Hotuba Mbadala ya ACT Wazalendo Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria Mwaka wa Fedha 2023/2024

HOTUBA YA WAZIRI KIVULI WA KATIBA NA SHERIA-ACT WAZALENDO NDG. VICTOR KWEKA KUHUSU MPANGO WA BAJETI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24.

Utangulizi.
Jana tarehe 25 April 2023 Wizara ya katiba na sheria iliwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23. Bunge liliijadili na kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 338.7 kwa ajili utekelezaji wa mpango huo.

ACT Wazalendo kupitia Wizara Kivuli ya Katiba na Sheria tumeupitia Mpango huo wa bajeti ambao umegusa taasisi zifuatazo zilizo chini yake; Tume ya Utumishi wa Mahakama (Fungu 12); Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Fungu 16); Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (Fungu 19); Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (Fungu 35); Mfuko wa Mahakama (Fungu 40); Wizara ya Katiba na Sheria - Wakala wa usajili ufilisi na udhamini na Taasisi ya Mafunzo ya uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Fungu 41). Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Fungu 55); Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Fungu 59);

Aidha, katika uchambuzi wetu tumehusisha mapitio ya utekelezaji wa bajeti wa mwaka 2022/23 na kutuwezesha kutoa mapendekezo yetu kama chama juu ya vipaumbele au maeneo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kwa mwaka huu wa fedha.
Maeneo saba (7) ya uchambuzi wa ACT Wazalendo kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

1. Kushughulikia urejeshwaji wa Watanzania wanaoshikiliwa na waliokutwa na makosa ya jinai Nchi za nje.
Miongoni mwa majukumu ya Wizara ni pamoja na kuratibu hurejesha kwa Watanzania au raia wa nchi zingine wanaotuhumiwa na uhalifu ili kuimarisha ushirikiano wa kisheria na mataifa. Katika kufanya hivyo Wizara inapitia mikataba ya urejeshwaji wa wahalifu watoro kutoka nchi mbalimbali na kujadili namna bora ya kuboresha mikataba husika.

Zipo taarifa za uhakika za kukamatwa kwa Watanzania 37 kati yao 24 walikuwa wavuvi kutoka Zanzibar na 13 kutoka Tanzania Bara ambao walienda kwa shughuli mbalimbali. Wavuvi hao walipatiwa vibali mapema mwezi Septemba 2017 kwa ajili ya kufanya shughuli za uvuvi kupitia Bahari ya Hindi. Mwezi mmoja baadae, yaani Oktoba 2017 kulitokea machufuko Nchini Msumbiji, ndipo wavuvi 24 na watanzania wengine (13) waliokuwa kwenye shughuli mbalimbali walikamatwa na kuwekwa magerezani. Hadi sasa zipo taarifa kuwa Watanzania 17 wamefariki wakiwa magerezani nchini Msumbiji na wengine kuendelea kushikiliwa bila msaada wowote.
Ukimya wa Serikali unaibua simanzi, sintofamu na kushusha imani za Ndugu, jamaa na marafiki juu ya hatima ya Ndugu zao waliopo vizuizini.

ACT wazalendo tunaitaka Serikali kupitia Wizara ya katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wizara ya Mahusiano ya Kimataifa na Mahusiano ya Afrika Mashariki Kufatilia mashtaka yote yanayowakabili Watanzania waliopo Nchini Msumbiji na Afrika ya Kusini na nchi nyengine kuhakikisha wanatendewa haki, na wanarudishwa nyumbani.

2. Ucheleweshaji wa upelelezi wa makosa ya jinai na mlundikano wa kesi katika mahakama.
Mfumo wa haki jinai nchini umekuwa na changamoto nyingi ambazo zinapelekea uonevu, ukandamizaji, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu. Maeneo makubwa yanayozaa madhila haya ni; Utaratibu wa ukamataji wa watuhumiwa; upelelezi wa makosa ya jinai; uendeshwaji na usikilizwaji wa mashauri mahakamani na utoaji wa adhabu.
Maeneo haya yanapelekea ukiukwaji wa haki za binadamu, kuwa na mlundikano wa mashauri unaosababisha msongamano wa mahabusu gerezani kwa sababu mbalimbali kama vile kutokamilika kwa upelelezi kwa muda mrefu.

Hoja hii inatumika na vyombo vya dola kuwashikilia watumiwa kwa muda mrefu hadi miaka 10, 15 hata 20. Pia, inaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi na hasara za kifedha kutokana na kuhudhuria mahakama mara kwa mara. Aidha baadhi ya watu kushawishika kutoa fedha ili kutaka kusaidia upelelezi kuwahi ili apate haki yake.

Hoja nyingine, watuhumiwa kukosa dhamana. Katika hoja hii inapaliliwa sana na uwepo wa Sheria nyingi zinazozuia dhamana au kuweka masharti magumu ya kupatikana kwa dhamana. Wananchi wengi wanajitikuta waathirika wa kunyimwa dhamana na kushikiliwa na vyombo vya dola kwa muda mrefu. Mifano ya Sheria hizo ni kama vile, Sheria ya Uhaini, Sheria ya kuzuia na kupambana na Ugaidi (Sura ya 19) 2002, Sheria ya Uhujumu Uchumi (2016), Sheria ya Unyang’anyi wa kutumia Silaha. Sheria na baadhi ya Vifungu vya sheria hizi zinatumika kuwakandamiza watu wenye mawazo ya kuikosoa Serikali au watu wasiokubaliana na viongozi wakubwa.

Katika, kushindilia hoja hii; juzi katika kuadhimisha Sherehe za Eid-fitri mwaka 2023 tuliona waraka wa viongozi wa dini ya Kiislamu wakielezea namna gani masheikh zaidi ya 151 ambao wanasota katika magereza mbalimbali nchini (Ukonga na Segerea 79; Gereza la Kisongo Arusha 27; Maweni Tanga 13; Butimba 11 na Gereza Kuu la Morogoro) kwa takribani miaka 10 tangu 2013. Inashangaza zaidi kuona watuhumiwa hawa wengine ni kutoka familia moja kuanzia kaka, baba, baba mdogo nakadhalika. Wananchi hawa wamekuwa wakinyimwa haki ya kujieleza katika mahakama kwa madai ya upepelezi kutokamilika huku wakiwa wamebambikiwa kesi za ugaidi. Sheria kandamizi zinatumika kuwabambikia kesi wapinzani wa Serikali na kuwaweka kizuizini kwa muda wowote watakaoona unafaa.

Hoja zingine ni; upatikanaji wa mashahidi, idadi ndogo ya rasilimali watu kama vile Majaji na Mahakimu, waendesha mashtaka na kadhalika.

Vilevile, Mifumo ya utoaji haki ni pamoja na kuwa na sheria bora, miundombinu thabiti ya utoaji haki (uwepo wa mahakama na nyumba za mahakimu kwa maeneo yenye umbali mrefu) ajira kwa mahakimu na majaji, urahishishaji wa usikilizwaji wa mashauri.
Kwa zaidi ya kipindi cha miaka 62 ya uhuru wa nchi yetu bado tuna maeneo mengi ambayo yanahitaji ujenzi wa majengo ya mahakama. Watu wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za utoaji haki ikiwemo uwepo wa vituo vya polisi ambavyo vinakuwa mbali na makaazi ya wananchi katika maeneo ya nchi yetu hasa vijijini.

ACT Wazalendo tunaitaka wizara ifanye maboresho ya mfumo wa upelelezi wa mashauri kwa kusimamia ukomo wa muda wa upelelezi na kuweka ukomo kwa makosa ambayo hayajawekewa ukomo ili kupunguza mlundikano wa kesi zinazochagizwa na upelelezi kutokamilika.

Pili, tunapendekeza kuwepo kwa dhamana kwa makosa yote na kuboresha utaratibu wa udhibiti wa dhamana kwa baadhi ya makosa. Ruhusa hii itaimarisha mfumo wetu wa haki jinai kwa kuondosha hila za kubambikiza kesi zisizo na dhamana ili kuwatesa na kuwakomoa wananchi.

Mwisho, Serikali ifanye mapitio ya Sheria zote kandamizi ili kuondoa vifungu vinavyotumika kuwaonea, kuwabagua na kuwanyanyasa wananchi.

3. Uchunguzi wa utekelezaji wa Sheria ya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargain).
Kwa miaka mitano minne mfululizo kuanzia 2019, tumekuwa tukitoa maoni kuhusu utaratibu wa Sheria ya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining).

Utaratibu wa makubaliano maalumu katika kesi ya jinai kati ya Mwendesha Mashtaka na Mshitakiwa ambapo Mshitakiwa anakubali kukiri kosa moja au zaidi katika makosa aliyoshitakiwa nayo ili apate nafuu ya kesi hiyo. Licha ya nia njema ya sheria hii, utekelezaji wake katika kipindi cha miaka takribani minne imekuwa na changamoto sana, imetumika kama nyenzo ya uporaji, unyang’anyi na dhulma. Sheria hii imekuwa mbadala wa upelelezi katika makosa ya uhujumu uchumi. Kwamba, ili umalize kesi, unaambiwa ulipe fedha ili utoke kwenye mikono dhalimu ya dola. Kutokana na hali hii, yapo malalamiko kwa watu kuporwa haki zao, mali zao na mambo mengi kinyume na sheria.

Mwaka 2022 katika uchambuzi wa ripoti ya CAG tuliibua hoja juu ya uporaji wa fedha uliofanywa na Ofisi ya Mwendesha Mashataka (DPP) kupitia Makabaliano ya Kukiri Kosa (Plea Bargain). Tulipendekeza ufanyike ukaguzi maalumu wa fedha hizo na iundwe tume ya majaji kufanya uchunguzi wa ukiukwaji wa haki katika mchakato huo. Tumeona ukaguzi maalumu umefanyika na CAG amependekeza ufanyike uchunguzi.

ACT Wazalendo tunarudia rai kwa Rais wa Jamhuri wa Muunga wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutekeleza pendekezo hilo la CAG. Hata hivyo, Chama chetu kinataka tume hiyo iwe ya kijaji yaani Judicial Commission of Inquiry.

4. Hatua za kukwamua mchakato wa Katiba mpya
Nchi yetu inapitia katika nyakati ngumu za mkwamo wa kisiasa. Serikali inapaswa kuweka fungu kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya kwa mwaka 2022/2023. Katiba imara ndio msingi wa haki, demokrasia na utawala bora wa sheria. Katiba yetu imepitwa na wakati na hivyo ni wazi tunahitaji mabadiliko ya katiba kwa kuandika katiba mpya ili kuendana na mazingira ya sasa na kuepusha nchi yetu kupita katika mkwamo wa kisiasa kwa maamuzi yatokanayo na utashi wa viongozi ambayo hayajawekewa utaratibu kisheria.

Pia Katiba mpya itaisaidia nchi yetu kurekebisha na kuimarisha mifumo ya kitaasisi na utendaji ikiwa ni pamoja na kuboresha miundo ya Serikali, na mapambano dhidi ya rushwa.
Kakika hotuba ya bajeti wizara ya katiba na sheria haijaonesha wazi ni Fungu kiasi gani limetengwa kwa ajili ya kukwamua mchakato wa katiba, haitoshi kusema kuwa Serikali inaandaa mchakato wa katiba, tulitegemea kuona mikakati ya wazi kama ambavyo Serikali imekua ikisema
ACT wazalendo tunaendelea kutoa mapendekezo yetu kwamba, ili kukwamua mchakato wa Katiba tumependekeza hatua zifuatazo;

Mosi, kupitiwa upya na kufanya marekebisho/mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Constitutional Review Act) na Sheria ya Kura ya Maoni (Referendum Act)
Pili, kujenga muafaka wa kitaifa kuhusiana na maeneo makubwa na muhimu yanayogusa mfumo wa kikatiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yamekuwa ndio chanzo na sababu ya mivutano katika maudhui ya Katiba Mpya. Maeneo hayo ni pamoja na Muungano na muundo wake, madaraka ya Rais, mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge (Legislature), Serikali (Executive) na Mahakama (Judiciary) na mfumo wa uchaguzi na uendeshaji wake.

Tatu, kuunda Timu ya Wataalamu Wabobezi (Constitutional Experts Commission), kutoka ndani ya nchi kadiri itakavyoonekana inafaa ambao watayaweka yaliyokubaliwa kwenye mwafaka wa kitaifa kupitia Mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa (National Consultative Conference)

Nne, Katiba Mpya kufikishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa KURA YA MAONI (referendum) ambapo iwapo itaungwa mkono na wananchi wengi (simple majority) wa upande wa Tanganyika na wananchi wengi (simple majority) wa upande wa Zanzibar, basi itakuwa imeridhiwa na kuidhinishwa rasmi.

5. Mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi na Vyama vya Siasa
Kalenda ya Uchaguzi inaonesha kuwa mwaka 2024 kutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na 2025 Uchaguzi Mkuu. Mtazamo wetu ni kuwa ili kuhakikisha jitihada za maridhiano na kuhakikisha haturejeshi nchi kwenye siasa za uhasama na uchaguzi usiokuwa wa haki, usawa na wenye ushindani, lazima dhamira hiyo itafsiriwe kwenye mchakato wa bajeti.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi si huru watendaji wake bado wanateuliwa na Rais hivyo ni lazima ifanyiwe marekebisho, vile vile Sheria ya vyama vya Siasa 2019 ilikuwa na lengo kuvidhibiti vyama vya siasa na kuua msingi wa kuanzishwa kwake kwa kumpa madaraka zaidi Msajili wa vyama. Hivyo Sheria zote mbili zinapaswa kuandikwa upya.

Nchi imeshuhudia matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika uchaguzi, kukiukwa kwa demokrasia kwa kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, na kupora haki za wapiga kura. Haya yote yametokana na sheria mbovu za uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa ambazo kwa makusudi zimekuwa zikipindishwa na wasimamizi ili kufurahisha utawala ulio madarakani.

Katika bajeti ya mwaka huu, tumeangalia katika vitabu vya randama, haijaelezwa kwa uwazi fungu gani na kiasi gani kimetengwa kwa ajili kukamilisha kwa michakato huo. Aidha, mpango haujaonyesha ikiwa mwaka huu itakuja sheria mpya ya uchaguzi na sheria mpya ya vyama vya siasa.

ACT Wazalendo tunarudia rai yetu kuwa Serikali itoe ratiba ya utekelezaji wa mageuzi ya kisiasa kama ilivyo kwenye mapendekezo ya kikosi kazi hatua kwa hatua ili itakapofika mwezi Novemba huu (2023) tuwe na Sheria mpya ya vyama vya Siasa, Sheria mpya ya uchaguzi na kwamba marekebisho ya Sheria ya mchakato wa Katiba mpya.

Tunataka kuona Taifa letu linaingia kenye Uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 tukiwa na Tume huru ya Uchaguzi na Sheria mpya ya vyama vya Siasa.

6. Changamoto katika mfumo wa utoaji wa Mafunzo ya Uanasheri kwa vitendo (LST).
Mjadala mkubwa kuhusu changamoto za Taasisi ya Mafunzoi ya Uanasheria kwa vitendo ulipata nguvu zaidi baada ya kwa matokeo ya mitihani ya Kundi la 33 tarehe 5 Oktoba, 2022 (ambayo yalionyesha ufaulu usioridhisha) na baadaye kupandishwa kwa ada ya masomo katika taasisi hiyo.

Wizara ilichukua hatua za kuunda kamati kwa ajili kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya wanafunzi na wadau wengine juu ya ufaulu. Kutokana na taarifa hiyo ya uchunguzi kuna changamoto ambazo tulitaraji zingiweza kutatuliwa au kuoneka mwangaza kupitia mchakato wa bajeti. Changamoto hizo ni kama vile upungufu na kukosa ubora wa Miundombinu ya kujifunzia; Kutokuwepo kwa mahakama ya kujifunzia, madarasa kukosa vifaa vizuri, upungufu wa wakufunzi na watumishi, kutokuwepo kwa mgahawa wa chakula na hostel.

Vilevile, kutokana na taarifa hiyo iliibua changamoto za kisera na kisheria (Masuala ya rufaa na utangazaji wa matokeo, mfumo wa utoaji wa matokeo kwa njia ya kieletroniki, kanuni na mifumo ya rufaa) ambazo zinahitaji bajeti ili kuweza kufanyiwa mapitio na marekebisho kama vile Mamlaka ya Baraza la Elimu ya Sheria (CLE) katika kusimamia elimu na taaluma sheria nchini.

Ili kukabiliana na changamoto za kimiundombinu Waziri aliahidi kuanzisha Fungu la bajeti kwa ajili ya Taasisi ya Mafunzo kwa vitendo ya sheria (LST) lakini tumeangalia kwenye vitabu vya randama hakuna fungu lililoanzishwa kwa ajili ya LST wala hakuna bajeti ya maendeleo ili kuboresha Miundombinu. Pia, hakuna bajeti wala mpango wa kuajiri wakufunzi kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji.

Hoja ya pili, kuhusu kupandishwa kwa ada ya gharama za mafunzo ya uanasheria kwa vitendo kutoka Shilingi 1,570,000/ hadi Shilingi 2,950,000/= kwa muda wa mwaka mmoja. Ongezeko hili la ada ni sawa na asilimia 88. Kwa mujibu wa utaratibu uliopo malipo hayo yanapaswa kufanywa kwa mkupuo ili uweze kukidhi vigezo vya kusajiliwa na kuendelea na masomo hayo.

Ongezeko hili la ada kwa wanafunzi wa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo linaongeza mzigo mzito kwao na kuwa kikwazo cha kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu sana. Wakati uhalisia unatuonyesha kuwa gharama za elimu zinapoachwa kwenye mabega ya wananchi, zinatengeneza matabaka ya upatikanaji wa elimu kati ya wenye nacho na wasio nacho.

Pia, uamuzi huu ni kufanya elimu hii kwa vitendo ni biashara na sio huduma. Kwa hiyo wenye uwezo ndio wataweza kununua na wasio na uwezo wataikosa. Uamuzi huu unapaswa kupingwa kwakuwa unakuza ubaguzi katika kupata haki ya elimu miongoni mwa watanzania kwa kigezo cha kipato.
ACT Wazalendo tunaitaka wizara ya Katiba na Sheria kuchukua za haraka kutatua changamoto zote zilizobainishwa na wadau.

Mosi, tunaitaka Wizara ya katiba na sheria itoe ruzuku ili kuiwezesha taasisi hiyo kumudu gharama za uendeshaji kuliko kuruhusu gharama hizo kubebwa na wanafunzi.
Pili, tunatoa rai kwa Wizara kupunguza gharama zingine ambazo bado zinabebwa na wanafunzi kwa asilimia 100 kwa kuweka mazingira wezeshi kama vile hostel na kutanua wigo wa mikopo ya Elimu kwa wanafunzi wa sheria kwa vitendo (LST).

Tatu, Kuhusu kuimarisha mafunzo kwa vitendo Serikali ianze kutekeleza mapendekezo ya kamati ya uchunguzi hususani kuhusu kusimamia kurejeshwa kwa Mahakama ya kujifunzia ambayo sasa inatumika kama Divisheni ya Mahakama Kuu (Rushwa na Uhujumu uchumi) na kuanzishwe mfumo wa kieletroniki katika uendeshaji wa mahakama (baadhi ya mahakama Dar) utakaounganishwa na madarasa ili kuwezesha wananfunzi kushuhudia mienendo ya mashauri.

7. Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Sheria
Uandishi wa nyaraka za Mahakama na matumizi ya Sheria kwa kiingereza umekua kikwazo kikubwa katika upatikanaji wa haki kwa Watanzania wengi na hupelekea kutumia gharama kubwa au kupoteza haki zao. Hivyo kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kutoa huduma za kimahakama na kwenye uandishi wa nyaraka za kisheria ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele na kuwekewa bajeti ya kutosha
Licha ya Serikali kubadili sheria na kufanya lugha ya mahakama kuwa Kiswahili bado sheria zetu nyingi zipo katika lugha ya kiingereza.

Licha ya uwepo wa jitihada za Mahakama kupitia jaji mkuu kutengeneza kanuni za matumizi ya lugha katika mashauri mbali mbali, bado jitihada hizo hajizakidhi haja na matakwa ya sheria kufanya Kiswahili kitumike katika sheria zetu ili kuwarahisishia wananchi kuwa na uelewa na sheria za nchi yetu. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inapaswa kufanya ufasiri wa sheria kuu na sheria ndogo kwa lugha ya Kiswahili ili kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi. Hii ni pamoja na kufanya urekebishaji wa zaidi ya Sheria 375 ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa ya jamii.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuweka mkazo katika kutafsiri na kuandika nyaraka za kisheria kwa Lugha ya Kiswahili kwa kutenga Bajeti maalumu kwa ajili hiyo ili kuwawezesha Watanzania kuelewa na kumudu kutafuta haki kwa urahisi.

Vilevile, tunaitaka Serikali kuweka wazi mikataba ya kitaifa na kimataifa kwa lugha ya Kiswahili ili kukuza uelewa wa wananchi katika mikataba inayoinufaisha nchi yetu.

Hitimisho
Katika wakati ambao taifa linatarajia mageuzi makubwa ya uendeshaji wa nchi yetu kwa kufanya mapitio ya sheria mbalimbali, kutungwa kwa sheria mpya, kuhuisha mchakato wa katiba mpya inategemewa wizara ya katiba kutazamwa kwa jicho la kipekee kibajeti. Ingawa, kitakwimu bajeti ya jumla ya wizara imeongezeka ikilinganishwa na ya mwaka jana. Lakini bado, inaacha wasiwasi kama inaweza kubeba dhima kubwa iliyopo kwenye safari ya mageuzi ya kisiasa. Tunaendelea kusisitiza kuwa tume ya kurekebisha sheria inapaswa kuongezewa uwezo mara dufu ili kubeba wajibu huu mkubwa kwa nchi yetu.

Imetolewa na;
Ndg. Victor Kweka,
Twitter: @Advocate_Kweka
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria
ACT Wazalendo.
26 April 2023.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK