January 29, 2021 4:42 PM

UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2021 UGANDA, NI UTANI MWINGINE KWA DEMOKRASIA YA AFRICA

 

Taarifa ya ACT Wazalendo, Idara ya Mambo ya Nje juu ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2021 nchini Uganda:

Januari 13, 2021 tulitoa taarifa kuhusiana na hali tete iliyougubika uchaguzi mkuu nchini Uganda uliokuwa umepangwa kufanyika siku inayofuata, tarehe 14 Januari, 2021.

Katika taarifa yetu, tulibainisha wasiwasi wetu kufuatia mfululizo wa matukio ya ukiukaji wa sheria, mashambulizi na uonevu wa vyombo vya dola dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani wakati wote wa kampeni. Tulilaani mashambulizi hayo yaliyokuwa yakifanywa na Polisi na vyombo vingine vya usalama dhidi ya vyombo vya habari, wanasheria na watetezi wa haki za binadamu.

Tulitoa wito kwa mamlaka nchini Uganda pamoja na wadau muhimu wa kikanda na kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua hatua za makusudi na za kiuwajibikaji kuisaidia Uganda isitumbukie kwenye machafuko.

Msimamo wetu ulioonesha kutoridhishwa kwa hali ya mambo katika uchaguzi mkuu wa Uganda ulitokana na rekodi za matukio na vitendo vya dhahiri ambavyo kwa taathira vinahitimisha ukweli kuwa misingi mikuu ya demokrasia ilikanyagwa na kusagwasagwa.

Masikitiko yetu makubwa ni kwamba kilichotokea katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa Uganda, hakikuwa kitu kingine, bali marudio ya kile ambacho utawala wa John Pombe Magufuli ulikifanya Zanzibar na Tanzania Bara kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Wakati huu tunapoandika taarifa hii, ni zaidi ya wiki (siku tisa) mshindani mkuu wa Rais Mseveni Ndugu Robert Kyagulanyi (Bobi Wine) bila hatia amefungiwa ndani kwake katika kifungo cha nyumbani tangu siku ya uchaguzi akiwa haruhusiwi kukutana na yeyote.

Uhuru na haki za Bobi Wine zinavunjwa. Kwa makusudi mazima, walimfungia ndani kwa lengo la kumzuia asiweze kuchukua hatua zozote za kisheria kupinga dosari na ukosefu wa uhalali wa uchaguzi uliofanyika. Hivi ni vitendo visivyokubalika katika macho ya demokrasia na haki za binadamu, na kwa vyovyote vile tunawajibika kulaani vikali.

Chama cha ACT Wazalendo kinasimamia na kupigania haki na misingi ya demokrasia. Tunajibidiisha kuhakikisha kwamba misingi muhimu ya kidemokrasia inapata nafasi ya kuchanua na kunawiri ndani ya Chama chetu, ndani ya Nchi yetu, ndani ya eneo letu la Afrika Mashariki, na katika bara zima la Afrika kwa ujumla.

Tuna hofu kubwa kwamba demokrasia ndani ya Afrika Mashariki imewekwa gizani na hatuna budi kusimama imara kuepusha hali hii kugeuka gonjwa lisilo na tiba.

Kwa kuzingatia hali hiyo, tunarejea tena wito wetu kuzitaka mamlaka nchini Uganda kuchukua hatua za haraka kuhakikisha haki na uhuru vinatamalaki. Usumbufu na uonevu wowote unaoendelea dhidi ya wanasiasa na asasi za kiraia unapaswa kukomeshwa. Vyombo vya dola vinapaswa kufanya kazi yake bila upendeleo, kuchunguza vitendo vyote vya dhuluma na uonevu na kuwachukulia hatua wahusika.

Licha ya ukandamizaji mkubwa uliofanyika dhidi ya upinzani katika uchaguzi huu, kuna mafanikio kadhaa kwa upinzani kupata viti Bungeni. Mathalani, Chama cha Umoja wa Kitaifa (NUP) kimeibuka na viti 56 vya Ubunge. Ni matumaini yetu kwamba NUP wataitumia fursa hiyo kuwezesha na kushinikiza mabadiliko muhimu ya kimfumo nchini Uganda na katika Bunge la Afrika Mshariki.

Tungependa kurejea wito wetu wa awali, njia pekee ya kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu katika nchi ni kutenda haki. Kila mmoja atende na kutendewa haki.


Imetolewa na:
Idara ya Mambo ya Nje,
ACT Wazalendo.
23 Januari, 2021.

Showing 1 reaction

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK