September 06, 2020 12:36 PM

AMANI NI TUNDA LA HAKI, BILA WAGOMBEA HAKUNA UCHAGUZI MKUU.

Tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, tayari kumejitokeza viashiria vya kuvuruga na kuhujumu uchaguzi kunakofanywa na vyombo vyenye dhamana ya kusimamia uchaguzi na amani ya Taifa kwa maana ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Jeshi la Polisi.

Vitendo hivyo, vikiachwa viendelee, bila shaka, vinaondoa uwezekano wa uwepo wa uchaguzi huru, haki na wenye kuaminika (free, fair and credible election).

Tangu awali, ACT Wazalendo tuliweka bayana kuwa mwaka 2020, kwa kutumia njia zote halali ikiwemo nguvu ya umma, hatutakubali vitendo vyovyote vya kuvuruga au kuhujumu uchaguzi ili kuisaidia CCM ambayo imeonesha dhahiri kuchokwa na wananchi.

Kwa mara ya mwisho, tunaikumbusha NEC, ZEC na Jeshi la Polisi kuacha mara moja vitendo hivyo kwa sababu vinaiweka rehani amani ya nchi. Amani na utulivu wa nchi upo mikononi mwao.

A: BILA WAGOMBEA, HAKUNA UCHAGUZI.

Kwenye zoezi la uteuzi wa wagombea wa Ubunge na Udiwani, Wasimamizi na Wasimamizi wa Uchaguzi ambao wengi ni makada wa CCM, wametumika kuhakikisha wagombea wetu na vyama vingine vya upinzani hawateuliwi. Kwa upande wa Zanzibar, katika majimbo 50, wagombea wetu 14 wameenguliwa. Kwa upande wa Bara, Kati ya wagombea 169 tuliosimamisha, ni wagombea 104 tu walioteuliwa.

Mbinu mbalimbali zimetumika kuwaengua wagombea wetu kinyume na utaratibu ikiwemo;

i. Wasimamizi wa Uchaguzi Zanzibar kughushi mapingamizi ambayo hayakuandikwa na wagombea (Mapingamizi hewa).

ii. Wagombea walioandika barua kwa waajiri wao kuenguliwa kwa kigezo cha kutopata ruhusa.

iii. Wasimamizi wa Uchaguzi kukataa kupokea picha za wagombea na kisha kuwaengua kwa kigezo cha kukosa picha kwenye fomu.

iv. Wasimamizi wa Uchaguzi kukataa kutoa kutoa au kupokea fomu za rufaa.

v. Wasimamizi wa Uchaguzi kutotoa sababu kwa maandishi sababu za kutowateua wagombea wetu

vi. Wasimamizi wa Uchaguzi kubuni mapingamizi nje ya yaliyoainishwa kwenye Kanuni na Maelekezo ya Uchaguzi (Mfano Kilombero kudai udhamini wa Katibu Mkuu).

vii. Wasimamizi wa Uchaguzi kukimbia ofisi zao na hivyobasi kuwanyima nafasi wagombea wetu kuchukua au kurejesha fomu (Ruangwa, Nachingwea, Mtama)

viii. Wasimamizi kubadilisha maandishi ya fomu za wagombea wetu.

ix. Wasimamizi wa Uchaguzi kukataa baadhi ya Wadhamini licha ya kwamba wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

x. Wasimamizi wa Uchaguzi Kutowateua baadhi ya wagombea kwa kigezo cha Chama "kutosajiliwa" kwenye Wilaya husika!!

xi. Wasimamizi wa Uchaguzi kukataa mihuri halali ya Mahakama

xii. Wasimamizi wa Uchaguzi kukataa mihuri halali ya Chama.

xiii. Wasimamizi wa Uchaguzi kufanya maamuzi kabla ya wagombea kupewa pingamizi au kabla ya kurejesha majibu ya pingamizi.

xiv. Wasimamizi wa Uchaguzi kupokea mapingamizi nje ya muda.

xv. Wasimamizi wa Uchaguzi kuwaengua wagombea kwa kigezo cha kushtakiwa na si kushtakiwa kama sheria inavyosema.

Chama chetu kimekata rufaa kwenye kila Jimbo na pale ambapo Wasimamizi wa Uchaguzi hawakutoa ushirikiano, tumeandika barua za malalamiko kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

MSIMAMO WETU.

1. Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwarejeshe wagombea wetu wote, Bara na Zanzibar waliongeliwa. Hatutakubali hata mgombea wetu mmoja kuenguliwa. Tunaendelea kusisitiza #HakunaWagombeaHakunaUchaguzi.

2. Dhamana ya amani ya Taifa ipo mikononi mwa NEC. Kwa kuzingatia hoja tulizozianisha hapo juu, NEC inapaswa kuwarejesha wagombea wetu wote. Umma upo tayari dhidi ya maamuzi kinyume na hayo.


B. IGP SIRRO, AMANI NI TUNDA LA HAKI!

Tarehe 4, mwezi huu Inspekta Jenerali wa Polisi Saimon Sirro alifanya ziara Pemba katika kile alichokiita "kuzungumza na wadau wa amani kisiwani Pemba". Badala ya kuweka mazingira ya amani, kwa masikitiko yetu, IGP Sirro ametumia ziara hiyo kutisha watu wetu na kuanza kuwasumbua viongozi wetu. Baada ya yeye kuondoka Pemba, bila shaka kwa maelekezo yake, baadhi ya viongozi na Wanachama wetu wameanza kukamatwa, kuhojiwa na kushikiliwa na Polisi. Hatua hii inalenga kujaribu kuwatisha viongozi wetu Pemba.

Waliokamatwa na kuhojiwa ni pamoja na Katibu wetu wa Mkoa wa Micheweni Ndugu Khatib Hamad Sheikh na Ndugu Hamad Akida Ali ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Mkoa wa Kichama wa Micheweni.

WITO WETU:

1. Tunamkumbusha IGP Sirro kuwa amani ni tunda la haki. Kuhubiri amani bila kusisitiza haki ni unafiki na kupoteza muda. IGP Sirro alipaswa kugusa kiini cha kile alichokiita viashiria vya kuvuruga amani Pemba ambacho ni kitendo cha Wasimamizi wa Uchaguzi na Maafisa wa Usalama, wote kutoka Bara kupelekwa kwenda kuvuruga uchaguzi Pemba.

2. Tunasisitiza msimamo wetu kuwa amani ya Pemba na Taifa kwa ujumla ipo mikononi mwa NEC na ZEC. Kama mgombea wetu hata mmoja akienguliwa kwa hujuma, tutatumia nguvu ya umma kupata tiba ya kudumu ya jambo hilo. Sisi viongozi wenyewe tutakuwa mstari wa mbele kwenye vuguvugu hilo.

HITIMISHO:

Kwetu ACT Wazalendo uchaguzi wa mwaka 2020 ni wa kipekee sana. Kwetu sisi amani itapatikana iwapo haki yetu pia itapatikana. Jitihada zozote za kutupora haki na ushindi wetu zitakutana na nguvu kubwa ya umma. NEC, ZEC na Jeshi la Polisi wanaweza kuiepusha nchi na machafuko kwa kutenda haki.

Showing 1 reaction

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK