ACT WAZALENDO YALAANI MASHAMBULIZI DHIDI YA CHAMA CHA CCC ZIMBABWE

FUJO DHIDI YA WAFUASI WA CHAMA CHA UPINZANI ZIMBABWE CCC ZIKOMESHWE MARA MOJA

Jana tarehe 27 Februari, 2022 magenge ya wahuni wa Chama tawala cha Zanu PF cha Zimbabwe walivamia mkutano wa kampeni za Chama cha Upinzani cha Citizen's Coalition for Change (CCC Zimbabwe) na kuwashambulia vibaya wafuasi wa chama hicho kwa mapanga, nyaya, mikuki na zana nyingine hatarishi.

Tukio hilo lilitokea eneo la Mbizo Kwekwe, wakati Rais wa Chama cha CCC akiwa jukwaani akiendelea na hotuba yake ya kampeni. Katika tukio hilo, tumeelezwa kuwa mtu mmoja alipoteza maisha na wengine 17 walijeruhia vibaya na kulazwa hospitali.

Matukio ya namna hii, yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na mara zote yakiongozwa na magenge ya Zanu PF dhidi ya Chama cha upinzani cha CCC Zimbabwe.

Tuna taarifa kuwa tukio hili limejiri huku siku mbili kabla palitolewa kauli za kichochezi kutoka kwa mmoja wa viongozi waandamizi wa Zanu PF aliyesikika akisema 'watawasaga saga CCC mithili ya chawa', kauli ambayo haikukanushwa.

Tunashawishika kuamini kuwa mashambulizi dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa CCC ni mkakati ovu wenye baraka zote kutoka Zanu PF.

Hata hivyo, licha ya madhila yote ambayo wametendewa, mara zote wafuasi wa CCC wamekuwa waungwana na wastaarabu wakiepuka njia na matumizi ya vurugu katika kuendesha siasa zao hata pale wanapochokozwa na kuonewa.

Tunaamini kuwa ni ustaarabu wao huo ndio umewezesha kutunza amani ya Zimbabwe na kuwaepusha Wazimbabwe na machafuko ya kisiasa, kwani kwa wingi wa ufuasi na ushawishi mkubwa walionao kwa jamii endapo wakichukua mkondo wa kujibu na kulipiza visasi, ni wazi yatatokea maafa makubwa. Tunawapongeza wenzetu hawa wa chama rafiki cha CCC kwa ustahimilivu wao.

ACT Wazalendo tunalaani vikali na kupinga matumizi ya fujo na matendo ya kiharamia yanayoendeshwa na Chama cha Zanu PF.

Aidha, tunatoa pole nyingi kwa Rais wa CCC Ndugu Nelson Chamisa na wanachama wote wa CCC kwa madhila yaliyowakumba. Tunawatia moyo wasirudi nyuma kwani ushindi na ukombozi wa Zimbabwe unakaribia.

Vitendo vilivyotendeka havikubaliki katika nchi zinazofuata misingi ya Demokrasia na Haki za Binadamu kama Zimbabwe. Ni vitendo vinavyofanywa na watu au Chama kilichofilika uwezo wake wa ushawishi wa kisiasa kwa wananchi. Ni vitendo vya aibu.

Ni uhuni na uhalifu mkubwa usiopaswa kufumbiwa macho bila kuchukuliwa hatua. Ni matarajio yetu vyombo vya kisheria Zimbabwe vitachukua hatua kali haraka kuwakamata wote walioshiriki katika fujo hizo na kuwajibishwa kisheria.

Tunatoa wito kwa Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC kumuonya Ndugu Emerson Mnangagwa kuacha mara moja siasa za kiharamia katika nchi yenye kuongozwa na demokrasia ya kikatiba.

Tunatoa wito pia kwa Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika ya Ulinzi na Utetezi wa Demokrasia na Haki za Binadamu Afrika na Duniani, kuangazia kwa karibu matendo ya uvunjaji wa haki za binadamu yanayofanywa na Zanu PF dhidi ya CCC na kuchukua hatua kali dhidi ya Chama hicho na wahusika wengineo.

Afrika inastahili siasa safi, siasa za hoja, siasa za ushindani, siasa za kistaarabu. Vyama na makundi ya vyama yaliyopoteza uhalali wa kisiasa hayapaswi kuruhusiwa kuwa chanzo cha fujo na vurugu katika nchi zetu. Zanu PF iwajibishwe ili iache mara moja uharamia dhidi ya wananchi.

Imetolwa na:


Fatma A. Ferej
Katibu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
ACT Wazalendo.
28 Februari, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK