Ukatili dhidi ya Wanawake, Wazee na Watoto ni janga. Lipatiwe ufumbuzi.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.


HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MAENDELEO YA USTAWI WA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO- ACT WAZALENDO NDG. JANETH J. RITHE KUHUSU MPANGO NA BAJETI YA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUMU KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.

Utangulizi
Jana tarehe 30 Mei, 2022 Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), aliwasilisha Bungeni mpango wa wizara na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/23. Bunge lilipokea, kujadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya shilingi bilioni 43.4, kati ya hizo shilingi bilioni 32.31 ni fedha za matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 11.09 ni kwa ajili ya miradi ya Maendeleo. Katika kuendeleza utaratibu wetu wa kufanya uchambuzi wa kila bajeti ya wizara. Sisi, ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Wasemaji wa kisekta ya kuisimamia, mimi Janeth Joel Rithe ambaye ni Msemaji wa Sekta ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto nimesikiliza na kuichambua hotuba na kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa bajeti za wizara hii kwa miaka iliyopita. Ninafahamu kuwa wizara hii changa lakini katika mfumo wa kibajeti ilikuwa inategemewa bajeti kupitia fungu la 53 wakati ikiwa kama idara kuu katika wizara ya afya.
Hivyo basi, katika hotuba yangu nimeweka hoja kuu nane (8) kuhusu mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwenye wizara hii kwa mwaka wa 2022/23.
1. Ufinyu wa bajeti unaifanya wizara kubaki kuwa ni idara
Pamoja na wadau mbalimbali kupokea kwa furaha hatua za uundwaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. Mpango na makadirio ya mapato na matumizi yaliyowasilishwa jana bungeni na Waziri inaonyesha wazi kuwa erikali haijajiandaa kuifanya hii ni wizara itakayoweza kukabiliana na changamoto ambazo hapo awali zilishindikana. Ni wazi kuwa bajeti ni nguzo muhimu sana katika kuhakikisha vipaumbele na mipango iliyowekwa inatekelezwa.
Ukitazama, katika mwaka huu bajeti iliyoidhinishwa na bunge ni shilingi Bilioni 43.4 kiasi ambacho ni pungufu kwa asilimia 5.6 kwa kulinganisha na bajeti ya mwaka 2021/22 (ambayo ilikuwa sh, bilioni 45.97) wakati ikiwa ni idara kwenye iliyokuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake, wazee na watoto. Aidha, kwa kulinganisha kiasi kilichotengwa kwa ajili ya wizara hii na bajeti kuu ya Serikali ni sawa na asilimia 0.11 pekee kwa mwaka huu. Kati ya fedha zote, fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ni kiasi cha shilingi Bilioni 11.09 sawa na asilimia 25 ya bajeti ya wizara ikiwa ni kiwango pungufu kwa bilioni 3.81 ukilinganisha na fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo mwaka 2021/22 ambapo ilitengwa bilioni 14.90 upungufu huu sawa na asilimia 25.5.


Hivyo basi, ufinyu huu wa bajeti unaipotezea Serikali uhalali wa kuifanya hii ni wizara inayojitegemea ikiwa mpango wake, vipaumbele na utengaji wa bajeti unafuata mwenendo ule ule kama ilivyokuwa ni idara kuu kwenye wizara.
ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo kwenye wizara hii ambayo inashughulikia mafunzo ya uanagenzi, uhamasishaji wa Maendeleo na uratibu wa fedha za mikopo ya vijana, wanawake na walemavu.


2. Uhaba mkubwa wa maafisa ustawi na Maendeleo ya jamii
Uhaba wa rasilimali watu kwenye sekta hii muhimu unapelekea kushusha ufanisi wa utendaji na kukwamisha utekelezaji wa mipango na majukumu.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara kupitia hotuba ya bajeti mwaka 2022/23, Waziri anaonyesha upungufu mkubwa wa maafisa wa ustawi na maafisa wa Maendeleo ya jamii hususani katika ngazi ya vijiji na kata. Taarifa zinaonyesha kuwa mahitaji ya maafisa Maendeleo ya jamii ni watumishi 5,296 idadi ya maafisa waliopo kwa sasa ni 3,014, kwahiyo kuna upungufu wa maafisa wa Maendeleo ya jamii 2,282 sawa na asilimia 43. Kwa upande wa maafisa wa ustawi wa jamii wanaohitajika ni 23,135 waliopo ni 740 na kufanya upungufu wa watumishi 22,395 sawa na asilimia 97 ya upungufu.
Katika bajeti ya mwaka huu hakuna kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kuajiri maafisa wa ustawi na Maendeleo ya jamii ili kukabiliana na upungufu uliopo. Waziri, Dkt. Gwajima ameishia tu kutaja changamoto bila kutenga fedha kukabiliana na changamoto yenyewe.


ACT Wazalendo, tunaishauri Serikali kuweka mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo kwa awamu ya miaka minne kwa kuhakikisha inatoa ajira kwa wastani wa watumishi 6,169 kila mwaka.
3. Ukatili dhidi ya wanawake, wazee na watoto
Vitendo vinavyosababisha athari za kimwili, kingono, kisaikolojia au mateso kwa wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na kutishiwa maisha, kunyimwa uhuru, iwe hadharani au kwa kificho vinazidi kuongezeka nchini kwetu. Ukatili dhidi ya wanawake kupitia mitandao ya kijamii, ubakaji, ukeketaji, vipigo kwa wanandoa, mauaji ya wanawake na watoto imekuwa ni jambo linaloonekana kuzoeleka nchini. Pia, matukio ya ulawiti na ubakaji kwa watoto vinazidi kushamiri tena vitendo hivyo vinafanywa na watu wao wa karibu kabisa, baba mzazi, baba wa kambo na ndugu wa karibu (walezi wao).
Utafiti ulifanywa mwaka 2021 wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF – Tanzania) na Shirika la ECPAT International na INTERPOL unaonyesha kuwa asilimia 4 ya watumiaji wa mtandao wenye umri wa miaka 12 – 17 nchini Tanzania ni manusura wa ukatili wa mtandaoni; watoto wengi hufanyiwa vitendo vya ukatili kupitia mitandao ya kijamii kama vileWhatsApp, Instagram, Facebook, Tik Tok, wanaofanya vitendo vya ukatili ni watu wanaofahamika na watoto wakiwemo Ndugu wa karibu na marafiki. Aidha watoto wanaofanyiwa ukatili hawajui namna na sehemu ya kutoa taarifa ili wapate msaada.
Pamoja na takwimu za Jeshi la Polisi kuhusu Hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani kuonesha kupungua kwa matukio ya ukatili yaliyoripotiwa mwaka 2021 ikilinganishwa na miaka iliyopita, bado tumeendelea kushuhudia matukio ya vitendo vya ukatili mara kwa mara kwenye vyombo vya habari hususan kupitia mitandao ya kijamii. Aidha, ripoti ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa ni dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo vilirikodiwa visa 5803, hii ikiwa ni sawa na visa 615 kwa mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa watoto nchini.
ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuweka mikakati Madhubuti ya kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto, hasa ukatili wa kingono, kimwili na udhalilishaji kwenye mitandao kwa kuboresha madawati ya jinsia, kuweka mifumo rahisi ya kuripoti na kudhibiti ukatili. Pia, tunaishauri Serikali kuunda tume maalumu ya kudhibiti ukatili wa kijinsia na kuhakikisha vyombo vya mahakama vinawezeshwa kimafunzo na kimfumo ili kusimamia kesi za ukatili kwa haraka na uhakika.

4. Kuongezeka kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
Ni jambo linalosikitisha kuona kasi kubwa ya kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingitra hatarishi kila mwaka. Serikali haionekani kustushwa na ongezeko hili lisilo la kawaida na kuchukua hatua stahiki kuondokana na tatizo lenyewe.
Tanzania imeridhia kutekeleza Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Mtoto (UNCRC). UNCRC ni chombo cha kisheria ambacho kinaelekeza na kinasisitiza haki za msingi za watoto duniani pote na hii inahusisha, haki ya kuishi, kujiendeleza/kuendelezwa kwa kadiri ya uwezo wa mtoto, kulindwa dhidi ya madhara na mazingira yanayoweza kumdhuru, kumnyanyasa na kutumiwa kwa njia ya kudhulumiwa; kushiriki kikamilifu katika maisha ya kifamilia, kitamaduni na kijamii.
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi imefikia jumla ya watoto 218,369 (Me 85,699 na Ke 132,670) hawa ni wale tu waliotambuliwa na wizara kati ya 2,398,354 wanaoishi katika mazingira magumu nchini. Katika mwaka huu bajeti iliyotengwa na wizara kiasi cha Bilioni 2.6 kwa ajili ya kukabiliana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na ukarabati wa mahabusu za magereza ya watoto. Utengwaji wa bajeti hauzingatii kiini kinachosababisha kuwepo kwa watoto wa mitaani na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Tunaishauri Serikali kuja na mpango wa kumaliza migogoro ya wanandoa, kukabiliana na umaskini na kusimamia huduma bure za afya, lishe na makazi bora.


5. Kasi ndogo ya Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi
Waziri imetoa Takwimu kuwa jitihada za Serikali za kuwezesha wanawake kiuchumi kwa katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya wanawake wajasiriamali 1,167 wamejengewa uwezo kupitia mafunzo yaliyotolewa katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Katavi na Tanga na takribani kiasi cha shilingi Bilioni 16.1 zilitumika kuwawesha wanawake hao.
Inasikitisha sana kwa Serikali kutangaza kuwezesha wanawake 1,167 nchi nzima. Kwa Mwenendo huu Serikali inaweza kuchukua zaidi ya miaka mia moja kukamilisha malengo ya kuwainua wanawake wote wapatao milioni 29.8.
Ni muhimu suala la uratibu wa uwezeshwaji wa wanawake nchini utengenezewe mwongozo na utaratibu utakaotumika ili kila mwanamke anapohitaji msaada ajue utaratibu utakaomwezesha kupata msaada kwa haraka na uhakika.

6. Huduma bora za afya na uzazi salama kwa wajawazito na mama na watoto.
Mazingira rafiki ya huduma za uzazi ni haki ya kila mwanamke na mtoto. Sera ya kutoa huduma za afya bure kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano (5) na wazee, ni kiini macho tu, yaani haitekelezwi kwa ufanisi. Kutotekelezwa kwa ufanisi unachangia pia kutokana na uhaba wa Miundombinu ya msingi katika vituo vya afya (zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na hospitali za rufaa za Mikoa). Aidha ukosefu wa vituo vya afya kwenye baadhi ya vijiji vinafanya umbali mrefu kufikia huduma za afya jambo linalosababisha wajawazito kujifungulia njiani, kukosa huduma bora na salama za uzazi na vifo vya mama wajawazito. Takwimu za wizara zilizo kusanywa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinaonesha vifo vitokanavyo na uzazi kuwa 1,580 mwaka 2021. Na hii, haijumuishi vifo zinavyotokea kwa ngazi ya jamii.
Pamoja na hali hiyo, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wenye miaka zaidi ya 60 wana haki ya kupata matibabu bure kwa mujibu wa sera ya matibabu bure kutoka katika vituo vya afya vya Serikali.
Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa na changamoto kubwa, tathmini yetu inaonyesha kuwa wastani wa asilimia 40 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanalazimika kulipia matibabu. Vilevile, kwa wajawazito wanalipishwa matibabu na inatokea hivyo kwa watu wenye miaka zaidi ya 60 hulazimika kulipia huduma hizo tofauti na utaratibu uliopo.
Tunaitaka Serikali ifuatilie kwa makini utekelezwaji wa sera hii ili kuhakikisha kuwa walengwa – ambao ni watoto, wajawazito na wazee wanapata haki zao za msingi.

7. Kuongezeka kwa matukio ya mauaji na vifo vya wanandoa na wanajamii.
Hali ya usalama ya wananchi hususani wanandoa na watu wenye uhusiano wa kimapenzi imezidi kuwa katika hali mbaya kwa takribani mwaka. Ndani ya mwezi Mei, 2022 kumeripotia zaidi ya matukio makubwa 8 ya mauaji ya wapenzi au wanandoa ama wanafamilia kwa sababu za wivu wa kimapenzi au kukosa maelewano katika ndoa/familia.
Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2021 watu 15,131 walifanyiwa ukatili wa kijinsia huku ripoti hiyo ikionyesha ongezeko la mauaji kwa wanawake walio katika ndoa.
Vilevile, ripoti iliyotolewa Septemba 2021 na jarida la Afrika kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia Tanzania miongoni mwa wanandoa, imeonyesha kuwa, asilimia 46 ya wanandoa hufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambapo asilimia 36 walifanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 32 walifanyiwa ukatili wa kisaikolojia na asilimia 13 walifanyiwa ukatili wa kingono.
ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kupitia jeshi la polisi kuimarisha uwezo wa kubaini matukio ya uhalifu na kuweka mazingira rafiki ya waathirika wa vitendo hivyo kutoa taarifa na taarifa kufanyiwa kazi.

8. Mazingira magumu ya wafanyabiashara wadogo na ushirikishwaji katika utungaji wa sheria ya Wamachinga.
Tumesikiliza hotuba ya waziri, tumeona mikakati iliyowekwa kuhusu wamachinga ni kwa ajili ya kuimarisha ofisi za viongozi wa wamachinga na sio katika kuboresha mazingira ya Wafanyabiashara wadogo (wamachinga, mamalishe, na wajasiriamali wengine) bado hayajawekewa mkakati wa kuondoa changamoto zao. Sekta ya biashara ndogo ina mchango mkubwa sana nchini kwenye pato la taifa wastani wa asilimia 22 na mchango wake kwenye sekta ya ajira ni wastani wa asilimia 14 ya nguvu kazi nchini zinapatikana kwenye biashara ndogo.
Hali ya sasa wafanyabiashara hawaonekani wakilindwa kisheria au shughuli zao kutambulika kama halali kwenye mchango wa uchumi wetu. Kwa, kifupi Wafanyabiashara wadogo hawachukuliwi kama injini ya maendeleo ya miji na majiji. Uamuzi wa kuwapanga Wafanyabiashara wadogo umetikisa uaminifu wao kwa taasisi za kifedha. Matukio ya kuungua moto kwa masoko ya Wafanyabiashara wadogo yamesababisha hasara kubwa sana kwa Wafanyabiashara.
Tafiti nyingi, zinaonyesha uhusiano uliopo katika shughuli za Wafanyabiashara wadogo na ukuaji na uendelezaji wa viwanda vidogo nchini. Asilimia 47 ya biashara ndogo zinahusisha bidhaa za kilimo ambazo zinaongezwa thamani.
ACT Wazalendo tunapendekeza kuwa Serikali kwa kuziweka pamoja na wizara ya Maendeleo ya jamii, Viwanda na uwekezaji na TAMISEMI kusikiliza na kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wadogo. Pia, katika mchakato wa kutunga kwa sheria ya wamachinga nchini, ushirikishwaji wa wamachinga uwe wa hali ya juu.

Hitimisho.
Bajeti ni chombo muhimu sana katika kupima vipaumbele vya matumizi ya fedha za umma katika kukabiliana na changamoto za wananchi. Katika kutazama bajeti ya mwaka huu haiakisi uhalisia wa mahitaji ya wizara. Wizara imetenga bajeti kama vile ni idara kuu ya wizara ya afya kama ilivyokuwa mwaka jana. Ni muhimu kwa Serikali kuona mikakati yake inatafsiriwa kwenye ugharamiaji wa mikakati hiyo kupitia bajeti. Aidha, changamoto za mauaji, ukatili dhidi ya wanawake, wazee na watoto ni muhimu zinapewa kipaumbele kama tulivyoshauri.


Ndg. Janeth Joel Rithe
Msemaji wa Sekta ya Ustawi na Maendeleo ya jamii, Wanawake na waototoi,
ACT Wazalendo
31 Mei, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK