SIKU YA WANAWAKE DUNIANI TUBORESHE MAISHA YAO

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI TUBORESHE MAISHA YAO

Leo ni siku ya kimataifa ya Wanawake duniani. Ni kumbukumbu inayoadhimishwa tarehe 8 Machi kila mwaka kutambua jitihada zilizofanywa na wanawake wavujajasho katika kupigania uwakilishi sawa wa kisiasa, usawa wa kichumi na kupinga udhalimu dhidi ya utu hususani dhidi ya wanawake.

Siku ya wanawake inabaki kuwa kipimo muhimu cha kutathmini mshikamano wa kimataifa miongoni mwa wanawake katika kuhakikisha jamii inatoa uelewa na inaendeshwa kwa usawa, utu na kupinga udhalimu. Siku hii pia huongeza chachu katika harakati za mapambano katika usawa wa kijinsia kwa wanawake na wanaume.

Kwa takribani karne mbili watu duniani kote wamekuwa wakiadhimisha siku hii, kwa namna mbalimbali hata kuwasahaulisha wanawake kuwa bado mapambano hayakamilika. Katika salam zake kwa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Anthonio Getterez amesema kubadilisha uwiano wa mamlaka ni muhimu si tu kama suala la haki za binadamu, bali pia ni kwa ajili ya Maendeleo ya kibinafsi, Kiafya na kiustawi.

Katika miaka 20 iliyopita Wanawake wameteseka zaidi kutokana na ukweli wa mfumo kandamizi wa kisiasa na kiuchumi. Hali mbaya ya maisha na ukandamizaji kwa wanawake huwa ni mara tatu, akiwa nyumbani, kazini na katika jamii. ACT Wazalendo inatambua kwamba ingawa mfumo dume na ubaguzi wa kijinsia umeenea katika jamii yetu, ni wanawake walalahoi ambao wanateseka zaidi kutokana na unyanyasaji wa kijinsia.

Hadi sasa, hatua za kushughulikia unyanyasaji dhidi ya wanawake zimekuwa za juu juu, za nusunusu na zikizingatia uelewa usio sahihi wa sababu kuu zinazozaa hali isyo sawa kwa wanawake.

Kutokana na ukweli huu katika siku hii ya Wanawake Duniani Sisi ACT Wazalendo tunaona tuitazame kwa jinsi gani tunaweza kufikia ukumbozi wa kweli wa wanawake katika jamii ya Kitanzania kutoka kwenye machungu mbalimbali katika kujitafutia mahitaji yao na majukumu ya msingi wanayobeba katika jamii zao ambazo mara nyingi zimekosa suluhisho. Hadi sasa wanawake hapa nchini wameendelea kukumbwa na ukosefu wa haki zao za msingi na usawa kazini, manyanyaso ya majumbani mwao na kwenye maisha yao ya kwaida kwa ujumla.

Mathalani katika baadhi ya Mikoa hapa nchini wanawake Wazee bado wameendelea kuripotiwa kuuawa kwa imani za kishirikina huku wanawake vijana wakiishia kufanyiwa vitendo vya kikatili na wengine kuuawa na weza au wapenzi wao kutokana na wivu wa mapenzi.

Aidha bado huduma za afya vijijini na zaidi maeneo ya pembezoni zimekuwa ni shida ya muda mrefu baadhi ya zahanati za vijijini zinakuwa na muhudumu mmoja tu, hakuna vifaa tiba, dawa ni masula amabayo yanarudisha nyuma maendeleo ya mwanamke.
Upatikanaji wa maji safi na salama maeneo ya mijini na vijijini bado ni changamoto kubwa nchini licha ya kuwapo juhudi za serikali kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo.

Kisiasa, bado hali ya siasa inawarudisha nyuma wanwake katika kuwania nafasi za uongozi na uwaklishi kutokana na kutokuwa na mazingira mazuri ya kisiasa kwa takribani miaka sita.

Ili kutimiza na kufikia malengo ya mapambano ya wanawake na kutambua mchango wao ACT Wazalendo tumekuwa tusisitiza kuchukua hatua stahiki na zinazopimika wakati wote. Hivyobasi, ni muhimu tuchukue jitihada za makusudi katika maeneo yafuatayo;

1. Kuhakikisha kunakuwa na fursa sawa za uwakilishi na uongozi katika vyombo vya uamuzi hususani kwa nafasi za kuteuliwa.

2. Kuimarisha na kuhakikisha hupatikanaji wa huduma za Kijamii kwa wote hususani elimu, afya, umeme na maji safi na salama hasa kwa maeneo ya vijijini.

3. Serikali iweka mifumo thabiti kuhakikisha angalau asilimia thelathini (30%) ya manunuzi yote ya ndani yatakayofanywa na Serikali kuu na Serikali za mitaa, yatatoka kwenye biashara zinazozomilikiwa na ushirkika wa wafanyabiashara wadogo wadogo wanawake.

4. Kusimamia hupatikanaji wa TUME HURU ya Uchaguzi ili kuhakikisha wanawake wanapata ujasiri wa kushiriki siasa.

5. Kukomesha ajira za kingono na unyanyasaji wa kijinsia maeneo ya kazi.

6. Kutambua biashara ndogondogo na kuziwekea utaratibu wezeshi wa kuendesha biashara hizo kwa kuondoa msururu wa kodi ili kutoa nafuu ya kodi.

7. Pia kuwaunganisha Wanawake na watanzania wengine katika mfumo wa hifadhi ya jamii, ili kuwalinda wanapopata na majanga, uzee na maradhi.

Mwisho niwapongeze wanawake wote nchini kwa Siku hii muhimu, nawasihi tuendelee kufanyakazi kwa bidii ili tuweze kujikwamua kimaendeleo, kama ilivyo kauli mbiu yetu ya mwaka huu ambayo inasema “Usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu”.

Imetolewa na;

Janeth Joel Rithe,
Msemaji wa Kiseka wa Ustawi wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto
(ACT Wazalendo)

Machi 8, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK