Tatizo la Mgao wa Umeme Nchini, Serikali na Mamlaka Ziwajibike.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA

Tatizo la mgao wa umeme nchini; Serikali na Mamlaka ziwajibike

Utangulizi:
Kwa takriban miezi miwili, nchi nzima imekuwa ikikabiliwa na tatizo la mgao wa umeme. Taarifa ya shirika la umeme nchini TANESCO imeeleza kuwa hali hii inatokana na kupungua kwa uzalishaji wa umeme wa maji kwenye vyanzo vya bwawa la Hale, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Pangani kutoka MW 256 mpaka MW 34.
Ingawa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma ya tarehe 30 Oktoba ilionyesha maeneo ambayo yangeathirika na sababu hiyo ni Mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro. Lakini kinyume chake tumeshuhudia mikoa yote nchini imekumbwa na ratiba za mgao wa umeme.

Kwa muda wa mwaka mmoja sasa kuongezeka kwa mgao wa umeme umekuwa ukikithiri siku hadi siku na sababu za kutokea kwa mgao huo zimekuwa zikibadilikabadilika. Miongoni mwa sababu za mara kwa mara zinazotajwa na Serikali ni mabadiliko ya hali ya hewa kufuatiwa na upungufu wa mvua (kipindi kirefu cha ukame), marekebisho ya mitambo na vituo vya kupozea umeme, hitilafu za kiufundi na wakati mwingine kuingiza teknolojia mpya kwenye mifumo ya usambazaji na huduma.
ACT Wazalendo tumepitia taarifa za Wizara kuhusu uwezo wa kuzalisha umeme wa nchi yetu unaonyesha kuwa chanzo kikuu cha umeme wetu unatokana na Gesi asilia ambacho kinazalisha Megawati 1021.32 sawa na asilimia 60.27 ya umeme wote, ikifuatiwa na chanzo cha Maji ambacho kinazalisha Megawati 574.60 sawa na asilimia 33.91 na Tungamotaka kinazalisha Megawati 10.5 sawa na asilimia 0.62. Umeme ambao haujaunganishwa kwenye Gridi ya taifa ni Megawati 38.83 ambao unazalishwa kwa kutumia mafuta ya petroli na dizeli ni Megawati 33.83 na umeme wa jua Megawati 5 unaozalishwa na mtu binafsi (NextGen Solawazi). Takwimu hizi zinaenda kufanya kiwango cha kufua umeme katika nchi yetu kuwa ni Megawati 1733.38.
Sambamba na uwezo wa uzalishaji wa umeme, takwimu zinaonyesha kuwa mahitaji ya juu ya umeme kwenye Gridi ya taifa ni Megawati 1335.01.

Ikiwa takwimu hizi ni sahihi, hoja za Serikali za uwezo mdogo wa uzalishaji ukilinganisha na mahitaji ya juu inahitaji ufafanuzi, hata kama ikiwa kweli uwezo wa uzalishaji umepungua kwa Megawati 232 kwenye mabwawa ya Kihansi, Hale na Pangani. Pia, mchango wa umeme wa maji kwenye Gridi ya taifa na ule wa Gesi asilimia ni ndogo sana.
Kwa nini ni uzembe wa Serikali na Mamlaka kupanga?
Huko nyuma tatizo hili lilidumu mara kwa mara na hasa wakati wa utawala wa awamu ya tatu na nne hali iliyoliingiza taifa katika kashfa kadhaa za ufisadi zilizofungamana na uagizaji wa mitambo ya kufua umeme ya Symbioni na Richmond.
Katika kulinasua Taifa na dhahama ya kiza, Serikali ya awamu ya nne ilijizatiti katika kuendeleza mradi wa uchimbaji gesi iliyogundulika maeneo ya bahari kuu kusini mwa Tanzania Mkoa wa Mtwara. Serikali ikaingia mkopo wa shilingi za kitanzania Tirioni 2.3 ili kusafirisha gesi toka Mtwara mpaka Dar es salaam. Baada ya kuliingiza taifa katika madeni kwa uendelezaji wa Gesi, Serikali imeendelea kuwekeza nguvu kubwa katika kuendeleza na kuanzisha miradi ya umeme wa maji huku ikitoa fedha kidogo kuendeleza umeme wa gesi.

Serikali imeshindwa kuweka vipaumbele kwa kuzingatia nguvu ya kifedha iliyopo na hitaji la nishati kwa taifa.Fedha zilizotumika katika miradi ya umeme ndani ya miaka 6 iliyopita shilingi Trilioni 4.4 zingeelekezwa kwenye miradi michache inayoendana na gharama kama vile Kinyerezi Extension I, Kikonge, mradi wa Gasi asilia Mtwara, mradi wa Gesi asilia Somanga Fungu na Maragarasi tungekuwa hivi sasa tumezalisha umeme MW 1164.5 ambapo ukiongeza na umeme tunaozalisha hivi sasa nchini wa MW 1605.86 tungeweza kuwa na jumla ya MW 2770.36 na kufanya Taifa lijitosheleze kwa kukidhi mahitaji ya umeme wa MW2677 zinazohitajika.
Mwaka huu wa fedha pekee Serikali imetenga shilingi Trilioni 1.44 na kuelekeza kwenye mradi wa umeme wa maji wa Mwalimu Nyerere huku ikijua kuwa fedha hizo hazitaukamilisha mradi mwaka huu na hakuna majibu ya uhakika kuwa ni kwa vipi mradi huu mkubwa hautoathiriwa na changamoto ya kupungua kwa kina cha maji.
Fedha hizi zingeelekezwa katika mradi wa kufua umeme kwa gesi wa Somanga Fungu, tungetumia bilioni 990 pekee na tungeweza kuzalisha MW 330 za umeme na hivyo Taifa lisingeweza kuwa kizani.

ACT Wazalendo kupitia taarifa hii tunaitaka Serikali ichukue hatua zifuatazo ili kukabiliana na changamoto ya mgao wa Umeme;
i. Serikali itumie wataalamu na Teknolojia za kisasa katika kufanya ukarabati wa Miundombinu ya kusafirisha na kupooza umeme ambayo haitosababisha mgao au kuzimwa kwa mitambo.
ii. Serikali na TANESCO watoe sababu halisi la kukosekana kwa umeme kwa kuwa sababu zao zinaacha mashaka na pia zieleze kwa sasa mahitaji halisi ya umeme ni kiasi gani na uwezo wa kuzalisha ni upi.
iii. Kuwekeza kwenye vyanzo vingine ambavyo havitoathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi kama vile umeme wa joto ardhi (geothermal), Urania (uranium) na umeme wa Gesi asilia (ambao tayari Serikali imewekeza fedha nyingi kuliko tija tunayoipata kama Taifa).

Hitimisho:
Nchi yetu imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme. Ina uwezo wa kuzalisha umeme wa maji kwa zaidi ya 4,000 MW na umeme wa joto ardhi (geothemal) kwa takribani 5,000 MW. Asilimia 10 ya nchi ya Tanzania inafaa kuzalisha umeme wa upepo. Mradi wa kuzalisha umeme kwa nguvu ya upepo mkoani Singida haukuwahi kuanza. Nchi nzima inafaa kuzalisha umeme wa jua. Aidha,uwepo wa gesi asilia wa zaidi ya futi za ujazo trilioni 60 itaiwezesha Tanzania kuzalisha umeme kutoka gesi asilia wa kutosha kwa miaka zaidi ya 100. Ingawa kwa sasa Tanzania inategemea gesi asilia kuzalisha umeme wake kwa kiasi kikubwa (asilimia 60) kuliko nishati nyingine yoyote lakini bado kuna fursa ya kuongeza uzalishaji huo kukidhi mahitaji yetu.
Vilevile, uwepo wa madini ya urani (uranium) unatupa watanzania nafasi ya kuzalisha umeme wa nyuklia kama tukiamua kama Taifa. Tafiti za Serikali yenyewe zinaonesha kuwa kuna madini ya urani katika mikoa ya Ruvuma, Dodoma, Singida, Manyara na Arusha japo hayajaanza kuchimbwa.

Imeandaliwa na:

Ndg.Isihaka Rashid Mchinjita,
Msemaji wa Sekta ya Nishati,
Twitter: @Isihakamchinji1
ACT Wazalendo.
04Novemba, 2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK