January 29, 2021 4:34 PM

TISHIO LA COVID-19 NI HALISI. VIONGOZI NA WANACHAMA TUCHUKUE TAHADHARI.


Maelekezo ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo kwa Viongozi na Wanachama kuhusu tahadhali dhidi ya tishio la mlipuko wa pili wa janga la Covid-19

Mwaka jana dunia ilikumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosambazwa na virusi vya Corona. Tangu Januari 30, 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipotangaza rasmi uwepo wa mlipuko wa virusi hivi, mataifa mengi yamepoteza mamia na maelfu ya watu kote ulimwenguni. Tanzania pia haijanusurika na dhahama hii.

Kama ilivyo tabia ya majanga ya namna hii wakati wote ambao yamepata kutokea duniani, yamekuwa na kawaida ya kujirudia kwa awamu mbili. Hivi sasa, dunia inakabiliana na mlipuko wa awamu ya pili wa virusi vya Corona.

Taarifa na takwimu za ongezeko la vifo vinavyotokana na janga hili kutoka maeneo na nchi mbalimbali kote ulimwenguni, zinatisha sana.

Licha ya kwamba mamlaka za hapa nchini kwetu zimezuia utolewaji wa takwimu rasmi za vifo vya Corona, taarifa tunazokusanya kwa njia zetu mbalimbali zinaonesha mlipuko huu unashika kasi nchini na watu wengi wanaangamia.

Kutokana na hali hiyo, Chama kinachukua hatua za makusudi kuepusha maafa na madhara yanayoweza kutokea zaidi. Mapambano dhidi ya virusi vya Corona sasa yarejee rasmi. Ule utamaduni wa kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka, uvaaji wa barakoa, na kuepuka kusogeleana sasa urejee.

Tuzingatie na kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na kupambana na janga la virusi hivi. Janga la virusi vya Corona haliwezi kuisha nchini kwa kujidanganya kuwa halipo. Tuchukue tahadhari.

Aidha, Chama kitachukua hatua za kuitaka serikali kuwajibika inavyostahiki katika mapambano dhidi ya virusi hivi ili kuokoa maisha ya watanzania yasizidi kupotea. Hatua ambazo serikali imezichukua tangu mlipuko wa kwanza mwaka jana na hata sasa tunavyokabiliana na mlipuko wa pili, haziridhishi na hatuoni kama iko makini na mapambano dhidi ya virusi hivi hatari.

Pamoja na Salamu za Chama: ACT Wazalendo, Taifa kwanza leo na kesho.

Ado Shaibu
Katibu Mkuu
ACT Wazalendo
29 Januari, 2021

Showing 1 reaction

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK