Tozo za Benki Hazikubaliki: ACT Wazalendo Tunazipinga
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
Kilio cha wananchi tozo mpya katika huduma za benki ; Serikali iwafute machozi.
Utangulizi
01 Julai 2022, Serikali kupitia waziri wa fedha na mipango Ndg. Mwigulu Lameck Nchemba alitangaza kupitia gazeti za serikali Na.478V kuanza kwa utekelezaji wa tozo ya miamala ya fedha kupitia benki. Utekelezaji wake ulianza papo hapo ambapo tumeshuhudia watumiaji wa huduma za kibenki wanapotoa fedha kwenye, ATMs, Kaunta, kupitia wakala wa benki na huduma za benki kupitia simu za mkononi wamekuwa wakikatwa kwa viwango tofauti tofauti.
Makato haya yameongeza mzigo mzito kwa watumiaji wa huduma za kibenki, itakumbukwa mwaka jana Serikali ilianzisha tozo kwenye miamala ya simu, wananchi walilalamikia sana kodi hiyo mpya na kupelekea kupunguza matumizi ya huduma za kifedha kwa chini wastani wa asilimia 25. Badala ya Serikali kutafuta namna ya kumpunguzia mwananchi mzigo imeenda kuanzisha kodi mpya kwa watumiaji wa huduma za kibenki.
Kuanzishwa kwa tozo mpya kwenye huduma za kibenki zimeibua hisia nzito kwa watumiaji wa huduma hizi. Kila kona ya nchi, wananchi wanalia kutokana na maumivu yaliyopandikizwa na tozo hizi.
ACT Wazalendo tunaungana na wananchi kupinga utekelezaji wa utaratibu huu wa kodi, kwa sababu zifuatazo;
i) Tozo hizi zinakata zaidi ya mara mbili kwenye chanzo kimoja, ni utaratibu usiokubalika kwenye mchakato wa kuanzisha chanzo cha mapato ya Serikali.
ii) Zitaenda kushusha ari na hamasa ya wananchi kutumia mifumo rasmi ya kifedha jambo ambalo linaenda kinyume na jitihada zilizofanywa huko nyuma za kuwaunganisha wananchi kwenye mifumo hii.
iii) Tozo hizi zitaenda kupunguza mzunguko wa fedha katika mifumo ya kibenki; Wananchi watapunguza kutumia huduma za kibenki ili kukwepa makato yasiyo ya haki kama tulivyoshuhudia mwaka wa fedha 2021/22 Serikali ilipoanzisha tozo kwenye miamala ya simu za mikononi ambapo kulikuwa na anguko hadi kufikia asilimia 25.6 pekee ya makusanyo sababu ya tozo.
iv) Tozo zitaenda kuongeza ugumu wa maisha kwa kila mtu, awe mfanyabiashara, mkulima, mamalishe au mvuvi.
v) Zinaenda kuwa kikwazo katika uchumi wa kidigitali na kurejesha utamaduni wa kuhifadhi fedha majumbani ambao unaweza kurejesha uvamizi na uhalifu.
Ni jambo la kushangaza kuona Serikali inajificha kwenye kivuli cha sheria kuhalalisha maamuzi yake yasiyojali maslahi ya wananchi wake. Utetezi wa Serikali kupitia Waziri wa fedha Ndg. Mwigulu Lameck Nchemba wakati wa kituo cha televisheni cha ITV kwamba suala hili limepitishwa na sheria bungeni haliwezi kubadilika, ni hoja ya hovyo na inaichora Serikali kwamba uhalali wake hautokani na kuwasikiliza na kuwashirikisha wananchi badala yake ni kwenye vyombo vya mabavu na kandamizi.
Katika historia yetu, tumeona hata utumwa, ukoloni, ubaguzi wa rangi ulikuwa unatekelezwa kwa kufuata sheria lakini waafrika tulisimama kuipinga kwa kuwa ni mifumo kandamizi, nyonyaji na inayodunisha utu wa walio wengi. Hivyo, hoja ya kisheria ina matobo sana ikiwa mantiki ya sheria yenyewe sio kukidhi matarajio, matakwa na masalahi ya walio wengi ambao ni wananchi.
Kwa hiyo, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kushughulikia suala hili ni pamoja na masuala yafuatayo;
1. Tunaitaka Serikali isitishe utekelezaji wa utaratibu huu ili kuwapa wananchi nafuu ya maisha.
2. Pili, Serikali iangalie vyanzo vingine vya mapato kwa kuzingatia utajiri wa nchi yetu kuanzia ardhi, madini, bahari, misitu na shughuli za biashara za ndai na nje. Itumie vyanzo vya uzalishaji mali kuliko kupitia mifumo ya huduma.
3. Tatu, Serikali iwe inawashirikisha wadau wanaoguswa na maamuzi yoyote yale ili kujenga uhalali wa uamuzi wowote ule.
Mwisho, ACT Wazalendo Serikali isipuuze vilio vya wananchi kote nchini kwa kisingizo chochote kile, athari zitakazotokana na kulazimisha utekelezaji wa kanuni hizi zinazowabebesha mzigo mkubwa wananchi ni kubwa kuliko malengo ya kifedha yanayotarajiwa kuvunwa na Serikali. Serikali iwafute machozi wananchi kwa kusitisha kabisa na pengo lake zifidiwe kwenye vyanzo vingine ambavyo havitaleta athari.
Imetolewa na:
Ndugu Juma Kombo
[email protected]
Naibu wa Sekta ya Fedha na Uchumi - ACT Wazalendo
21 Agosti, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter