TUCTA Inawauza Wafanyakazi: Kikokotoo Kipya cha Mafao Kitawaumiza Wastaafu.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
Uwekezaji, Mashirika ya Umma na hifadhi ya Jamii.

TUCTA Inawauza Wafanyakazi: Kikokotoo Kipya cha Mafao Kitawaumiza Wastaafu.
Utangulizi:
Hivi karibuni, yametokea maamuzi makubwa kuhusu hatima ya wafanyakazi nchini, tangu Mei Mosi, kuanzia ongezeko la kima cha chini cha mshahara, ukomo wa umri wa wategemezi wa Bima ya Taifa ya Afya na kikokotoo cha mafao ya ustaafu, hatima ya fao la kujitoa. Shangwe za kupandishwa kwa mshahara, zimezima uhalisia wa maumivu ya kanuni za kikokotoo cha mafao ya uzeeni (kikokotoo cha mafao ambacho kinapunguza mafao yanayolipwa kwa mtumishi aliyestaafu)

Ukimya wa TUCTA na vyama vingine vya wafanyakazi juu ya maslahi ya wafanyakazi na wastaafu, umetustusha sana. Kama chama tumeona hali hii inaweza kuathiri mustakabali wa wafanyakazi na wastaafu nchini. Kukalia kimya kutetereshwa kwa mifumo ya hifadhi ya jamii ni sawa na jaribio la kuteteresha Maisha ya askari wanaojitoa kwa ajili ya kuliendeleza taifa, matokeo yake ni kuvunja ari, hamasa na ufanisi wa kazi kwa wafanyakazi waliopo.
Kwenye, uchambuzi wa chama cha ACT Wazalendo tutaenda kuzungumzia mambo mawili; mosi, ujio wa kikokotoo na kuanza kwake kutumika rasmi Julai Mosi 2022 na hatima ya fao la kujitoa.
A: Kikokotoo na hatma ya wafanyakazi
Serikali imetangaza (tarehe 26 Mei, 2022) kanuni mpya za mafao katika skimu ya hifadhi ya jamii. Miaka mitatu iliyopita (2018) Serikali ilipitisha Bungeni kanuni za mifumo ya hifadhi ya jamii iliyoambatana na kanuni mpya za kukokotoa mafao ya kustaafu ya wafanyakazi. Kanuni hii (kikokotoo) ilipingwa na wafanyakazi, wanaharakati na wanasiasa kila kona kwa hoja za wazi kabisa; Moja, hatari iliyotangazwa na Serikali ya kufilisika kwa mifuko (kwa kipindi hicho, PSPF na LAPF) ni hoja iliyokosa nguvu, kwa kuwa kufilisika kwa mifuko kulitokana na madeni ya Serikali iliyokopa kwenye mifuko hiyo. Hivyo, makosa ya Serikali na warasimu wa mifuko hiyo hayapaswi kubebeshwa kwenye mabega ya wastaafu kwa kuwapunja mafao yao. Pili, hoja ya kufilisika kwa mifuko ilitiliwa shaka, kwa kuwa inafahamika kuwa mifuko hiyo imewekeza kwenye miradi mingi mikubwa na fedha nyingine zimetumika kufadhili miradi ya Serikali.
Kutokana na hoja na kelele za wafanyakazi na wadau wengine, iliilazimisha Serikali kupitia Rais wa wakati huo (Hayati, John Pombe Magufuli), kusimamisha matumizi ya kanuni hizo na kuahidi kuanza kutumika 2023. Sababu za kusitishwa kwake ni pamoja na kuipa mifuko ya hifadhi ya jamii muda wa kujiimarisha kifedha ili baadaye ziweze kupata nguvu ya kuwahudumia wastaafu. Kutoa muda kwa Serikali kulipa madeni yake inayoidaiwa na mifuko hiyo ambayo ilikuwa zaidi ya trilioni 4.7, lakini Serikali haijalipa madeni yote inayodaiwa. Aidha, kupata mwafaka wa pande zote juu ya kanuni zinazoweza kutumika.
Serikali imerejesha kikokotoa kilekile kimya kimya
Tumestushwa sana na pendekezo la TUCTA la kikokotoo kinacho poromosha mafao na uamuzi wa Serikali kutangazo kanuni mpya zinatumia kikokotoo cha 1/580 badala ya 1540, pia malipo ya mkupuo ya mafao (kiinua mgongo) ya mtumishi aliyestaafu atalipwa kwa asilimia 33 badala ya 50% inayotumika sasa, umri wa kuhudumiwa mstaafu ni miaka 12.5 badala ya miaka 15.5. Kurejeshwa kwa kikokotoo hiki kikiwa na marekebisho madogo tu ya asilimia za mkupuo kutoka 25 iliyopendekezwa na Serikali, bado haiendi kuwasaidia wastaafu badala yake inaenda kuwaumiza.
Mfano, kwa mfanyakazi aliyestaafu akiwa amechangia kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii kwa miaka 30 na ikiwa mshahara wake wa mwisho ulikuwa Tsh. 1,200,000. Mafao ya Mtumishi huyu kwa kutumia kanuni hizi mbili yatakuwa kama yafuatayo;
• Kanuni za zamani (Kikokotoo cha 1/540, miaka 15.5 na malipo ya mkupuo 50%);
o Pensheni ya mwaka (Full pension) ilikuwa Sh. 9,600,000.
o Malipo ya mkupuo/Kiinua mgongo (Lumpsum/commuted pension) ilikuwa Shilingi Milioni 74.4 (74,400,000).
o Pensheni ya Mwezi (Posho) ilikuwa Sh. 400, 000.

• Kanuni Mpya _mwaka 2018 (Na marekebisho ya 2022); (Kikokotoo cha 1/580, miaka 12.5 na malipo ya Mkupuo 33%)
o Pensheni ya mwaka (Full Pensheni) itakuwa Sh. 8,937,931.03
o Malipo ya Mkupuo/Kiinua mgongo (Lumpsum pension) itakuwa Sh. Milioni 36.8 (36,868,965)
o Pensheni ya Kila mwezi (posho) itakuwa Sh. 499,034.
Kwa kuangalia mchanganuo huo, hapo juu ni wazi kwamba kanuni mpya inaenda kumpunguzia mstaafu mafao yake karibia kila kipengele kinachohusika na mafao. Kwa uchambuzi tulioufanya inaonyesha dhahiri kuwa;
1) Kikokotoo cha 1/580 kinaenda kupunguza mafao ya mtumishi aliyestaafu ya mwaka kwa asilimia 6.9

2) Pia, kinapunguza malipo ya mkupuo (lumpsum) ya kiinua mgongo kwa asilimia 50.5 ukilinganisha na kanuni za awali.

3) Vilevile, kinafupisha umri wa kuhudumiwa mstaafu kwa takribani miaka mitatu kutoka miaka 15.5 ya awali hadi 12.5

4) Kwa kutumia ukokotozi wa wastani wa miaka mitatu ya mshahara wa juu badala ya kiwango cha mshahara wa mwisho kutashusha mafao ya wastaafu kwa asilimia 7.08

5) Mwisho, kutakuwa na ongezeka kwenye posho ya kiinua mgongo ya kila mwezi kwa asilimia 24.7 lakini kwa kukokotolewa jumla ya mafao atakayepokea kwa miaka 12.5 yanaongezeka kwa asilimia 0.6 pekee kutokana na kufupishwa kwa miaka mitatu tofauti na awali.

Msimamo na Mapendekezo ya ACT Wazalendo kuhusu kikokotoo kipya
Sisi, ACT Wazalendo tunaamini kuwa mfumo wa hifadhi ya jamii husaidia kulinda maisha ya watu na kutoa uhakika wa kuishi vizuri unapokutwa na majanga au kupoteza uwezo wa kufanya kazi kwa namna yoyote ile. Hatupaswi kuwaadhibu wazee wetu kwa kukubali kanuni hizi kandamizi zinazoenda kuwapunja mafao yao na kufupisha muda wa kuwahudimia kwa kuwakadiria kifo mapema zaidi. Aidha, hatukubaliani na uamuzi wa Serikali kuwabebesha wastaafu mzigo wa gharama kwa makosa ya utendaji mbovu wa menejimeti za mifuko na madeni ya Serikali.
Kutokana na mtazamo huu, tunaitaka Serikali kufanya mambo yafuatayo ili kuhakikisha wafanyakazi wastaafu wananufaika na michago yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii;
i. Tunaitaka Serikali kulipa madeni yote inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa mkupuo mmoja ili kuiwezesha mifuko kujiendesha na kuhudumia wateja wake kwa wakati.
Ripoti ya CAG 2020/21 imeonyesha kuwa kuna deni la trilioni 1.5 ikiwa ni mikopo isiyolipwa na Serikali na taasisi zake mbalimbali. NSSF inadai Trilioni 1.17 (Mkopo 490.16 bilioni na riba 684.42 bilioni) na PSSSF inadai 323.98 bilioni. Madeni haya yana muda mrefu kati ya mwaka 1 hadi15. Pia, deni la Serikali linalotakana na michago yake ya wastaafu kabla ya mwaka 1999 (shilingi trilioni 2.45). Jumla, ya madeni ya Serikali kwenye mifuko ni trilioni 3.95. Madeni haya yakilipwa itaboresha uwezo wa mifuko kwa zaidi ya asilimia 40.
ii. Tunaitaka Serikali kurejesha kanuni za zamani za mwaka 2017 (Social security Schemes- Pension benefits harmonization rules)
Tunaitaka Serikali kurudi kwenye kanuni za mwaka 2017 ambazo zinatoa mafao ya malipo ya mkupuo kwa 50%, kikokotoo kuwa ni 1/540, umri wa kuishi baada ya kustaafu ni miaka 15.5 na 50% inayobaki ya mafao ya mtumishi iwe pensheni ya kila mwezi. Vilevile, ichukue mshahara wa mwisho wa mstaafu badala kuchukua wastani wa mishahara mitatu ya juu. Kwa kutekeleza hatua ya kwanza tuliyoipendekeza hili litawekezana kwa urahisi zaidi.
iii. Menejimenti za mifuko ya hifadhi ya jamii kufanya uwekezaji wa miradi itakayoleta faida kuendena na mahitaji ya wanachama.
Moja ya changamoto zinazopunguza uwezo wa mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSF na PSSSF) kuhudumia wanachama wake ni kufanya uwekezaji usiolingana na faida inayopata. Kiwango cha faida za uwekezaji kwenye majengo na miradi mengine ni kidogo na kimekuwa kikishuka kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2017 hadi 2021. Ongezeko la uwekezaji katika majengo ya uwekezaji haulingani na mapato halisi kwani yanaendelea kupungua.
iv. Vyama vya wafanyakazi nchini vishikamane kama ilivyofanya miaka mitatu nyuma kupinga udhalimu huu.
Vyama vya wafanyakazi na wadau wengine tushikamane kupaza sauti ili kuhakikisha wafanyakazi wa nchi hii waone kustaafu ni heshima badala ya adhabu. Pia, wafanyakazi ni wastaafu watarajiwa, wasipopigania haki yao wakiwa na nguvu hawatoweza wakizeeka.
B: Mafao ya kujitoa
Mjadala wa fao la kujitoa ulihitimishwa kwa kupitishwa kwa sheria mpya ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2017. Licha ya kelele kutoka kwa wadau mbalimbali, Serikali iliweka pamba masikioni na badala yake ikaanzisha fao la kukosa ajira. Uzoefu wa utekelezaji wa sheria hiyo unaonyesha wazi kuwa fao la kukosa ajira haliwezi kuwa mbadala wa fao la kujitoa. Hivyo basi, tunaishauri Serikali kufanya mapitio ya sheria ili kurejesha fao la kujitoa. Pia, fao la kukosa ajira lipanuliwe kwa kuhusisha watu wote walikosa ajira (ambao wenye sifa na haki ya kuajiriwa lakini kutokana na ukosefu wa ajira nchini wameshindwa kupata ajira) tofauti na ilivyo sasa.

Hitimisho:
Hatua ya Serikali kung’ang’ania kutumia kanuni mpya ya kikokotoo baada ya mjadala wa miaka mitatu na mapendekezo mbalimbali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa nchi hii. Ni dhahiri kuwa Serikali imeamua kupuuza sauti za muda mrefu za wafanyakazi na kuonyesha kuwa lengo lake ni kuwaumiza wastaafu. Ujio wa kanuni hizi, kwa kumlipa mstaafu asilimia 33 ya mafao ya mkupuo, kwa miaka 12.5 na kikokotoo cha 1/580 ni kuwakandamiza na kuwanyonya wazee wetu waliotumikia taifa hili kwa jasho na damu tena katika mazingira magumu ya mishahara kiduchu, ambayo inayowafanya kuishi kwenye mzunguko wa madeni kila uchao. Aidha, ni wazi kuwa kanuni hizi zitashusha ari, hamasa na ufanisi wa kazi kwa wafanyakazi wa nchi hii. Ni matumaini yetu kuwa mapendekezo tuliyotoa yanaenda kusaidia mifuko ya hifadhi ya jamii na watumishi kwa ujumla wake, ni muhimu kwa Serikali kuyafanyia kazi kwa nguvu zote kunusuru hali ya wafanyakazi.


Ndg. Mwanaisha Mndeme
Msemaji wa Sekta ya Uwekezaji, Mashirika ya Umma na hifadhi ya Jamii
[email protected]
ACT Wazalendo
30 Mei, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK