Mara baada ya Mfumo wa Vyama vingi kuanzishwa hapa Tanzania kulikuwa na juhudi kubwa za Mashirika ya Kimataifa kuimarisha Vyama vya Siasa ili kujenga Mfumo Madhubuti wa Demokrasia ya Vyama Vingi. Katika Juhudi hizi ndipo Kituo cha Demokrasia kilianzishwa na ndugu Daniel Loya kupewa mzigo wa kuendesha kituo ambacho kilihusisha Vyama vya Siasa vyenye Wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpaka mauti yanamkuta Ndugu Loya alikuwa bado anaendesha chombo hiki muhimu sana katika kujenga Demokrasia madhubuti nchini Tanzania.
Mwanzoni mwa Mwishoni mwa Mwezi Januari mwaka huu nilikutana na Ndugu Loya Ofisini kwangu akija kunifahamisha kuwa napaswa kukabidhiwa rasmi Uenyekiti wa TCD. Tulizungumza mambo kadhaa ya kuwezesha kuifanya TCD kama jukwaa la kujenga maelewano miongoni mwa Wanasiasa ili kujenga uvumilivu wa kisiasa na kufanya mabadiliko muhimu ya sheria zetu kwa minajili ya kuhakikisha kuwa chaguzi zinakuwa Huru, Haki na zinazoaminika na kujenga utamaduni wa Uvumilivu wa kisiasa. Tulikubaliana kuwa katika mwezi huu wa Februari tuanze baadhi ya kazi ambazo tunapaswa kuzifanya ili kuirejesha TCD katika hali iliyokuwa nayo kabla ya mwaka 2015. Tulipanga kuzungumza tena, lakini Mwenyezi Mungu amepitisha uwezo wake na kumchukua kabla ya mazungumzo hayo na kuanza utekelezaji wa mipango yetu.
Katika mazungumzo yangu ya mwisho na ndugu Loya alinieleza mikwamo kadhaa ya kisiasa nchini haswa suala la Katiba Mpya licha ya juhudi kubwa za TCD kukutanisha viongozi wa Vyama vyenye Wabunge ili angalau kufanya mabadiliko madogo (minimum reforms) kuwezesha chaguzi Huru na Haki.
Loya ametangulia mbele ya haki akiwa na masikitiko makubwa sana kwetu wanasiasa kwa kushindwa kukubaliana mambo ya msingi na kuweka mbele maslahi ya vyama vyetu ama kung’ang’ania hoja chache muhimu lakini ngumu na kuacha hoja nyingi muhimu lakini zinazokubalika na pande zote. Aliongea kwa uchungu sana kuhusu hili na kunisihi sana katika kipindi changu kama Mwenyekiti wa TCD nijaribu kuwaunganisha Viongozi angalau kukubaliana katika mambo ambayo yanakubalika kwa wote na kuendelea kujadiliana kwa mambo ambayo hatukubaliani. Bahati mbaya mzigo huo wote Loya ananiachia peke yangu! Nitajitahidi kutekeleza wosia wake huo kwangu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Subhana Wataala.
Nami pia nilimpa wosia wangu. Nilimwambia aandike Kitabu kuhusu ushiriki wake katika kufanya kazi na Wanasiasa kupitia TCD. Alinikubalia lakini Mungu amemchukua. Ni wajibu wa watu wote ambao walifanya kazi na ndugu Loya kuona namna ya kuhakikisha kuwa kazi zake zinatunzwa na kuenziwa katika mifano ya watu ambao walitoa sehemu kubwa ya maisha yao katika kujenga Mfumo Madhubuti wa Vyama Vingi Nchini kwetu.
Leo tunamuaga ndugu yetu katikati ya misiba mingi sana. Ni muhimu kuwa na Mshikamano mkubwa kama Taifa ili kukabiliana na misiba hii. Tuwe pamoja na familia za wafiwa na kuwaombea kwa Mungu wavuke salama mitihani hii.
Kwa Familia ya Ndugu Loya, sisi kama TCD tutaendelea kumuenzi ndugu yetu kwa kufanya kazi ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na Mfumo Madhubuti wa Demokrasia katika hali ya Amani, Haki na Maendeleo endelevu kwa watu wetu. Tunawaombea kwa Mungu sana. Tunamwombea kwa Mungu ndugu yetu ampe utulivu wa milele. Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa na Jina lake Lihimidiwe. Amen.
Zitto Kabwe,
Kiongozi wa Chama ACT Wazalendo,
Mwenyekiti Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter