TABORA: MAMBO 10 MUHIMU YALIYOJITOKEZA KTK ZIARA YA KUWASIKILIZA WANANCHI WA MKOA WA TABORA

MAMBO 10 MUHIMU YALIYOJITOKEZA KTK ZIARA YA KUWASIKILIZA WANANCHI WA MKOA WA TABORA

Leo tarehe 30/11/2022 tunahitimisha ziara ya siku 21 Mkoani Tabora katika shughuli za ujenzi wa chama na kuwasikiliza wananchi mkoani Tabora. Katika kipindi hiki Tumeweza kuwafikia wananchi katika majimbo yote 12 ya mkoa wa Tabora.

Aidha tunawashukuru wananchi, wanachama na Viongozi wa ACT Wazalendo waliojitokeza na kuunga mkono chama chetu kwa kujiandikisha katika mfumo wa ACT Kiganjani na kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na kuainisha kero zao. Zoezi la usajili wa wanachama limefanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini ni zoezi endelevu ambapo tumeshaweka mfumo imara wa kiutendaji ndani ya chama ili liendelezwe na makatibu wetu wa chama wa kata zote za mkoa wa Tabora.

Katika ziara yetu hii yamejitokeza masuala muhimu kumi yaliyoibuliwa na wananchi:

1. Mgao mkali wa umeme unaofikia kati ya saa 18 hadi saa 12 kwa siku.

Kumekuwa na mgao mkali wa umeme katika mkoa wa Tabora ambapo wananchi hukosa umeme kwa kati ya saa 18 mpaka 12 kwa siku. Mgao huu umetokana na kupungua kwa umeme kuliko tangazwa na TANESCO hivi karibuni kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutokana na upungufu wa uzalishaji wa umeme unaotokana na maji.

Wananchi wanahoji kwa nini mgao huu haukuwapo katika kipindi cha utawala uliopita wa awamu ya tano na umeibuka awamu hii. Sehemu kubwa ya wananchi wanahoji uwajibikaji wa Waziri wa Nishati aliyopo sasa.
Tunatoa wito kwa wizara kutafutia suluhisho la kudumu tatizo hili ili kuiepusha jamii na taharuki isiyo na lazima.

Wizara ya Nishati ikizingatia mapendekezo yetu tuliyoyatoa ya kutumia gesi iliyopo nchini kuzalisha umeme kwa kuitekeleza miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi ya Mtwara na Somanga Fungu. Miradi hii ikikamilika itatuingizia umeme wa uhakika wa gesi wa Megawatts 620 na hivyo kutuondoa kwenye utegemezi wa umeme wa maji unaoligharimu Taifa.

2. Gharama za kuunganishiwa umeme vijijini kutokutekelezwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali.

Wananchi wamehoji uhalali wa kijiji kimoja kuwa na bei tofauti ya gharama za kuunganishiwa umeme ambapo baadhi ya vitongoji huunganishiwa kwa shilingi 27,000 na vingine shilingi 370,000 mpaka 380,000.

Mfano kijiji cha Sikonge vitongoji vya Isangerunge na Ukangavili gharama za kuunganishiwa umeme ni shilingi 27,000 wakati vitongoji vingine vya kijiji hicho hicho ni shilingi 280,000. Wananchi wameiomba wizara kulishughulikia suala hilo kwani hawamudu gharama za kuunganishiwa umeme kwa shilingi 380,000.

Kwa mujibu wa Tangazo la bei za kuunganishiwa umeme lililotolewa na TANESCO tarehe 05/01/2022 bei ya kuunganishiwa umeme vijijini ni shilingi 27,000 na mijini ni shilingi 320,960. Kinachoendelea hapa Tabora ni mkanganyiko usioeleweka wa utekelezaji wa Tangazo hili. Tunamshauri Waziri wa Nishati kufuatilia mkanganyiko huu wa kiutekelezaji usiobeba hata mantiki ya uamuzi wake wa kurejesha bei za umeme kubwa mijini na ndogo vijijini.

Aidha, tunarejea wito wetu wa kuitaka serikali ibebe gharama zote za kuwaunganishia umeme wananchi umeme na kuwabakishia gharama za matumizi ya huduma ya umeme. Gharama hizi zinafanya wananchi katika maeneo ambayo umeme umefika kushindwa kunufaika na huduma hiyo.

3. Hofu

Wananchi bado kwa sehemu kubwa ya mkoa wa Tabora wanaishi kwa hofu kutokana na vitendo vya watendaji wa vijiji na kitisho cha kuuawa na askari wa maliasili.

Kwanza, kumekuwa na hofu ya kujihusisha na masuala ya kisiasa ikihofiwa kutengwa katika upatiwaji wa huduma za kijamii kama vile kunyimwa fedha za kaya masikini TASAF na mbolea ya ruzuku na misaada inayotolewa na serikali kwa wananchi. Watendaji wa vijiji wamekuwa wakitumia mbinu hii kama njia ya kunyamazisha harakati za kisiasa. Aidha watendaji wamekuwa wakiwahoji wananchi na Viongozi wanaojihusisha na masuala ya siasa za vyama vya upinzani katika namna ambayo inawafanya wasihisi uhuru wao kama raia.

Tunatoa wito kwa watendaji wote wa serkali mkoani Tabora kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha mara moja tabia hii. Chama chetu kitachukua hatua ikiwemo kumfikisha mahakamani Mtendaji yeyote atakayebainika kutisha wananchi au kuwanyima haki zao kwa sababu za kisiasa.

Pili, vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu vinavyofanywa na askari wa maliasili ni hofu iliyoenea maeneo mengi kandokando ya hifadhi. Kumekuwa na matukio ya vitisho, kufukuzwa kwa wananchi walio karibu ya maeneo ya hifadhi na kupotezwa kwa watu wanohisiwa kukiuka sheria za uhifadhi. Katika kijiji cha Msumbiji kata ya Msenda, Kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Sudi alifuatwa nyumbani kwake na askari wa maliasili wakimtuhumu na kosa la kujihusisha na shughuli za kukata magogo kwenye hifadhi na kisha kutoweka nae na hajaonekana kwa wiki ya tatu sasa. Viongozi wetu wa ACT Urambo wamemuuliza OCD juu ya tukio hili ambapo sisi tumeelezwa na rafiki yake pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji kijijini na kujibiwa kuwa hajui na wala kijana huyo hayuko mikononi mwa jeshi la polisi.

Tunatoa wito wa uchunguzi wa namna ambavyo askari wa maliasili wanatekeleza wajibu wao. Kwani maeneo yote ambapo yanazunguka hifadhi yana visa vya namna hii.

4. Unyanyasaji na utaratibu wa hovyo katika mgao wa fedha za TASAF

Fedha zinazotolewa kwa kaya masikini kupitia mradi wa TASAF hazisimamiwi vema na hivyo kupelekea vitendo vya unyanyapaa kwa wazee wasiojiweza na walemavu. Wazee hawa hulazimishwa kufanya kazi ngumu ikiwamo kuchimba visima na kuvunja mawe. Hali hii ipo eneo kubwa na Tumeikuta Ilolangulu ikiwahuzunisha sana wazee ambapo nyakati zingine hulazimishwa kuzibakisha kwa Mtendaji kwa hoja kuwa wacheze kibubu yaani kuzihifadhi.

Tunatoa wito kwa mamlaka zinazohusika kusimamia muongozo wa fedha za kaya masikini na kuwachukulia hatua watendaji wanaozitumia fedha hizi kunyanyasa wazee na walemavu.

5. Wananchi kutolipwa fidia kwa wakati wanapolazimika kuondoka kwenye nyumba au kuharibiwa mazao yao kupisha miradi ya maendeleo.

Eneo lote la ujenzi wa barabara kutoka Tabora kwenda Kigoma katika umbali wa mita 7 zilizoongezwa kama ukingo wa barabara halijalipwa fidia pamoja na kuwa lilisha fanyiwa tathmini miaka mitano iliyopita.

Aidha, katika vijiji vya kandokando na barabara hiyo wananchi wamepisha mradi wa kupitisha umeme huku wakifanyiwa tathmini ya mali zao bila kulipwa fidia kwa miaka miwili sasa.

Inafahamika kuwa mara baada ya tathmini wananchi waliofanyiwa tathmini mali zao ikiwamo nyumba hawaruhusiwi kuziendeleza. Hali hii huwafanya waishi kwenye wakati mgumu kwani wanashindwa kuhama kwa kuwa hawajalipwa na wanashindwa kuendeleza makazi yao kwa kuwa wameshafanyiwa tathmini.
Tunazitaka mamlaka husika hasa TANROADS na TANESCO kulipa fidia haraka wananchi ili kuwaondolea mazingira magumu yaliyosababishwa na miradi yao. Aidha, tunapata shaka imewezekana vipi miradi hii kukamilishwa kabla ya fidia kulipwa.

6. Utaratibu usio rafiki wa ugawaji wa mbolea ya ruzuku.

Pamoja na serikali kutumia mabilioni ya fedha za Watanzania kutoa ruzuku kwenye mbolea huenda matarajio yasifikiwe.

Ziko changamoto mbili kubwa ambazo ni muhimu zifanyiwe kazi haraka.
Changamoto ya kwanza ni mbolea kufikishwa makao makuu ya halmashauri na kutakiwa zifuatwe na wananchi wa vijijini hapo ilipo. Hii inafanya wananchi wasipate huduma kwa urahisi.

Changamoto ya pili ni kuchelewa kwa mbolea. Mbolea ya ruzuku isipofika kwa wakati haitoleta tija inayotarajiwa. Huu ni msimu wa kilimo ambapo maeneo kadhaa bado mbolea haijafikishwa.

7. Uhaba mkubwa wa maji katika maeneo mengi ya mkoa wa Tabora.

Kuna shida ya maji hasa kwenye majimbo ya Igunga, Sikonge na Tabora Kaskazini.

Mradi wa maji wa Ulyanyama ulioanza wakati wa Rais Kikwete na Rais akaahidi utaondoa tatizo la maji kata za Tutuo, Sikonge na Tabuta haujakamilishwa mpaka leo na ile ahadi nyingine ya Rais Magufuli ya kutumia fedha zilizobaki katika mradi wa maji ya ziwa Viktoria Tabora kuyafikisha Sikonge haijakamilika mpaka leo.
Tabora haistahiki kuwa na shida ya maji hasa baada ya mradi mkubwa wa maji ya ziwa Viktoria kufika Tabora.

8. Ukosefu wa Madawati Shule za Msingi.

Karne ya 21 watoto wetu wa shule za msingi mkoani Tabora wanakaa chini kupata elimu yao. Kitendo hiki ni mauaji ya ndoto za watoto wetu. Watoto wanajifunza sayansi ili waingie katika Dunia ya sayansi na teknolojia katika mazingira ya ujima (zama za kiza).

Wanafunzi wa shule za msingi Mwanzugi na Buyumbanansia zilizopo katika mji mdogo wa Mwanzugi Igunga wanakaa chini hawana madawati. Mwanzugi ndiyo wakulima wakubwa wa Mpunga Igunga na wanaongoza kwa kuiingizia mapato Halmashauri ya Igunga. Wana Mgodi wa Mawe ambapo kila siku zaidi ya lori 30 za tani 20 mpaka 30 husafirisha mawe kupeleka Dodoma kwa ujenzi lakini watoto wao katika eneo hilo hawana madawati shuleni.

Hiki ni kiwango kikubwa cha kutojali tunachokifanya kwa kizazi chetu wenyewe. Maisha haya ni kama vile Watanzani wamekodi serikali na hawana serikali yao.

Tunaishauri serikali kulinusuru taifa na dhahama ya kizazi cha kale kisicho na elimu ndani ya karne ambayo Dunia imepiga hatua kubwa katika elimu.

Wakurugenzi na Mkuu wa Mkoa wakiamua kutimiza wajibu wao hatutokuwa na aibu hii. Tabora iliyosheheni misitu haistahiki kuwatendea watoto wake ukatili mkubwa kiasi hiki.

9. Mahindi ya ruzuku yanayouzwa kwa bei ya 81,000 mpaka 90,000 kwa gunia hayajawafikia wananchi wa vijijini na pia bei hii ni kubwa.

Serikali imesambaza mahindi ya ruzuku mkoani Tabora ili kuwasidia wananchi wanaokabiliwa na gharama kubwa ya bei za vyakula. Hatua hii ya serikali ni nzuri. Hata hivyo ina mapungufu kadhaa.
Kwanza, bei inayouzwa ya shilingi 81,000 mpaka 90,000 kwa gunia pamoja na kuwa ina nafuu bado ni ghali. Serikali ione uwezekano wa kuuza mahindi haya kwa bei ya angala 60,000 . Hali ya kiuchumi ya wananchi kwa sasa ni ngumu sana hawana uwezo wa kumudu gharama hii.

Pili, serikali ihakikishe mahindi haya yanafika vijijini badala ya kuyauza kutokea mijini kwani gharama za kuyafuata zinawarudisha wananchi kwenye ugumu ule ule ambao serikali inajaribu kuupunguza.

10. Malipo ya Wakulima wa Tumbaku. Serikali isimamie walipwe.

Wakulima wa Tumbaku wanadai malimbikizo ya fedha zao za tumbaku iliyonunuliwa miaka miwili iliyopita. Kampuni ya tumbaku ya PCL iliyoitwa ya wazawa iliyochukua tumbaku yao msimu 2020/2021 imeshindwa kuwalipa kwa miaka mitatu sasa. Rais Samia aliahidi wakulima hawa kulipwa lakini bado mpaka sasa wanadai fedha zao.

Katika wakati huu ambapo wakulima wa tumbaku wanapanda upya tumbaku ni muhimu serikali ikawanusuru na kukata tamaa kwa kilimo cha Tumbaku. Tabora ndiyo mkoa pekee ambao unalima tumbaku kwa wingi hapa nchini. Wakulima wakikatishwa tamaa na uzalishaji kushuka uchumi wetu utayumba. Maumivu ya wakulima wa Tumbaku ni maumivu kwa watu masikini ambapo serikali inawajibika kuwasaidia. Wakulima wa tumbaku walipwe sasa.

Mwisho tunatoa wito kwa wawakilishi wa Wananchi wa Tabora Wabunge na Madiwani kusimamia maslahi ya Wana Tabora.
Tungependa kuona changamoto hizi zinazowakabili wananchi wa Tabora ndizo zinazojadiliwa katika vikao vya Halmashauri na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uchaguzi wa Mwaka 2020 uliifanya Tabora iwe na wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi pekee ambapo pia kinaunda serikali. Ikiwa kazi yenu itakuwa kuisifu na kuishangilia tu serikali, basi wananchi hawa wataisubiri 2025 kwa uchungu mkubwa.

Imetolewa na:

Ndg. Isihaka Rashid Mchinjita-Msemaji Sekta ya Nishati

Ndg. Kuluthum Mchuchuli- Msemaji TAMISEMI

Ndg. Selemani Misango- Naibu Msemaji Sekta ya Kilimo

30 Novemba, 2022.

Tabora. 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK