UCHAMBUZI WA ACT WAZALENDO MKOA WA LINDI KUHUSU RIPOTI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI(CAG) KWA HALMASHAURI ZA MKOA WA LINDI KWA MWAKA WA FEDHA ULIOISHIA TAREHE 30/6/2021.

UCHAMBUZI WA ACT WAZALENDO MKOA WA LINDI KUHUSU RIPOTI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI(CAG) KWA HALMASHAURI ZA MKOA WA LINDI KWA MWAKA WA FEDHA ULIOISHIA TAREHE 30/6/2021.

Ndugu Wanahabari.
Act Wazalendo imekuwa na utamaduni wa kuchambua ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kila mwaka mara baada ya kuwasilishwa bungeni.Hatua hii imekuwa ikilisaidia taifa kujenga morali wa kujadili na kufuatilia hoja za kiukaguzi zilizoibuliwa kwa lengo la kuiwajibisha serikali.
Kuanzia mwaka 2022 jukumu hili limeanza kufanywa na waziri kivuli wa fedha na uchumi wa Act Wazalendo na ambapo waziri mkuu kivuli wa Act Wazalendo ametoa maelekezo kwa wasemaji wa kisekta wengine kufanya hivyo wakati watakapochambua bajeti za wizara za serikali zinazowasilishwa bungeni kwa mwaka wa fedha 2022/2023.maagizo haya yanaiwezesha Act Wazalendo kupanua wigo wa mjadala kwa kuyaangalia karibu maeneo yote yaliyoibuliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na hivyo kuwawezesha wananchi kuhoji,kufuatilia na kuiwajibisha serikali katika mawanda mapana zaidi na ili kufikia lengo halisi la kutolewa kwa ripoti ya CAG.
Act Wazalendo mkoa wa lindi imefuatilia chambuzi zilizokwisha fanywa na msemaji wa kisecta wa fedha na baadae kazi nyingine iliyofanywa na msemaji wa kisekta wa TAMISEMI.Tunawapongeza kwa kuibua hoja zilizotikisa mjadala wa kitaifa katika ripoti ya CAG na ni matarajio yetu kuwa wahusika watawajibika na kuwajibishwa.
Katika kuunga mkono hatua hii adhwimu ya chama chetu,sisi ACT Wazalendo mkoa wa Lindi tumeamua kuchambua ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa halmashauri za mkoa wa lindi.Tunaamini kuwa hatua yetu hii itaendeleza mjadala na ari ya uwajibikaji kwa ustawi wa mkoa wetu wa lindi na taifa kwa ujumla. Aidha uchambuzi wetu huu umejikita katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ya serikali za mitaa.

UCHAMBUZI


Uchambuzi wetu huu utajikita ktk maeneo 10 yenye hoja za kiukaguzi zilizoibuliwa na mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali.Huu utakuwa ni mchango wetu katika kuzitaka mamlaka husika na wahusika wote kuwajibika kwa amana waliyopewa na wananchi kuisimamia.
1.Marekebisho ya miamala ya fedha bila kuzingatia kanuni zilizowekwa kwa lengo la kuficha ubadhirifu.
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali amegundua kuwapo kwa marekebisho ya Ankara na ufutaji wa miamala katika mfumo wa makusanyo ya mapato (LGRCIS) yenye thamani ya shilingi 2,626,096,232 katika halmashauri ya wilaya ya Nachingwea bila kufuata utaratibu.
Utaratibu unataka ili kufanya marekebisho katika mfumo ni lazima maafisa masuuli wahusishwe na uwepo ushahidi wa maandishi. Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali hakupewa ushahidi wa maandishi uliotumiwa na maafisa husika kufuta na kurekebisha miamala hiyo.
Jambo hili linathibitisha kuwapo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.Tunatoa wito kwa Takukuru na DPP kuwachukulia hatua maofisa wote ambao wamejihusisha na kufanya marekebisho ya miamala iliyokosewa bila kufuata utaratibu na bila kuzingatia matakwa ya mfumo wa udhibiti wa mapato ya ndani.Aidha mamlaka za nidhamu ziwasimamishe mara moja wote waliohusika ili kupisha uchunguzi.


2. Halmashauri za manispaa ya lindi na halmashauri ya wilaya ya Nachingwea zimefanya manunuzi yasiyoidhinishwa bodi za zabuni.
Kanuni ya 55 (2),163(4) na 185(1) ya kanuni za ununuzi wa ummah za mwaka 2013 inakataza mamlaka za serikali za mitaa kutotoa zabuni isipokuwa kama zabuni hiyo imeidhinishwa na bodi husika.
Kinyume kabisa na utaratibu huu wa kikanuni, halmashauri ya manispaa ya lindi ilifanya manunuzi yenye thamani ya shilingi 202,413,617 na halmashauri ya wilaya ya Nachingwea imefanya manunuzi ya shilingi 319,774,247.
Ununuzi wa namna hii unatia mashaka na ni kiashiria cha kuwapo kwa ubadhirifu unaofanywa na wakurugenzi kwa kushirikiana na maafisa manunuzi.ikiwa hakuna unachoficha hauna sababu za kukwepa taratibu zilizowekwa.
Tunamtaka Waziri Tamisemi kuwachukulia hatua wakurugenzi wa halmashauri husika na maafisa manunuzi wa halmashauri za manispaa ya lindi na Wilaya ya Nachingwea.


3.Halmashauri za wilaya za kilwa,liwale na manispaa ya lindi zimefanya manunuzi bila kushindanisha wazabuni.
Kanuni ya 164(1) ya kanuni za ununuzi wa umma yam waka 2013 inaagiza taasisi inayofanya manunuzi kupata nukuu za bei kutoka kwa wazabuni/wauzaji wasiopungua watatu.
Hata hivyo hiyo siyo hali halisi inayojitokeza hapa mkoani Lindi.Halmashauri tatu zimefanya manunuzi bila kufuata utaratibu huu uliowekwa na kanuni.
Halmashauri ya manispaa ya lindi imefanya manunuzi yenye thamani ya shilingi 126,859,509,Halmashauri ya wilaya ya kilwa imefanya manunuzi ya shilingi 86,955,460 na halmashauri ya wilaya ya liwale imefanya manunuzi ya shilingi 86,052,055.manunuzi yote haya yamefanyika bila ya kushindanisha wazabuni.
Ukiukwaji huu wa kikanuni unatoa mwanya wa rushwa na ununuzi wa bidhaa kwa bei kubwa kuliko bei halisi. Ni wazi kuwa wakurugenzi na maafisa manunuzi wamefanya ukiukwaji wa kanuni wa makusudi kwa maslahi yao na si maslahi ya ummah.

4. Halmashauri ya manispaa ya lindi imefanya ujenzi wa miradi yenye thamani ya shilingi 1,824,993,550 bila ya kuandaa mchanganuo wa vifaa.
Kipengele cha 11.1 cha miongozo ya nguvu kazi kwa taasisi nunuzi nchini Tanzania uliotolewa na mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa ununuzi wa umma unazitaka idara zinazofanya ununuzi kueleza kazi za ujenzi au matengenezo zinazotakiwa kutekelezwa.kipengele cha 11.2 cha muongozo huohuo kinaeleza kuwa ikiwa idara ya watumiaji ni tofauti na idara yenye ujuzi wa kitaalamu,basi idara ya watumiaji itapaswa kuomba wataalamu kutoka idara hiyo (au mtumishi mwenye taaluma stahiki ndani ya taasisi nunuzi au kwa ushirika na taasisi nyingine nunuzi) ili kubainisha upeo wa kazi kwa kuandaa michoro, vipimo na mchanganuo wa idadi ya bidhaa kwa ajili ya kutekeleza kazi husika.
Manunuzi ya vifaa bila mchanganuo huweza kusababisha kununua vifaa visivyo na ubora,kununua vifaa vingi kuliko mahitaji na hivyo kupelekea kupata hasara. Lindi tunao uzoefu wa kushuhudia viongozi na watendaji wa serikali wakigawana vifaa vya ujenzi kutoka katika eneo ambalo lilipaswa kujengwa kiwanda cha cement.kitendo cha kununua vifaa bila mchanganuo ni mwanya mwingine wa watendaji wa serikali kujinufaisha na vifaa vya ziada na kuendeleza ufujaji wa mali za ummah.

5. Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa imelipa madeni ya shilingi 67,325,972 ambayo hayakuorodheshwa katika madeni ya halmashauri kwenye ripoti ya fedha yam waka uliopita.
Agizo la 22(1) la randama za fedha za serikali za mitaa za mwaka 2009 linataka matumizi yanayostahili kulipwa yalipwe katika mwaka husika;na kama yasipolipwa yatakuwa deni ili kuepuka matumizi Zaidi katika mwaka unaofuata.
Kitendo cha kulipa fedha ambazo hazikuripotiwa kama deni kinaleta tafsiri mbili
(i) Watendaji walificha deni ili kutoonesha kuwa kuna fedha zimetumika kinyume na taratibu na hivyo kusababisha deni kwenye matumizi halisi ya serikali
(ii) Watendaji wanaandaa mwanya wa kuwa na matumizi ya ziada katika mwaka ujao wa fedha na hivyo kuvuruga dhana nzima ya kuzingatia bajeti zinazopitishwa na madiwa.
Hali hii ina akisi udhaifu mkubwa katika mfumo wa udhibiti wa matumizi na hivyo kutoa mwanya kwa watendaji wa serikali kufanya ubadhirifu wa fedha za ummah.

6.Matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa jimbo.

Kifungu cha 11(1) na (2) cha sharia ya mfuko wa jimbo sura ya 16 ya mwaka 2009 inaitaka kamati ya mfuko wa jimbo kuidhinisha mapendekezo yote ya miradi kutoka kata zote za jimbo na miradi mingine yeyote ambayo kamati inaona kuwa ina manufaa kwa jimbo. Fedha za mfuko wa jimbo zinapaswa kutumika katika miradi ya maendeleo ambayo imeibuliwa na wananchi.
Halmashauri ya manispaa ya lindi imetumia fedha za mfuko wa jimbo shilingi 66,095,139 katika miradi ya maendeleo ambayo haikuibuliwa na wananchi.
Aidha halmashauri ya wilaya ya liwale imetumia fedha za mfuko wa jimbo shilingi 37,347,071 katika miradi ya maendeleo ambayo haikuibuliwa na wananchi
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali amebaini kuwa fedha tulizoziainisha hapo juu hazikuzingatia utaratibu huu wa kisheria.
Mwenyekiti wa kamati ya jimbo ni mbunge wa jimbo husika.ni wito wetu kwa wabunge wa manispaa ya lindi kusimamia sharia kwa maslahi ya wananchi wanaowatumikia.

7. Halmashauri ya wilaya ya Nachimgwea ilikusanya shilingi 4,960,395 lakini hazikufikishwa benki.
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali amebaini kuwa halmashauri ya Nachingwea ilikusanya fedha tajwa hapo juu toka vyanzo mbalimbali lakini hazikupelekwa benki.
CAG ameshauri katibu mkuu ofisi ya rais Tamisemi awasiliane na vyombo vya uchunguzi ikiwa pamoja na TAKUKURU na jeshi la polisi kuhakikisha vinafanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki dhidi ya maofisa waliohusika.
Sisi tunaona kuwa huu ni wizi wa wazi na haulihitaji jeshi la polisi kusubiri maombi ya katibu mkuu ofisi ya rais Tamisemi ili wafanye uchunguzi.sheria ya makossa ya jinai (penal code) inatoa mamlaka kwa jeshi la polisi kufanya uchunguzi pindipo linapopata taarifa ya uhalifu.Taarifa hii ya CAG inatosha kumfanya DPP kuanzisha uchunguzi na kisha kuchukua hatua.

8. Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea imefanya uwekezaji usio na faida wa shilingi milioni 209.91 katika kituo cha redio na ujenzi wa vibanda katika kituo cha mabasi Nachingwea.
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali amebaini matumizi ya shilingi milioni 209.91 kwa kufanya mikataba ya ujenzi wa majengo ya maduka na ofisi ya kukatia tiketi ambayo yayana wapangaji kwa muda mrefu na kuanzisha kituo cha redio kilichosajiliwa kama kituo cha jamii ambacho hakijiendeshi kibiashara.
Ni wazi kuwa kutofanya upembuzi yakinifu ndiyo chanzo cha kuanzishwa kwa miradi hii inayoakisi matumizi ya fedha ya ummah yasiyojali vipaumbele na kuendelea kubebesha mzigo wa gharama wananchi. Tunaunga mkono pendekezo la CAG la kuitaka menejimenti ya halmashauri (a) kuboresha mazingira ya kibiashara katika kituo kipya cha mabasi ili kuvutia wafanyabiashara (b) ikigeuze kituo cha redio Nachingwea kuwa redio ya kibiashara ili iweze kufanya kazi bila kutegemea ruzuku ya halmashauri.

9. Ukusanyaji wa ushuru wa huduma bila kuthibitisha kiasi halisi cha makusanyo.
Halmashauri ya wilaya ya kilwa na Mtama zilikusanya ushuru wa huduma bila kupata ushahidi wa taarifa za mauzo ghafi kutoka mamlaka au taasisi husika ili kuthibitisha kiasi kilichokusanywa.kilwa ilikusanya shilingi 749,369,267 na mtama ilikusanya shilingi 73,167,756.
Kukusanya fedha toka taasisi bila ya uthibitisho wa kiasi halisi kilichokusanywa na taasisi hizo hakuwezeshi kutoa picha halisi ya makusanyo na hivyo kuwa mwanya wa kufanyika kwa ubadhirifu.Serikali izingatie ushauri wa CAG ili kudhibiti makusanyo katika ushuru wa huduma.


10. Halmashauri ya Mtama haikuhuisha taarifa za bajeti ya mapato katika mfumo wa mapato.
Aya ya 5.2 ya muongozo wa ukusanyaji mapato wa mamlaka za serikali za mitaa wa mwaka 2009,inazitaka halmashauri kuweka malengo yanayoweza kufikiwa huku ikizingatiwa mfumuko wa beiongezeko la watu na mabadiliko ya sheriana kanuni katika mwaka wa bajeti .pia kifungu cha 3.2.9.2 cha mwongozo wa mtumiaji (toleo la 0.2) la mfumo wa taarifa za mkusanyaji mapato wa serikali za mitaa(LGRCIS) kinahitaji bajeti ya kila chanzo cha mapato kuingizwa katika mfumo huo.
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali hakukuta taarifa za bajeti ya vyanzo vya mapato katika halmashauri yam tama ya shilingi 1,607,651,487.
Kitendo hiki kilicho kinyume na miongozo tuliyoinukuu hapo juu huondosha uwezekano wa usahihi katika taarifa za fedha.
Sisi tunaona kuwa huu ni mwanzo wa uholela wa kuanzisha makusanyo bila kujali kama yaliainishwa katika bajeti au laa ! ambapo pia hufanya kuwa na ugumu wa kupima umakini wa makusanyo kutoka katika vyanzo vya mapato ya halmashauri.
Pamoja na kuunga mkono ushauri wa CAG katika hoja hii ,sisi tunaona huu ni uzembe mkubwa wa kiutendaji ambapo wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Hitimisho
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ametuonesha kuwa kati ya fedha shilingi bilioni 17 zilizokusanywa na halmashauri sita za mkoa wa lindi ,shilingi bilioni 9 zina hoja za kiukaguzi.hii ni sawa na 52% ya fedha zilizokusanywa .Hii maana yake ni kuwa katika kila shilingi 100 zinazochangiwa na wananchi katika mkoa wa lindi shilingi 52 zipo hatarini kuibiwa ua zimeibiwa.
Mkoa wa lindi ni moja ya mikoa masikini sana hapa nchini .mapato yake ya ndani yana akisi shughuli za uzalishaji mali zinazofanyika.halmashauri iliyo na makusanyo mengi ni ya Nachingwea iliyokusanya shilingi 4,644,531,000 na ya mwisho ni manispaa ya lindi iliyokusanya shilingi 1,158,000,000 katika mwaka wa fedha ulioishia mwezi juni mwaka 2021 na kukaguliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.
Katikati ya umasikini huu wa kutupwa bado unakuta kile kipato kidogo walichonacho kinakutana na ubadhirifu,uzembe na hujuma za kutozingatia vipaumbele wala kufuata miongozo.
Tunatoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua watu wote waliobainishwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali katika ripoti hii.
Aidha tunatoa wito kwa wabunge na madiwani kuhoji na kusimama kidete dhidi ya ubadhirifu na uzembe ulioibuliwa na CAG. Tunawaagiza madiwani wetu wa ACT wazalendo kusimama kidete wakati wa kujadili ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.
Pamoja na uchache wao lakini wakijenga hoja madhubuti wanaweza kushawishi madiwani wengine au kuweka rekodi ya kupigania maslahi ya wananchi dhidi ya watendaji wa serikali wanaohujumu Mkoa wetu.

 

Imetolewa na:

Isihaka R.Mchinjita
Mwenyekiti ACT Waazalendo Mkoa wa Lindi

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK