UCHAMBUZI WA RIPOTI YA CAG YA MWAKA 2020/2022 : TUNAENDELEA KULIPIA GHARAMA ZA KUENDESHA NCHI GIZANI

 

UCHAMBUZI WA ACT WAZALENDO KUHUSU RIPOTI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA (CAG) UNAOISHIA MWEZI JUNI 2021.

 

Tunaendelea kulipia Gharama za kuendesha Nchi Gizani.

Ndugu Wanahabari,
,
A: Utangulizi

Chama cha ACT Wazalendo, chama ambacho kimeendelea kujipambanua kama chama mbadala, kinachojielekeza katika kujadili masuala makubwa ya kitaifa na kupendekeza suluhu yake. Mwaka huu, kinaendeleza utamaduni wake wa kufanya uchambuzi katika mambo muhimu machache kutoka kwenye Ripoti ya CAG 2020/2021.

Mapema mwaka huu, chama kiliazimia kuunda Kamati ya Kuisimamia Serikali na kuwateua wananchama wake katika sekta mbalimbali kama ‘Wasemaji wa Sekta’ mahususi. Uchambuzi huu wa ripoti ya CAG kwa miaka inayofuata utakuwa unafanywa na Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi. ACT Wazalendo Tutaendeleza utamaduni wetu wa miaka yote wa kufanya uchambuzi wa ripoti ya CAG kuhusu taarifa hii muhimu sana kwa nchi yetu na Watanzania kwa ujumla.

Kwa kuzingatia utamaduni wetu, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha taarifa yake kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021; Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, tumeijadili na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia kama nyenzo ya kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kwa nafasi yetu ya kuwa chama mbadala nchini na kama Chama cha Upinzani Bungeni.

Baada ya uchambuzi huu, tunatarajia kuwa mamlaka husika zitachukua hatua mahususi za kujibu hoja zote kwa mujibu wa sheria kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na hatimaye kusafisha Hesabu za Serikali. Hoja nyingi za ukaguzi zinajirudiarudia mwaka hadi mwaka, hivyo ni tunatoa rai kwa Bunge kuhakikisha kuwa Katiba na Sheria zinaheshimiwa ili kuondoa hoja sugu.

Kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku za nyuma, uchambuzi wetu utajikita kwenye mambo makubwa Kumi (10) ambayo tunaona ni muhimu Watanzania kuyatambua na kuyatolea mapendekezo ili yaweze kuchukuliwa hatua. Hii haina maana kuwa mambo muhimu ni hayo kumi tu, la hasha.
Ripoti za mwaka huu zina mambo mazito mengi sana. Waziri Mkuu Kivuli, ndugu, Dorothy Semu ameagiza Wasemaji wote wa Kisekta kuchambua kwa kina maeneo yanayogusa sekta zao na kutoa taarifa kwa Umma. Kwa uchambuzi huu tutajikita kwenye maeneo 10 tu.

 

UCHAMBUZI:

Kwa Mujibu wa ripoti hii ya CAG, thamani ya Jumla ya Hoja za Ukaguzi katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 kwa ujumla wake na kwa ripoti zote 3 kuu – Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ni Shilingi trilioni 5.8 ikilinganisha na mwaka 2019/2020 kwa ujumla wake thamani ya hoja za ukaguzi ilikuwa ni Shilingi Trilioni 3.6 na Dola za Marekani Milioni 596.

1. Fedha kutumiwa bila kupita Mfuko Mkuu wa Hazina limekuwa tatizo sugu.

Katika uchambuzi wetu wa mwaka 2021, tulionyesha kuwa kuna fedha za Serikali ambazo zimetumika bila kufuata utaratibu wa kikatiba, ambao unailazimu Serikali kupitisha mapato na matumizi yake kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina.
Katika mwaka wa Fedha 2019/20 Serikali ilitumia Shilingi Trilioni 2.2 bila kupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hoja kama hii ilikuwepo mwaka juzi na imejirudia tena mwaka huu japo kiwango cha fedha kimepungua.
Katika Mwaka 2020/2021 Jumla ya Matumizi yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.2 yalifanyika bila kupita Mfuko Mkuu. Kwa mujibu wa maelezo ya CAG, sehemu kubwa ya fedha hizi zilitokana na mikopo na misaada kutoka kutoka nje ya nchi.

Matumizi ya fedha za Serikali bila kupita kwenye Mfuko wa Hazina ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi yetu Ibara ya 135(1) ambayo inaelekeza kuwa ni lazima kila fedha ya Serikali itunzwe kwanza kwenye Mfuko Mkuu kabla ya kutumika na kuidhinishwa na CAG.

Ibara ya 135(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa;
“Fedha zote zitakazopatikana kwa njia mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa fedha za aina iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, zitawekwa katika mfuko mmoja maalumu ambao utaitwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali”.

Ibara ya 136(3) inamtaka CAG kuidhinisha kutolewa kwa Fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina. Hivyo Fedha ambazo zimetumika bila kwanza kupita Mfumo wa kikatiba, zinakosa idhini ya CAG na hivyo zinaweza kuwa zinatumika kinyume cha Bajeti na kinyume cha Sheria zilizotungwa na Bunge.
Pamoja na hayo, matumizi ya aina hii ni kichaka cha kuficha ubadhirifu kwani kutumia fedha namna hii kunamnyima CAG kufanya kazi yake ya Udhibiti wa Fedha za Umma.

Tutaonyesha mifano ya miaka minne tu ya Fedha ambazo hazikupita Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali;


Mwaka wa Fedha Fedha zilizotumika bila kupita kwenye mfuko mkuu
(Tshs)
2017/18 Bilioni 800
2018/19 Trilioni 1.7
2019/20 Trilioni 2.2
2020/21 Trilioni 1.2

Mwaka huu, licha ya kupungua kwa kiwango cha fedha kilichotumika bila kuingia Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, kwa umoja wetu kama taifa hatupaswi kukalia kimya uvunjifu huu mkubwa wa Katiba. Fedha hizi kutokupita kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ni kichaka cha kukwepa udhibiti wa CAG ili kufanya ubadhirifu.
Uvunjifu huu wa Katiba ulioshamiri miaka ya hivi karibuni unapaswa kukemewa kwa nguvu. Tunamtaka Waziri wa Fedha na Mipango ahakikishe kuwa taratibu zinafuatwa ili katiba kuheshimiwa. Hakuna dawa ya tatizo hili isipokuwa mamlaka kuheshimu Katiba ya nchi.

Niwakumbushe kuwa tangu mwaka 2015/16 CAG amekuwa akionyesha namna
Katiba haiheshimiwi katika kufuata utaratibu wa matumizi ya Serikali. Lakini pia, taarifa yake imeendelea kuonyesha jinsi mifumo ya udhibiti katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali haizingatiwi. Mwaka 2015/16 palikuwa na tofauti ya Shilingi Trilioni 2.9 katika masalio ya fedha kwenye hesabu jumuifu lakini Serikali haikuweka wazi (no disclosure) kiasi cha kusababisha hesabu jumuifu za Taifa kutokuwa sahihi na hii ilisababisha taifa kupata Hati Mbaya ya Ukaguzi.
Mwaka huu pia, Hesabu Jumuifu za Taifa zimepata hati yenye mashaka. Yote haya yanatokea kwa sababu ya kukosekana kwa mifumo madhubuti ya uwajibikaji kwani uvunjifu wa katiba ya nchi ni kosa kubwa linalostahili adhabu kubwa.

Tunarudia kuitaka Serikali kufuata Katiba kwa kufanya matumizi ya Fedha Mara baada ya kuwa zimepitia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa Fedha ambazo Wafadhili huzituma moja kwa moja kwenye miradi kupitia Wizara, Idara na Wakala za Serikali, taratibu za kihasibu zifanyike kwa ajili ya kuzitambua kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ili kumwezesha CAG kufanya Udhibiti na Ukaguzi kwa mujibu wa Katiba.

2. Madai ya Watumishi wa Umma Shilingi Bilioni 429

Katika kipindi cha miaka 7 sasa watumishi wa Umma wa Tanzania hawajapandishiwa mishahara licha ya gharama za maisha kuongezeka kwa kasi kubwa. Pamoja na madhila haya, hata kwenye stahiki zao za kisheria Serikali imewabania kama ambavyo imethibitishwa na CAG kuwa malimbikizo ya madai ya watumishi wa Umma yameongezeka.

Kwa mujibu wa Kanuni Na. 23 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma ya mwaka 2009, madai ya Watumishi yanatakiwa yalipwe mara tu yanapotokea. Hata hivyo, CAG ameonyesha kuwa madai yanayotokana na watumishi kutokulipwa kwa Wakati, malimbikizo ya mishahara ya waajiriwa wapya na waliopandishwa madaraja, makato na posho za watumishi yamefikia shilingi bilioni 429.

Ripoti ya CAG ya 2020/21 inaonyesha kuongezeka kwa madai haya kutoka Sh. bilioni 334.15 kwa mwaka wa fedha 2019/20 hadi Sh. bilioni 429.80 kwa mwaka huu wa ukaguzi ni sawa na ongezeko la 28%.

Hali hii inaondoa morali ya Watumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao wa kuhudumia wananchi wetu na ndio maana hata utoaji huduma nchini ‘service delivery’ umeendelea kuporomoka. Serikali isiyowajali watumishi wake ambao ndio wanaifanya iwepo itajali nini?

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iwalipe watumishi wote malimbikizo ya madai yao mara moja kwa mkupuo ili kuwawezesha kukabiliana na gharama za maisha ambazo zimeendelea kupanda miaka hii ya karibuni.

Pia, tunawasihi Watumishi wa Umma kupitia Vyama vya Wafanyakazi kusimama kidete kutetea maslahi yao bila ya woga. Miaka 7 ya mateso ambayo wamepitia inatosha na huu ni wakati wa Vyama vya Wafanyakazi kushikamana kuhakikisha kuwa haki zao zinapatikana, ACT Wazalendo itakuwa nao bega kwa bega katika mapambano yao.

ACT Wazalendo inapendekeza kuwa malimbikizo ya Madai ya Wafanyakazi yatambuliwe katika takwimu za Deni la Taifa na Serikali itazame uwezekano wa kuweka sokoni Bondi maalumu kwa ajili ya kupata Fedha za kulipa malimbikizo yote kwa mkupuo na kuweka mfumo mpya wa kuhakikisha kuwa hakuna madeni mapya yanayozalishwa siku za usoni.

3. Madai ya Wazabuni kwa Serikali yafikia Shilingi Trilioni 3.6

Uchambuzi wetu umebaini kwamba, mwaka 2020/2021 madai ya wazabuni kwa Serikali (accumulated libalities OR Payables) yalikuwa na jumla ya Shilingi Trilioni 3.6 kutoka Shilingi Trilioni 3.1 mwaka 2019/20. Madai ya Wazabuni dhidi ya Serikali yaliongezeka kwa shilingi bilioni 500 kutoka mwaka uliopita.

Hiki ni kiwango kikubwa sana cha Fedha za watu ambazo Serikali inazishikilia mkononi baada ya kupokea huduma za Wazabuni hao. Hali hii inasababisha mdororo wa uchumi, kwani Serikali inashikilia Fedha za wakandarasi, wafanyabiashara na watoa huduma na hivyo kudumaza shughuli za uzalishaji mali, na wakati mwingine kufukarisha wananchi.


Mwenendo wa Madai ya Wazabuni na Watoa Huduma kwa Serikali kwa miaka mitatu iliyopita ni kama ifuatavyo:


Mwaka wa Fedha Deni
(Tshs Trilioni)
2017/18 3
2018/19 2.7
2019/20 3.1
2020/21 3.62

Wizara zinazoongoza kwa madeni ya muda mrefu ni pamoja na:

- Wizara ya Ulinzi Shilingi Trilioni 1
- Jeshi la Polisi Shilingi Bilioni 641
- Wakala wa Barabara TANROADS shilingi Bilioni 705
- Wizara ya Afya Shilingi Bilioni 264
- Jeshi la Wananchi Shilingi Bilioni 314

Madeni haya ya muda mrefu pamoja na kuumiza wazabuni lakini pia yanazalisha riba na kuongeza mzigo wa madeni kwa Serikali. Pia, kitendo cha Serikali kutlipa watoa huduma wake kinapuguza mzunguko wa Fedha na kupelekea kudumaa kwa uchumi wa nchi.

Uchambuzi wa Ripoti ya CAG unaonyesha kuwa Madeni yanayodaiwa ndani ya miezi 12 mpaka Juni 2021 yalifikia Sh. 1.15 trilioni, ongezeko la 16%, hivyo, iwapo Serikali haitayashughulikia madeni haya kwa wakati yanaweza kusababisha kuongezeka kwa madeni ya muda mrefu na yataathiri sifa ya Serikali kwa wauzaji bidhaa.

Msisitizo wetu kama ACT Wazalendo ni kuwa Serikali ilipe madeni yote ya watoa huduma kwa mkupuo ili kuchangamsha Uchumi kwa kuongeza mzunguko wa Fedha.
Pia, Serikali iweke mfumo mzuri wa kulipa watoa huduma kwa wakati ili kuwasaidia kukuza shughuli zao na hivyo kuongeza ajira na kuondoa umasikini wa Wananchi.

Kwa kuwa madeni haya yanatambuliwa katika Deni la Ndani tunashauri uchambuzi wa kitaalamu ufanyike wa namna ya kulipa wadai kwa njia ya Hati Fungani maalumu na hivyo kuongeza ukwasi katika uchumi na vile vile kuwezesha Serikali kuhudumia madeni haya bila ya shinikizo kubwa katika mapato yake ya ndani.

Tunapendekeza pia kuwa Serikali ipange Bajeti katika Bajeti zake za nchi kila mwaka kulipa madeni ya nyuma kwa mfumo huo wa Hati Fungani na kuhakikisha kuwa inaepuka kutengeneza madeni mapya. Deni la Ndani lina madhara makubwa kwa shughuli za uchumi kwani Serikali inakuwa inashindana na sekta binafsi katika soko la madeni na kwa kuwa Serikali hailipi kwa wakati inaua shughuli za uchumi.

4. Ubadhirifu wa Shilingi Bilioni 279.5 katika miradi mbalimbali

Katika uchambuzi wetu tumebaini ubadhirifu wa thamani ya shilingi bilioni 279.5 kutoka katika miradi mitatu;
i. Ubadhirifu katika mradi wa ujenzi wa vihenge vya NFRA kuhifadhia chakula.
Uwezo wa Nchi yetu kuhifadhi chakula ni mdogo sana, tunaweza kuhifadhi nafaka mpaka tani 400,000 kwenye vihenge na maghala ya Taifa. Mwaka 2014 kulikuwa na mavuno makubwa ya mahindi kiasi kilichopelekea mahindi mengi kuoza kwa kunyeshewa na mvua kwa sababu ya ukosefu wa vihenge.

Baada ya janga hili, Serikali iliazimia kuanzisha mradi wa kukarabati vihenge vipya maeneo mbalimbali nchini kama vile Makambako, Songea, Iringa, Doodoma nk. Lengo likiwa ni kuwezesha Taifa kuhifadhi chakula kwa wingi ili kukinga mabaa ya njaa nyakati za ukame.

CAG katika ripoti yake amefanya ukaguzi kuhusu mradi huo ambao ulipaswa kukamilika mwaka 2017. Muda wa kukamilika ulisogezwa mbele mpaka Disemba 2020 lakini mradi huo haujakamilika. Kwa mujibu wa CAG wakandarasi wawili walipewa kazi, mmoja ya kukarabati maghala yaliyopo sasa, kampuni ya UNIA SP.2.00 kutoka Poland. Mkandarasi mwengine ni Kampuni ya FERRUM SA kutoka huko huko Poland. Mradi mzima uligharimu jumla ya shilingi Bilioni 134.2 na wakandarasi walilipwa 65% ya fedha zote za mradi.

Mradi huu haujakamilika mpaka leo na CAG alipotembelea maeneo ya mradi hapakuwa na dalili yeyote ya shughuli za mkandarasi. Kiufupi, kama Taifa tumepigwa shilingi bilioni 87.2 na HAKUNA Vihenge wala maghala. Inasikitisha sana kuwa Serikali imekubali kutapeliwa kwa uzembe wa kiwango hiki.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iwasiliane na Ubalozi wa Poland nchini ili kuwapata wakandarasi hawa na hatua stahiki kuchukuliwa na kuhakikisha mradi unakamilika. Poland ni nchi ya mwanachama wa EU na kuna taratibu kwa nchi za EU kuhusu wakandarasi wa namna hii. Serikali itumie njia za kidiplomasia kuhakikisha fedha za watanzania zinapata haki yake.
ii. Ubadhirifu kwenye bandari ya Tanga
Eneo jengine kubwa lenye ubadhirifu unaotisha ni kwenye Bandari ya Tanga. Hii imetokana na “Mkandarasi Mkuu” aliyepewa Kazi na Mamlaka ya Bandari kumpa kazi hiyo “Mkandarasi Mbia” kwa gharama ya chini na hivyo mkandarasi wa kwanza kupata faida ya shilingi bilioni 64.3 bila ya kufanya kazi.

Kwa maneno ya CAG mwenyewe “Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari iliingia mkataba na “Mkandarasi Mkuu” wa shilingi bilioni 172.36 tarehe 3 Agosti 2019 wa muda wa mwaka mmoja hadi kufikia mwezi Agosti 2020 kwa ajili ya kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli katika bandari ya Tanga, kufanya tathmini ya athari za kimazingira, na kununua vifaa kwa ajili ya shughuli za bandari. Kwa kulingana na mkataba, gharama ya kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli katika Bandari ya Tanga ilikuwa ni shilingi bilioni 104.92 (asilimia 60 ya bei yote ya mkataba). Hata hivyo, mnamo tarehe 1 Agosti 2019, “Mkandarasi Mkuu” iliingia makubaliano na “Mkandarasi Mbia” kwa ajili ya kazi ya kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia Meli kwa bei ya mkataba dola za marekani milioni 18.15 sawa na shilingi bilioni 40.46 kwa kipindi cha miezi 11 bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. Pia “Mkandarasi Mkuu” aliingia mkataba na “Mkandarasi Mbia” hata kabla ya kusaini mkataba wake na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)”.

Kuingia mkataba bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Bandari ilikuwa ni kinyume na Kifungu Kidogo cha 4.4 cha Masharti ya Jumla ya Mkataba kati ya Mamlaka ya Bandari na Mkandarasi Mkuu ambacho kinaizuia Mkandarasi Mkuu kutoa sehemu ya kazi kwa Mkandarasi mwingine, na ikiwa kuna uhitaji wa kutoa kazi kwa kampuni nyingine kutekeleza kazi zilizoko kwenye mkataba kuna taratibu za kisheria za kufuata.
Pia taarifa ya CAG inaonyesha, kazi ya iliyofanywa na “Mkandarasi Mbia” iligharimu fedha ndogo sana kulinganisha na mkataba aliokuwa nao. Hii inaonyesha dhahiri kulikuwa na makubaliano ya kifisadi kati ya wakuu wa Bandari na mkandarasi.

ACT Wazalendo tunataka hatua kali kuchukuliwa kwa Mkandarasi Mkuu kurejesha fedha zote za ziada na kupigwa marufuku kupewa zabuni yeyote nchini katika kipindi cha miaka 10. Vile vile maofisa wote wa Serikali na Mamlaka ya Bandari waliohusika na ubadharifu huu wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

iii. Ubadhirifu katika mradi wa Mkulazi bilioni 128.3

Mwaka 2019, TANROADS iliingia mkataba kinyume na utaratibu na sheria za nchi. Mkataba huo uliipa TANROADS mamlaka ya kusanifu, kuleta, kusimika na kuzindua mtambo wa kiwanda uliogharimu jumla ya shilingi bilioni 128.3. CAG alibaini mkataba huu haukuwa na vielelezo vya uhakiki wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama inavyotakiwa na kanuni ya 59(1) ya kanuni ya manunuzi ya umma ya mwaka 2013.

Aidha, kampuni ya Mkulazi haikuwa na jukumu la kusimamia mkataba huo kutokana na makubaliano ya awali kufanyiwa marekebisho na kuipa TANROADS mamlaka ya kusaini mkataba na kusimamia mradi huo.
Kiutaratibu, malipo kwa ajili hiyo hufanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa sekta Binafsi baada ya kupokea hati na nyaraka za malipo kutoka kwa wakala wa barabara.

Kutofuatwa kwa taratibu za manunuzi kulisababishwa na kukosekana kwa uwazi katika maandalizi ya zabuni, kuomba, tathmini na kutoa zabuni kunakoweza kusababisha hatari, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mitambo isiyokidhi viwango vinavyotakiwa, kununua mtambo kwa bei kubwa, kuchelewa kuletwa kwa mitambo uliionunuliwa na hivyo kushindwa kupata thamani ya fedha katika
mkataba huo.

 

5. Kuvunja Mikataba kiholela, kumesababisha nchi kupata hasara ya shilingi Bilioni 478

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwa na muenendo wa viongozi wa Serikali kusitisha kiholela mikataba ambayo taasisi za Serikali ziliingia na makampuni binafsi kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali.

Katika mwaka wa fedha 2020/21, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Idara ya Jeshi la Magereza walikatisha mikataba mitatu yenye thamani ya Sh. bilioni 126.55 kutokana na wakandarasi hao kutofanya kazi vizuri.

Pia, ripoti ya CAG kwenye Mashirika ya Umma imeonekana kuwa Serikali imebidi kuilipa kampuni ya symbion jumla ya dola za Marekani milioni 153.4 sawa na shilingi bilioni 352, kutokana na kitendo cha kuvunja mkataba wa kufua umeme na kampuni hiyo bila ya kufuata taratibu. Hasara hizi zimetokana na maamuzi ambayo hayazingatii sheria na kubebesha mzigo mzito Serikali hasa wananchi ambao kodi zao hutumiwa kulipia hasara hizi.

Hata hivyo CAG alibaini kuwa taasisi hizo hazikufuata taratibu za kusitisha mikataba kulingana na matakwa ya mikataba, ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro na kuomba ushauri wa kisheria kutoka kwa mamlaka husika ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hatua hizi za uholela zimesababisha hasara kubwa kwa Serikali.


ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuheshimu mikataba na kufuata taratibu za sheria kama inatakiwa kusitisha mikataba husika ili kuepeuka hasara kama hizi. Taasisi za Serikali ziepuke kufanya maamuzi bila kwanza kupata ushauri wa kisheria wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Watanzania wamechoka kubebeshwa mizigo inayotokana na maamuzi ya holela yanayofanywa na viongozi kwa maslahi yao. Watanzania wamechoka ndege zao kukamatwa ughaibuni na kupata aibu ya kudaiwa kwa sababu tu viongozi wao wamefanya maamuzi kiholela.

Tunamtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali atoe waraka wenye ushauri na maelekezo ya kisheria kwa Taasisi zote za serikali na Mashirika ya Umma. Kwanza, kusitisha hatua zozote ambazo wamezichukua au kupanga kuzichukua kuhusu mikataba mpaka kwanza kuwasiliana na Ofisi ya CAG ili kupata ushauri na pale ambapo kuna migogoro ya kimkataba juhudi zifanyike ili kutatua kwa mazungumzo kwa lengo la kuepuka hasara ambazo zitatokana na maamuzi ya kuvunja mikataba.


6. Wizi mkubwa wa Shilingi Bilioni 71 Mamlaka ya Bandari Tanzania

CAG alifanya ukaguzi maalumu katika Mamlaka ya Bandari Tanzania na kubaini ubadhirifu wenye thamani ya shilingi Bilioni 71. Ubadhirifu huu ulihusisha haswa Bandari ya Mwanza na Bandari ya Dar es Salaam ambapo fedha za umma zilikuwa zinahamishwa kupelekwa Mwanza na kutumiwa bila kufuata taratibu.

Kwa mfano, Ukaguzi wa taarifa za benki zilizowasilishwa na uongozi wa TPA ulibaini kuwepo kwa miamala 157 yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 34.67 ya kuhamisha fedha kutoka Makao Makuu ya Mamlaka ya Bandari Tanzania kwenda Bandari ya Mwanza. Katika ukaguzi huo CAG hakuona ushahidi wa maombi ya kuhamisha fedha shilingi bilioni 22.6 zilizotumwa kwenda Mwanza.

Pia, kukosekana kwa ushahidi wa idhini ya kuhamisha fedha Shilingi Bilioni 24.29 zilizotumwa Bandari ya Mwanza Kati ya miamala 157 ya kuhamisha fedha. CAG kaonyesha miamala mingi zaidi ambayo haina nyaraka wala uthibitisho wa matumizi yake kwa shughuli za Umma kwenda Bandari ya Mwanza.

Fedha hizi zilikuwa zikihamishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kati ya mwaka 2015 na 2020. Zilikuwa zinapelekwa kufanya nini hakuna anayejua. Hata CAG hajatoa majibu yanayoridhisha katika eneo hili.


7. Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere

Mwaka jana tulifanya uchambuzi kuhusu Mradi wa kuzalisha Umeme wa bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambapo CAG alibainisha hoja nzito ambazo tulisema zinaonyesha kuwa mradi huu wenye kugharimu shilingi trilioni 6 unatekelezwa kwa uholela mkubwa.

Hoja kubwa ambayo tulihitaji mjadala mpana, tena mjadala wa kitaalamu ni ile ya kazi ya ushauri wa mradi kufanywa na taasisi ya Serikali. Mradi huu unatekelezwa na Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kupitia kitengo cha (TECU) ambaye ni mhandisi mshauri anayesimamia mradi. TECU ni TANROADS.
Katika Ripoti ya CAG ya mwaka huu tunaona ndani yake kazi ambazo TANROADS walizifanya kwa sekta ambazo hawahusiki nazo na zimeleta ubadhirifu mkubwa ikiwemo Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi na hata Uwanja wa Ndege wa Chato. Miradi yote ambayo TANROADS wamehusika ina hoja za ukaguzi zenye dalili UBADHIRIFU MKUBWA.

Katika Ripoti ya Mwaka huu pia CAG ametoa hoja za ukaguzi kuhusu Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere. CAG amesema katika Taarifa yake kuwa kucheleweshwa kwa ukamilishwaji wa mradi kutaligharimu zaidi taifa (kuongeza muda wa utekelezaji na fedha kwa wakandarasi na washauri); Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mradi wa kufua umeme katika Bwawa la Nyerere umefikia asilimia 48.02 hadi Disemba 2021 tofauti na matarajio ambayo ilitakiwa kufikiwa asilimia 94.7.

Ujenzi ulipangwa kukamilika kwa muda wa miezi 42 sawa na miaka mitatu na miezi sita kuanzia 15 Disemba 2018 na kumalizika 14 Juni 2022. Lakini hadi sasa utekelezaji wake upo kwenye 48%, jambo ambalo litapelekea kuongezwa kwa muda na fedha zaidi ili kufikia malengo. Muhimu zaidi ni kuwa Fedha za wananchi wa maeneo ya Rufiji hazijatolewa.

Taarifa inaonyesha kuwa Mkandarasi kutotoa gharama ya uchangiaji wa maendeleo kwa jamii kiasi cha shilingi bilioni 196.5 hadi leo na muda wa mkataba unaenda kumalizika. Ni kwanini Serikali imekalia kimya jambo hili la kimkataba? Mkataba wa Ujenzi unataka kuwa 3% ya gharama zote za ujenzi zitakwenda kama Corporate Social Responsibility kwa Wananchi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo Mradi huu upo. Hebu Fikiria shilingi bilioni 196 za watu wa Rufiji na Wilaya zingine ambazo zinaguswa na mradi zingebadili namna gani maisha ya watu wetu.

ACT Wazalendo inawashauri Wabunge na Madiwani kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazoguswa na Mradi wa Bwawa la Nyerere wakutane na Mkandarasi kuweka makubaliano ya namna zitakavyolipwa Fedha zao ili waweze kutekeleza masuala ya maendeleo katika maeneo yao.

Vile vile tunaitaka Serikali kufanya marejeo ya mradi huu na kupendekeza namna bora zaidi za kuutekeleza ili kuwa na manufaa kwa nchi yetu.

8. Madai na Madeni ya Mashirika ya Umma

Katika Ripoti ya Mwaka huu CAG ameeleza kwa kina hali ya mashirika ya Umma nchini. Ameeleza kuwa katika Mashirika ya Umma 200 aliyoyakagua, mashirika 45 ni ya biashara na yaliyosalia ni ya huduma. Vile vile ameeleza kuwa Serikali ilitoa ruzuku ya Jumla ya Shilingi trilioni 5.9 kwa Mashirika ya Umma.

Hizi ni taarifa muhimu sana katika kufanya tathmini ya kuona kama nchi yetu inafaidika na Mashirika ya Umma au la. CAG pia ameonyesha mashaka yake makubwa katika suala zima la ukusanyaji duni wa madai ya Mashirika ya umma uliopelekea kuwa na madai kwa mashirika 93 kiasi cha shilingi Trilioni 3.71 na hivyo kuchelewesha maendeleo ya mashirika hayo katika kuchochea ukuaji wake na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Madai ya shilingi trilioni 3.4 ya mashirika ni kwa mashirika mengine ambapo kampuni binafsi kiasi cha Sh. Trilioni 1.45 na mashirika ya Serikali kiasi cha Shilingi Trilioni 1.97. Madai haya yanaathiri mtiririko wa fedha katika taasisi hizi, na hivyo kusababisha kutotekelezwa kwa shughuli zilizopangwa za mashirika yenyewe. Tunapendekeza kuwa Taasisi za Serikali zinazodaiwa na Mashirika ya Umma zilipe na kumaliza madai haya mara moja.
Kuhusiana na madai kwa kampuni binafsi tunashauri kuwa hatua za kisheria zichukuliwe ili kukusanya madeni.

Hata hivyo CAG ameonyesha pia kuwa Mashirika ya Umma yanadaiwa jumla ya shilingi trilioni 7.9 na taasisi mbalimbali na kampuni binafsi. Madeni haya ambayo hayajalipwa kwa zaidi ya mwaka mmoja yameongezeka kwa 16% kutoka mwaka 2019/20. Hii ni takribani madeni kutoka kwenye mashirka 71.

Tunaitaka Serikali ifanye tathmini ya kina ya Mashirika ya Umma ili hatua stahiki zichukuliwe kuondokana na mashirika ambayo hayana sababu za kuwepo na kuimarisha yale ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu.


9. Mchwa wamejaa tele Serikali za Mitaa

Katika uchambuzi wetu wa taarifa ya CAG tumebaini moja wapo ya chanzo cha hasara katika Halmashauri zetu nchini zinatokana na uwepo wa mianya na udhaifu katika mifumo iliyowekwa kuratibu makusanyo ya mapato ya Halmashauri kupitia Mawakala, Watumishi na mashine za kukusanyia mapato, POS. Baadhi ya watumishi na mawakala wamekuwa wakitumia mbinu za udanganyifu, kinyume na utaratibu na mifumo ya ukusanyaji mapato kwa mbinu za kughushi stakabadhi, kutokuwasilisha mapato kwa njia rasmi na kutumia njia za dirisha la nyuma kufanya makusanyo.

Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam – Manispaa ya Ilala, ilipata hasara ya Bilioni 10.3 ambazo hazikuwasilishwa na mawakala na watumishi kwenye Halmashauri. Watumishi na Mawakala hao walitumia mbinu ya kubadili taarifa za mfumo wa kutoa stakabadhi.

Pia, uchambuzi wetu umebaini hasara kwenye Halmashauri zetu zinasababishwa na udanganyifu wa maafisa wa Halmashauri kwenye ufanyaji malipo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali. Njia ambazo watumishi hutumia kusababisha hasara hizi ni; kufanya malipo zaidi ya gharama halisi za miradi, kufanya malipo hewa kwa kutumia mbinu ya kulipa fidia kwa watu hewa na ukosefu wa umakini pale Halmashauri zinapoingia ubia na Wakandarasi ambao huwa chini ya viwango na kusababisha hasara.

ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Serikali ichukue hatua kali kwa Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa upotevu mkubwa wa mapato ambao umetokana na wizi kupitia mashine za kukusanya mapato. Vile vile Serikali iimarishe mfumo wa makusanyo ili kuziba mianya kama hii nchi nzima.

 

10. Hali mbaya ya kifedha ya Mifuko ya PSSSF na NSSF

Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG tumebaini kuwa kwa mwaka 2020/21 mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) ulilipa gharama za mafao pensheni kuzidi mapato ya michango kwa shilingi bilioni 767. Hali imekuwa hivi kwa miaka mitatu mfululizo 2018/19 (bilioni 307) na 2019/20 mafao yalizidi mapato yatokanayo na michango kwa bilioni 232.

Mwenendo huo wa mfuko wa PSSSF, utapelekea kupoteza uwezo wake wa kuwahudumia waastaafu wetu. Hivyo tunaitaka serikali kukamilisha malipo ya deni lake la trilioni 2.45 ikiwa sehemu iliyobaki ya deni la michango ya serikali kwa watumishi kabla ya mwaka 1999.

Mifuko ya Hifadhi ya jamiii (PSSSF na NSSF) kuidai serikali na taasisi zake Mikopo ya Sh. Trilioni1.5
Pamoja na madeni yanayoikumba mifuko hii, bado serikali na taasisi zake imeendelea kukopa na kuchelewesha kulipa madeni inayodaiwa. Uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG imeonyesha kuwa kuna deni la trilioni 1.5 ikiwa ni mikopo isiyolipwa na serikali na taasisi zake mbalimbali. NSSF inadai 1.17 trilioni (Mkopo 490.16 bilioni na riba 684.42 bilioni) na PSSSF inadai 323.98 bilioni. Madeni haya yana muda mrefu kati ya mwaka 1 hadi 15.
Serikali, taasisi na mashirika zilipe deni hili la mikopo iliyochukuliwa kutoka kwenye mifuko hiyo ili kuwezesha PSSSF na NSSF kufanya kazi zake lengwa kwa ufanisi.

C: Hitimisho

Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2021 umeibua hoja nyingi za ukaguzi ambazo tusingeweza kuchambua zote. Ilikuwa wakati mgumu sana kuamua hoja ipi tuichambue na ipi tuache. Hata hivyo, tumeamua kuwa Wasemaji wa Kisekta wa chama watazichambua katika Taarifa zao za kibajeti.

Ripoti ya Mwaka huu inaumiza moyo sana hasa kutokana na ubadhirifu ambao unaepukika isipokuwa tu kwa kuwa nchi ilikuwa gizani hapakuwa na nafasi ya kufanya hivyo. Ubadhirifu katika Miradi kama ya Mkulazi ambayo tumeeleza katika uchambuzi wetu ama maamuzi kuhusu zao la Korosho ambayo yamepelekea uzalishaji kuporomoka kwa kasi au wizi katika bandari ya Tanga ambao tumeona katika uchambuzi huu ni mambo yanatia simanzi mno.
Kwa kuwa Ripoti hii ipo wazi kwa Umma ninawasihi Watanzania waisome kwa kina na kuendelea kuichambua kila mtu kwa namna yake anayoona inafaa. Sisi ACT Wazalendo tutaitumia kama nyenzo ya kuisimamia Serikali katika shughuli zetu kama Chama Cha Siasa cha Upinzani.

Ripoti ya Mwaka huu imeendelea kudhihirisha kiwango kikubwa cha uholela katika uendeshaji wa Serikali na haswa katika usimamizi wa Fedha za Umma na uendeshaji wa Miradi.

Gharama ya uendeshaji wa Nchi kwenye giza ndio hizi tunazoziona katika Ripoti ya CAG. Hoja hizi za Ukaguzi ni sehemu ndogo sana ya uvundo mkubwa uliopo katika nchi yetu.

Ahsanteni Sana.


Imetolewa na;
Emmanuel Lazarus Mvula
Waziri Kivuli, Fedha na Uchumi - ACT Wazalendo
Aprili 14, 2022

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK