TICTS ISIPEWE MKATABA MPYA. IMESHINDWA KAZI

Maoni ya ACT Wazalendo Kuhusu Utendaji Kazi wa Kampuni Binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS)

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa miaka mingi, pamekuwa na mjadala wa mara kwa mara juu ya utendaji kazi usioridhisha wa kampuni binafsi ya Kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (Tanzania International Containers Terminal Service- TICTS). Sehemu kubwa ya mjadala umewahusisha wadau wa biashara, viongozi wa Serikali, wabunge na wataalamu.

Hivi karibuni wadau wa biashara wametoa mapendekezo yao wakiisihi Serikali kutokuipa mkataba mpya kampuni hiyo mara baada ya kumaliza mkataba wake mwaka huu. Pia, Waziri Mkuu Ndugu Kassim Majaliwa mwezi Aprili mwaka huu alinukuliwa na vyombo vya habari akitoa agizo kwa kampuni hiyo kuimarisha utendaji kazi wake ili kuondoa kero ya ucheleweshaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Katika hali hiyo, ACT Wazalendo kupitia (mimi- Ally Saleh) ambaye ni Msemaji wa Sekta ya Habari na Uchukuzi ACT Wazalendo tunatoa mapendekezo yetu kwa Serikali na mamlaka ya namna ya kushugulikia suala hili.

Historia ya maamuzi ya Serikali kuachia uendeshaji (kukodisha) wa kitengo cha ushushaji, upakizaji na uhifadhi wa makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kampuni binafsi ulisukumwa na mtazamo wa Serikali kujiondoa kwenye uendeshaji wa uchumi na biashara kwa madai kuwa kutawezesha utendaji kazi kwa ufanisi kwa taasisi zilizokuwa zinasimamiwa na Serikali.

Tarehe 5 Mei, 2000 Serikali ilisaini mkataba wa ukodishaji wa kitengo cha Makasha cha Bandari ya Dar es Salaam kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA) na International Containers Terminal Service Inc (ICTSI) ya Ufilipino na Tanzania International Containers Terminal Service - TICTS. Kwa mujibu kwa mkataba huo ICTSI alikuwa ni Mwekazaji wa Kimkakati (Strategic Investor) na TICTS ni kampuni ya uendeshaji (Terminal Operator) ambayo iliundwa na wanahisa (wa ndani na nje ya nchi) kwa ajili ya kuendesha kitengo cha Makasha.

Matarajio ya kukodisha kitengo cha Makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kwa makampuni binafsi yalikuwa ni;
i) Kuboresha utendaji ili kuongeza mchango wa sekta ya bandari katika uchumi wa taifa,
ii) Kupunguza gharama za kuhudumia shehena za makasha zinazopita bandari yetu ili kuhimili ushindani na nchi jirani,
iii) Kuvutia shehena za ndani na nje ya nchi zinazopita katika bandari yetu na mwisho,
iv) Kuingiza Teknolojia mpya na kuwawezesha wazawa kupata mbinu mpya za usimamizi na uongozi wa bandari.
Hivi sasa, mkataba wa TICTS unapoelekea ukiongoni, kuna hoja kwamba taasisi hiyo haikufanikiwa kufanya yaliyotarajiwa kwenye matakwa ya mkataba. Malalamiko ya utendaji wake yametiliwa mkazo zaidi na wafanya biashara na waagizaji, ambao wamekuwa wakibeba mzigo wa gharama za uchelewaji wa kufunga meli na kuondosha mizigo yao madai yakiwa dhidi ya TICTS.
Wakosoaji wa TICTS wanadai kwamba, kwa mujibu wa mkataba taasisi hiyo ilitakiwa iwe inawekeza katika kuimarisha eneo la kuweka na kupokea makontena, ambapo kampuni hiyo katika mkataba wake ilitakiwa iwe inakuza huduma zake za kuhudumia makontena kwa asilimia 37 kwa mwaka lakini hilo pia halijatekelezwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali 2020/21 inaonyesha kuwa kuna ucheleweshaji wa ushushaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam jambo linalopelekea malalamiko ya wateja na kuathiri ufanisi wa utendaji wa bandari. CAG alionyesha meli za mizigo na mafuta zinachukua wastani wa siku tatu hadi nane (8) kupakua mizigo kinyume na mipango ya mamlaka ya bandari ya kuhakikisha inapunguza hadi kufikia siku mbili. Ni wazi kuwa kukaa kwa meli muda mrefu bandarini kunaathiri ufanisi wa Mamlaka na kunapunguza ushindani wa kibiashara na bandari za nchi nyingine.
Takwimu zinaonyesha uwalakini na madhaifu ya TICTS ikilinganishwa na bandari za nchi jirani kama Kenya. Mwaka 2021 bandari ya Dar es Salaam iliongeza uingizaji wa makontena kwa asilimia 0.8% kwa kiasi cha 606,169 ya futi 20 kutoka ya mwaka mmoja nyuma au kabla kwa makontena 601,654. Wakati huohuo, mshindani mkuu wa bandari ya Dar es salaam yaani Bandari ya Mombasa mwaka 2019 walikuwa na uingizaji wa makontena milioni 1.4 mwaka 2019 na mwaka huu, bandari hiyo inatarajia kuingiza hadi makontena milioni 2, vyombo vya habari nchini vimeripoti.
ACT Wazalendo inaamini kwamba, dhima ya Serikali ya kuwekeza kwenye mashirika ya umma ni kukuza uchumi kwa madhumuni ya kupata mapato, kusogeza na kutoa huduma kwa urahisi kwa jamii na kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi, kudhibiti utoaji wa huduma na kulinda maslahi ya taifa lakini pia kutengeneza ajira zenye staha na usalama kwa wananchi wake. Mfumo wa sasa wa ukodishaji na uendeshaji wa sekta ya kuhudumia makasha katika bandari ya Dar es Salaam ni dhahiri kuwa una hatarisha maslahi ya umma.
Kwa hivyo ACT Wazalendo katika suala hili la TICTS ina mapendekezo yafuatayo:
1. Kwanza, tunaungana na wadau wengine kuwa suala la ukodishwaji au kutokodishwa tena TICTS lichukuliwe na lifanyiwe maamuzi katika hali ya uzalendo mkubwa kwa maana ya kujali maslahi ya taifa.

2. Pili, Serikali isitishe nyongeza ya mkataba wa kukodisha kitengo cha makasha kati yake na Kampuni binafsi ya Kimataifa ya kuhudumia makontena (TICTS). Kwa kuwa ni wazi imeshindwa kukidhi matarajio ya kukodishwa kwake.

3. Tatu, Serikali ifanye uchambuzi wa kina katika kutoa zabuni kwa kampuni zenye sifa ya kimataifa kwa kuipima TICTS kwenye utendaji wake mzima wa miaka 20 na faida zake na uwezo wa kufikisha malengo mapya yatakayokuwa katika mkataba ujao.

4. Serikali, iiwezeshe Mamlaka ya Bandari kusimamia kitengo cha makasha cha Bandari ya Dar es Salaam katika wakati wa mpito ambapo itakuwa kwenye mchakato wa kutafuta mwekezaji mwingine.

5. Aidha, kwa kuwa imetajwa kuwa moja ya kilichochangia hali ya sasa ni kuwa Serikali kutowekeza ipasavyo kwa yale inayowajibika nayo, ni vyema jambo hilo sasa lisimamiwe kwa umuhimu mkubwa ili kuongeza ufanisi.

Imetolewa na;

Ally Saleh
Msemaji wa Sekta ya Mawasiliano, Teknolojia, Habari na Uchukuzi
ACT Wazalendo
Twitter: @allysalehtz Facebook: Ally Saleh
21 Julai, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK