Utendaji Mbovu wa TANESCO Unagharimu Taifa

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA NISHATI ACT WAZALENDO NDG. ISIHAKA MCHINJITA KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA 2022/23.
Utangulizi:
Ndugu Waandishi wa Habari,
Jana tarehe 01 Juni, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipokea na kuanza kujadili hotuba ya bajeti wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambayo itajadiliwa kwa siku mbili (2) (jana na leo mjadala unaendelea na Bunge litaidhinisha bajeti hiyo). Wote tunafahamu kuwa bajeti ni nyenzo muhimu na kuu katika kugharamia utoaji wa huduma ya nishati na kuleta uhakika wa utekelezaji wa miradi, progamu na mikakati ya sekta zote nchini.

Kutokana na umuhimu wake, bajeti ya Sekta ya Nishati imekua ni miongoni mwa bajeti zinazofuatiliwa kwa makini na wananchi, wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi. Aidha, wananchi pamoja na wadau mbalimbali wamekua wakitoa maoni yao kuhusu vipaumbele vya bajeti. Tukitambua umuhimu huu, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Nishati tumefanya uchambuzi wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23. Katika hotuba hii, uchambuzi wetu utahusisha maeneo tisa (9) kuhusu bajeti ya Nishati kwa mwaka huu na mapendekezo kuhusu maeneo ya vipaumbele ambayo tunaona yanafaa kuwa sehemu ya mipango na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuatia
Ndugu Waandishi wa Habari,
Zifuatazo ni hoja kuu tisa (9) kuhusu mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwenye Wizara hii kwa mwaka wa 2022/23.
1. Ufinyu wa bajeti na ucheleweshaji wa utekelezaji wa Miradi:
Utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2020/2021 Wizara ilipanga kutumia sh. T. 2.197 lakini ilipata sh. Trilioni 1.35 sawa na asilimia 61.5 ya bajeti yote ambapo kipaumbele ilikuwa uzalishaji umeme MW 4159.5 katika miradi ya Julius Nyerere (MW 2,115), Rusumo (MW 80), Kinyerezi I – Extension (MW 185), Ruhudji (MW 358), Rumakali (MW 222), Malagarasi (MW 49.5), Umeme wa Jua (MW 150), Umeme wa Upepo (MW 200), JotoArdhi (MW 200), Makaa ya Mawe (MW 600)
Bajeti ya mwaka 2021/2022 Wizara iliendelea na vipaumbele vilevile na ikaachana na mradi wa kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe MW 600 na hivyo kubaki na miradi mingine na pia kuendelea na miradi ya njia za kusafirishia umeme kaa ilivyokuwa kwa mwaka 2020/2021.

Ukiangalia miradi ya kipaumbele, gharama halisi ya miradi, fedha zilizotengwa kwa mwaka husika wa bajeti na muda wa makisio wa miradi kukamilika havina mahusiano kama tutakavyoainisha hapa chini.
S/NO MRADI WA UZALISHAJI UMEME GHARAMA YA MRADI FEDHA ZILIZOKWISHA TUMIKA FEDHA ZILIZOTENGWA 2021/2022 MUDA WA UTEKELEZAJI WA MRADI
1. Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere
– MW 2,115 Shilingi trilioni
6.55 Trilioni 2.495 Shilingi Trilioni 1.4 Juni,
2019 - Juni, 2022.
2. Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Ruhudji –
MW 35 Shilingi bilioni 958.25 Shilingi bilioni
125.13. Shilingi bilioni 65.60 Agosti,
2021 - Julai, 2024
3. RUMAKALI -222MW&NA UJENZI WA NJIA KV220, KM150 Shilingi bilioni 913.14 TSH 20.03B Shilingi bilioni 30.03 Julai, 2021 - Juni, 2024.
4. RUSUMO 80MW&NJIA YA KUSAFIRISHIA UMEME 220KV KM Shilingi
bilioni 265.9 0 Fedha za nje
Shilingi bilioni 3.85 Desemba, 2021
5. Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi
Asilia wa Kinyerezi I Extension – MW 185 Shilingi bilioni
435.48. TSH. 346.9B Shilingi bilioni 88.58 JULY 2021-JUNE2022
6. MARAGARASI-MW49.5 Shilingi bilioni 324.83. 0 Shilingi milioni 231.41 Septemba, 2021 - Septemba,
2024.
7. KAKONO-MW87&NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME KV 220 KM38.5 NA UKARABATI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME KYAKA Shilingi
bilioni 676.47 0 Shilingi
milioni 150 Desemba, 2021 -
Desemba, 2024.
8. KIKONGE MW300&UJENZI WA KUSAFIRISHA UMEME KV220 KM53 Shilingi trilioni 1.76 0 hilingi bilioni 1.04 NOV2022-DEC2025
9. GAS ASILIA MTWARA-MW300 NA UJENZI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME KV 400 NA KM 253 Shilingi
bilioni 990.47. 0 Shilingi milioni 50 AGOST 2022-AGOST 2024

10. GAS ASILIA SOMANGA FUNGU-MW330 NA UJENZI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME KV400 NA KM253 Shilingi bilioni
994.94. 0 FEBR 2023-DEC 2025


Ukiangalia hapa utaona Wizara imepanga kutumia sh trilioni 13.994 katika kipindi cha miaka mitano ili kuzalisha MW 4026.5 za umeme, lakini mpaka kufikia bajeti ya 2020/2021 ilishatumia sh.T2.8419 na ilitenga sh.T1.572 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 huku ikiwa na uzoefu wa kupata fedha ilizotenga kwa wastani usiozidi asilimia 65 kwa miaka mitatu nyuma.
Hii ni maana yake ni kuwa hata kama ingepata fedha zote wizara ingekuwa imetumia Shs 4.4171T kati ya Shs 13.994T na hivyo kubakiwa na hitaji la sh. T 9.5769 wakati imebakiwa na miaka mitatu ya utekelezaji wa mpango huu. Tumeutathmini mwenendo huu wa utekelezaji wa bajeti na kubaini yafuatayo:
i. Wizara imeshindwa kutekeleza vipaumbele kwa kuzingatia nguvu ya kifedha iliyopo na hitaji la nishati kwa taifa. Fedha zilizotumika trilioni 4.4 zingeelekezwa kwenye miradi michache inayoendana na gharama kama vile Kinyerezi Extension I, Kikonge, mradi wa Gasi asilia Mtwara, mradi wa Gasi asilia Somanga Fungu na Maragarasi tungekuwa hivi sasa tumeshazalisha umeme MW1164.5 ambapo ukiongeza na umeme tunaozalisha hivi sasa nchini wa MW 1605.86 tungeweza kuwa na jumla ya MW 2770.36 na kufanya Taifa lijitosheleze kwa kukidhi mahitaji ya umeme wa MW2677 zinazohitajika.

ii. Mipango ya hovyo ya kibajeti imepelekea miradi ya umeme kutokamilika kwa wakati na hivyo kulibebesha taifa gharama kubwa ya ucheleweshwaji wa fedha za miradi kwa wakati na kushindwa kuihudumia miradi hiyo. Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2021 inaonyesha wizara imeshindwa kufikia lengo la ujenzi wa njia za kusafishia umeme kwa asilimia 75 ya KM 4095 na uzalishaji mpya wa umeme wa MW3428.78 huku mkandarasi wa mradi wa JK Nyerere akidai fidia ya sh. Billioni 8.53 kutokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara kwenye mradi.
Hali hii inayoonekana katika miradi ya kuzalisha umeme ndio pia inayoonekana katika miradi ya kusafirisha na kusambaza umeme,
Katika bajeti ya mwaka 2021/2022 katika mradi wa kusafirisha umeme Msongo wa KV 400 kutoka Rufiji, Chalinze hadi Dodoma unao gharimu sh.Billion 453.18 umetengewa sh Billioni 180 B na huku waziri akieleza kuwa Mradi huu ungekamilika mwezi Juni 2022 ili utumike kusafirishia umeme kutoka bwawa la Mwl Nyerere. Kila mpango hapa unadhihirika kuwa ni zao la kutojali uhalisia wa matokeo.
2. Utendaji mbovu wa shirika la umeme TANESCO unaligharimu Taifa:
Shirika la umeme Tanzania TANESCO limebeba jukumu la kuzalisha, kusambaza na kuuza umeme. Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali amebaini upungufu wa wafanyakazi 2,419 katika shirika. Upungufu huu unadhoofisha utendaji wa shirika hadi kupelekea kuchelewa kwa umeme wateja kati ya siku 7 mpaka 481. Hali hii imeligeuza shirika kuwa genge la wala rushwa kwa wateja inaopaswa kuwahudumia.
TANESCO imekutwa na hoja zenye mapungufu kwenye taarifa ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali ikihusisha tathmini isiyo ya haki na kuondolewa kwa wazabuni katika zabuni, ongezeko la gharama hadi bilioni 3.6 katika manunuzi zinasababishwa na mchakato wa ununuzi kuchukua muda mrefu, manunuzi nje ya bajeti, kushindwa kuanzisha kiwanda cha nguzo za saruji kinachomilikiwa na TANESCO, Kuchelewa kwa Majadiliano Kuhusu kumalizika au Kuongeza Muda wa Mkataba wa Ununuzi wa Umeme katika Kampuni ya Songas uliokwisha Januari 17,2021.
Ni wazi kuwa udhaifu wa Tanesco kiutendaji na kimaadili kunahitaji hatua za kiusimamizi na kiuwajibikaji ikiwemo:
i. Kuajiri wafanyakazi wa kutosha ili kuiwezesha TANESCO Kutimiza wajibu wake
ii. Kuwajibisha watu wote wanohusishwa na hoja za ubadhirifu zilizoibuliwa na Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali.
3. Usiri wa mikataba na ukosefu wa umakini katika mikataba unalisababishia taifa hasara:
Mnamo tarehe 7 Julai 2011, Shirika la Umeme Tanzania liliingia mkataba na Kampuni ya Symbion Power LLC wa kukodi mitambo ya kufua umeme iliyopo katika eneo la Shirika la Umeme Tanzania Ubungo, Dar es Salaam kwa miaka miwili hadi kufikia tarehe 19 Septemba 2013 kukiwa na nafasi ya kuongezeka muda wa mkataba. Pia, Shirika la Umeme Tanzania lilitia saini mkataba wa ununuzi wa umeme kutoka Symbion mnamo tarehe 10 Disemba 2015. Baada ya hapo, mzozo ulitokea baina ya Shirika la Umeme Tanzania na Kampuni ya Symbion Power LLC kuhusu uhalali wa mkataba wa ununuzi wa umeme. Mnamo tarehe 24 Mei 2016, Shirika la Umeme liliizuia Kampuni ya Symbion kuingiza umeme kwenye mtandao wa gridi ya Shirika la Umeme la Tanzania kwa mujibu wa masharti ya mkataba wa ununuzi wa umeme.
Mwaka 2017, Kampuni ya Symbion Power LLC na mwanahisa wa kampuni hiyo walifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Biashara (ICC) na mwaka 2019 walipeleka maombi ya usuluhishi kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID). Hatimaye, Serikali ya Tanzania na Shirika la Umeme la Tanzania walihusika kwenye madai ya jumla ya dola za Marekani bilioni 1.57.
Mnamo tarehe 21 Mei 2021, pande zote zilikubaliana kutatua suala hilo kwa kusaini mkataba wa maelewano ambapo Shirika la Umeme Tanzania lilitakiwa kulipa dola za Marekani milioni 153.43 kwa kusitisha mkataba.
Usimamizi usiofaa wa mkataba, ukosefu wa umakini kwa Shirika la Umeme Tanzania na kushindwa kutathmini athari za kifedha kabla ya kusitisha mkataba kumesababisha upotevu wa fedha za Serikali.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kufanya marudio ya taratibu zake za mikataba kwa kumuhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia, iweke utaratibu wa kuweka wazi mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi hii ili kila mwananchi ashiriki kuchangia, kukosoa na kuboresha pale inapobidi.
Pamoja na haya, tunaitaitaka Serikali kuwachukulia hatua wote waliohusika katika uzembe huu ulioligharimu Taifa.
4. Miradi mikubwa ya nishati kutekelezwa kwa kasi ndogo na kupuuza maslahi ya Wananchi katika maeneo ya miradi:
Miradi ya nishati mikubwa inayoendelea kwa sasa ni mradi wa uzalishaji umeme bwawa la Mwl Nyerere na ujenzi wa kiwanda cha kuchanjua gesi kuwa kimiminika Likong’o Lindi.
Miradi hii yenye gharama kubwa inahitaji umakini wa hali ya juu na ni sharti wananchi katika maeneo ya utekelezaji washirikishwe na kunufaika na miradi husika.
i. Mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere- Rufiji

Mradi huu ulianza mwaka 2019 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2022. Mpaka sasa mradi umeshatumia Shilingi Trilioni 3.6 kati ya Trilioni 6.5 zinahitajika ili mradi ukamilike.
Mradi unakabiliwa na changamoto ya kutopewa fedha zinazostahiki ili ukamilike kwa wakati. Hivyo hakuna uwezekano kwa mradi huu kukamilika mwezi Juni 2022 kama ilivyoelezwa na hotuba za bajeti za waziri wa nishati katika kipindi chote kuanzia mwaka 2019/2020. Taarifa zinaonyesha kuwa Mradi utakamilika mwezi Juni, 2024. Ni wazi kuwa Serikali itatumia fedha za ziada kwa ajili ya kumlipa mkandarasi ili kukamilisha Mradi huu kutokana na kuongeza muda wa utekelezaji.

Aidha, kwenye eneo la kutozingatia maslahi na haki ya wananchi, Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali amebaini kuwa kiasi cha fedha Shilingi bilioni 196 zilizopaswa kutumika katika miradi ya maendeleo ya jamii kwa wananchi wanaoishi eneo hili la mradi hazijatolewa na wananchi hawajui kinachoendelea. Uendelezaji wa miradi yenye maslahi kwa taifa inapokosa kuinufaisha jamii inayozunguka mradi huzusha taharuki na nyakati zingine vurugu za umma kudai haki yao kama ilivyotokea Mtwara wakati wa utekelezaji wa mradi wa bomba la kusafirishia gesi kutoka Mtwara hadi Dar es salaam.

ACT Wazalendo tunatoa wito kwa wizara kuzuia kiasi hicho cha fedha za fidia ya wananchi kutoka fedha zitakazoingizwa kwa mkandarasi mwaka huu wa bajeti kwani ilipaswa kufanywa hivyo tangu zilipotolewa fedha za mwanzo kabisa kwa mujibu wa mkataba.

ii. Mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) wa likong’o lindi.

Huu ni mradi mkubwa uliotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya gesi hapa nchini
Mradi huo unatarajia kutumia gesi kutoka katika vitalu namba 1, 2 na 4 Vyenye jumla ya futi za ujazo Trilioni 46 vilivyopo bahari kuu mkoani Lindi na kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ambapo gharama za mradi huu zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 30 sawa na takriban Sh70.5 trilioni.

Hata hivyo, utekelezaji wa mradi huo umekuwa ukipigwa danadana kutokana na kutokamilika kwa majadiliano baina ya wawekezaji wa mradi huo uliopo kusini mwa Tanzania.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia shirika la maendeleo la Petroli nchini (TPDC) na Kampuni ya Baker Botts (UK)LLP wametia saini mkataba wa huduma ya ushauri elekezi katika mradi wa LNG tarehe 5/1/2022 hatua ambayo imeleta matarajio kuwa mradi utakwenda kuanza.
Mwaka 2019 Serikali ilisema mradi huo ungeanza ujenzi mwaka 2022 na kukamilika mwaka 2028. Hata hivyo, mabadiliko hayo mapya ya kuanza kwa ujenzi yasingebadilisha matazamio ya awali ya kukamilisha mradi huo mwaka 2028.

Aliyekuwa Waziri wa nishati Dk Kalemani wakati wa hotuba yake ya bajeti mwaka 2021/2022 alisema kazi zilizotekelezwa hadi kufikia mwezi Machi, 2021 katika mradi huo wa LNG ni pamoja na kukamilisha malipo ya ShT 5.7 bilioni kwa ajili ya fidia na riba kwa wananchi 642 waliopisha mradi; na kuweka mpaka eneo la mradi (Likong’o, Mto Mkavu na Masasi ya Leo). Uchunguzi wetu umebaini kuwa, jumla ya TZS Bilioni 5.2 imelipwa kwa wananchi 676 kati ya 693 watakaopisha mradi katika eneo la Likong’o, Lindi na hivyo bado wananchi 17 bado hawajalipwa.

Aidha wananchi hawa waliolipwa ni wale waliofanyiwa tathmini mwaka 2014 katika eneo la kuanzia mita 301 mpaka mita 4071 toka barabara kuu itokayo Dar es salaam kwenda Lindi mpaka kufikia eneo la bahari.

Wananchi waliofanyiwa Tathmini mwaka 2015 katika eneo lenye makazi ya watu kuanzia mita 0 mpaka 300 toka barabara kuu hawajalipwa fidia na wamekuwa wakipewa maelekezo mapya kila baada ya muda. Wakati maandalizi ya utekelezaji wa mradi huu yakiwa katika hatua ya majadiliano ni vema Serikali ikafanya yafuatayo;
(1) iwalipe wananchi 17 ambao bado hawajalipwa waliopo katika eneo lililokwishalipwa
(2) liwalipe fidia wananchi waliofanyiwa tathmini katika eneo la makazi ili waweze kuendeleza makazi mapya kwani sasa mashamba yao yamechukuliwa na kubakishiwa makazi huku shughuli zao za kilimo zikiwa hazitekelezeki katika eneo husika
(3) Serikali iwahamishie wananchi hawa eneo la Nagiriki ambalo lilishaandaliwa kwa ajili ya kuwahamishia.
(4) Fidia ya kuhamisha makazi ihusishe kuwajengea nyumba katika eneo jipya watakalohamishiwa.
5. Kupanda kwa bei ya mafuta na wajibu wa Serikali:
Mwenendo wa bei ya mafuta ya Petroli, Diseli na mafuta ya taa, umekuwa ukiongezeka kila mwezi tangu tarehe 01 Julai, 2021. Kwa kipindi chote Serikali haikuwa inachukua hatua madhubuti za kuleta unafuu au kushusha bei hizo ili kuzuia kutokea kwa mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.
Bei za rejareja za mafuta ya Petroli, Diseli na Mafuta ya Taa kwa mwezi julai, 2021 ilikuwa Shilingi 2,249 kwa kila lita ya Petroli, Diseli ilikuwa Shilingi 2073 na mafuta ya taa ilikuwa ShT, 1,957. Kupanda kwa bei hizi za mwezi Julai kutokea mwezi Juni, 2021 kwa sehemu kubwa zilichangiwa na sera za kikodi na sheria ya fedha ya mwaka 2021/22 ambayo ilifanya mabadiliko kwa ongezeko la tozo ya mafuta kwa Shilingi 100 kwa kila lita moja ya mafuta ya Petroli na dizeli na kuongezeka kwa ada ya Petroli kwa Shilingi 100 kwa kila lita moja ya mafuta ya taa. Ndio maana zilipelekea kuongezeka kwa bei hizo kwa Shilingi 156 kwenye Petroli, Diseli iliongezeka Shilingi 142 na mafuta ya taa iliongezeka Shilingi 164.
Ukilinganisha bei mpya zilizotangazwa juzi na kuanza kutumika jana tarehe 01 Juni 2022 ambazo zinaonyesha kuwa bei ya rejareja ya Petroli kwa Dar es Salaam ni ShT, 2,994 kwa lita, Diseli ni ShT. 3, 131 na mafuta ya taa ShT. 3,299 na bei za mwezi Juni, 2021 ambazo zilikuwa Shilingi 2,249 kwa Petroli, Diseli ShT. 2073 na mafuta ya taa ni Shilingi 1,957. Ongezeko la mwaka mzima ni Shilingi 745 kwa Petroli, Diseli ShT. 1058 na mafuta ya taa Shs,1342.
Kwa hiyo, kwa Mwenendo huu bado tunaona hali ni mbaya, wananchi wanaumia. Tunafahamu nafuu iliyopatikana kutokana na ruzuku ya Serikali ya Shilingi bilioni 100, lakini kama tulivyoona bado haitoshi. Sisi ACT Wazalendo, tumekuwa na msisitizo huo wa kuitaka Serikali iondoshe kodi ya Shilingi 500 kwa kila lita. Tulitoa msisitizo huo tangu mwezi April ambapo bei za mafuta kwa rejareja zilikuwa ShT, 2861 kwa lita ya Petroli, huku Diseli ikiwa 2,692 na mafuta ya taa 2,682. Tuliamini kuwa kwa kuondosha tozo ya Shilingi 500, ingeweza kuleta ahueni angalau kufikia bei zinazolingana na mwezi Julai na Agosti, 2021.
ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali kufanya zaidi kwa kuhakikisha inaondoa tozo ya Shilingi 500 kwa kila lita ya Petroli, Diseli na mafuta ya taa. Pia, tunasisitiza umuhimu wa Serikali kuingilia kati kwa kuyawezesha mashirika ya TIPER na TPDC kununua na kuuza mafuta ili kuhakikisha unafuu zaidi unapatikana. Aidha, azma ya Serikali kuweka Miundombinu ya kuwa na hifadhi ya mafuta kimkakati itengewe fedha haraka kwa ajili ya utekelezaji.
6. Hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme nchini:
Katika zama za sasa, upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika huchochea ukuaji wa uchumi (Uzalishaji viwandani na mashambani) na utoaji wa huduma zingine kama vile elimu, mawasiliano, usafiri na uchukuzi, matibabu na huduma za utawala. Kwa hiyo, umeme una nafasi na mchango mkubwa sana katika maisha yetu kama jamii na nchi kwa ujumla wake.

Pamoja na umuhimu huu tunaona huduma ya umeme nchini bado sio ya uhakika. Pamekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara. Kwa hali hii ni wazi kuwa kutosimamiwa vyema huduma ya upatikanaji wa umeme unarudisha nyuma uwekezaji mkubwa kwenye viwanda, kuzorotesha mifumo mingine ya huduma kama vile matibabu, uchukuzi na mawasiliano na masuala ya utawala.

Mwenendo wa uwezo wetu wa kuzalisha umeme kwa mujibu wa taarifa za wizara kutoka kwenye hotuba ni kuwa, ongezeko la uzalishaji wa umeme nchini kwa mwaka 2021/22 ni megawati 124.92 sawa na asilimia 7.94 kwa kulinganisha na uzalishaji wa mwaka uliopita ambao ulikuwa na jumla MW 1608.46 wakati uzalishaji wa sasa ni 1,733.38. Mahitaji ya juu ya umeme katika mfumo wa Gridi ya Taifa yameongezeka na kufikia MW 1,335.01 ikilinganishwa na MW 1,201.02 zilizokuwa zimefikiwa mwaka 2020/21, sawa na ongezeko la asilimia 11.16.

Aidha, ongezeko la watumiaji kutokana na usambazaji wa umeme vijijini linakuwa kwa asilimia 13.54 kila mwaka. Ni dhahiri kuwa kasi ya uzalishaji na usambazaji haulingani, jambo linalopelekea kuwa na upungufu wa uwezo wa kuhudumia wananchi, hivyo changamoto za kukatika kwa umeme mara kwa mara hutokea,

Mwezi Oktoba mwaka 2021, nchi yetu ililazimika kuzima mitambo yake ya umeme wa kutumia maji kwa takribani mwezi mzima kwa kuwa wastani wa maji ya uzalishaji ulikuwa chini ya kiwango kinachotakiwa kusukuma mitambo na ulipofika mwezi Decemba, mitambo ya umeme wa maji ambayo huweza kuzalisha hadi megawati 561, ilizalisha megawati 110 pekee, kwa mujibu wa TANESCO.
Hali hii inatokea katika wakati ambao nchi yetu imeshafanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya gesi asilia.
Taifa letu linaweza kuepuka changamoto ya kutokuwa na umeme wa uhakika kwa kuitumia vema fursa ya gesi asilia tuliyonayo.

7. Gharama za kuunganisha umeme zinapaswa kuwa jukumu la Serikali:
Katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021, Serikali ilipunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wa mijini kufikia Shilingi 27,000. Hatua hii ilipokelewa kwa furaha na wananchi walijitokeza kwa wingi ili kupata huduma hii muhimu. Katikati ya mwaka wa bajeti 2021/2022 Serikali ilirejesha gharama za awali za kuunganisha umeme kwa kile kilichoelezwa kuwa ni gharama halisi ya kuunganisha umeme. Hatua hii iliyoleta maumivu kwa wananchi ni matokeo ya Serikali kukimbia wajibu wake wa kutoa huduma muhimu kwa umma.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameeleza kuwa kutokana na kutoza bei za chini za Umeme. Katika Shirika la Umeme Tanzania, ilibainika lilipoteza Shilingi bilioni 105.49 kutokana na kupunguza bei za nishati ya umeme na gharama za uunganishaji wa umeme. Kiasi cha Shilingi bilioni 88.39 hakikukusanywa kutoka kwa wateja 300,697 kwa sababu ya kushusha bei ya kuunganisha umeme mwaka 2020/21 kutoka Shilingi 320,960 hadi Shilingi 27,000 (kiwango kilichotumika vijijini pekee). Vilevile, Shilingi bilioni 17.10 hazikukusanywa kutoka kwa wateja 208,319 kutokana na kubadilisha madaraja ya matumizi ya umeme kutoka daraja la juu la T1 kwenda la chini la DI katika mwaka wa fedha 2020/21.

Kiasi hiki cha fedha kinachosemwa kuwa ni hasara ikiwa tu dhana kuhudumia wananchi haipewi kipaumbele na badala yake ni fahari kutumia fedha hizi za umma kuwarahisishia huduma wananchi. Ikiwa tunataka Taifa letu lipige kasi ya maendeleo kwa kuwezeshwa na sekta ya nishati, wajibu wa kusambaza miundo mbinu ya umeme hadi majumbani ubaki kuwa ni wajibu wa Serikali na wananchi walipie huduma ya umeme.

Hatua ya Serikali kuunda kamati ya kufanya tathmini ya maeneo yenye sifa za vijijini kwa maeneo ya mijini ili kufanya gharama ya umeme kushuka ni kupoteza rasilimali bure. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali itekeleze wajibu wake huo.
8. Kushindwa kuunganisha umeme katika miradi ya kimkakati ya taifa:
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali ameonesha kuwa Tanesco ilishindwa kuunganisha migodi 25 katika gridi ya taifa kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Tunafahamu mchango wa migodi katika uchumi wa taifa letu. Kitendo cha kutounganisha umeme kwenye migodi, tunailazimisha migodi itumie nishati ya mafuta na hivyo uendeshaji wa migodi kuwa ghali na kuligharimu taifa. Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa migodi yote mikubwa nchini inaunganishwa katika gridi ya taifa ili ipate umeme wa uhakika na Serikali ingejipatia faida kwa kuuza umeme kwenye mashirika haya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali anasema kuwa “kama Shirika la Umeme Tanzania lingeipatia migodi umeme, gharama za mafuta kutoka nje ya nchi yanayoagizwa na migodi zingeweza kuokolewa na badala yake fedha hiyo zingetumika ndani ya nchi kupitia ununuzi wa umeme na hivyo Shirika la Umeme Tanzania lingenufaika kwa mauzo ya umeme kwenye sekta ya madini. Kwa mfano, Kampuni ya Stamigold ilitumia lita 7,102,904 za dizeli mwaka 2020/21 zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 14.72 kwa bei ya Shilingi 2,073 kwa lita. Iwapo Shirika la Umeme Tanzania lingeunganisha migodi hii kungepunguza misamaha ya kodi inayotolewa kwenye migodi katika ununuzi wa mafuta na kuongeza mapato kwa Shirika.”

ACT Wazlendo tunasisitiza kuwa ni muhimu kwa Serikali kufungamanisha sekta za uzalishaji na sekta hii ya nishati ili kuokoa gharama tunazotumia kwenye uzalishaji ambazo hazilinufaishi taifa letu.
9. Kasi ndogo ya matumizi ya Nishati Mbadala:
Nishati ni hitaji muhimu sana katika Maisha ya mwanadamu, kutokana na uhitaji huo inatoa msukumo mkubwa kwa uharibifu wa mazingira. Zaidi ya asilimia 85 ya wananchi vijiji wanategemea kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha Nishati ya kupikia majumbani. Huku Dar es Salaam ikitegemea kuni na mkaa kwa asilimia 78.2 na kutumia 70% ya mkaa wote unaozalishwa nchini. Kiwango cha ukataji wa miti kinakadiriwa hekta 372,000 kwa mwaka kiasi cha kutishia usalama wa misitu nchini.
Ukiangalia mipango ya bajeti tangu miaka ya 2016 hadi 2021, Serikali inataja kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kuwa ni eneo la kipaumbele kwenye Wizara ya Muungano na Mazingira. Lakini, Serikali haijaweka nguvu ya kuhakikisha matumizi ya kuni na mkaa yanaondoshwa kwa kuweka mazingira mazuri ya usambazaji wa gesi, kuharakisha mazungumzo na uwekezaji kwenye gesi asilia ya Lindi, ambayo itashusha gharama za gesi kwa wananchi.

Pia, hadi sasa bado zipo taasisi za Serikali zinatumia kuni na mkaa kuwa ndio nishati ya kupikia, mathalani magereza, hospitali, shule na vyuo, kambi za jeshi la kujenga taifa na kambi za mafunzo ya polisi.

Sisi ACT Wazalendo tuliweka wazi katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 katika kuhakikisha tunakuwa na nishati mbadala kuwa; “Serikali ya ACT Wazalendo itasambaza bomba la gesi majumbani kwa matumizi ya kupikia ili kupunguza gharama za kutumia umeme, kununua mitungi ya gesi na kuokoa mamilioni ya misitu inayopotea kila mwaka kwa matumizi ya kupikia majumbani.”

Hivyo, tunaitaka Serikali isiishie kuweka kwenye hotuba tu mkakati wa kutumia nishati mbadala, badala yake iwekeze kwenye nishati ya jua, umeme wa maji, gesi asilia ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yana athari kubwa kwenye mazingira.

Hitimisho:
Bajeti ni nyenzo muhimu sana katika kupima vipaumbele vya matumizi ya fedha za umma katika kukabiliana na changamoto za wananchi na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi. Katika kutazama bajeti ya mwaka huu ya wizara ya nishati trilioni 2.91 inaweza kuonekana ni bajeti kubwa. Lakini uhalisia wa gharama za miradi katika sekta ya nishati ni dhahiri kwamba bado ni tone dogo sana. Pia, ni muhimu kwa Serikali kuboresha utekelezaji wa bajeti kwa kuhakikisha inatoa fedha zilizotengwa kwa wakati ili kuepusha kulipa gharama za ziada kwa wakandarasi na watoa huduma wengine. Aidha, utendaji wa TANESCO unapaswa kutazamwa upya na kuimarishwa kwa maslahi mapana ya wananchi. Ni wakati sasa wa kumaliza mazungumzo na wawekezaji wa Mradi wa Gesi Asilia Lindi, ili kulihakikishia taifa uhakika wa nishati na uendelevu wake.

Ahsanteni sana.
Imetolewa na:
Ndg. Is-haka Mchinjita
[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Nishati
ACT Wazalendo
02 Juni, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK