Hotuba Mbadala ya ACT Wazalendo Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

HOTUBA YA WAZIRI KIVULI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI-ACT WAZALENDO NDG. MTUTURA ABDALLAH MTUTURA KUHUSU MPANGO WA BAJETI WA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24.

Utangulizi.
Jumanne tarehe 02/05/2023 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Ndg. Abdallah Hamis Ulega (Mb) aliwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania. Licha ya Bunge limeshapitisha bajeti hii, bado ipo fursa ya kuendelea kujadiliana ili kwa wakati uliopo yapo mambo yanaweza kufanyiwa marekebisho madogo ili kuhakikisha mpango na bajeti unaakisi mahitaji ya wananchi.

Kutokana na umuhimu huo, ACT Wazalendo kupitia kwa Msemaji wake wa sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliifuatilia hotuba hiyo na kuifanyia uchambuzi wa kina ili kubaini kama hotuba hiyo inaakisi hali halisi ya utatuzi wa changamoto zinazowakuta Wafugaji na Wavuvi hapa nchini.

Kupitia uchambuzi wa Msemaji wa sekta ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi tumeibua hoja zifuatazo kuhusu bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

A. Sekta ya Mifugo.
1. Ukamataji wa mifugo maeneo ya hifadhi.
Kumekuwa na unyanyasaji mkubwa sana kwa wafugaji hapa nchini unaofanywa na askari wa hifadhi kwa kutumia kisingizio cha wafugaji kuvamia maeneo ya hifadhi. Pamoja na kutenga maeneo ya hifadhi na maeneo ya malisho bado kumekuwa na ukamatwaji holela wa mifugo na utozwaji wa faini kubwa kinyume cha sheria za nchi.

Kumekuwa na tabia endelevu ya askari wa maliasili kuvamia wafugaji na kutaifisha mifugo yao kisha kuiuza kinyemela pasipo kufuata kanuni za mauzo ya minada kwa mali zinazotaifishwa, kupigwa risasi au kuwatoza faini kubwa kinyume cha sheria.Katika siku za hivi karibuni Kumekuwa na manung’uniko makubwa kwa wafugaji wa wilaya ya Kaliua wakiituhumu mamlaka ya hifadhi ya ISAWIMA kuwakamatia ng’ombe wao na kutoza faini kubwa ya kiasi cha Tsh 106,000 kwa kila ng’ombe na mchungaji wa ng’ombe kutozwa faini ya shilingi Milioni moja licha ya kufanya shughuli za malisho katika maeneo halali kimipaka na hifadhi husika.

Kutaifisha mifugo inayokamatwa katika maeneo ya hifadhi, mathalan mwezi Diemba 2022 Mifugo zaidi ya 2035 ilikamatwa na kutaifishwa katika hifadhi ya taifa ya Tarangire pamoja na hilo kumekuwa na kasumba mbaya kwa askari wetu ya kupiga risasi baadhi ya Mifugo na wengine kuwauza huko huko porini kinyume cha taratibu. Hii inawafanya wafugaji hapa nchini kuishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

ACT Walendo tunatoa wito kwa Taasisi za Serikali hasa mamlaka za hifadhi kuacha mara moja uonevu na unyang’anyi na kufuata sheria ili kuwafanya wafugaji wetu kuendesha shughuli zao kwa uhuru na Amani waweze kujitengenezea uchumi wao na kuboresha maisha yao.

Aidha tunaitaka Serikali itenge maeneo ya kutosha ya malisho ili wafugaji alishe mifugo yao katika maeneo hayo.

2. Upungufu wa Chakula cha Mifugo nchini
Hali ya upatikanaji wa chakula cha mifugo kwa mwaka 2022/23 imekuwa sio ya kuridhisha hususani mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo na Wanyama wengine. Hali hii imetokana na baadhi ya maeneo kutonyesha vizuri mvua katika maeneo yanayopata mvua za vuli. Takwimu za mifugo iliyoripotiwa kufa kutokana na kukosa malisha ilifikia hadi 240,000 kwa mwaka 2022/23.

Kwa upande mwingine, upatikana wa chakula cha mifugo inayotokana na mchanganyiko wa viwandani nao haikuwa nzuri. Chakula cha mifugo kama vile, kuku, chakula cha kunenepeshea ng’ombe na mbuzi, chakula cha Samaki. Kutokana na upungufu wa uzalishaji wa mazao ya nafaka nchini na uratibu mbovu wa soko la nafaka (Mazo mengi kuuzwa nje bila kuzingatia mahitaji ya ndani) ambazo hutumika kama malighafi za uzalishaji wa chakula cha mifugo. Imepelekea kupanda zaidi kwa gharama za chakula cha mifugo. Gharama ya chakula cha mifugo pia imeendeelea kuwa juu kutokana na Serikali kutotilia mkazo sekta hii kwa kuipa umuhimu stahiki.

Kwa mwaka 2022 ni maeneo 22 tu mapya ya kuzalisha vyakula vya mifugo yamesajiliwa katika mikoa nane (08) hapa nchini, pamoja ya kuwa sisi tuna rasilimali za kutosha ambazo tumekuwa tunawauzia Zambia na Kenya malighafi za kuzalisha chakula cha kuku na Samaki kutoka maeneo ya Bukoba, Geita, Mwanza na Simiyu ambazo ni dagaa na konokono zinazopatikana katika ziwa Victoria lakini chakula kingi cha kuku na Samaki tunavyotumia hapa nchini vinatoka nchini Zambia.

Mpango wa bajeti ya wizara kwa mwaka 2023/24 haujazingatia au kutoa kipaumbele katika kukabiliana na changamoto hizi ambazo tunaona zitaenda kutuathiri zaidi katika msimu huu ambao upatikanaji wa mvua umekuwa wa kusuasua au zimekuja kwa kuchelkewa sana.
ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali, kuweka mazingira wezeshi ya kujengwa viwanda hapa nchini ili viweze kusaidia upatikanaji wa uhakika na kwa gharama ndogo ili kukuza uchumi wa wafugaji na uchumi wa nchi.

Pili, Serikali itenge maeneo makubwa maalum ya Malisho ya chakula cha Ng’ombe Mbuzi na Kondoo Ili kukidhi hitaji la chakula cha Mifugo nchini, wafugaji wengi wanasafiri umbali mrefu kutafuta malisho na maji hali inayosababisha wakati mwengine wafugaji kuingia katika maeneo ya kilimo au hata hifadhi.

3. Migogoro ya wakulima na wafugaji.
Migogoro ya wakulima na wafugaji kwa miaka ya hivi karibu imezidi kushika kasi kubwa hapa nchini. Migogoro hii kwa sehemu kubwa hutokana na mifumo ya umiliki na matumizi ya ardhi miongoni mwa makundi haya mawili. Athari za migogoro hiyo imepelekea kuwa na mapigano baina ya wakulima na wafugaji, mauaji, uharibifu wa mali, ulemavu na kutoa matishio ya amani na usalama nchini. Mikoa ambayo inaonyesha kuchomoza kwa kasi ya Migogoro hiyo kwa sasa ni Mikoa ya Kusini (Lindi, Mtwara, Ruvuma), Magaharibi Kigoma na Katavi ambayo zamani hakukuwa na migogoro hiyo kabisa.

Sababu kubwa ya migogoro ni kutokuwa na mazingira mazuri ya ufugaji hususani malisho na malambo ya kunyweshea mifugo yao. Serikali inakwepa jukumu la kusimamia uboreshaji wa mazingira ya ufugaji ili kuwa na huduma hizo kwa wafugaji wadogo. Uzoefu unaonyesha migogoro inatokea kipindi cha kuanzia mwezi wa June hadi mwanzoni mwa mwezi Januari kila mwaka. Kipindi ambacho mito, mabwawa na nyasi hazipatikani kwa urahisi kwenye maeneo ya malisho ya mifugo. Hivyo, wafugaji kuswaga mifugo yao kwenye maeneo ya wakulima ili wapate maji na malisho ya kutosha.

Aidha, migogoro kati ya wananchi Wafugaji na Mamlaka za hifadhi imezidi kushika Kasi hapa nchini, Mamlaka za Hifadhi bila kujali athari kwa wananchi zimekua zikichuka maamuzi ya kumega maeneo ya wananchi na kuyatia kwenye Hifadhi jambo linaloacha madhara makubwa sana kwa wananchi mfano mzuri wa kadhia hii ni Mgogoro kati ya Wafugaji wa eneo la Ngorongoro. Migogoro ya wafugaji na hifadhi Kigoma (Kageramkanda Kasulu, Mpeta Nguruka), Tunduru hifadhi ya Selous.

Migogoro ya Wakulima na Wafugaji kwa miaka 62 ya Uhuru Inashawishi kuonesha kuwa kama Serikali ya CCM haijashindwa kuongoza nchi hii basi ni migogoro inayotelekezwa kwa ajili ya Maslahi fulani ya watu. Wakulima si maadui wa Wafugaji, mipango dhaifu na utengaji mdogo wa maeneo ya Wakulima na Wafugaji ndio vinasababisha wafugaji kulisha maeneo ya kilimo na wakulima kulisha maeneo ya Mifugo. Wafugaji wanalazimika kuhamahama kutokana na uhaba wa malisho na Malambo ya maji.

ACT Wazalendo tunatoa wito kwa Serikali kutatua changamoto za malisho na kuchimba mabwawa (marambo) ya kunyweshea mifugo. Pia Serikali iainishe umiliki wa ardhi na kuwarejeshea maeneo waliyotaifisha ili kuondoa migogoro inayoendelea hapa nchini.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali isitishe kabisa tabia ya kupanuwa maeneo ya hifadhi Kwa kuwanyang’anya wananchi maeneo yao ya kulisha mifungo na Kilimo. Kwani upanuzi huo unafifisha jitihada za wafugaji na wakulima katika uendeshaji wa shughuli zao za uchumi.

Tunaitaka Serikali Kusitisha Mpango wake wa kuwahamisha Wananchi jamii ya Wafugaji wa Ngorongoro Badala yake ikae na wananchi hao na kukubaliana namna Bora ya kusuluhisha Mgogoro huo.

4. Masoko ya mazao ya mifugo bado ni changamoto kubwa.
Hotuba ya Wizara ya mifugo na uvuvi bado imeshindwa kutupa majawabu ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao yatokanayo na mifugo. Mazao hayo ni pamoja na Nyama, Ngozi, Maziwa, pembe, kwato na Mifupa. Bado wafugaji hawana uhakika wapi watauza maziwa, Nyama, Ngozi na mazao mengine ya mifugo kama tuliyoanisha hapo awali. Hii inasababisha baadhi ya mazao mengine kuyatupa Kwa kukosa soko.

Serikali imeliambia Bunge kuwa imetafuta Masoko kupitia Maonesho na maadhimisho Maonesho ya Sabasaba, Maonesho ya Nanenane, maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani, Vipeperushi na vitabu pamoja na Ziara za Rais wa Awamu ya Sita katika nchi mbalimbali.

Katika kikao Cha Serikali na Wadau wa Sekta ya ngozi mwaka 2020 walitaja Soko la ngozi Kama changamoto kubwa kwao.
Hata hivyo licha ya Soko la nyama kutanuka Duniani hasa katika Nchi za Falme za Kiarabu, Komoro na Nchi nyengine za Asia lakini bado Jitihada za Serikali kutafuta Soko ni ndogo sana, na Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijaelewa wazi ni njia gani wataitumia kupata Masoko zaidi na Kuhakikisha Mazao ya Mifugo nchini yanapata Masoko ya Uhakika.

ACT Wazalendo tunaishauri Serikali ifungamanishe sekta hii na ya viwanda na Biashara kupitia TANTRADE Ili tupate viwanda vya kutosha vya Maziwa, Usindikaji wa Nyama na Ngozi pamoja na mazao mengine ya mifugo ili kuwawezesha wafugaji kupata masoko yenye uhakika na bei mzuri ili waweze kukuza uchumi wao.

Pili, Ili Kuongea ufanisi na uwajibikaji Tunaitaka Serikali ianzishe Bodi Moja ambayo itasimamia Mazao yote ya Mifugo (Nyama, Maziwa, Ngozi na Kwato) tofauti na ilivyo Sasa ambapo Kuna Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa tu.
Tatu, tunaishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ione namna Bora ya kuwapatia wawekezaji wa ndani nafuu ya uwekezaji (Investment Incentives)

Nne, Tunaitaka Serikali itumie vizuri Balozi zetu kutafuta masoko ya Bidhaa za Mifugo huko nje, kama balozi zetu zikitafuta vizuri Masoko ni wazi Wafugaji watapata tija ya ufugaji na kuchangia pakubwa katika Pato la Taifa na kukuza uchumi wa Wafugaji.

B. Sekta ya Uvuvi.
5. Kufungwa kwa Shuguuli za uvuvi Ziwa Tanganyika
Tangu Serikali ilipotangaza nia ya kulifunga Ziwa Tanganyika kwa kuzuia shughuli za uvuvi iliibua hofu kubwa sana kwa wadau wa mazao ya uvuvi kwenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa ambao kwa sehemu kubwa wanategemea ziwa hilo kwa kuwa itaenda kuwaacha bila ya kuwa na shughuli mbadala za kujikimu.

Ingawa, ACT W azalendo tunatambua kuwa Serikali za Tanzania, Burundi Zambia na DRC kwa pamoja zimeazimia kufunga kwa miezi mitatu shughuli za uvuvi kwenye ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu kuanzia tarehe 15 Mei 2023 hadi tarehe 15 Agosti mwaka huu. Bado tunaona hatua hizi hazitoacha athari sawa kwa pande zote lakini sio njia sahihi za kushughulikia changamoto zozote zinazodhaniwa kumalizwa kwa kuchukua hatua hizo.

Maeneo mengi ya nchi yetu yanayojihusisha na shughuli za uvuvi, wananchi wa maeneo hayo hawana shughurli zingine mbadala za uchumi, kufunga ziwa kunawafanya kujiingiza katika matukio ya kiuharifu.

ACT Wazalendo hatubaliani na hatua hii ya Serikali kutokana na ukweli kuwa Serikali yenyewe ilikiri tangu mwaka 2022 kwamba takwimu za mwaka 2011 zinazotumiwa na wataalamu hazifai tena kutumika kufanya tathmini ya shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika. Aidha, kutoshirikishwa na kuchukua maoni kwa wavuvi ni kunyima fursa ya hatua nzuri zisizoacha athari kwa wanufaika.

Hivyo, tunaitaka Serikali kusitisha azma yake ya kufungwa kwa shughuli za uvuvi kwenye ziwa Tanganyika hadi ushirikishwa wa wadau hawa ufanyike.

Aidha, ikionekana ni lazima kufungwa kwa shughuli hizo lifungwe kwenye maeneo ya fukwe pekee kwa kuwa kisayansi mazalia ya samaki hufanyika kwenye fukwe za maziwa hali halisi ya samaki kuzaliana na maeneo ya kina kirefu shughuli za Uvuvi zingekuwa zinaendelea.

6. Serikali itengeneze Bandari za Uvuvi na inunue Meli za uvuvi ili kuiinua sekta ya Uvuvi nchini.
Shughuli za uvuvi kwenye maji ya asili huendeshwa na wavuvi wadogo ambao huchangia zaidi ya asilimia 95 ya Samaki wote wanaozalishwa nchini na asilimia tano (5) iliyobaki huchangiwa na uvuvi wa makampuni (kibiashara). Takribani miaka sitini na mbili (62) sasa, bado Serikali inaburuza miguu kufanya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa bandari za uvuvi katika pwani ya nchi hii, licha ya nchi yetu kubarikiwa kwa kuwa na fukwe ndefu. Kutokuwepo kwa bandari ya uvuvi inachochea kupoteza mapato ambayo yangepatikana kutokana na leseni, tozo kwa meli zinazovua katika ukanda wa bahari na fukwe.

Katika hotuba ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka fedha 2022/23, Serikali imeishia kutaja tu kukosekana bandari ya uvuvi kuanzia Tanga hadi Mikindani, Mtwara kunaipotezea Serikali mapato, uvuvi wa bahari kuu unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa meli kwa wavuvi wetu, Serikali iliahidi kuwa hadi kufikia mwezi Januari 2022 Tanzania itakuwa imeshaleta meli mbili (2) za uvuvi. Lakini katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu inadhihirisha kuwa meli hazijanunuliwa yalikua ni maneno matupu.

Serikali imedanganya umma, hakuna bandari ya uvuvi iliyojengwa wala meli iliyonunuliwa.
Waziri Wa Mifugo na Uvuvi ndg. Abdallah Ulega Amaeliambia Bunge kuwa Mpango wa Kununua meli bado Upo kwenye Maandishi ya Mpango wa Biashara (business plan) ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ambapo itashirikisha Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP),
Kuhusu Bandari ya Uvuvi Serikali Waziri amelieleza Bunge kuwa Katika mwaka wa Fedha 2022/23 Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa masoko ambapo Mkandarasi amekamilosha Usanifu kina (Detail Design) umefanyika na kazi imeanza.

Bado miradi ya Bandari za Uvuvi nchini haijapewa kipaumbele na Serikali, ukosefu wa Bandari na Meli za Uvuvi vinadumaza shughuli za Uvuvi katika Bahari kuu na kuzorotesha Sekta ya Uvuvi na kuwaacha wavuvi katika umasikini wakutupwa.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali ijenge bandari za uvuvi Mikoa ya Tanga, Pwani (Mafia) Dar es Salaam, Lindi na Mtwara. Aidha, Serikali inunue meli za Kitaifa za uvuvi pamoja na kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kwa Kukamulisha haraka kwa kuzindua menejimenti ya Shirika na kukamilisha ukarabati wa jengo la makao makuu yaliyopo Kigamboni ili kuboresha na kuimarisha sekta ya uvuvi wa bahari kuu.

7. Uvuvi haramu.
Kumekuwa na doria mbalimbali zinazoendeshwa kwa lengo la kudhibiti uvuvi haramu. Hii ni hatuwa njema, kwani Uvuvi kwa njia haramu zinazoangamiza samaki na mazalia yake haziwezi kuungwa mkono na Chama Makini Cha ACT Wazalendo.
Tusichounga mkono, ni doria kugeuka kuwa kero kubwa kwa wavuvi na kusababisha mianya ya rushwa kwa maafisa uvuvi hapa nchini. doria hizi zimekuwa zikiwakumba mpaka wanunuzi wa samaki kwa lengo la kitoweo.

Doria hizi zinaendeshwa kama njia ya kujipatia kipatocha ziada maafisa wa Idara ya Uvuvi.
Kuna utaratibu umeanzishwa na maafisa uvuvi wa kuwataka wavuvi wasio na leseni ya Uvuvi, wachange fedha na kuwakabidhi ili wawaruhusu kufanya uvuvi.
Wasipofanya hivyo inapita doria kali inayokamata vifaa vyao na kuviteketeza na kuwapiga faini kubwa.

ACT Wazalendo kimeamua kupaza sauti ili Serikali ifanye uchunguzi juu ya malalamiko haya ya wavuvi aidha Serikali ielewe kuwa mfumo wa doria umeshindwa kuliondowa tatizo la Uvuvi harama na badala yake umesababisha ukandamizaji kwa wavuvi na kuwanufaisha maafisa wa uvuvi. ACT Wazalendo tunapendekeza yafutayo kuondoa tatizo la Uvuvi haramu;

Mosi, Kutoa Elimu ya kutosha kwa wavuvi juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazalia ya samaki
Pili, kutowa hamasa kwenye taasisi za fedha kutowa mikopo Kwa wavuvi wadogo Ili wapate nyenzo sahihi za uvuvi zitakazowsletea tija.
Tatu, Kufunga viwanda vyote vinavyokaidi kusitisha kutengeneza vifaa haramu vya uvuvi. Kuendelea kuwaachia kuzalisha vifaa hivyo, vikinunuliwa na wavuvi ndipo Serikali inajitokeza, hakuleti taswira inayofaa ya Utawala Bora.

Hitimisho.
Bajeti inayotengwa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itazamwe upya na kuboreshwa ili iweze kukidhi matakwa ya sasa ya sekta hizo.
ACT Wazalendo hatuoni sababu kwa nini Sekta hizi mbili zisitowe mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa. Kuendelea kutenga bajeti ndogo ni muendelezo wa kudumaza Sekta hizi mbili na hatimaye kuwa muendelezo wa kuwafukarisha wafugaji na wavuvi ambao ni kundi kubwa la watanzania. Serikali iangalie mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi, ili sehemu kubwa ya thamani imwendee mfugaji na mvuvi.

Imetolewa na;
Ndg. Mtutura Abdallah Mtutura
Twitter: @MtuturaAbdallah
Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
ACT Wazalendo.
04 Mei, 2023

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK