Tatizo la Maji nchini, Serikali Iwajibike. Itekeleze mapendekezo yetu sasa.
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
Mgao wa maji Dar es salaam na tatizo la upatikanaji wa maji nchini.
Utangulizi
Ndugu Waandishi wa Habari
Kama mnavyofahamu kuwepo kwa taarifa rasmi ya Serikali kupitia Mamlaka ya Maji ya Mjini Dar es Salaam (DAWASA) ya mgao wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani. ACT Wazalendo tumepokea taarifa hiyo kwa uzito mkubwa, ingawa tunatumia hali ya upatikanaji duni na mgao wa maji kwa Dar es Salaam kama msingi wa kutazama hali ya upatikanaji wa maji nchi nzima. Kwahiyo, kwenye mkutano huu tutaelezea tatizo la uhaba wa maji nchi nzima na hali ya upatikanaji wa maji Dar es Salaam. Mwisho tutatoa mapendekezo ya kukabiliana au kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa Dar es Salaam na nchi nzima.
A: Uhaba na mgao wa Maji Dar es Salaam
Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwa muda mrefu umekuwa sio wa uhakika au hutolewa kwa mgao wa wastani masaa 8-16 kwa siku. Yapo maeneo zinapita hadi siku tatu hadi nne (4) yanaweza kukosa huduma za maji. Kuanzia mwezi Februari 2022 hadi hali imekuwa mbaya zaidi kwa wakazi wa Kinondoni, Ubungo na Ilala hasa hasa maeneo ya Ubungo hadi kibamba, mbezi juu, Bonyokwa kutajwa kwa uchache.
Awamu hii, Serikali imetangaza rasmi kadhia hii ya upatikanaji wa maji kwa muda wa wiki moja kuanzia tarehe 25 hadi 30 Oktoba, 2022. Sababu zilizoelezwa na Serikali ni kushuka kwa uzalishaji wa maji kwenye vyanzo vya Mto Ruvu (Ruvu chini na Ruvu juu) kutoka lita milioni 466 hadi lita milioni 300 kwa siku.
Sisi, ACT Wazalendo tunasikitishwa na hoja hii ya Serikali ambayo imekuwa ikutumiwa miaka yote tangu kupatikana kwa Uhuru, miaka 60 sasa. Tunaona hoja hii ni ya kivivu kutokana na sababu zifuatazo ambazo zinaelezea tatizo hili kwa upana zaidi;
Moja, hata wakati ambao nchi inakuwa kwenye kipindi cha mvua au kutokwepo kwenye ukame hali ya mgao inakuwepo kinachotofautisha na sasa ni hali ya kuongezeka kwa masaa ya mgao. Takwimu zinaonyesha mahitaji ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam ni wastani wa lita milioni 544 kwa siku ambapo uwezo wa uzalishaji ni lita milioni 472 kwa siku. Maji yanayozalishwa yanakidhi mahitaji kwa asilimia 70 kwa wastani wa saa 14 kwa siku.
Pili, mtandao wa DAWASA umefikia asilimia 56 tu ya makazi ya Dar es Salaam. Takribani asilimia 44 ya eneo la Mkoa halina mtandao wa mabomba ya DAWASA kutokana na uwekezaji mdogo. Kutokana na ufinyu wa mtandao, upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam hautoshelezi mahitaji, huduma ya maji hutolewa kwa maeneo yenye mtandao wa Mabomba. Hivyo kulazimika kutumia visima kama vyanzo vikuu vya huduma ya maji.
Tatu, Maeneo machache (20%) yaliyopo hasa katika Wilaya ya Kinondoni, Ilala na Ubungo hupata huduma ya maji kwa saa kati ya 20-24 wakati zaidi ya asilimia 40 hupata maji kwa mgawo wa wastani wa saa kati 8-16 kwa siku na asilimia 40 nyingine hupata masaa 6-10 kwa siku.
Hivyo, tatizo la uhaba wa maji na mgao sio la kipindi cha kiangazi pekee ni la wakati wote, linapaswa kutazamwa kwa uzito mkubwa.
Ndugu Waandishi wa Habari
Tumesikia Serikali kwa muda mrefu ikielezea dhamiri ya kumaliza tatizo la maji kwa mkoa wa Dar es Salaam kwa kutekeleza miradi kadhaa;
• Upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini hadi matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi. Lengo la mradi huu ni kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 182 hadi 270 kwa siku
• Upanuzi wa chanzo cha Ruvu Juu na ujenzi wa bomba kuu hadi matanki ya Kibamba na Kimara.
• Mradi wa visima virefu 20 Kimbiji na Mpera na Uchimbaji wa Visima vya Majaribio.
o Visima vya maeneo ya Mpera vitahudumia wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto, Chanika, Luzando, Pugu, Mpera, Chamanzi, Kitunda, Ukonga, Kinyerezi, na Uwanja wa Ndege; na visima vya maeneo ya Kimbiji vitahudumia wakazi wa maeneo ya Temeke, Kisarawe, Kibada, Kimbiji, Kigamboni, Tuangoma, Mkuranga, Kongowe, Mbagala, Kurasini, Mtoni, Tandika, Keko na Chang’ombe.
• Mradi wa kupunguza upotevu wa maji (Non-Revenue Water -NRW)
o Mradi huu ni kwa ajili ya kupunguza uvujaji wa maji na maji yasiyolipiwa kutoka asilimia 47 ya sasa hadi asilimia 25 ifikapo mwaka 2020.
• Mradi wa Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza majisafi.
• Ujenzi wa bwawa la Kidunda
Miradi hii imebakia kuwa kama wimbo wa taifa, kuimbwa kila uchao bila kuwa na utekelezaji wa haraka. Dar es Salaam kama mji kielelezo cha nchi yetu inakabiliwa na uhaba wa maji na mgao usioisha vipi kwa mikoa ya pembezoni hali itakuwaje?
ACT Wazalendo tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe kumaliza changamoto ya uhaba wa maji kwa Dar es Salaam.
i. Serikali iharakishe kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya Ujenzi wa bwawa la kidunda na Mradi wa visima virefu 20 vya Mpera na Kimbiji.
ii. Kushughulikia tatizo la upotevu wa maji unaotokana na uchakavu wa Miundombinu ya kusambaza maji.
iii. Kuharakisha matumizi ya mfumo wa kieletroniki wa kufuatlia taarifa za maji katika utaratibu wa usambazaji wa maji
B: Tatizo la upatikanaji wa maji katika miji mingine na Vijijini.
Mahitaji ya maji kwa umma yanaongezeka kwa 7% kila mwaka, lakini uzalishaji wetu wa maji unaongezeka kwa 2% kwa mwaka. Sababu kubwa ya uzalishaji kuwa chini sana tofauti na uhitaji, ni uwezo mdogo wa Wizara ya Maji kusimamia miradi mbalimbali ya maji, jambo linalochangia miradi mimgi ya maji kutotoa maji kabisa ama kuzalisha kiwango kidogo cha maji. Kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 uzalishaji wa maji nchini ni 56% tu ya uhitaji wa maji wa wananchi, hivyo kupelekea wananchi kutumia muda mwingi na gharama kubwa kutafuta maji.
Asilimia 80 ya watanzania wanaokadiriwa kuwa Milioni 60 wanaishi vijiji, licha ya idadi kubwa ya watu kuonekana wanaishi vijijini na mchango wao katika pato la taifa kupitia shughuli za kilimo, uvuvi, madini na mazao ya misitu. Hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ni asilimia 74.5. Ijapokuwa asilimia hizo zinatajwa kwa maana miradi iliyofika sio upatikanaji wa huduma ya maji, uhalisia unaonyesha kuwa kutokana na kutofanyika kwa ukarabati na uwekezaji mdogo kati ya miradi ya maji iliyowekezwa vijijini takribani asilimia 30, haifanyi kazi kwa ufanisi au imekoma kabisa kutoa huduma ya maji.
Changamoto ya upatikanaji wa Maji inachangia sana kuwashikilia watu wa vijijini kwenye dimbwi la umasikini. Gharama za maji wanazotumiwa wananchi ili waweze kuishi ni kubwa mno maeneo ya vijijini kiasi kwamba zinazidi wastani wa pato la mtu mmoja (per capital income) kwa siku.
Nitatoa mfano wa Kijiji cha Gehandu huko Hanang, mkoani Manyara ambako mwananchi ananunua maji pipa moja la lita 200 kwa shilingi 7000 na familia moja inahitaji angalau pipa moja kwa siku kwa matumizi ya kujibana kabisa ya maji. Kwa hiyo mwananchi huyu atahitaji takribani shilingi milioni 2.5 kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu ya kutumia yeye na familia yake. Kwa familia ya Watu 6, huu ni wastani wa 16% ya kipato cha kila mwanafamilia hata mtoto mdogo wa siku 1 kutumika kununua Maji.
Hivyo familia moja inatumia wastani wa kipato cha mtu mmoja kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu. Lazima familia hii iendelee kushikwa kwenye mtego wa umasikini. Zaidi muda unaotumika kutafuta haya maji ni mkubwa sana, na upatikana kwa mateso ya kubeba maji haya kwa kutumia Wanyama kama punda, lakini maji yenyewe yakiwa ni chanzo cha maradhi kwa kuwa si safi na salama.
Hali hii ya upatikanaji wa maji umevikumba vijiji vingi sana nchini, tulipita kuanzia Songea, Tunduru, Newala, Tandahimba, Masasi na Maeneo mengi tu ya kusini hawana maji.
Ndugu Waandishi
Tatizo la maji nchi, sio janga la asili ni uzembe wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi wa kumaliza changamoto hizi. Miongoni mwa sababu kuu ni kama zifuatazo;
i. Kuna miradi ya Maji iliyokaa kwa muda mrefu bila kukamilika na mingine kushindwa kutekelezwa.
• Mfano kuna Mradi wa Same-Mwanga-Korogwe wenye uwezo wa kuzalisha maji lita million 103.7 na wenye kipande cha tatu cha kusambaza maji katika Mji wa Mwanga kinachoghalimu dola za marekani 36.70 kipande kingine cha nne kinahusu ujenzi wa miundombinu ya kusambaza Maji katika Mji wa Same kinachotekelezwa kwa thamani ya dola za marekani 35.25. Mradi huu utekelezaji wake ulianza mwaka 2014 miaka 8 iliyopita hadi sasa haujakamilika
• Mradi wa Uboreshaji wa huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Katika Jiji la Mwanza na Miji ya Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya Euro million 104.5. Licha ya kuanza kwa mradi baadhi ya maeneo bado watu wa Misungwi, Magu, Mkolani na Lamadi wanalia hawana maji safi yaliyo wafikia katika maeneo yao kama ilitarajiwa. Katika hili ni aibu kuona Jiji la Mwanza ambalo 53.2% ya eneo lake limezungukwa na Maji baridi watu wake hawana Maji.
• Ujenzi wa Mabwawa ya Kimkakati 40 katika jitihada za kuongeza na kuhakikisha upatikanaji wa maji katika kipindi chote cha mwaka.
o Mabwawa hayo yanayo pangwa kujengwa ni Farkwa (Dodoma), Kidunda (Morogoro) na Ndembera (Iringa). Bwawa la Farkwa litatumika kwa ajili ya usambazaji maji katika Jiji la Dodoma na Wilaya za Chemba na Bahi; pamoja na kilimo cha umwagiliaji.
o Bwawa la Kidunda litatumika kwa ajili ya kuhakikisha Mto Ruvu unakuwa na maji katika kipindi chote cha mwaka; kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa umeme;
o Bwawa la Ndembera litatumika kwa ajili ya kuhakikisha Mto Ruaha unakuwa na maji katikakipindi chote cha mwaka na uzalishaji wa umeme.
ii. Ubadhirifu mkubwa katika miradi ya Maji, unalitafuna taifa.
Kumekua na wimbi kubwa sana la ubadhillifu wa fedha za miradi ya maji inayopelekea ucheleweshwaji wa upatikanaji wa maji katika maeneo husika hili linadhibitiswa na ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali CAG za mwaka 2021 inaeleza kuwa kumekuwa na ubadhirifu wa shilingi bilioni 37.1 na dola za kimarekani milioni 6.05 ambao ulikua na malengo mbalimbali ya kuwezesha maji yanapatikana sehemu husika.
iii. Ufinyu wa bajeti ( Mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya maji) na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya maji.
Katika mwaka huu wa fedha Bunge limeidhinisha jumla ya shilingi bilioni 709. 361 kwa ajili ya wizara ya maji. Kati ya fedha hizo, kwa ajili ya miradi ya maendeleo zimetengwa shilingi bilioni 657.889 na fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 57.462. Kwanza, kwa kuilingalisha na bajeti ya mwaka huu na mwaka uliopita 2021/22 bajeti hii ni pungufu kiasi cha shilingi bilioni 110.381 sawa na asilimia 13.46 ya kuporomoka. Pili, bajeti hii ya maji haiendani na mahitaji halisi ya maji nchini kwetu.
Mwenendo huu wa bajeti, utachukua miaka mingi zaidi ili kukabiliana na changamoto za sasa za upatikanaji na usambazaji wa maji mijini na vijijini. Mathalani miradi minne ya mkakati ya ujenzi wa mabwawa ya maji ya Kidunda, Farkwa, Lugoda na Songwe ili iweze kukamilika inahitaji jumla shilingi trilioni 3.2
iv. Kutokuwepo kwa Mpango Mkuu wa Maji ili kuwezesha utekelezaji wa Miradi ya usambazaji Maji
v. Ukadiriaji wa mahitaji ya Maji usiojitoshereza wakati wa kupanga ili kuepuka makadirio kuwa ya juu au chini.
vi. Uwepo wa Pampu isiyotumika kutokana na uwezo usiofa. Mfano , katika mradi wa upanuzi wa Bomba la Ziwa Victoria hadi Tabora-Nzega-Igunga Mjini, uwezo wa pampu ulikuwa wa juu zaidi ikimaanisha kuwa kulikuwa na uwezo wa pampu ambao hautumiki ( Uwekezaji usio na tija).
vii. Ukubwa Usiofaa wa Mabomba na Matangi kulingana na Makadirio wa Mahitaji ya maji . Mfano ni upanuzi wa mtandao wa Bomba la Ziwa Victoria hadi Tabora-Nzega-Igunga Mjini ulisanifiwa kupita kiasi na umekuwa ukisababisha uharibifu katika maunganisho ya Maji kwa sababu ya mgandamizo mkubwa.
viii. Kushindwa kuzingatia Usanifu wa Miradi ya Maji kwa ajili ya utendaji endelevu wa mradi wa Maji (Uwezo wa pampu, Ukubwa wa Tangi, Mtambo wa kusafisha Maji na Ukubwa wa Bomba)
ACT Wazalendo kutokana na hali hii tunarudia mapendekezo yetu kama tulivyosema katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025.
i. Serikali ichukue mkopo nafuu wa muda mrefu wa Shilingi Trilioni 10 kutoka Benki za Maendeleo ili kutekeleza mradi mara moja na mapato ya ‘fuel levy’ yatahudumia mkopo huo mpaka utakapomalizika kulipwa.
ii. Serikali itoe ruzuku kwa Mamlaka za maji ili kuziwezesha kupanua na kuboresha miundombinu ya maji katika maeneo yao. Upanuzi wa miundombinu ya maji utazingatia mahitaji, usawa na mipango ya miji/vijiji na si nani anaweza kulipa ankara, shabaha ni kuyafanya maji kuwa huduma ya muhimu na sio biashara.
iii. Huduma za maji zinazotolewa na watu binafsi ili kudhibiti usalama wa maji na gharama za huduma hiyo.
iv. Serikali iimarishe mfuko wa taifa wa maji kwa kuupa chanzo cha uhakika cha mapato kutoka Ushuru maalumu utakaotokana na matumizi ya mafuta ya Petroli nchini.
Hitimisho:
Mwisho, Tanzania ni nchi pekee barani Africa iliyozungukwa na Maziwa makuu na yenye jumla ya mabonde 9. Hifadhi ya maji kwa Mwaka kwa ajili matumizi mbalimbali kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Wizara ya Maji mwaka 2019 ni mita za ujazo billion 126 huku maji ya juu ya Ardhi yakiwa na mita za ujazo billion 105 na chini ya Ardhi yakiwa ni mita za ujazo billion 11
Hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira unachora mstari mkubwa wa usawa wa kimaendeleo uliopo kati ya mijini na vijijini. Kwa takribani miaka 61 ya uhuru wa nchi yetu wanakijiji zaidi ya asilimia thelathini hawajawahi kuona maji ya bomba na kuyatumia, ni wazi kwa watu hawa hawajanufaika na matundu ya uhuru wa nchi yao. Ili kuweza kuwaondoa wananchi kwenye unyonge na manungúniko haya hatuhitaji kuwa na mbwembwe nyingi bali vitendo. Vitendo ni kutenga fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maji. Maji ni uhai.
Ahsante sana kwa kutusikiliza!
Ester A. Thomas
Msemaji wa Sekta ya Maji
ACT Wazalendo
Twitter:
29 Oktoba, 2022
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter