Vijana waliojitolea wapewe ajira. Kuwatelekeza haikubaliki.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA

Kuwatelekeza Vijana Waliojitolea Kufundisha Watoto Wetu ni Kuvunja Ari za Walimu
1. Utangulizi.
Ni miaka miwili sasa tangu Serikali ilipotangaza nafasi za ajira na kuajiri wataalamu wa uhandisi katika shule za ufundi nchini. Uamuzi wa kuajiri wataalamu wa fani hizo ambao hawakusomea ualimu ulitokana na upungufu wa walimu katika shule za ufundi nchini. Vijana walioajiriwa walikuwa na fani za uhandisi ujenzi, uhandisi mitambo, uhandisi umeme na uhandisi wa vifaa vya umeme ambao waliajiriwa kama walimu Daraja la IIIB na Daraja la IIIC.

ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa sekta ya vijana, kazi na ajira tumesikitishwa sana kubaini kuwa hadi mwaka huu 2022 vijana hao hawajapatiwa barua za ajira ama barua za kuthibitishwa kazi. Kitendo hiki cha kutopatiwa barua za ajira kinaenda kinyume na sheria na kanuni za utumishi wa umma (kifungu na 6(4) na kanuni ya 6(h), ambazo zinataka mwalimu baada ya muda wa matazamio (probation) kupatiwa barua ya ajira au kupewa muda miezi 6 wa ziada ikiwa amethibitika kutokuwa na uwezo.

Hali imekuwa tofauti sana kwa vijana hawa jambo linalopelekea kutoelewa hadhi yao (status) kama ni watumishi au wanachukuliwa watu wanaojitolea. Aidha, athari za kutothibitishwa au kupewa Barua ya ajira ni kukosa stahiki zao wawapo kazi kama zifuatazo;
• kupandishwa cheo,
• Kuhama/kuhamishwa kituo cha kazi (transfer)
• Hawawezi kupewa mafao yao ya kustaafu,
• Kukopa fedha Benki,
• hata wakifa ndugu hawatapewa mirathi.
Hivyo, barua ya ajira /barua ya kuthibitishwa kazini ni kielelezo kikubwa sana na muhimu sana. Leo vijana hawa wanaishi bila kujua hatima yao, wanapoteza ari na hamasa ya kazi.

2. Tumebaini nini?
ACT Wazalendo tumefuatilia suala hili kwa karibu katika chombo kinachohusika na walimu ambacho ni Tume ya Utumishi wa Walimu (Teachers' Service Commission -TSC). Madai yao kwamba vijana hao sio walimu kitaaluma hivyo wao kama TSC hawawezi kuwathibitisha kazini au kuwapa barua ya ajira.
Majibu haya ni dhihaka na dharau kubwa kwa vijana hawa walioamua kujitoa na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha ubora wa elimu yetu na kutimiza malengo ya kupata vijana wenye ujuzi na stadi za ufundi. Malipo ya uzalendo kwa nchi yao yanapaswa kuwa dhihaka na kejeli za namna hii?

Uzoefu unaonyesha kuwa hii sio mara kwanza kwa nchi yetu kuajiri walimu ambao kitaalamu sio hawakusomea ualimu hususani inapotekea mahitaji mkubwa wa walimu. Kwa mfano wakati shule za kata zilipoanzishwa nchini Serikali iliajiri vijana kwa mtindo huu 2006, 2008 na 2010. Taarifa zinaonyesha kuwa baadhi yao walipata misukosuko ya kufukuzwa kazi hasa katika kipindi cha sakata la vyeti ‘feki’ sababu hawakuwa na barua ya ajira. Serikali inataka kurudia tena makosa yale yale kwa vijana hawa?

3. Mapendekezo
Ili kuondoa hofu, wasiwasi na kuhakikisha haki za ajira za vijana hawa, ACT Wazalendo tunapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe haraka;

i. Serikali iwatambue kama watumishi wenye taaluma ya uhandisi ambao kituo chao cha kazi ni shule.
ii. Serikali kupitia waajiri wa walimu hao au watoke hadharani kuhusu hatima yao ili kuondoa wasiwasi walio nao.
iii. Ofisi ya Rais TAMISEMI na wizara ya fedha wachukue wajibu wa kuwapeleka masomoni hata kwa awamu vijana hao kuchukua diploma ya juu (Post- graduate diploma) ya ualimu ili wapate hadhi ya ualimu kama ilivyo kwa wengine.


Abdul Omar Nondo.
Msemaji wa Sekta ya Vijana kazi na ajira.
ACT Wazalendo
Twitter: @abdulnondo2
Facebook: Abdul Nondo
13 Oktoba, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK