira ya kisheria yanapaswa kuwekwa ili kudhibiti utashi wa watawala au mtu binafsi kuamua juu ya haki ya habari, uhuru wa habari na vyombo vya habari.
Katika Ilani ya Uchaguzi ACT Wazalendo 2020 2(1) tulieleza namna ya kuhakikisha uhuru wa habari na haki ya kupata habari unavyopaswa kuzingatiwa kwa kufanya marekebisho ya sheria. “Serikali ya ACT Wazalendo, ndani ya MIEZI SITA ya kwanza itafuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya habari, na kutengeneza sheria, kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru na weledi na ukuaji wa sekta ya habari.”
2. Kutotabirika kwa vifurushi na kuongezeka kwa gharama za vifurushi vya mitandao ya simu
Ni kwa muda mrefu malalamiko ya wananchi kuhusu gharama za vifurushi na data hayajashughulikiwa kwa kukidhi matarajio ya wananchi. Mambo ambayo wananchi wamekuwa wakilalamikia ni kubadilika mara kwa mara kwa vifurushi vya data na muda wa maongezi, vifurushi vya data kuisha bila mtumiaji kufanya matumizi yoyote, kuisha kwa data tofauti na matumizi na gharama za vifurushi kuwa juu sana (kupunjwa kwa vifurushi hususani data na muda wa maongezi).
Itakumbukwa kuwa Desemba 2020, mjadala ulipamba moto kuhusu huduma za intaneti na simu nchini kwetu, jambo lililopelekea Serikali kutunga kanuni mpya mwezi Machi 2021 (Kanuni hizo zinasimamia vifurushi vya dakika za kupiga miongoni mwa mitandao ya nchini, bando ya intaneti na meseji), Hatimaye, kupelekea makampuni ya simu nchini kuja na bei mpya za vifurushi ambazo zilileta maumivu zaidi ya walivyotarajia kiasi cha kuwaongezea gharama za maisha.
Mabadiliko haya ya kikanuni hayajawasaidia wananchi kupunguziwa gharama za vifurushi wala kudhibiti uwezekano wa makampuni kubadilisha vifurushi mara kwa mara kwa kadri wapendavyo. Bado changamoto za vifurushi kuisha bila matumizi inajitokeza mara kwa mara kwa wateja, kuongezeka kwa gharama za vifurushi kunakotokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya vifurushi.
Katika hotuba ya bajeti ya Serikali na mpango wa utekelezaji wa vipaumbele vyake, haijazingatia kushughulikia kusimamia kushusha gharama za vifurushi hususani upatikanaji wa data.
ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kuhakikisha inatoa huduma ya data bure maeneo yote ya umma kama vile hospitali, shuleni, vyuoni maofisini na maeneo ya masoko ili kushusha gharama za matumizi. Pia, Serikali isimamie kwa umakini mkubwa haki ya kutochanganyiwa muda wa maongezi na vifurushi, vilevile namna bora ya kupunguza zaidi gharama za vifurushi na viwe vyenye kutabirika.
3. Maeneo mengi nchini yanakosa mawasiliano na mtandao wa simu za mkononi.
Wakati Serikali ikipiga mbiu ya kuhakikisha inaleta mageuzi ya kidigitali, tunaona kuwa kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano hususani kwa maeneo ya pembezoni ni ndogo sana. Kwa mujibu wa taarifa wizara ya mwaka 2022 ni kuwa asilimia 69 ya ardhi ya Tanzania (Geographical Coverage) imefikiwa na huduma ya mwasiliano ya simu za kiganjani ikilinganishwa na asilimia 66 mwaka 2021. Kwa maana nyingine kuwa sehemu ya wananchi kwa wastani wa asilimia 31 hawapati huduma ya mtandao wa simu. Aidha, takwimu zinaonyesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu umeweza kufika katika kata 1,180 zenye vijiji 3,616 na wakazi zaidi ya milioni 13.75 kwa maeneo ya vijijini.
Aidha, yapo maeneo mengi ya mipakani na baadhi ya Halmashauri hazipati kabisa huduma za matangazo ya Redio ya TBC au Televisheni. Kwa mujibu wa Takwimu za wizara mwaka wa fedha 2021/22 ni kuwa usikivu wa uhakika wa TBC upo katika halmashauri 107 kati ya halmashauri 164 Tanzania Bara. Hali huwa ni tofauti kwa maeneo ya mipakani mara nyingi wanasikiliza Redio za nchi jirani. Inasikitisha katika miaka sitini ya uhuru wa nchi yetu, wapo wananchi ambao wameachwa nyuma kiasi cha kutokuwa na uwezo wa kupata Habari aidha kwa simu au redio ama televisheni.
Changamoto hizi, humalizwa kwa Serikali kuamua kuwekeza kwa kutenga fungu la fedha za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano vijijini ni wa uhakika.
Tunaishauri Serikali katika mwaka huu na miaka ijayo ihakikishe mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) unatengewa fedha za kutosha ili kuimarisha mtandao wa mawasiliano nchini.
4. Usalama na ulinzi wa taarifa za kimtandao kwa watumiaji.
Katika kuendea dhana ya Tanzania ya kidigitali ni muhimu kuweka mikakati dhabiti juu ya usalama wa kimtandao kwa wananchi wanaotumia mitandao. Pamoja na kujenga miundombinu ya Teknolojia ya habari kulinda taarifa (privacy) za watumiaji.
Tunatambua zilikuwepo jitihada za kuwa na sheria ya kulinda taarifa za watumiaji ili zisiweze kuibwa kwa ajili ya makampuni mbalimbali dunia. Tunaamini kuwepo kwa sheria ya Ulinzi wa taarifa (Data Protection) ni kuhakikisha usalama na usiri wa taarifa zinazotembea katika mtandao na kuzuia udukuzi wa aina yoyote na kwa hivyo kulinda na kuimarisha utayari wa biashara kupitia kwenye mtandao kwa mfano biashara ya fedha na kuifungua nchi kilimwengu zaidi.
Tunapendekeza kuwa Sheria itizame kwa makini namna ya kubeba Teknolojia ya kisasa za kubeba, kutunza na kusafirisha data kama vile sayansi ya Blockchain ambayo ndio ufunguo mkuu wa biashara ya kutunza taarifa na kusafirisha fedha kwa usalama na kwa uhakika na hivyo kuvutia kustawi kwa eneo hilo hata Tanzania ikikusudia kuingia biashara za eneo hilo.
Aidha, tunapendekeza kuwa Serikali ifanye tathmini na uchambuzi mara kwa mara wa vihatarishi vya usalama katika mtandao na mifumo ya kompyuta kwa lengo la kubaini mapungufu yaliyopo dhidi ya mashambulio ya mtandao (cyber-attacks).
@5. Uhuru wa vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari.
Ingawa, mageuzi makubwa katika sekta ya habari, uchagizwa au kusukumwa na uvumbuzi, kuboreshwa kwa miundombinu ya habari ikiwemo vyombo vya Habari, na teknolojia ya Habari. Nafasi ya Waandishi wa habari na vyombo vyenyewe vya habari ni muhimu sana ili kupata ubora wa habari (maudhui).
Kwa miaka mingi sana, Waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira magumu yanayotokana na kujidhibiti au kudhibitiwa katika utafutaji na utoaji wa habari hususani zinazogusa tabaka tawala (watawala wa kiuchumi na kisiasa). Kudhibitiwa na kujidhibiti kunapelekea vitisho na kupunguza uhuru wao kwa ujamla.
Ushahidi wa miaka sita (6) ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano, tumeona namna kukithiri kwa kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini kunavyoweza kuondosha weledi, uhuru na kujiamini kwa wanahabari. Tulishuhudia kufungwa kwa vyombo vya habari vilivyoonekana kuripoti au kutoa taarifa inayoenda kinyume na watawala, kupotea kwa Waandishi wa habari.
Wanahabari walionusurika waliamua kujidhibiti na kujichuja, vyombo vilivyosalimika viliamua kujisalimisha kwa kutoa taarifa za kusifa na kuabudu upande wa wenye nguvu. Ni wakati sasa wa kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unashamiri.
Ni wakati wa kuweka mifumo ya kuwezesha uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari usipokwe au usiamuliwe kwa utashi wa mtu mmoja au watu wachache.
6. Kasi ndogo ya Mradi wa vifaa vya TEHAMA na kuunganisha shule na mtandao wa intaneti
Katika bajeti ya mwaka 2021/22 Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilisema itaenda kutekeleza mradi wa kuunganisha mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule za umma 151. Kwa kila shule ni kompyuta 5 na printa 1. Na wamefanikiwa kuziunganisha na intaneti shule 100. Katika mwaka huu Serikali imesema itatekeleza Mradi kwenye shule 150, kwa kutumia Takwimu hizi na Mwenendo huu wa miaka takribani tatu. Nidhahiri kuwa itachukua miaka 30 ili kuweza kuziunganisha shule za sekondari 4700 na shule za msingi zipatazo 17,000.
Ni rai yetu kuwa Serikali isifanye jambo hii kama ni hisani kwa wanafunzi badala yake ichukuliwe kuwa tehama katika shule zetu ni nyenzo muhimu katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji.
7. Wizi wa simu, utapeli wa kimtandao na simu za kilaghai ndani nchi.
Kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuhusu uwajibikaji mdogo wa Serikali katika kushughulikia matukio yanayoripotiwa kuhusu wizi wa simu, utapeli wa kimtandao, na arafa za kilaghai. Pamoja na Serikali katika bajeti za kila mwaka ikiomba kutengewa fedha kwa ajili ya kuimarisha Mfumo utakaowezesha kuzuia matumizi ya simu zilizoripotiwa kuibiwa, kupotea, kufanya ulaghai au kuharibika pamoja na kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango.
Serikali inataja Takwimu kuwa kuna jum¬la ya simu 943,554 zilizizoibiwa pamoja na zikiwemo sisizo na viwango na zenye namba tambulishi zilizonakiliwa (Duplicate International Mo¬bile Equipment Identity - Duplicate IMEIs) zimebainika na ku¬fungiwa. Lakini uhalisia ni kuwa wananchi wengi wanakutwa na matatizo ya kimtandao lakini jeshi la polisi linashindwa kutumia mifumo kwa haraka kunusuru dhuluma na upotevu badala yake inataka kuongeza maumivu kwa wananchi kwa kuwataka walipia gharama za kufuatilia.
8. Kukosekana kwa bodi za wakurugenzi kwa taasisi nne (4) za wizara.
Bodi ya wakurugenzi ni chombo kinachowajibika kufanya maamuzi yanayotoa mwelekeo wa shirika kwa maslahi ya umma. Bodi za wakurugenzi ni mamlaka za usimamizi wa mashirika ya umma ambazo kazi yake ni kuhakikisha utendaji wa taasisi unakuwa wa ufanisi na tija kwa maslahi ya umma. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG amebaini mashirika manne (4) ya umma yaliyopo chini ya wizara ya Habari, mawasiliano na teknolojia ya habari. Mashirika hayo ni Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Shirika la Posta, Mamlaka ya udhibiti wa mawasiliano (TCRA) na TUME ya TEHAMA.
Shirika la utangazaji (TBC) hakuna bodi ya wakurugenzi tangu oktoba 2019, wakati huo Shirika la Posta hakuna bodi tangu Mei, 2021, Mamlaka ya udhibiti wa mawasiliano (TCRA) hakuna bodi tangu Novemba 2021 na TUME ya TEHAMA hakuna bodi tangu Machi 2019.
Ni Dhahiri kutokuwepo kwa bodi za wakuregenzi za mashirika haya, yameathiri kwa kiasi kikubwa sana ufanisi na utendaji wa majukumu ya mashirika.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuondoa mfumo wa uteuzi wa bodi za mashirika kwa Rais uende kwa Waziri wenye dhamana.
Hitimisho.
Katika kuelekea kwenye mabadiliko makubwa ya kidigitali mchango wa sekta ya habari ni mkubwa sana. Kwa hiyo, ipo haja kwa Serikali kuwekeza vya kutosha ili kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inakuwa vizuri ili kuboresha na kuimarisha uchumi wetu. Pia, sekta ya habari katika muktadha wa kitanzania inakabiliwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti wa kidola. Sheria, kanuni na taratibu nyingi zilizopo tumerithi maudhui ya kikoloni katika kuitazama sekta ya habari na uhusiano wake na dola. Kwa hiyo, sura na sifa za dola na silka za mtawala wa wakati huo ndio zinaakisi sheria na Mwenendo wa vyombo vya habari na tasnia habari kwa ujumla. Uelekeo wa namna hii, hauleti afya katika jamii ya watu huru na sekta yenyewe. Hivyo basi, sasa ni wakati sahihi wa kufanya mabadiliko ya mifumo ya sheria na kanuni zote zenye sura na sifa ya ukandamizaji (kikaburu na kikoloni).
Ally Saleh
Msemaji wa Sekta ya Mawasiliano, Habari, Teknolojia ya habari na uchukuzi.
ACT Wazalendo
[email protected]
21 Mei, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter