Udini na Ukabila havina nafasi kwa Tanzania. Agizo la Msajili wa Hazina lisitishwe.

MAONI YA ACT WAZALENDO KUHUSU AGIZO LA MSAJILI WA HAZINA KUWATAKA WATUMISHI WA UMMA WAWASILISHE WASIFU (CV) ZENYE KUONYESHA DINI NA KABILA IKIWA NI JAMBO LENYE MASHAKA KATIKA UPATIKANAJI WA HAKI.

Utangulizi

Chama cha ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Kisekta Wizara ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Muungano kinatoa msimamo wake juu ya tamko la Msajili wa Hazina Ndugu Eric Mkuki la kuwataka watumishi wa umma kuwasilisha wasifu wao (CV) wenye kipengele cha dini na kabila, jambo ambalo linasababisha hali ya wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi na linazua mashaka katika upatikananji wa haki.

Utaratibu huu ulitumika wakati wa ukoloni na ulijaa ubaguzi na kukosekana haki katika ajira, hivyo kipengele hicho cha dini na kabila la mtu katika utumishi wa umma kiliondolewa kwa lengo la kuleta haki na usawa katika ajira.

Agizo la Msajili wa Hazina linaenda kinyume na kifungu cha 7(4) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazii ya mwaka 2019, inayokataza ubaguzi dhidi ya mfanyakazi katika sera yoyote ya ajira au utendaji katika ya rangi, utaifa, kabila au mahali alipotokea, uasili, uasili wa taifa, uasili wa kijamii, mtazamo wa kisiasa au dini.

Tamko la Msajili wa Hazina linaleta hali ya wasiwasi kama serikali ina mpango wa kuzingatia dini na kabila la mtu katika kupandisha vyeo au kuwapa fursa watumishi. Vile vile, uharaka wa jambo hili unaongeza utata na wasiwasi kwa baadhi ya watumishi.

Kitendo cha serikali kuendelea kuwaomba watumishi wa umma taarifa hizo mara kwa mara inaashiria uwepo wa usimamizi mbovu wa kuhifadhi nyaraka katika Ofisi ya Msajili wa Hazina akiwa kama mlezi wa taasisi na mashirika ya umma jambo ambalo linaashiria kukosekana kwa ufanisi wa utendaji wa kazi serikalini katika sekta ya utumishi wa umma.

ACT Wazalendo tunaamini kuwa tamko la Msajili wa Hazina linaleta mashaka katika upatikanaji wa haki. ACT Wazalendo tunaamini katika haki na usawa kwa watumishi wote wa Umma kama sheria za nchi zinavyotaka kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 13(1) (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kuwa: -

‘’Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria’’.

‘’Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.”

ACT Wazalendo tumeainisha madhara yanayoweza kuletwa na agizo la Msajili wa Hazina ikiwa ni pamoja na kuleta utenganishi au upendeleo kwa atumishi wa umma kutoka katika misingi ya uasili, rangi, jinsia, dini, mtizamo wa kisiasa, uasili wa kitaifa au jamii, hivyo kuzuia au kunyima usawa katika fursa za kazi au ajira.

Vile vile, agizo hili linaweza kuleta unyanyapaaji wa mfanyakazi au mtumishi wa umma katika sehemu za kazi kutokana na udini na ukabila wa mtu au mtumishi wa umma.

Iwapo serikali itaruhusu agizo hilo la Msajili wa Hazina, basi linaweza kuwa hatari kwa usalama wa nchi na kuweza kuligawa taifa kwa misingi ya dini na ukabila.

Mapendekezo Yetu:

• Tunatoa rai kwa serikali kusitisha mara moja agizo la Msajili wa Hazina kutaka watumishi wa umma watambulike kwa dini na makabila yao. Agizo hilo ni hatari kwa mustakabali wa umoja na utengamano wa taifa letu.

• Kuhusu suala la kuwaagiza watumishi wa umma kuwasilisha wasifu (CV) wao mara kwa mara, ni vyema serikali ikawa na utaratibu wa kutunza nyaraka kielektoniki na kuwe na usimamizi mzuri.

Sisi ACT Wazalendo kupitia ilani yetu ya chama ya 2020 kurasa ya kumi na sita na kumi na saba tulilenga kubadilisha kabisa mfumo na utendaji wa Tume ya Maadili ya Umma ili kuipa nguvu na nyenzo za kusimamia kikamilifu maadili ya utumishi wa umma, kwa kuweka utaratibu wa kisheria utakaoelekeza uteuzi wa Viongozi wa Tume hii kufanywa na Tume ya Kijaji, chini ya Jaji Mkuu na kufanyiwa usaili na kuthibitishwa na Bunge/Kamati ya Bunge ili kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi na siyo kwa viongozi wachache wanaowateua.

ACT Wazalendo tupo tayari kutoa ushirikiano na mawazo katika kuiimarisha sekta hii ya utumishi wa umma kwani sote tunajenga nyumba moja.

Imetolewa na:

PAVU JUMA ABDALLA
Msemaji wa Kisekta,
Wizara ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Muungano.

24 Februari, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK