Suala la maendeleo ya viwanda limebaki katika hotuba na maneno matupu ya viongozi, ni hatari.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA ACT WAZALENDO NDG. HALIMA NABALANG’ANYA KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.

Utangulizi:
Siku ya Ijumaa ya tarehe 6 Mei 2022, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb.), aliwasilisha Bungeni mpango wa Wizara na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na maeneo ya kipaumbele ambayo wizara itajielekeza nayo kwa mwaka huu. Sisi, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Viwanda na Biashara tumeisikiliza, kuisoma hotuba hiyo kwa lengo la kuichambua na kuimulika ili kuona kwa kiasi gani ina akisi matarajio na matamanio ya wananchi. Katika kufanya wajibu wetu, hotuba hii ya Msemaji wa Sekta ya Viwanda na Biashara wa ACT Wazalendo imeangazia maeneo makuu saba (7) kuhusu hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23.

1. Mwenendo hafifu wa mchango wa viwanda katika pato la taifa na kutengeneza ajira:
Mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa letu bado hauridhishi, tofauti na matarajio ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (5) - National five years development plan 2015/16 – 2020/21. Mpango ulibainisha kwamba, ili nchi yetu ifanikiwe kufika uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025, ni sharti sekta ya uzalishaji (manufacturing) ichangie wastani walau wa 40% katika pato la taifa ifikapo 2025.
Katika kufuatilia utekelezaji wa bajeti na mwenendo wa mchango wa sekta ya viwanda kwa miaka mitatu; (3) yaani 2019, 2020 na 2021 taarifa za wizara zinaonyesha kuwa mchango viwanda katika uchumi unaporomoka kila mwaka. Kwa mwaka 2019/20 mchango wa sekta ya viwanda kwenye pato la taifa ulikuwa 8.5% 2020/21 ulikuwa 8.4% na mwaka 2021/22 ulikuwa ni 8.0%.
Pamoja na hayo, taarifa ya ofisi ya taifa ya takwimu (NBS, 2021) inaonyesha mchango wa sekta ya viwanda kwenye ajira ni 8.0% pekee. Kwa mujibu wa Waziri wa uwekezaji, viwanda na biashara katika hotuba ya bajeti ameeleza ajira zinazotokana na viwanda ni takribani 345,615 kwa mwaka 2021 ukilinganisha ajira 370,485 zilizozalishwa mwaka 2020. Ndani ya mwaka mmoja, ajira 24,870 zimepotea.
Kwa kutazama mwelekeo huu wa sekta ya viwanda ni wazi mpango wa taifa unapotea, dira ya viwanda kuwa injini ya kusukuma maendeleo na ustawi wa wananchi inafifia. Suala la maendeleo ya viwanda linabaki katika hotuba na maneno matupu ya viongozi, ni hatari.
2. Ukosefu wa mahusiano na kufungamana kwa sekta ya viwanda na uzalishaji wa malighafi - kilimo, uvuvi na madini:
Katika historia ya nchi yetu na nchi nyingine nyingi Afrika hususani katika dunia ya tatu ajenda ya viwanda kwa muda mrefu imekuwa ikijadiliwa kwa namna tofauti tofauti. Katika kufuatilia hotuba ya bajeti na mipango ya wizara kwa mwaka huu, ina ukosefu wa mahusiano na uwiano mdogo sana wa malengo ya ujenzi/ uwekezaji wa viwanda na sekta ya uzalishaji wa malighafi hususani kilimo.
Hakuna viwanda vya kutosha kujikita katika usindikaji wa mazao ya kilimo (hususani mazao mkakati) na uzalishaji wa bidhaa muhimu kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini. Shabaha ya sasa ya uwekezaji na uendelezaji wa viwanda sio katika kujenga uwezo wetu wa nchi kujinasua katika hali ya utegemezi.
Takwimu za viwanda kwa mujibu wa wizara ni kuwa tuna viwanda vidogo sana 62,400 sawa na 77.07%, viwanda vidogo ni 17,267 navyo vinachukua 21.33% na viwanda vya kati vipo 684 sawa na 0.84% na viwanda vikubwa vipo 618 sawa na 0.76%. Licha ya takwimu hizi bado mazao mengi yanapotea shambani, uhakika wa masoko ya wakulima wetu bado ni mdogo sana. Mazao kama ya kahawa, pamba, chai, ufuta, korosho na chikichi ndio mazao yanayoongozwa kuuzwa nje na kwenda kuwa malighafi katika viwanda vya nchi zingine.
Kwa upande mwingine sehemu kubwa ya mahitaji yetu ya bidhaa za viwandani kwa ajili ya walaji wa ndani huagizwa kutoka nje, bidhaa kama vile mafuta ya kula, ngano, nguo, viatu na dawa. Wakati huo huo, tunapoteza fedha nyingi kuingiza chuma nchini, saruji, nondo na bati.
Katika bajeti ya Serikali mwaka huu, fedha zilizotengwa kuendeleza viwanda vinavyoweza kuleta uhusiano na uwiano na sekta za uzalishaji bado ni kidogo, hivyo haiwezi kukidhi shabaha ya kufungamanisha uzalishaji na maendeleo ya viwanda.
Katika Ilani ya ACT Wazalendo 2020 tulisema “Tutafungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda, kwa kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinapata zaidi ya asilimia 80 ya mahitaji yao kutoka kwa wakulima, na kwamba wakulima wanafaidi bei nzuri ya mazao yao na soko la uhakika,”
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuhakikisha inasimamia uwekezaji na ujenzi wa viwanda unaotegemea zaidi malighafi kutoka ndani. Pia, Serikali ifungamanishe uendelezaji wa viwanda na sekta ya madini hususani makaa ya mawe na chuma ya hivyo, kuharakisha utekelezaji wa Mradi Linganga na Mchuchuma.
3. Kupanda kwa bei za bidhaa muhimu nchini:
Kumekuwa na mwenendo wa kupanda kwa bei za bidhaa nchini Tanzania kusiko kwa kawaida kwa takribani miezi tisa (9) mfululizo kuanzia Mwezi Julai 2021 mpaka Mei 2022. Bidhaa zilizo panda bei ni zile zinazotokana na Mazao ya Chakula na vinywaji na zile za viwandani ambazo sio chakula.
Katika hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 waziri wa uwekezaji, viwanda na biashara amekiri kuwepo kwa janga hili na kusema kuwa bidhaa zimepanda kwa wastani wa 50% hadi 149% (japokuwa hali zipo bidhaa zimepanda kwa zaidi ya 200%). Bidhaa za chakula kama vile mchele, unga, unga wa ngano na maharage. Mafuta ya kula, vifaa vya ujenzi (bati, nondo na saruji). Pamoja na pembejeo za kilimo kama vile mbolea. Hali ya ongezeko kubwa la bidhaa limepandisha gharama za maisha kwa wananchi. Pamoja na kuonyesha mfumo wa bei wa bidhaa na kuongezeka kwa gharama za maisha, Waziri hajatoa namna bora ambavyo Serikali inashughulikia suala hili ili kutuliza maumivu na ugumu wa maisha kwa wananchi.
ACT Wazalendo inaendelea kusisitiza kuwa Serikali ipunguze ushuru wa bidhaa kwa uagizaji wa mafuta ya kula ushuke mpaka 10% tu kutoka 35% ya sasa, hivyo hivyo kwa ngano na Sukari, ili kuwanusuru wananchi.
Pili, kwa upande wa mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya taa Serikali isimamishe kwa muda tozo yenye thamani ya Shilingi 500 kwa lita ya Mafuta.

4. Mfumo mbovu wa Stakabadhi za Ghala:
Wizara ya uwekezaji, viwanda na biashara kupitia Bodi ya Leseni ya Maghala (Tanzania Warehouse Licensing Board - TWLB) inasimamia mfumo wa Stakabadhi za mazao ghalani ulioanzishwa kisheria kwa Sheria Na. 10 ya mwaka 2005 na kutekelezwa kwa kanuni za mfumo za mwaka 2006. Mfumo huu sasa unatumika katika maeneo mbalimbali nchini kwa mazao ya Korosho, Kahawa, pamba, Ufuta, tumbaku, Mpunga na Mahindi.
Uzoefu wa utekelezaji wa mfumo huu umekuwa ukiacha maumivu makubwa sana kwa wakulima wetu badala ya kuwa msaada. Serikali na vyama vya ushirika wamekuwa madalali wa mazao badala ya kuwa watafuta wateja wa bei yenye tija kwa wakulima. Mfumo huu wa masoko unawanufaiaha zaidi watumishi wa vyama vya ushirika, watumishi wa Serikali na Wafanyabiashara wanaonunuwa mazao kwa mtindo wa kangomba. Mazao yaliyoathirika zaidi na sheria hii ni korosho, ufuta, mbaazi na tumbaku.
Katika kutazama mpango wa bajeti na vipaumble vya Serikali kwa mwaka 2022/23 hatujaona mkakati wa kuboresha mfumo huo ili kuwezesha na kunufaisha wakulima na kuboresha sekta ya viwanda kupitia kuimarisha kwa kilimo chetu.
ACT Wazalendo tunapendekeza mfumo wa malipo wa stakabadhi ghalani uimarishwe uwe wa kieletroniki na uwe wa papo kwa papo.
Pia, utumike mfumo wa soko la bidhaa (commodities exchange) kwa kuwashirikisha moja kwa moja wakulima wenyewe.
5. Mazingira magumu ya wafanyabiashara wadogo na viwanda vidogo nchini.
Kwa kutazama uelekeo wa hotuba ya bajeti ya wizara, mikakati iliyowekwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara imewagusa zaidi Wafanyabiashara wa kati na Wafanyabiashara wakubwa. Mazingira ya Wafanyabiashara madogo (wamachinga, mamalishe, na wajasiriamali wengine) bado hayajawekewa mkakati wa kuondoa changamoto zao. Sekta ya biashara ndogo ina mchango mkubwa sana nchini kwenye pato la taifa wastani wa asilimia 22 na mchango wake kwenye sekta ya ajira ni wastani wa asilimia 14 ya nguvu kazi nchini zinapatikana kwenye biashara ndogo.
Hali ya sasa ya wafanyabiashara hawaonekani wakilindwa kisheria au shughuli zao kutambulika kama halali kwenye mchango wa uchumi wetu. Kwa, kifupi Wafanyabiashara wadogo hawachukuliwi kama injini ya maendeleo ya miji na majiji. Uamuzi wa kuwapanga Wafanyabiashara wadogo umetikisa uaminifu wao kwa taasisi za kifedha. Matukio kuungua moto kwa Wafanyabiashara wadogo yamesababisha hasara kubwa sana kwa Wafanyabiashara.
Tafiti nyingi, zinaonyesha uhusiano uliopo katika shughuli za Wafanyabiashara wadogo na ukuaji na uendelezaji wa viwanda vidogo nchini. 47% ya biashara ndogo zinahusisha bidhaa za kilimo ambazo zinaongezwa thamani.
ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Serikali kwa kuziweka pamoja wizara ya viwanda pamoja na wizara ya TAMISEMI kusikiliza na kuondoa vikwazo kwa wafanya biashara wadogo.
6. Utekelezaji wa mkataba wa Eneo Huru la Biashara kwa nchi za Afrika (Africa Continental Free Trade Area)
Katika vipaumbele vya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni kuendeleza majadilianao na utekelezaji wa mikataba wa huduma wa biashara wa eneo huru la biashara kwa nchi za Afrika. Kwa taarifa na takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa uuzaji wetu wa bidhaa ndani soko la Afrika Mashariki kutoka Tanzania umefika thamani ya trilioni 1.86. Serikali itumie fursa hiyo kuongeza masoko ya bidhaa zetu nchini. Kutokana na fursa hiyo tunaendelea kusisitiza kuwa tuimarishe majadiliano na kuwekeza nguvu kwenye mkataba huu kuliko kuingia kwenye makubaliano ya EPA.
7. Kufufua viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazoweza kukidhi mahitaji ya ndani:
Kama tulivyoonyesha huko nyuma kuwa bado uzalishaji wa viwanda vyetu nchini hauendani na mahitaji ya ndani. Hii ni kusema kuwa viwanda vyetu vinazalisha bidhaa nyingi za anasa au bidhaa kwa ajili ya kusafirisha nje. Serikali ilianzisha mamlaka ya ukanda maalum wa mauzo ya nje (EPZA). Kwa tathmini yetu kutokana taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa bado uwepo wa viwanda hivyo hatuzalishi kwa kukidhi mahitaji yetu ya ndani. Ni muhimu kwa Serikali kusimamia sekta ya viwanda kwa ajili kukidhi mahitaji ya wali wengi (goods for mass consumption).
Ni rai yetu kuwa Serikali ianze sasa na ionyeshe kwenye bajeti yake katika kufufua viwanda vya nguo, viatu na vifaa vya kilimo. ACT Wazalendo kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi 2020 tulisema kuwa “serikali ya ACT Wazalendo itawezesha ufufuaji wa viwanda vya kuchakata pamba na kuzalisha nguo (textile industries) ili kuzalisha bidhaa kama vile vitenge, vijora, madera na batiki zenye ubora wa hali ya juu”
Hitimisho:
Ni muhimu kwa Serikali kupambanua usimamizi wa mipango yake ya kibiashara katika nyanja zote zinazohusika ili kuboresha usimamizi na kutafsiri mipango na vipaumbele katika utekelezaji. Katika mpango wa bajeti kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali haijaonyesha jinsi itakavyo oanisha sekta ya viwanda, biashara na sekta mtambuka. Ni rai yetu kama ACT Wazalendo, kwamba Wizara itabeba misimamo ya chama chetu kwa uzito ili kuiwezesha sekta ya viwanda na biashara kufikia uwezo wa kutoa ajira na kuwaletea wananchi maendeleo kwa kasi inayotakiwa.

 

Imetolewa na:
Ndugu. Halima Nabalang’anya
hnabalang’[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Viwanda na Biashara - ACT Wazalendo.
09.05.2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK