Wananchi Walipwe Fidia Stahiki na kwa Wakati: Bonifasia

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA
WIZARA YA ARDHI NA MAENDELEO YA MAKAZI

HOTUBA YA MSEMAJI WA KISEKTA WIZARA YA ARDHI NA MAENDELEO YA MAKAZI NDG. BONIFASIA AIDAN MAPUNDA KUHUSU MPANGO NA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

Utangulizi
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angela Mabula Alhamisi tarehe 27 Mei, 2022 amewasilisha Bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22. ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa sekta ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Ndg. Bonifasia A. Mapunda, tumetumia siku mbili tangu kuwasilisha kwake kuipitia, kuichambua na kuzalisha maoni yetu kuhusu utekelezaji wa bajeti zilizopita, vipaumbele na mpango mpya wa bajeti ili kutoa fursa ya kuendeleza mjadala na kuleta mabadiliko tarajiwa kwenye sekta hii muhimu inayogusa Maisha ya watu. Katika kutekeleza wajibu wetu uchambuzi wetu utaangazia hoja tisa (9) na mapendekezo yetu kwa kila hoja.

1. Wananchi kucheleweshewa na kutolipwa kwa fidia za ardhi.
Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Utwaaji Ardhi Na. 47 ya Mwaka 1967 kinataka kiasi kinacholipwa kama fidia kiwe cha haki, cha kutosha, na kilipwe mara moja ndani ya miezi sita. Vinginevyo, riba sawa na ile itolewayo na benki za biashara katika amana za kudumu itatozwa hadi pale fidia itakapolipwa.

Kuna changamoto kubwa sana kuhusu utaratibu wa uthamini wa fidia, utolewaji wa fidia na ulipwaji wa fidia kwa wananchi kutoka kwa taasisi au mashirika ya serikali, makampuni na taasisi za nje yanapotwaa ardhi kwa ajili ya miradi.

Malalamiko ya wananchi kuhusu kucheleweshewa katika kulipwa fidia au kulipwa kiwango cha chini ama kutolipwa kabisa ni mengi sana lakini serikali kupitia wizara ya ardhi na Maendeleo ya makazi haichukulii kwa umuhimu juu ya changamoto hizi.

Mifano ni mingi sana kuanzia kwenye miradi mikubwa kama vile miradi ya Liganga na Mchuchuma, Mradi wa usindikaji wa gesi asilia wa Lindi, Mradi wa kupitisha bomba la gesi maeneo ya Mbande Dar es Salaam tangu mwaka 2012 hadi leo wapo wananchi hawajalipwa na wale waliolipwa wamelipwa miaka ya hivi karibu kwa kutumia tathmini iliyofanywa miaka kumi nyuma.

Hoja ya ucheleweshwaji wa fidia inathibitishwa pia na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa eneo la Liganga na Mchuchuma “kuhusu miradi ya Mchuchuma na Liganga zilibainisha gharama za fidia ya shilingi bilioni 4.48 kwa Mchuchuma na shilingi bilioni 8.84 kwa Liganga ambazo zililenga kulipa fidia kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya miradi. Hata hivyo, hadi wakati wa ukaguzi huu, hakuna mpango wa kulipa fidia hiyo ambao umefanywa licha ya kupita miaka sita.”

2. Upimaji na urasimishaji wa ardhi ya Vijiji

Mwenendo wa upimaji wa ardhi umekuwa na kasi ndogo sana ukilinganisha na mahitaji ya wananchi hivyo kupelekea uanzishwaji wa makazi holela. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya Vijiji 12,319 vilivyopo nchini, ni vijiji 10,762 ambavyo vimepimwa. Bado kuna idadi ya Vijiji 1,557 ambavyo havijapimwa.

Aidha, mchakato wenyewe wa upimaji umezalisha matukio yanayosababisha ongezeko la migogoro ya mipaka ya vijiji hii ni kutokana na ushirikishwaji hafifu wa wananchi wakati wa zoezi la upimaji wa mipaka.

Pia, kipaumbele kikubwa kwenye upimaji kimewekwa kwenye ardhi ya jumla na hasa kwenye miradi ya viwanja kwa kuwa imekuwa ikitumika kama chanzo cha mapato kutokana na uuzwaji wa viwanja.

Hii imesababisha hali ya upimaji wa ardhi za vijijini na hasa suala la utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji kuwa hafifu kwa kuwa haionekani kama chanzo cha mapato huku ikichangia ongezeko la migogoro ya ardhi inayotokana na kukosekana kwa upimaji.

Hali hii haikubaliki kwa namna yoyote katika umri wa miaka 60 ya uhuru.
Katika nyakati na zama ambazo shughuli za upimaji wa ardhi zimeboreshwa na kurahishwa kwa teknolojia na mbinu za kisasa, haiyumkiniki Serikali kushindwa kukamilisha upimaji wa Vijiji. Kutokamilishwa kwa upimaji wa Vijiji, kunalimbikiza na kuchochea migogoro ya ardhi na matumizi holela katika maeneo hayo. Tunaitaka Serikali ikamilishe mara moja upimaji wa Vijiji vyote vilivyopo nchini.

3. Kukithiri kwa migogoro ya ardhi vijijini na mijini.
Mfumo wa sasa wa milki ya hatima kuwa katika mikono ya Rais, umeendeleza ukiritimba na uhodhi wa dola linapokuja suala la ardhi. Rais ana mamlaka ya kutwaa, kuhawilisha, na kufuta hati ya ardhi ya mtu yeyote sehemu yeyote nchini na kwa ukubwa wowote anaoutaka kwa kile kinachoitwa ‘maslahi ya umma.’ Utaratibu tulionao ulitumika tangu kipindi cha ukoloni ili kuwasaidia wakoloni kupora ardhi ya wananchi.

Dola kuhodhi milki ya hatima ya ardhi ni jambo linaloathiri kwa kiwango kikubwa demokrasia kwa ujumla na kupunguza uwazi katika utawala wa nchi na kutoa mwanya kwa wabadhirifu na wala rushwa kuendeleza maovu yao bila kuwajibika. Kupitia taasisi zake, uchukuaji wa maeneo kwa jina la hifadhi, rachi ya taifa, vyombo vya ulinzi na usalama (Jeshi la wananchi na Magereza) serikali imekuta inachochea na kuzalisha migogoro.

Leo, tunaona nchi yetu imeendelea kughubikwa na migogoro ya ardhi katika maeneo na ngazi mbalimbali. Migogoro mingi imekuwa ikisababishwa na kutopimwa, kupangwa na kurasimishwa kwa ardhi, rushwa inayopelekea kuhamisha umiliki wa ardhi kinyemela, ukosefu wa ushirikishwaji katika mipango ya matumizi ya ardhi. Mipango na Mikakati mingi ya Serikali inayowekwa kukabiliana na migogoro ya ardhi inakwamishwa na kasi hafifu ya kukabiliana na vyanzo vya migogoro hiyo.

Tunaitaka Serikali kuunda Tume Maalum ya Taifa kwa ajili ya Uchunguzi (na kufanyia kazi mara moja mapendekezo yatakayotolewa) wa athari walizozipata na wanazozipata wananchi juu ya uporaji, uvamizi na unyang'anyi unaotokana na sera mbovu za ardhi zinazotekelezwa na Serikali zinazokumbatia soko huria bila kujali maslahi ya wananchi wanyonge.

4. Ukandamizaji na uporaji wa ardhi ya wananchi wa Ngorongoro.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni ardhi inayomilikiwa kimila na wananchi wa jamii ya wafugaji wa kimasai wa tarafa ya Ngorongoro yenye vijiji 25. Serikali imetangaza kuwaondoa wananchi hao kwa madai kuwa wananchi hao wanaharibu mazingira na ikolojia ya eneo hilo.

Jitihadi za muda mrefu za serikali kuwaondoa wafugaji hawa zina halalishwa kwa nguvu za vyombo vya habari, mashirika ya kimataifa na taasisi zingine zinazonufaika na uporaji wa haki za wanakijiji hao. Licha ya kupokea ukinzani mara zote, serikali ya awamu ya sita (6) inaenda kuweka rekodi ya ktimiza adhma ya kumalizia vitendo vya uporaji. Hali ya haki ya kupata, kutumia na kumiliki ardhi kwa wananchi hawa imekuwa tofauti kabisa na watanzania wengine, licha ya sheria za nchi kuwapa haki hiyo.

Wamekuwa wakikosa haki ya kushiriki na kushirikishwa katika maamuzi, wamekuwa wakikosa haki ya kujiendeshea shughuli za kupata uwezo wa kujikimu, huduma bora za Miundombinu, wamekosa huduma za afya, maji na elimu.
Serikali inatazama fedha zinazoletwa na utalii kuliko kuangalia hatima ya wananchi wake. Hivyobasi, imekuwa ikijenga hoja za chuki dhidi ya wafugaji hawa ili waweza kuwaondoa. Hoja za kuongezeka kwa idadi ya watu, kupotea kwa baianuai wakati uzoefu wa miaka mingi unaonyesha wananchi wa jamii ya kimasai wameishi Ngorongoro pamoja na wanyama pori bila kuathiri ikolojia imedhihirisha upekee wa eneo hilo la urithi wa dunia na kuthibitisha kuwa jamii ya wamasai si chanzo cha uharibifu wa hifadhi na ikolojia ya Ngorongoro, bali ni washirika muhimu wa uhifadhi.

Sisi, ACT Wazalendo tunaamini kuwa kulinda na kuhifadhi haki ya Wananchi wa Ngorongoro kutumia ardhi ya Ngorongoro ambayo ni urithi wao wa vizazi na vizazi. Hatua zozote zenye kuathiri haki za wananchi wa Ngorongoro kuishi na kutumia ardhi yao sharti zifuate na kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi.
ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza kuwa serikali iwashirikishe wananchi kwa kufanya mjadala kati yake na wafuga hao. Pia, serikali isitiozshe kabisa mchakato wa kuwahamisha wamasai hawa na iacahane na mapendekezo yaliyotolewa na ripoti ya mesto.

5. Kasi ndogo ya utekelezaji wa Mipango Miji
Kasi ya ukuaji wa miji nchini kwetu ni kubwa sana, hali hii inatokana na kiwango cha ongezeko la watu katika miji mingi nchini kuendelea kupaa kila mwaka. Vilevile, uhamiaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini kumepelekea kupanuka kwa maeneo ya miji. Pia idadi ya miji inaongezeka kadri vijiji vinavyopanuka na kubadilika kuwa miji. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 1967 wakazi wa miji walikuwa asilimia 5.7 na mwaka 2012 iliongezeka kufikia asilimia 29.1. Ukuaji wa miji nchini una kasi ya asilimia 7 – 11 kwa mwaka kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.5 kwa Afrika
Kasi ndogo ya upimaji wa miji imeendelea kusababisha ujenzi wa makazi kwa uholela bila mpangilio katika miji yetu. Kutopangiliwa kwa miji kusababisha wananchi wengi kuendelea kuishi katika hali na mazingira duni ya makazi. Vilevile kumeendelea kusababisha wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo hayajapimwa na kupangiliwa wakose huduma muhimu za miundombinu ya maji safi na maji taka, huduma za usafi wa mazingira, ukosefu wa usalama, barabara na hadhi mbovu ya makazi na miundombinu ya barabara.

Juhudi za Serikali kuhakikisha kasi ya upimaji wa maeneo ya makazi inakuwa mbele ya kasi ya mahitaji ya makazi kwa wananchi zinaonekana kushindikana. Kama tulivyozungumza katika Ilani yetu ya Uchaguzi, tunaitaka Serikali kupitia Wizara hii ifute gharama za upimaji wa viwanja nchi nzima, na ibebe gharama za kupanga miji.

6. Uporaji wa Ardhi kwa jina la uwekezaji.
Uchambuzi wa mwelekeo na mtazamo wa serikali kupitia hotuba na kauli za viongozi kuhusu ardhi, umejengeka kuona kwamba ardhi ni mtaji au bidhaa. Kwa mtazamo huu, ardhi inapaswa itumike kutengeneza faida zaidi kuliko kukidhi mahitaji ya kijamii.

Kwa muktadha huu, ardhi inawekwa kwa ajili ya wawekezaji au inachukuliwa kutoka kwenye miliki ya vijiji au wanavijiji ili kupatiwa mtu mmoja atakayetumia kwa ajili ya kupata faida. Dhana iliyojengwa na watawala kwa muda mrefu kwamba wazalishaji wadogo ni kikwazo cha Maendeleo, hivyo serikali inapaswa kuwapa fursa au kuwawezesha wakulima wakubwa hasa wawekezaji kuweza kupata ardhi kwa urahisi kwa misingi ya kwamba ndio wenye uwezo na ujuzi wa kuyaendeleza maeneo yao kwa faida. Kwa kutokuzingatia tatizo la msingi lilipo utekelezaji wa kipengele hiki tumeishia kuona uporaji na unyang’anyi wa ardhi za vijiji na wanavijiji,Maeneo mengi ya ardhi ya Wananchi yameendelea kukumbwa na kadhia ya kuporwa au kunyang'anywa ardhi kisheria kwa jina la uwekezaji.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha visa vya wananchi hasa wazee, wajane na masikini wakinyang'anywa na kuporwa ardhi zao. Visa hivi wakati mwingine vimekuwa vikipelekea matukio ya mapigano na mauaji kutokana na ugomvi wa kugombania ardhi.

Vilevile, kuna Wananchi ambao wamekuwa wakilazimishwa au kulazimika kuhama katika ardhi zao ili kupisha uwekezaji wa Serikali au watu, taasisi na makampuni binafsi wamekuwa wakipunjwa fidia.

ACT Wazalendo tunataka kuona Malalamiko na vilio hivi vya wananchi vinaisha kwani Sera na Sheria za Ardhi zinapaswa kumlinda mwananchi. Serikali iharakishe na kukamilisha zoezi la kupima, kurasimisha na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili kuepusha migongano na mivutano. Mamlaka za Halmashauri zijengewe uwezo stahiki na kuwezeshwa ipasavyo ili ziweze kushugulikia migogoro ya ardhi upesi na kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha ardhi imepimwa na kurasimishwa kwa wananchi.

Vilevile, mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji yaimarishwe, kusimamiwa na kujengewa uwezo ili yaweze kushugulikia, kuamua na kutatua masuala ya ardhi katika maeneo yao kwa wakati.

7. Uboreshaji wa nyumba za makazi
Pamoja na kujiendesha kibiashara, Shirika la Nyumba la Taifa lina dhima na wajibu mkubwa katika kuwahudumia wananchi na kushiriki ipasavyo kutatua changamoto ya ukosefu wa makazi bora kwa wananchi. Shirika hili bado halijaweza kuwa rafiki kwa wananchi wengi masikini na wa kipato cha kati. Hata hivyo, mahitaji ya Makazi bora kwa wananchi mijini na vijijini bado ni makubwa na yanaongezeka kwa kasi mwaka hadi mwaka. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuliwezesha Shirika hilo liweze kuwekeza vya kutosha katika nyumba za makazi ya Wananchi na kuwapangisha kwa gharama nafuu.

Changamoto nyingine ya shirika imekuwa ni miradi mingi inayoanzisha kukwama njiani au kuchelewa kukamilika na hivyo kusababisha hasara kwa shirika. Tunaitaka Serikali kuisimamia Bodi na Menejimenti ya Shirika ili liweze kujiendesha kwa ufanisi na kuwahudumia wananchi.

8. Haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake na vijana
Haki za wanawake katika kupata, kutumia, kumiliki na kufanya maamuzi juu ya ardhi hazizingatiwi ikilinganishwa na wanaume. Hii ni kutokana na mila na desturi zinazowanyima wanawake njia halali za kumiliki ardhi ikiwemo kurithi ardhi za wazazi na wenza wao na hivyo kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Wanawake wanapewa fursa ya kutumia ardhi na kufanya shughuli za uzalishaji lakini wanaume ndio wanaoamua namna ya kutumia mapato yanayotakana na nguvu ya mwanamke.

Wakati hali iko hivyo, makundi haya yana umuhimu wa pekee kimkakati katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii endapo yataweza kupata nafasi ya kumiliki ardhi hasa kwa ya uzalishaji mali. Ni muhimu Serikali ikaweka utaratibu wa kuhamasisha na kurahisisha umilikaji ardhi kwa Vijana na Wanawake badala ya kusubiri mirathi. Hii ni pamoja na kuhakikisha Wanawake na Vijana wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na kunufaika na fidia au faida ya rasilimali ardhi ya familia.

9. Mapitio ya sera na sheria za ardhi
Serikali kuanzisha mchakato wa mapitio ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013. Sheria na Sera hizi zilikuwa na malengo ya kuboresha usimamizi na utawala wa ardhi, na kutenga maeneo mahususi kama ardhi ya kilimo. Hata hivyo, michakato ya utungaji wa sheria na uandaaji wa sera ilifanyika kwa ukimya bila kushirikisha makundi makubwa ya wazalishaji wadogo. Kwahiyo, msukumo wa mabadiliko yaliyopo kwenye sera na sheria sio madai halisi ya makundi ya wazalishaji wadogowadogo bali mwendelezo wa shinikizo la siku nyingi wa kundi linalotaka kuona ardhi inabinafsishwa na kufanywa dhamana ya kuombea mikopo kwenye taasisi za kifedha.
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kufanya mapitio upya ya sera kwa kuwashirikisha wananchi wote ikiwa na mrengo wa kujali maslahi ya walio wengi (ambao ni wanavijiji na wazalishaji wadogo wadogo).

Hitimisho
Changamoto kubwa ya maendeleo ya sekta ya Ardhi na Makazi pamoja na kasi ndogo ya utatuzi wa migogoro na matatizo yanayoikabili Sekta hii kwa kiasi kikubwa inatokana na uwezeshaji hafifu wa bajeti ya Serikali unaopelekea Wizara kushindwa kuwekeza vya kutosha katika kukabiliana na changamoto zilizopo. Vilevile, kushindwa kutekeleza mipango na mikakati inayobuniwa katika kukuza mchango wa Sekta ya Ardhi na Makazi kwenye pato la Taifa na wananchi. Tunaitaka Serikali kuhakikisha inatekeleza ipasavyo mipango ya kibajeti kwa kuhakikisha fedha zinapatikana na kutolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Ardhi na Maendeleo ya Makazi ni Sekta inayohusu moja kwa moja ustawi wa mwananchi.
Imetolewa na:

Bonifasia Aidan Mapunda
Msemaji wa kisekta Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi,
ACT Wazalendo
28 Mei, 2022.
Dar es Salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK