August 18, 2020 5:25 PM

TAARIFA KWA UMMA

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe leo Agosti 18, 2020 amewatambulisha rasmi
viongozi wa timu ya kampeni ya kitaifa ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Katika kikao chake na waandishi wa habari katika Ofisi za chama, Magomeni Dar es Salaam , Zitto
aliwataja, Mwenyekiti wa Timu ya kampeni ya ACT –Wazalendo kuwa ni Ndugu Joran Bashange ambaye
ni Naibu Katibu Mkuu Bara pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Wakili Emmanuel Lazarus Mvula ambaye
atakuwa Meneja wa kampeni Taifa.


Pia katika mkutano huo na waandishi wa habari, Kiongozi wa chama amezungumzia matukio ya utekwaji,
kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na wagombea waliotia nia katika nafasi ya ubunge na udiwani
ndani ya chama cha ACT- Wazalendo katika Jimbo la Ruangwa mkoani LIndi.
Aliwataja wahanga wa matukio hayo kuwa ni Said Ally Nangendekwa ambaye alipigwa na kujeruhiwa
nyumbani kwake Agosti 9 2020.


Mwingine ni Joakim Ng’ombo ambaye alitekwa, kupigwa Agosti 12 na kuokotwa wilayani Mkuranga mkoani
Pwani Agosti 13 akiwa na hali mbaya ambapo awali alitibiwa katika Hospitali ya Temeke na sasa
amehamishiwa Hosptali ya Taifa ya Muhimbili baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya zaidi.


Mtu wa tatu ni Bakari Abdallah Nanyambo ambaye ni mgombea udiwani wa ACT- Wazalendo
alishambuliwa kwa mapanga na watu wasiojulikana ambapo hivi sasa anaendelea na matibabu katika Kituo
cha Afya Mbekenyera mkoani Lindi. Matukio haya yote yameripotiwa katika vituo vya polisi mkoani humo.
Kutokana na matukio hayo, kiongozi wa chama ameomba yafuatayo yazingatiwe:


1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ifuatilie kwa karibu na kutolea ufafanuzi matukio haya kama
niya kisiasa basi ikemee na kuchukua hatua.
2. Wanachama wa ACT- Wazalendo wachukue hatua za kujilinda, kulinda viongozi wao na mali za
chama
3. Chama kinawaagiza wanachama wote kufuata taratibu za kisheria wakati wote kuelekea Uchaguzi
Mkuu na pale wanapoona haki zao au haki za wengine zinavunjwa watetee na kuzuia uvunjwaji
wa haki kwa kuripoti matukio hayo mahali panapohusika.


Imetolewa na
Arodia Peter
Afisa Habari, ACT-Wazalendo

18 Agosti, 2020.

Showing 1 reaction

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK