September 22, 2020 9:12 AM

Wafanyabiashara, Sekta Binafsi na Uwekezaji nchini: ACT Wazalendo itafanya nini? #IlaniACT2020

ACT Wazalendo inaamini kuwa Sekta binafsi ndio Injini ya kuendesha Uchumi wetu na kuzalisha Ajira. Hivi sasa 91% ya Ajira zote rasmi Nchini Tanzania zinatokana na Sekta Binafsi. Wafanyabiashara wanaowekeza mitaji yao wanapaswa kuwekewa mazingira mazuri ya kufanya Biashara ili Serikali ipate Mapato ya Kodi na tozo mbalimbali kuendesha Nchi ikiwemo kutoa Huduma muhimu kama vile Maji, Afya, Elimu na Utawala. Ili kuwekeza ni lazima Watu waweke Akiba Lakini uwiano wa Akiba kwa Pato la Taifa Tanzania ni 16% na mahitaji ni angalau 30%. Hivyo lazima kutumia Akiba za Watu wa Nchi nyengine kuwekezwa nchini ( Foreign Direct Investments ) ili kuzalisha Ajira nchini, kuongeza Mapato ya Watu na kuongeza Akiba ya ndani.

Katika Kipindi cha 2020-2025 Serikali itakayoundwa na ACT Wazalendo na Vyama washirika itachukua hatua zifuatazo ili kukuza, kuendeleza na kulinda Sekta Binafsi, Wafanyabiashara na Uwekezaji

1. Itapitia mifumo yote ya kodi na kuhakisha kunakuwa na kodi rafiki kwa wananchi ili kuhakisha biashara zinakua na kuimarika na siyo kuwa na mfumo wa kodi ambao utapelekea kufunga au kuua biashara.

2. Itaondoa mfumo unaomlazimisha mfanyabiashara kulipa kodi kabla hajaanza kufanya biashara.

3. Itawapa wananchi uhuru na kuondoa urasimu katika kuanzisha na kuendesha biashara yoyote ikiwa ni pamoja na uhuru wa kununua na kuuza bidhaa zozote halali ndani na nje ya nchi bila vikwazo vyovyote.

4. Itarasmisha udalali wa kiasili kwa kuutambua, kuupa leseni na masharti ya kuwezesha Haki katika Biashara ya Mazao.

5. Itawezesha ufufuaji na uendelezaji wa viwanda vya kuchakata Pamba na kuzalisha nguo (textile industry) kwa kutunga sera na Sheria zitakazowezesha kupambana na Biashara haramu ya nguo ( smuggling of textile goods ), kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango sifuri Kwa vifaa vyote ambavyo ni malighafi kwa viwanda vya nguo, na kutoa mikopo Maalumu kwa Kipindi Maalumu yenye riba Maalumu ya kiwango cha mfumuko wa Bei kwa mnyororo wa thamani wa Pamba mpaka Nguo ( Cotton to Cloth ).

6. Itatoa ruzuku ya kikodi kufidia gharama za uzalishaji kwa Viwanda vinavyozalisha Bidhaa zinazotumiwa na Wananchi wengi zaidi kama vile Sukari, Mafuta ya kula na Vitabu/Karatasi kwa kulipia 50% ya Gharama za Umeme.

7. Itarekebisha sera za kodi ili kuirejesha katika hali yake ya kawaida sekta ya Utalii pamoja na mnyororo wake ambayo imeathirika sana na janga la COVID 19. Marekebisho hayo yatahusisha kutoa ruzuku kwa Kampuni za Utalii na kulinda Ajira za Wafanyakazi wa Sekta ya Utalii.

8. Itaweka vivutio vya kikodi ili kuwezesha sekta binafsi kujenga miundombinu wezeshi na muhimu kwa mfumo wa ubia. Hii itaipa Serikali pumzi ya kujielekeza kwenye kutoa huduma muhimu kwa wananchi, kuepuka kuongeza Deni la Taifa na kukuza sekta binafsi.

9. Itaweka vivutio vya kibajeti na kikodi kwenye Miradi yote ya Kilimo cha Umwagiliaji na Viwanda vyote vya kuongeza thamani ya mazao ya Kilimo.

10. Itarekebisha muundo mzima wa makato kutoka kwenye mapato ya Waajiri na Waajiriwa ili kuchochea matumizi kwenye uchumi kwa;

- Kupunguza Kodi ya Mapato kwa Wafanyakazi (PAYE ) kima cha chini mpaka 8% kutoka 9% ya sasa kwa kuanzia Mapato ya Shilingi 500,000 kwa Mwezi na kiwango cha Juu mpaka 25%
- Kurekebisha Tozo ya kuongeza Ujuzi (Skills Development Levy) kwa kuishusha mpaka 2% na italipwa na Waajiri wote ikiwemo Serikali na Taasisi zake zote.
- Kupunguza makato ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi WCF mpaka 12% kwa ujumla wake ( Mwajiri 7% na Mwajiriwa 5% ). Bima ya Afya na Fidia kwa Wafanyakazi itajumuishwa katika Mafao ya Hifadhi ya Jamii.
- Itaimarisha sheria ya kuzuia ukwepaji wa Kodi wa Makampuni ya Kimataifa ili kuokoa Mapato sawa na 5% ya Pato la Taifa ambayo yanapotea kupitia mbinu za kihasibu zinazofanywa na Multinational Corporations. Kuwezesha hili Serikali itaingia mikataba ya kimataifa inayosadia mataifa kuzuia ukwepaji wa kodi.

Showing 1 reaction

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK