A: UTANGULIZI
Ndugu Watanzania
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa tukiwa salama. Aidha niwashukuru nyinyi waandishi wa habari pamoja na vyombo vyenu vya habari mnavyoviwakilisha kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwapasha wananchi yanayoendelea nchini pamoja na mazingira magumu ya kazi mliyonayo. Ahsanteni Sana.
Ikiwa zimepita siku 12 tangu Uchaguzi (Uchafuzi) Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 ambapo wananchi walinyimwa fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa ngazi ya Rais, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Jamuhuri ya Muungano na Rais, Wawakilishi na Madiwani kwa upande wa Zanzibar.
Najua, na naamini nanyi mnajua, kuwa hazikuwa siku 12 rahisi, ni siku 12 za mauaji wa wananchi wenzetu, utekaji wa watendaji wetu, ukamataji wa wagombea, wafuasi na wanachama wetu, ubambikiaji wa kesi na makosa mbalimbali kwa waliokamatwa, utesaji wa majeshi na vikosi kwa wanachama wetu, udhalilishaji wa Wanawake waliokamatwa, na wizi wa kura wa hali ya juu ulioondoa kabisa hadhi ya Tanzania kama Taifa la Kidemokrasia.
Katika kipindi cha siku hizi 12 zilizopita, tumeweza kukusanya taarifa na ushahidi wa matukio mbalimbali ya kikatili yaliyofanywa na vyombo vya Dola. Hivyo basi, kuanzia leo, na kila nitakapopata nafasi, mimi na Viongozi wenzangu wa ACT Wazalendo tutakuwa tunazungumza nanyi Wanahabari, katika mfululizo wa mikutano yetu ya kuwajulisha mambo mbalimbali yaliyojiri na yanayoendelea nchini, tunayotendewa pamoja na hatua ambazo tunachukua. Huu utakuwa ni mkutano wetu wa kwanza katika mfululizo huo wa mikutano.
A: Wananchi Wenzetu 13 Wameuawa kwa Kupigwa Risasi
Ndugu Watanzania
Wananchi 13 wameuawa kwa kupigwa risasi na mabomu katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, mauaji haya yamefanyika zaidi kati ya Oktoba 27 na 29 Mwaka huu. Kati ya watu waliouawa mwanamke ni mmoja na wanaume ni 12. Mkubwa zaidi kati ya hawa waliouawa ni ndugu Chumu Kombo Saidi, mwenye umri wa miaka 45. Wanne kati ya waliouawa ni vijana chini ya miaka 20.
Mdogo zaidi kati ya waliouawa ni mtoto wa miaka 16 tu, nduguMasoud Salim Fadhi, aliyeuawa kwa kupigwa risasi ya tumbo, nyumbani kwao Mafya, katika jimbo la Wingwi, Pemba. Kijana mdogo amekatishwa maisha yake kwa sababu ya madaraka ya watu wachache tu wa CCM wasiokubalika na wananchi, na jambo baya zaidi ni kuwa vyombo majeshi yetu Watanzania, yenye wajibu na jukumu la kulinda uhai wa vijana wetu, ndio yaliyofanya mauaji hayo.
Damu za watu hawa 13 hazitapotea bure, Sisi ACT Wazalendo tutahaikisha uchunguzi wa vifo vyao unafanyika, wote waiohusika wanachukuliwa hatua, na haki za watu hawa pamoja na familia zao zinalindwa. Nimeambatanisha Orodha ya wote waliouawa katika taarifa yangu hii, kwa sababu za kimaadili, sitaambatanisha picha za wote hawa waliouawa ambazo tunazo.
B: Wananchi Wenzetu 102 Wamejeruhiwa kwa Risasi, Mabomu na Vipigo vya Wanajeshi, Wanawake Wamedhalilishwa, Mmoja AMEBAKWA
Ndugu Watanzania
Wananchi wenzetu 102 wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi, mabomu pamoja na vipigo vya wanajeshi. Wananchi 32 kati ya hao wana majeraha ya risasi, kuna ambao bado wako hospitalini na kuna waliopata ruhusa, watu 68 wana majeraha ya vipigo vya nyaya za umeme, marungu, magongo, shoka na fimbo za Polisi.
Mmoja wa majeruhi hawa ni mjumbe wetu wa Kamati Kuu, Ismail Jussa Ladhu, huyu alivunjwa mkono pamoja na bega, na jana amefanyiwa upasuaji mkubwa jijini Nairobi kurekebisha sehemu 9 zilizovunjika vibaya katika bega lake, upasuaji ambao ulifanyika kwa mafanikio makubwa.
Majeruhi mwenye umri mkubwa zaidi ni mjane Saada Ali Hassan, wa Garagara, Unguja, mwenye umri wa miaka 75, ambaye wanajeshi wetu walirusha bomu chumbani kwake lililomuunguza vibaya sana. Ana majeraha makubwa usoni na kichwani. Jana, Mwenyekiti wa Chama na aliyekuwa Mgombea Urais wetu wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alimtembelea Bi Saada pamoja na kwenda kuona nyumba yake iliyoharibiwa kwa bomu.
Unyama zaidi umefanyika kwa wanawake, nitatoa ushuhuda wa matukio machache kwa sababu ya muda. Makamu Mwenyekiti wa Vijana Taifa, Khadija Anuar, aikamatwa Pemba Oktoba 27, akapigwa mno, kisha akaachiwa. Akakamatwa tena Oktoba 29, akapigwa zaidi na kuachiwa kwa bahati mbaya, ameshindwa hata kulazwa hospitali, anajiuguza nyumbani, maana bado anatishiwa maisha. Huyu ni binti mdogo tu, Kiongozi wa Vijana wa chama chetu, anateswa namna hii.
Mwengine aliyepata kipigo sana ni dada yangu Mauwa Moh’d Mussa, mgombea Ubunge wa ACT Wazalendo wa Jimbo la Shaurimoyo, yeye alipigwa mno kwa waya, nondo na marungu. Alikamatwa Kwamtipura, Unguja.
Ukatili haujaishia hapo tu, mwanamke mmoja, ambaye sitamtaja jina kwa sasa, mkazi wa Kwamtipura, Unguja, alivamiwa kwake na wanajeshi, kudhalilishwa kwa kushikwashikwa viungo vyake vya siri, na kisha wakaamua KUMBAKA. Inaumiza sana.
ACT Wazalendo itadai haki za wote hawa, itahamasisha Michango ya wanachama wake ili kugharamia matibabu ya majeruhi hawa, na itahamasisha michango ya kukarabati nyumba ya Bi Saada iliyoharibiwa kwa bomu. Zaidi tutatafuta msaada zaidi kwa mama yetu wa Kwamtipura aliyebakwa.
C: Wanachama wa ACT Wazalendo 199 Wamekamatwa Mpaka Sasa
Wanachama na Viongozi wa ACT Wazalendo 199 Wamekamatwa mpaka sasa, wengi wao wameshikiliwa kwa Siku 8, wameachiwa juzi Ijumaa. Wengi wa tuliokuwa wagombea pia tulikamatwa, na tunaendelea kuripoti Polisi, ikiwemo mimi Zitto Kabwe, Mwenyekiti wetu wa Chama Maalim Seif, Madiwani Allumbula na Rashid Jumbe wa Kata za Kasingirima na Mwanzange, pia kuna wanachama wetu ambao wanaendelea kushikiliwa, hawa ni pamoja na Viongozi wetu watano (5) wa Jimbo la Liwale wanaoshikiliwa Lindi Mjini, pamoj na Vijana wetu 14 wanaohusika na ujumlishaji wa matukio Zanzibar.
D: Ni Siku 12 za Kushikiliwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa ACT Zanzibar, Nassor Mazrui
Miongoni mwa wanaoshikiliwa ni Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, Huyu alitekwa Unguja akiwa na Vijana wa ujumlishaji wa matokeo wa ACT Wazalendo Zanzibar (Tallying Center) 32, Polisi baadaye walikiri kumshikilia yeye pamoja na Vijana hao, baadhi ya Vijana wetu wameachiwa juzi baada ya kushikiliwa kwa siku 8, wakiwa wamepigwa mno kwa waya, fimbo na marungu, msichana mmoja akiwa amekaribia kuhribiwa jicho kwa sababu ya kipigo.
Naibu Katibu Mkuu Mazrui alipigwa mno wakati akikamatwa, majirani walioshuhudia wakati akipewa kipigo nje ya Hoteli ya Mazsons walitoa ushuhuda, na walimchukua akiwa tayari amezimia baada ya kipigo, tangu hapo hakuwa aliyewahi kumuona Mazrui, Leo ni siku ya 12, hatujui kama yu hai ama la, na kama alipata matibabu baada ya kipigo hicho. Mazrui ni mgonjwa pia, alifanyiwa upasuaji wiki kadhaa kabla ya Uchaguzi, hatujui kama anapatiwa dawa zake ama la.
Ofisi ya Kamishna wa Makosa ya Jinai (DCI) walitueleza kuwa wanamshikilia Mazrui, na kwamba wamemsafirisha kutoka Zanzibar (kinyume na Sheria) kumleta hapa Tanzania Bara, Japo hatukumuona.
Kesho Wanasheria wetu wataiomba Mahakama iwatake Polisi wamlete Mahakamani Mazrui, ama waache kumshikilia kwa Siku 12 kinyume na utaratibu.
F: Kuendelea kwa Hujuma, Vipigo na Kamatakamata
Bado hujuma dhidi ya wanachama na viongozi wetu zinaendelea. Jana vikosi vya SMZ vilivamia kisiwa cha Tumbatu na kuanza kupiga wananchi, na taarifa tunazozipokea kutoka Pemba ni kuwa kuna mpango wa Majeshi pamoja na Usalama wa Taifa wa kuchoma maeneo kadhaa ili kupata sababu ya kuendelea kuwakamata viongozi wetu. Tunajua kuhusu hilo.
Hatua za Jumla Ambazo ACT Wazalendo Tumeshachukua
1: Tumeandika Barua kwa Jumuiya ya Madola pamoja na Umoja wa Afrika kuwaomba wafanye uchunguzi Juu ya Uchaguzi wa Oktoba 28 pamoja na kusimamia kufanyika kwa Uchaguzi Mpya baada ya huu kuharibiwa.
2: Tumeandika Barua kwa Taasisi zote zinahusika na Masuala ya Haki za Binaadam kuwajulisha Juu ya Madhila ambayo tunapitia na kuomba washirikiane nasi katika kulinda uhai wa watu wetu na kudai haki zetu. Taasisi hizo ni Amnesty International, Human Rights Watch pamoja na Mahakama ya ICC.
3: Tumeziomba Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kutokutoa ushirikiano kwa Serikali zote mbili, za Muungano na ile ya Zanzibar, kwa sababu hazina uhalali.
4: Tumekataa kuutambua Uchaguzi huu, na tumeitisha Maandamano ya Amani ya Wananchi yasiyo na kikomo tangu Novemba 2.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Novemba 8, 2020
Dar es Salaam
Showing 1 reaction