ZITTO: SERIKALI ITEKELEZE MAKUBALIANO YAKE NA TCD YA UWEZESHAJI

MAELEZO (RISALA) YA MWENYEKITI WA KITUO CHA DEMOKRASIA TANZANIA NDG. ZITTO ZUBERI RUYAGWA KABWE KUMKARIBISHA MHESHIMIWA RAIS SAMIA SULUH HASSAN KATIKA MKUTANO WA KITAIFA WA HAKI, AMANI NA MARIDHIANO JIJINI DODOMA TAREHE 5 APRILI, 2022


Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kituo cha Demokrasia Tanzania ni Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali iliyoundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mabaraza ya Madiwani nchini. Kituo kilisajiliwa rasmi mwaka 2005 kama Jukwaa la kuwezesha vyama vya siasa kukutana, kuzungumza, kuendesha program za pamoja katika kuimarisha mfumo wa vyama vingi na utamaduni wa demokrasia ya vyama vingi, kutatua migogoro miongoni mwao na kushauri masuala mbalimbali kwa Serikali kwa manufaa ya Taifa. Vyama wanachama wa TCD hivi sasa ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha ACT Wazalendo, Chama cha Wananchi – CUF na Chama cha NCCR-Mageuzi. Vyama vya Siasa visivyo na uwakilishi katika vyombo vya hivyo ni vyama shiriki vya TCD na vinawakilishwa katika vikao vyote vya kikatiba vya TCD kupitia uwakilishi maalumu.
Mheshimiwa Rais, Kituo kimeandaa mkutano huu wa Kitaifa katika utamaduni wake wa miaka zaidi ya kumi ya kuwa na mikutano ya kuponya majeraha kila baada ya uchaguzi mkuu tangu mwaka 2005. Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu hatukuweza kufanya mkutano kama huu, ambao huwa tunauita kwa jina la mkutano wa ‘HEALING THE WOUNDS’, baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 na baada ya uchaguzi wa mwaka 2020. Ninachukua nafasi hii kwa niaba ya Viongozi wenzangu wa Vyama vya Siasa kukushukuru sana kwa kukubali kuja kutufungulia mkutano wetu huu.
Mheshimiwa Rais, Mkutano huu ni mwendelezo wa mchakato wa mazungumzo ambao uliuanzisha ulipoamua kuja hapa Dodoma katika ukumbi huu kufungua mkutano wa wadau wa Demokrasia ulioitishwa na Baraza la Vyama vya Siasa mnamo Mwezi Desemba mwaka 2022. Tangu ufungue mkutano ule ambao ulizalisha Kikosi Kazi cha Rais cha kushughulikia Hali ya Siasa na Demokrasia Nchini hatua kubwa zimepigwa katika kuweka sawa mazingira ya kufanya Siasa. Kwa furaha kubwa katika mkutano huu leo utahutubia wadau wa demokrasia katika hali ambayo mazingira ya kisiasa ni mazuri kwani hatua mbalimbali zimechukuliwa chini ya uongozi wako kuondoa vikwazo vya watu wote kushiriki katika michakato wa majadiliano ya kitaifa. Hongera sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Rais, mapendekezo yatakayotokana na Mkutano huu yatakuwa ni mchango katika Kazi za Kikosi Kazi chako ambacho umekipa jukumu la kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazokabili mazingira ya kufanya siasa na demokrasia katika nchi yetu. Baada ya kazi ya siku mbili, tutapeleka maazimio ya mkutano huu kwa Kikosi Kazi ili yaweze kufanyiwa kazi zaidi na kuwasilishwa kwako kwa hatua zinazofuata. Katika mkutano huu TCD imewaalika pia wajumbe wa Kikosi Kazi ili pia wasikilize maoni ya wadau katika kuboresha mapendekezo yao kwako.
Mheshimiwa Rais, pamoja na mambo mengine Mkutano huu utajikita katika kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria mbili ambazo kwa hakika ndio sheria kuu zinazozungumzwa sana na wadau wa Siasa. Sheria hizo ni Sheria ya vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi. Nachukua fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadam kwa msaada mkubwa waliotupa wa kutuandilia rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria kwa ajili ya kuwa na mjadala uliopangika katika mkutano huu. Vile vile mbele yako niwashukuru sana Taasisi ya TWAWEZA na Foundation For Civil Society kwa kufanya kazi kwa karibu na TCD kuhakikisha kuwa Mkutano huu unafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Rais, mwezi Julai mwaka huu nchi yetu inatimiza miaka thelathini tangu turejeshe demokrasia ya mfumo wa vyama vingi. Kama itakupendeza Mheshimiwa Rais na kama taratibu za Serikali zitakuwa zimekamilika kufuatia taarifa ya Kikosi Kazi, tutafurahi tutakapokuwa tunaadhimisha miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi tuwe tumefanya maboresho ya sheria ya vyama vya siasa.
Mheshimiwa Rais, katika mkutano huu pia tutatazama nyuma ili kupata mafunzo ya kwenda mbele. Tumewaomba Viongozi wa kisiasa waliokuwa wanaongoza TCD mwaka 2014 kuzungumza nasi kuhusu nini kilikwamisha mabadiliko madogo ya katiba yaliyokubaliwa na vyama vya TCD pamoja na Serikali. Lengo la majadiliano haya ni kujifunza kutokana na makosa ya nyuma ili kuweza kusonga mbele. Ninawashukuru sana Mheshimiwa Kanali Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara na Mheshimiwa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF kwa kukubali kukaa kwenye meza ya majadiliano na kutukumbusha hali ilivyokuwa na nini tufanye ili kufikia majawabu ya kwenda mbele.
Mheshimiwa Rais, ni matarajio yetu kuwa mkutano huu utafanyika katika kuangazia na kuzingatia misingi ya Haki, uhuru wa maoni, umuhimu uhuru wa vyombo vya maamuzi na utoaji haki, kutokuwa na ubaguzi na kuheshimiana.
Mheshishimiwa nimalize maelezo yangu haya kwa kusema mambo 3. Moja ni ombi kwako na mawili ni pongezi kwa watu wawili maalumu.
Nianze na pongezi kwako Mheshimiwa Rais kwa kukiamini Chombo hichi licha ya hali halisi kuwa chombo chetu hiki kilikuwa ‘dormant’ kwa muda mrefu tulipokuomba uje katika shughuli zetu hukusita kutukubalia mara moja. Hii inaonyesha dhamira yako ya dhati ya kusaidiana na watanzania wenzako kujenga Tanzania yenye maelewano. Sio tu ulitukubalia kuja kufungua mkutano huu lakini ulikubali hadharani ili kila mtu asikie. Tulifarijika sana na kwa hakika tunafarijika sana. Tutajitahidi kuendelea kutumia jukwaa hili kumaliza tofauti zetu ili sote kwa pamoja tujenge Tanzania yenye Haki, usawa na demokrasia madhubuti na inayoshamiri.
Mheshimiwa Rais, Kesho nitakuwa ninakabidhi uongozi wa TCD kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama chako, Chama cha Mapinduzi. Muda wangu wa uongozi umekwisha tangu tarehe 25 Februari 2022. Hata hivyo Chama chako walisema kuwa ni vema kukamilisha mkutano huu kisha niwakabidhi zamu yao ya uongozi. Nina imani kuwa Mwenyekiti mpya wa TCD kutoka CCM, Kanali Abdurahman Kinana, ataendeleza taasisi hii kwa juhudi kubwa. Tunamjua na anaijua vizuri TCD. Ni muumini wa siasa za majadiliano. Kufika kwako hapa leo sio tu ni heshima kubwa kwa Kituo lakini pia ni ‘endorsement’ kwa komredi Kinana, Mwenyekiti wetu mpya.
Mheshimiwa Rais, kabla ya kuchukua uongozi wa Taasisi yetu nilipitapita kuomba msaada wa kuwezesha kuirejesha TCD katika hadhi yake ya awali. Wengi niliowafuata waliniambia kuwa TCD haiwezi kuinuka tena. Wengine wakasema tuache ijifie, lakini mtu mmoja aliamua kuamini ndoto yetu ya kuifufua taasisi yetu. Sio mwengine bali ni Mheshimiwa Balozi wa Falme ya Denmark hapa nchini Balozi Mette Norgaard Dissing-Spandet. Nimesema nimtaje hadharani mbele yako Mkuu wa Nchi yetu kuonyesha shukrani zetu za dhati. Kwa muda wa miezi Sita alitusaidia kuwezesha mikutano yetu yote ya kikatiba kufanyika. Vile vile kwa kuwa wao wanafunga ubalozi wao alipeleka salamu za kutuombea kwa wenzake wanaobakia. Naamini kuwa wana diplomasia wengine watakuwa na moyo kama wake wa kuamini taasisi ya watanzania inayoendesha ajenda za kitanzania inaweza kuaminiwa na ikafanya mambo mema kwa faida ya Tanzania. Nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wadau muhimu kama vile Open Society Initiative for Eastern Africa (OSIEA), International Republican Institute (IRI), National Democratic Institute (NDI), Electoral Institute for Sustainable Democracy (EISA), Hans Seidel Foundation, Ubalozi wa Uingereza, Freedom House na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa michango yao ya kuwezesha mkutano huu. Asanteni sana
Mheshimiwa Rais, nimalizie kwa ombi mahususi kwa Serikali. Kituo hiki kinachoundwa na vyama vya Tanzania ni hatari sana kuachwa kuendeshwa kwa fedha za misaada kutoka nje. Ndio maana Serikali ya Awamu ya Nne iliamua kwa makusudi kutoa ruzuku ya uendeshaji kwa Kituo hiki kutoka katika Bajeti yake ya Serikali ya kila mwaka. Kituo kiliingia Mkataba na Serikali kwa ajili hiyo. Kwa niamba ya Viongozi wenzangu wa TCD ninakuomba Mheshimiwa Rais Makubaliano yale kati ya Serikali na TCD yarejee kutekelezwa katika Mwaka ujao wa Fedha unaoanza Julai 2022.
Baada ya Maelezo hayo nashukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupa heshima hii kubwa. Asanteni sana kwa kunisikiliza

Zitto Kabwe
5/4/2022

Dodoma. 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK