Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari: Sheria kandamizi zifutwe

Miaka 30 ya Maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya habari; Vikwazo na wajibu wa kiukombozi wa vyombo vya habari.

Utangulizi
Leo tarehe 3 Mei 2023 ni siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani katika siku hii hutumika kutathmini uhuru wa vyombo vya habari duniani kote, kutetea, kulinda na kuvipigania vyombo vya habari dhidi ya mashambulizi ya uhuru wao na kutambua, kuenzi kazi zilizofanywa na wanahabari waliopoteza maisha katika kutekeleza majukumu yao.

Siku hii inabaki kuwa muhimu sana kutokana na ukweli kuwa ili umma uweze kufurahia haki na uhuru wa kupata habari na kujieleza bila hofu inahitajika kuwe na uhuru huo wa vyombo vya habari. Wakati tunaadhimisha siku hii, hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini bado hautabiriki. Vikwazo vinavyozuia uhuru wa vyombo vya habari ni kama vifuatavyo;

Mosi, athari za siasa za ukiritimba wa chama kimoja. Nchi yetu imejengwa katika utamaduni kandamizi, uliotokana na ukiritimba wa muda mrefu wa mfumo wa chama kimoja (uhodhi wa siasa). Uhodhi wa siasa huanzia na kutoruhusu shughuli za kisiasa au kundi jingine linaloweza kuratibu masuala yanayohusu maslahi ya watu nje ya Chama dola yaani vyama vya ushirika, vyama vya wanafunzi, vikundi vya vijana na wanawake, vilabu vya mipira na michezo mbalimbali na vyama vya wafanyakazi vyote hupondokea kwenye mwamvuli wa chama dola.

Utamaduni huu kwa muda mrefu ulizuia uhuru wa kutoa maoni, fikra na mawazo tofauti. Watu waliokuwa wanakosoa, walipitia wakati mgumu au kukosa jukwaa la kihabari la kueleza mawazo yao. Ikiwa maslahi ya makundi mbalimbali nje ya chama dola hayawezi kuruhusiwa basi mitazamo yoyote ya uhuru na haki ya kujieleza kwa maslahi hayo hayawezi kuruhusiwa vilevile. Hivyo vyombo mbalimbali vya habari; magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni (online media) hayawezi kuwa huru. Hali hii haijabadilika sana hadi leo tunapoadhimisha siku hii.

Pili, mfumo wa sheria kandamizi kwa vyombo vya habari. Tangu uhuru hadi sasa Tanzania imekuwa ikitunga sheria za habari zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na zinazokazia ukali wa sheria zilizopo ambazo ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi.

Sheria hizo ni kama vile Sheria ya huduma ya habari 2016, Sheria ya Magazeti ya 1976, Sheria ya Usalama wa Taifa 1977, Sheria ya kupata habari 2016, Sheria ya Mawasiliano ya kieletroniki na Posta 2010, Kanuni za maudhui ya mtandaoni 2018, Sheria za makosa ya kimtandao 2015 (Kanuni za jumla za 2016), na Sheria ya Takwimu 2015 (pamoja na marekebisho yaliyofanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali) (Na. 3), 2018.

Kwa kuangazia hoja hizi mbili ni wazi kuwa utamaduni kandamizi wa nchi umezaa sheria zinazojinaisha uandishi wa habari na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari. Hayo yote ndiyo tumeshuhudia kuwepo kwa vitendo vya vitisho, mashambulizi, vifungo, kufungiwa kwa vyombo vya habari, kufutwa kwa baadhi ya magazeti alimradi kuvifanya visifanye majukumu yao kwa uhuru.

Kutokana na hali hii ACT Wazalendo katika kuadhimisha miaka 30 ya uhuru wa vyombo vya habari tunaendelea kupigania mazingira mazuri ya uhuru huo. Kwa kutaka hatua zifutazo yafuatayo;

1. Tunaitaka Serikali kufuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya Habari na kutengeneza sheria mpya kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru na weledi na ukuaji wa sekta ya Habari.

2. Tunatoa wito kwa Serikali kusimamia uanzishwaji wa Baraza huru la habari nchini ili kulinda na kutetea haki na masilahi ya wanahabari

3. Kuanzishwa mchakato wa mabadiliko ya Sera ya utangazaji na uandishi ili kulinda na kukuza uchumi na mazingira ya wanahabari wote

4. Tunaitaka Serikali iratibu soko la mitandao ili kupunguza gharama za vifurushi vya intaneti kwa ajili ya kuchochea Maendeleo ya Teknolojia ya habari nchini.

Mwisho, mwenendo wa sasa wa kisiasa duniani kote unaashiria kusinyaa kwa demokrasia, hasa uhuru wa habari na haki kuwasiliana. Waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na asasi za kiraia ni muhimu kutumia fursa hii kuhakikisha sheria kandamizi zote zinaondoshwa ili kuwasaidia kutekeleza majukumu yao.

Mwl. Philbert Macheyeki
Twiiter: @PMacheyeki
Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi
ACT Wazalendo
03 Mei, 2023

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK