Uwekezaji wa Kibajeti Mifugo na Uvuvi Hauridhishi: Mtutura
OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.
Sekta ya Mifugo na Uvuvi
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA KILIMO, MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI NDG. MTUTURA A. MTUTURA KUHUSU MPANGO NA BAJETI YA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023.
Utangulizi
Jana tarehe 25 Mei 2022, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Ndg. Mashimba M. Ndaki aliwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, ilifuatilia hotuba na kufanya uchambuzi wa kina kwa lengo la kubainisha ni kwa kiasi gani imeendana na matarajio ya wafugaji na wavuvi hapa nchini. Kupitia uchambuzi wa Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi tumekuja na hoja tisa (9) kuhusu bajeti ya wizara ya mifugo na uvuvi kwa mwaka wa fedha 2022/23.
A: Sekta ya Uvuvi
1. Operesheni, doria na faini kandamizi kwa wavuvi.
Operesheni maalumu zilizoendeshwa na Serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi mwaka 2018 hususani, Operesheni Sangara(Ziwa Victoria), Operesheni Jodari (Bahari ya Hindi) na Operesheni MATT (Dhidi ya uvuvi wa mabomu na baruti) pamoja na operesheni za kawaida na doria zinazofanywa kila siku zikiwa na lengo la kudhibiti uvuvi haramu. Ingawa operesheni na doria katika hali ya kawaida zinabeba nia njema, matokeo na athari zake, kwa namna zilivyoendeshwa na zinavyoendeshwa zinaacha makovu na madhila makubwa kwa wavuvi wadogo wadogo. Uendeshwaji wa operesheni na doria hizi zimejenga dhana kuwa wavuvi ni wahalifu wasiopaswa kushirikishwa badala yake huadhibiwa.
Matokeo ya operesheni iliyobebwa na dhana ya uvuvi ni uhalifu hazipambani dhidi ya uvuvi haramu badala yake zinageuka njia ya kuwafilisi wavuvi na kuwatajirisha maafisa wanaoendesha operesheni hizo. Tumeshuhudia vitendo vya kinyama kama vile kuwa kwa wavuvi, kuteswa, kuwekwa kuzuizini na kuumizwa katika maeneo yote yaliyoendeshwa doria na operesheni maalum, kunaonyesha matumizi makubwa ya nguvu na hata risasi za moto. Pia, kumekuwa na faini zisizo za kisheria ambazo zinawatajirisha baadhi ya maafisa uvuvi na kuwaumiza wavuvi. Aidha, doria na operesheni zinakamata mali na vifaa vya wavuvi na kuziteketeza kwa moto, hadi leo kwenye baadhi ya ofisi za mamlaka za Usimamizi wa bahari (BMU’s) na vituo vya Jeshi la Polisi hapa nchini kuna idadi kubwa ya mitumbwi na vyombo vya uvuvi vinavyoozea na kuharibikia huko.
Kwa ujumla, vitendo hivi vinavyoendeshwa bila weledi hupelekea kupoteza uhai, kuacha ulemavu na kujeruhi wavuvi, kuharibiwa kwa vifaa vya uvuvi na kusababisha baadhi ya wavuvi kuacha kabisa shughuli za uvuvi. Yapo, matukio yamepungua lakini bado fikra, mitazamo na dhana za operesheni zimejengeka kwenye sura hii tuliyoileza.
ACT Wazalendo tunaishauri serikali kuwainua wavuvi kwa kuwahakikishia masoko na kutoa mikopo yenye masharti nafuu na kuwaunganisha katika mfumo wa hifadhi ya jamii kwa ajili kupata huduma za matibabu na mafao ya uzee, ulemavu na majanga.
Vilevile, tunaitaka serikali ianze kwa kuvifungia viwanda au kuzuia viwanda vinavyozalisha nyavu haramu ili kudhibiti uzalishaji. Kitendo cha serikali kuwaandama wavuvi na kuwafilisi huku wakiviacha viwanda vikiendelea kuzalisha bidhaa zilizoharamishwa matumizi yake hapa nchini ni mwenendo usioleta mahusiano mazuri kati ya Watawala na Watawaliwa.
2. Serikali imedanganya; hakuna bandari ya uvuvi wala meli za uvuvi, tunaendelea kupoteza mapato na kufukarisha wavuvi.
Shughuli za uvuvi kwenye maji ya asili huendeshwa na wavuvi wadogo ambao huchangia zaidi ya asilimia 95 ya Samaki wote wanaozalishwa nchini na asilimia tano (5) iliyobaki huchangiwa na uvuvi wa makampuni (kibiashara). Takribani miaka sitini na moja (61) sasa, bado serikali inaburuza miguu kufanya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi katika pwani ya nchi hii, licha ya nchi yetu kubarikiwa kwa kuwa na fukwe ndefu. Kutokuwepo kwa bandari ya uvuvi inachochea kupoteza mapato ambayo yangepatikana kutokana na leseni, tozo kwa meli zinazovua katika ukanda wa bahari na fukwe.
Katika hotuba ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka fedha 2022/23, Serikali imeishia kutaja kuwa kukosekana bandari ya uvuvi kuanzia Tanga hadi Mikindani Mtwara kunaipotezea serikali mapato makubwa. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilisema itakamilisha upembuzi wa kina (bathymetric, topographic and geotechnicalsurvey) katika eneo la Mbegani, Bagamoyo na kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi. Hadi, leo hakuna hata Shilingi iliyotengwa kwa ajili ya kuanza kwa mchakato wa upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa bandari ya uvuvi katika fukwe za nchi hii. Mikakati inayotajwa ni maneno matupu, inawahadaa Watanzania.
Aidha, uvuvi wa bahari kuu unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa meli kwa wavuvi wetu, Serikali mwaka jana iliahidi kuwa hadi kufikia mwezi Januari Tanzania itakuwa imeshaleta meli mbili (2) za uvuvi, Lakini katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu inadhihirisha kuwa meli hazijanunuliwa. Serikali imedanganya umma, hakuna bandari ya uvuvi wala meli.
ACT Wazalendo inaitaka Serikali ijenge bandari za uvuvi Mikoa ya Tanga, Pwani (Mafia) Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Aidha, Serikali inunue meli za Kitaifa za uvuvi pamoja na kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili kuboresha na kuimarisha sekta ya uvuvi wa bahari kuu.
3. Upotevu mkubwa wa mazao ya uvuvi
Upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa unaokadiriwa kufikia asilimia 40. Sehemu kubwa ya wanaoshiriki shughuli za uvivu ni wavuvi wadogo wadogo, ambao mara nyingi nyenzo na zana uvuvi na kuhifadhiwa mazao ya uvuvi huwa ni duni sana, Samaki wanapotea kwa kuharibika kutokana na ukosefu wa Miundombinu bora na yenye ufanisi kama vile, viwanda vya kuchakata Samaki, mialo ya kuanikia Samaki, maghala- majokofu na barafu kwa ajili ya kuhifadhia. Pia, kuna changamoto ya ukosefu wa uhakika wa masoko ya mazao ya uvuvi.
Kwa mujibu wa ripoti ya wizara kuna maghala ya kuhifadhi mazao ya uvuvi 90, viwanda vikubwa vya kuchakata mazao ya uvuvi 16, viwanda vya kati vitano (5) na viwanda vidogo 33. Vilevile, kuna viwanda nane (8) vya kuchakata mabondo ya Sangara na viwanda vitano (5) vya kutengeneza zana za uvuvi.
ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kuchukua hatua kwa kuimarisha ushirikiano na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekta Binafsi katika kujenga na kuboresha masoko, mialo na kuwekeza katika Ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kutengeneza zana za uvuvi.
4. Kuongezeka kwa maeneo tengefu na hifadhi ya bahari
Katika zama hizi zinazoongozwa na sera za utandawazi (soko huria), upo msukumo mkubwa sana wa kuona wazalishaji wadogo ni kikwazo cha Maendeleo. Dhana ya uwekezaji ni kuweka mazingira mazuri kwa wazalishaji wakubwa aghalabu kutoka nje, kuzalisha kwa ajili kuvuna faida zaidi bila kujali kukidhi mahitaji ya ndani. Msukumo huu umeendelea kuathiri pia sekta ya uvuvi, tumeona Ongezeko kubwa la maeneo ya bahari yanayoitwa hifadhi ya bahari (marine parks) na maeneo tengefu yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za utalii na uvuvi mkubwa unaofanywa na makampuni ya kibiashara kutoka nje mengi na machache ya ndani.
Kuongezeka kwa maeneo tengefu na hifadhi ya bahari, yanaongeza ufinyu wa maeneo ya uvuvi kwa wavuvi wadogo na kusababisha operesheni za mara kwa mara zinazoambatana na mateso kwa wavuvi.
ACT Wazalendo inatoa rai kuangalia mikakati yote ya Maendeleo. Wazalishaji wadogo wanapaswa kupewa kipaumbele kama ndio nyenzo za kufikia shabaha ya Maendeleo ya watu.
5. Tozo na leseni kwa wavuvi zitazamwe upya.
Takwimu zinaonyesha kuwa shughuli za uvuvi kwenye maji ya asili huendeshwa na wavuvi wadogo ambao huchangia zaidi ya asilimia 95 ya samaki wote wanaozalishwa nchini na asilimia tano (5) iliyobaki huchangiwa na uvuvi wa makampuni makubwa (kibiashara). Aidha, wastani wa tani laki nne zinatoka kwenye uvuvi mdogo, Lakini shughuli za wavuvi wadogo zina mnyororo wa tozo kuanzia kulipia ada za vikundi vya Usimamizi wa bahari (ambavyo sio vyama vya wavuvi), tozo za masoko, tozo za halmashauri na ushuru wa TRA.
Pia, changamoto ya leseni za uvuvi; kuna matatizo makuu mawili katika eneo la leseni. Moja, leseni inayotolewa na halmashauri moja haitumiki halmashauri nyingine, kwa lugha nyepesi mvuvi anayevua halmashauri ya Mkinga, Tanga akienda Pangani-Tanga anapaswa kulipia ushuru mwingine. Pili, viwango na mfumo wa leseni vinamnyonya mara mbili mvuvi.
ACT Wazalendo tunatoa rai kwa serikali kuweka mfumo unganishi kama ilivyo kwa madereva ambao wakipatiwa leseni sehemu yoyote nchini, wana uwezo wa kuendesha vyombo popote pale. Pia, itazamwe mantiki ya kuwatoza wavuvi kupitia leseni ni kuzuia.
B: Sekta ya Mifugo
6. Kasi ndogo ya kutatua migorogoro ya wafugaji na wakulima
Kwa mujibu wa hotuba ya wizara ya mwaka huu inayonyesha imeweza kutatua migogoro 28 pekee nchi nzima. Katika mwaka 2021/2022 Serikali inasema imefanya mikutano 13 ya utatuzi wa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi imefanyika katika Mikoa ya Katavi (4), Rukwa (4), Pwani (3), Lindi (10), Mtwara (2), Tanga (1) na Songwe (4). Kutokana na mikutano hiyo jumla ya migogoro 13 imetatuliwa na mingine ipo katika hatua mbalimbali za utatuzi.
Kwa uchambuzi wetu, migogoro hii inatokana na kukosekana kwa mifumo imara inayolinda haki na maslahi mapana ya wazalishaji wadogo katika ardhi. Mfano, mfumo wa umilikaji wa ardhi, changamoto za upatikanaji wa rasilimali za maji na malisho zinazoathiri wazalishaji wadogo. Hii ni pamoja na kasi ndogo ya kutenga na kumilikisha ardhi kulingana na taratibu za kisheria au kimila. Aidha, uporaji wa ardhi unafanywa kwa jina la uwekezaji au unafanywa taasisi za serikali kwa kile kinachoitwa “kwa manufaa ya umma”
ACT Wazalendo tunaishauri Serikali kuweka sera na sheria zenye mrengo wa kuwekeza rasilimali na uwezeshaji kwa wazalishaji wadogo ambao ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara.
7. Uhakika wa biashara ya mifugo na mazao yake bado ni mdogo.
Katika hotuba iliyowasilishwa jana bado imeshindwa kutuonesha ni kwa namna gani Serikali imejipanga katika kuwatengenezea wafugaji masoko ya mazao ya mifugo. Mazao yapatikanayo kutokana na mifugo ni pamoja na nyama, ngozi, maziwa, pembe na mifupa.
ACT Wazalendo inaishauri Serikali ifungamanishe sekta ya mifugo na viwanda ili wafugaji wawe na uhakika wa masoko na pia waendeshe ufugaji wenye tija. Njia sahihi ambayo Serikali inawajibika kuchukuwa ni kuandaa mazingira wezeshi kwa wawekezaji kuvifufua viwanda vya nyama Shinyanga, cha ngozi Mwanza na cha maziwa Utegi Rorya. Kwa vile Mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga, Mwanza na Geita ni mikoa ya wafugaji, vikifufuliwa viwanda hivi vitawasaidia wafugaji kuwa na uhakika wa masoko. Pia serikali iweke msisitizo wa kufunguwa masoko zaidi ya nje ili kuwaongezea tija wafugaji.
8. Ukosefu wa malisho na marambo ya maji ya mifugo.
Moja ya kero sugu kwa wafugaji ni malisho na upatikanaji wa maji kwa mifugo yao. Kero hii imezaa migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji. Mara kadhaa Serikali imeshauriwa kupima ardhi ili kubainisha maeneo ya kilimo na ya ufugaji, lakini hadi sasa bado haijachukuwa hatuwa madhubuti.
Chama cha ACT-Wazalendo, kinaitaka Serikali kukamilisha Mpango wa kupima ardhi za vijiji na kutenga maeneo ya wakulima na yale yanayofaa kwa ufugaji ili kukomesha kabisa mizozo inayohatarisha maisha ya Watanzania. Pia Serikali ikomeshe tabia ya kumega maeneo ya raia na kuyafanya MAPORI TENGEFU. Serikali ni lazima ithamini utu wa watu kwanza, kwani bila kujitosheleza kwa chakula, utu wa mtu huwa kwenye rehani.
ACT Wazalendo tunaishauri serikali kuandaa mazingira wezeshi kwa wawekezaji watakaoleta mitambo ya kisasa ya kusindika vyakula vya mifugo ili kupunguza bei za vyakula hivyo kutokana na ushindani utakaojitokeza baina yao.
9. Ukamataji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi
Wafugaji wadogo kama ilivyo kwa wakulima wadogo wanakabiliwa na changamoto ya uporwaji wa mali zao kwa jina na kuvamia maeneo ya hifadhi. Takwimu zinaonyesha kuwa Idadi ya mifugo iliyoporwa na kunyang’anywa kutoka kwenye mikono ya wafugaji inafanya idadi ya Milioni 6.24 kwa mwaka 2020.
Kukamatwa kwa mifugo hii kutoka mamlaka za hifadhi na baadhi ya askari wa hifadhi ni kinyume na taratibu za sheria za nchi hii. Hali za namna hii zinawafanya wafugaji waonekane kama wakimbizi, au kana kwamba nchi si huru. Licha ya jitihada za serikali kukabiliana na changamoto hii, ni muhimu sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya uhifadhi na utalii kubadilishwa kimtazamo ili kuwaona wafugaji ni wadau muhimu wa Maendeleo badala ya mtazamo wa sasa, unao wachukuliwa wafugaji wadogo wadogo na wa asili kuwa ni kikwazo cha Maendeleo, hivyo wanapaswa kupotezwa.
Hitimisho:
Uwekezaji wa kibajeti katika sekta ya mifugo na uvuvi hauridhishi licha ya mchango wake katika pato la taifa kuwa ni mkubwa, kwa mujibu wa taarifa ya wizara (Hotuba ya bajeti- 2022/23) sekta ya mifugo na uvuvi kwa ujumla inachangia asilimia 8.2 kwenye pato la taifa kwa mchanganuo kuwa sekta ya mifugo kuchangia asilimia 7.1 na uvuvi kuchangi asilimia 1.1 ya pato la taifa. Pamoja na kutoa mchango huo, lakini utengwaji wa bajeti kwa miaka takribani kumi kuanzia 2011/12 hadi sasa kiasi kinachotengwa huwa hakizidi asilimia 1, hukomea kwenye asilimia 0.15 hadi 0.36. Aidha, ni dhahiri kuwa sekta ya mifugo na uvuvi imetawaliwa zaidi za wafugaji na wavuvi wadogo wadogo, kupuuza sekta hii ni kuwatupa watanzania walio wengi ambao wanatumia shughuli hizi kujikwamua kutoka kwenye hali ya umasikini. Pia, changamoto za utitiri wa kodi na tozo kwa wavuvi na sekta nzima kwa ujumla wake, unawashindilia kwenye umasikini na kuwafanya wafugaji na wavuvi kutonufaika na jasho lao.
Mwisho, Serikali inapaswa kuweka vipaumbele vya kuhakikisha, uhifadhi, uchakataji na utafutaji wa masoko ya uhakika na yenye tija kwa bidhaa za mifugo na uvuvi vinatengewa fedha za kutosha. Vilevile, Serikali iondoshe tozo, kodi zinazoweka vikwazo vya ukuaji na kuongeza mzigo kwenye sekta hizi muhimu.
Imetolewa na;
Ndugu Mtutura A Mtutura
Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
ACT Wazalendo.
26 Mei, 2022.
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter