Siku 100 za Kuwaweka Wazanzibari pamoja:

Na: Zitto Kabwe, 

Kongozi wa Chama cha ACT Wazalendo.

Tarehe 7 Disemba 2020 Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi alimwapisha Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na hivyo Kutekeleza Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2010 Kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hivyo, kama Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo mtazamo wangu katika Makala Hii fupi ni mtazamo wa mwanachama wa chama ambacho ni mshirika mdogo ( junior partner ) katika Serikali.

Kwanza, Chama cha ACT Wazalendo kinampongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya 8 ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri na kubwa ambayo ameifanya katika kipindi cha siku 100 tangu kuapishwa kwake.

Ni vigumu kupima kazi za Rais katika siku 100 Kwa sababu mara nyingi katika nchi zetu ambazo hazina muda wa mpito siku hizo hutumika kuunda Serikali. Hata hivyo baadhi ya matendo, maneno na haiba hutoa sura ya mwelekeo wa Serikali mpya. Baraza la Wawakilishi Ndio kwanza linakutana na hakuna hata muswada Mmoja wa sheria ambao Baraza limepelekewa na Serikali mpya. Nitatumia maneno, matendo na ‘gestures’ katika kutazama siku hizi 100.

Katika siku 100 za mwanzo wa awamu yake, Mheshimiwa Rais Mwinyi ameonyesha uongozi na utayari wa kushughulikia changamoto kubwa za Zanzibar za mpasuko wa siasa, umoja wa kitaifa, rushwa na ubadhirifu, changamoto katika utoaji wa huduma za jamii, kukwamua changamoto zinazoikabili sekta binafsi, kukuza uchumi na kutatua tatizo la ajira.

Tunapongeza hatua za awali alizozioenyesha za kutatua mpasuko wa siasa Zanzibar katika kauli zake na vitendo. Dhamira hiyo imejionyesha katika nia na utayari wake wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kumteua Mheshimiwa Maalim Seif Sharrif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kuteua wawakilishi wawili kutoka chama cha ACT, kuanza kuachiwa kwa watuhumiwa wa kisiasa waliokuwa magerezani na teuzi zake Serikalini ambazo zimeepuka kasumba iliyotawala huko nyuma ya kubagua sehemu ya Wazanzibari.

Uteuzi wa Vijana wengi, wa kike na wa kiume ni ishara nzuri sana kuhusu Zanzibar inayokuja kwani hawa Vijana waliopewa majukumu mazito ndio viongozi wajao. Wizara nyeti kama Utalii ( 82% ya Mapato ya fedha za kigeni ya Zanzibar na 31% ya Pato la Taifa la Zanzibar) kupewa kijana mwanamke ni hatua kubwa Kwa Wanawake wa Zanzibar. Wizara ya Vikosi vya SMZ, Fedha na Uwekezaji kuwa chini ya Vijana pia ni jambo jema sana. Hata nafasi zilizobaki za Wizara zinazotokana SUK kutakuwa na vijana wazuri.

Pili, Tumetiwa moyo na hatua ambazo Rais Mwinyi amechukua za kukemea na pale ilipobidi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi na watumishi wa umma. Hali hii imerudisha kiasi nidhamu Serikalini. Hali kadhalika hatua ya kutembelea maeneo zinapotolewa huduma za afya, wepesi wake wa kukutana na wadau wa sekta ikiwemo sekta binafsi na utayari wake wa kutatua kero zao. Tumefarijika pia kuwa naye anakerwa na kutokuwapo kwa ufanisi wa kuridhisha katika maeneo ya bandari na ukusanyaji mapato.
Uamuzi wa haraka wa kuchunguza kuanguka kwa jengo la Maajabu na kuwekwa wazi kwa muhtasari wa Taarifa ya uchunguzi kulikofanywa na Waziri wa Utalii ni ishara ya mwenendo mpya wa Uwajibikaji katika kushughulikia mambo ya Umma.

Tatu, Pamoja na hatua hizo za kutia moyo, ninaamini kazi iliyo mbele ya Serikali ya Awamu ya 8 ambayo sisi ni sehemu yake, bado ni kubwa. Tunaamini kuwa hatua hizi za awali na nia njema zitaweza kuleta matunda yaliyotarajiwa ikiwa zitaendana na mabadiliko ya mifumo na ujenzi wa taasisi imara zitakazoendeshwa kiuweledi na kufuata misingi ya uwajibikaji. Ni matarajio ya wengi kuwa katika muda uliosalia, Rais Mwinyi kwa kushauriana na Makamu wake wa Kwanza, Mheshimiwa Maalim Seif watajielekeza katika mageuzi ya utumishi wa umma, mageuzi ya vyombo vya ulinzi na kuundwa kwa Tume ya Ukweli na Upatanisho (Truth and Reconciliation Commission) kuutafutia majawabu ya kudumu mpasuko wa siasa wa Zanzibar ambao umekuwa ukijidhihirisha kabla, wakati na baada ya chaguzi kuu. Matukio hayo yamedhihirisha kuwa, Katiba ya Zanzibar ya 1984 Toleo la 2010, pamoja na kufanikiwa kutupa majawabu ya kisheria, haijatupatia majawabu ya kisiasa.

Juhudi za Mabadiliko ya kiuchumi Zanzibar na mikataba mbalimbali mbalimbali inayosainiwa imeamsha ari ya kufufua uchumi wa Zanzibar. Bandari, Uwanja wa ndege na nishati ya Umeme ni maeneo muhimu sana kwa maendeleo ya Zanzibar. Theluthi mbili ya uchumi wa Zanzibar Kwa kipimo cha Pato la Taifa ni Utalii na Biashara. Utalii sura yake ni Uwanja wa Ndege na Biashara sura yake ni Bandari. Tumeona Rais akianza kazi ya Bandari ndani ya siku 100 na hatua za kurekebisha menejimenti ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.

Hata hivyo, Zanzibar inahitaji Uhuru katika masuala ya sera za Mitaji ( capital market policies ) ili Uwekezaji wa Bandari uwe na Faida kubwa kwa Zanzibar na kwa Tanzania. Ni vema SUK ifanye kazi kubwa kushawishi Serikali ya Muungano kuruhusu Benki Kuu ya Tanzania Ofisi ya Zanzibar kuwa na ‘autonomy’ katika Sera za Uwekezaji na mabenki. Mfano mzuri wa kutazama ni mahusiano ya China na Hongkong. Rais Mwinyi na Makamo wake Maalim Seif na Serikali nzima wana wajibu wa kuwezesha hili kutokea.

Ninamtia moyo Rais Mwinyi kuendeleza kazi nzuri ambayo amekwishaianza na tunaahidi kuendelea kumpatia ushirikiano wetu wote katika kuiletea Maendeleo Zanzibar. Tunawashajiisha wanachama wa ACT na Wazanzibari wote kwa ujumla kuendelea kuunga mkono Serikali yetu na viongozi wetu. Zanzibar itajengwa na sisi wote.

Siku 100 za mwanzo zilikuwa siku za kuwaweka Wazanzibari pamoja. Siku, Wiki, Miezi na Miaka iliyobaki ni ya kuwafanya Wazanzibari kufaidu matunda ya mapinduzi badala ya kuendeleza masimulizi ya mapinduzi.

Kila la kheri Rais Mwinyi na Serikali nzima ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK