HOTUBA YA MSEMAJI WA KATIBA NA SHERIA ACT WAZALENDO NDG. VICTOR KWEKA KUHUSU HOTUBA YA SERIKALI BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.

HOTUBA YA MSEMAJI WA KATIBA NA SHERIA ACT WAZALENDO
NDG. VICTOR KWEKA KUHUSU HOTUBA YA SERIKALI BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.

Utangulizi:

Leo tarehe 28 April 2022 Wizara ya Katiba na Sheria imewasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 huku ikijikita kwenye maeneo yanayogusa; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Ofisi ya Taifa ya Mashtaka; Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania; Tume ya Utumishi wa Mahakama; Wakala wa usajili ufilisi na udhamini; Taasisi ya Mafunzo ya uanasheria kwa Vitendo Tanzania.
Katika uchambuzi wetu ACT Wazalendo, tumegusa maeneo makuu saba (7) kutoka katika hotuba ya Wizara ya Katiba na Sheria kama ifuatavyo:

1. Mabadiliko ya katiba - Katiba Mpya
Miaka ya hivi karibuni, nchi yetu imepitia katika nyakati ngumu za mikwamo ya kisiasa. Serikali inapaswa kutenga fungu kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya mchakato wa kupata katiba mpya inayoleta matumaini ya demokrasia na maendeleo kwa wananchi. Katiba imara, yenye sauti za wananchi ndiyo msingi wa haki, demokrasia na utawala bora wa sheria. Katiba yetu ya hivi sasa, imepitwa na wakati na hivyo ni muhimu kwa taifa kufanya mabadiliko ya katiba. ACT Wazalendo, tunaungana na wadau wengine wa kisiasa kuisihi Serikali kukubali mapendekezo yetu ya kuandika katiba mpya ili kuendana na mazingira ya sasa na kuepusha nchi yetu kupita katika mikwamo Zaidi ya kisiasa itokanayo na maamuzi, utashi wa viongozi na ambayo hayajawekewa utaratibu kisheria. Pia, Katiba Mpya itaisaidia nchi yetu kurekebisha na kuimarisha mifumo ya kitaasisi na utendaji ikiwa ni pamoja na kuboresha muundo ya Serikali, na mapambano dhidi ya rushwa.
Serikali ya awamu ya nne iliweka kipaumbele katika swala la katiba mpya, hata hivyo ni wazi kwamba mchakato ule uliharibiwa kwa makusudi na wanaCCM kwa kufanya mchakato kusimama hadi sasa. Katika kipindi cha mwaka 2015-2020 Serikali ya awamu ya Tano haikuweka kipaumbele katika swala la katiba mpya kwa kua haikuona umuhimu wake na kuishia kujali tuu maslahi yake ya kisiasa. Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikisitasita katika kuweka kipaumbele kuhusu mchakato wa katiba mpya.
2. Mabadiliko ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa
Sambamba na mabadiliko ya Katiba, ni wazi kwamba kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi sasa nchi yetu imepitia katika kipindi kigumu cha mkwamo wa kisiasa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa demokrasia katika chaguzi zote za nchini. Nchi imeshuhudia matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika chaguzi, kukiukwa kwa demokrasia kwa kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, na kupora haki za wapiga kura. Haya yote yametokana na sheria mbovu za uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa ambazo kwa makusudi zimekuwa zikipindishwa na wasimamizi ili kufurahisha utawala ulio madarakani.
ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuweka fungu kwa ajili ya uandikwaji wa sheria mpya ya vyama vya siasa na uchaguzi ili kuimarisha utawala wa sheria kwa kuweka usawa, uhuru katika uchaguzi na haki ya vyama vya siasa kufanya shughuli zake kisheria.
Sheria bora za Uchaguzi na Vyama vya siasa vitachagiza demokrasia makini na thabiti na utawala wa sheria katika chaguzi na shughuli za vyama vya siasa.

3. Ufanyike uchunguzi na fidia kwa wote walioporwa fedha zao kabla na baada ya uwepo wa sheria ya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargain).
Sheria ya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) imeweka utaratibu wa makubaliano maalumu katika kesi ya jinai kati ya Mwendesha Mashtaka na Mshitakiwa ambapo Mshitakwa anakubali kukiri kosa moja au zadi katika makosa aliyoshitakiwa nayo ilia pate nafuu ya kesi hiyo. Licha ya nia njema ya sheria hii, utekelezaji wake katika kipindi cha miaka takribani minne imekuwa na mashaka na kupelekea vitendo vinavyokiuka haki. Sheria hii imetumika kama nyenzo ya uporaji, unyang’anyi na dhuluma. Pia, imekuwa mbadala wa upelelezi katika makosa ya uhujumu uchumi. Watuhumiwa ili wamalize kesi, inawataka walipe fedha ili watoke kwenye mikono dhalimu ya dola.
Utekelezwaji wa sheria hii sio wa pande mbili, hakuna makubaliano mwendesha mashtaka ndio mwenye uamuzi - mshtakiwa anapewa chaguo moja tu_kukiri kosa. Kutokana na hali hii, yamekuwepo malalamiko kwa wananchi kuporwa haki zao, mali na mambo mengi yanayotendeka kinyume na sheria. Mwaka 2020-2021 tumeshuhudia malalamiko mengi ya watu kuporwa fedha, mali na malalamiko mengi yanayofanana na hayo. Hata hivyo tumeshuhudia kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wa Hai kwa tuhuma zinazofanana na hizo zikiwemo za matumizi mabaya ya madaraka. ACT Wazalendo inaitaka Serikali ya awamu ya sita kuweka fungu la fidia kwa wale wote waliopoteza mali na fedha zao wakati wa kipindi cha mwaka 2015 - 2021 kwa kufanya uchunguzi na kubaini wananchi wote waliopoteza mali zao kwa matumizi mabovu ya madaraka.

4. Uimarishaji wa mfumo wa utoaji haki
Katika kuangalia mnyororo wa mfumo wa haki jinai nchini hususan kuanzia ukamataji wa mtuhumiwa; upelelezi wa makosa ya jinai; uendeshwaji na usikilizwaji wa mashauri mahakamani na utoaji wa adhabu; pamekuwa na changamoto kubwa zinazopelekea kuwa na mrundikano wa mashauri. Hii imesababisha msongamano wa mahabusu gerezani kwa sababu mbalimbali kama vile kutokamilika kwa upelelezi kwa wakati, watuhumiwa kunyimwa dhamana, kungoja upatikanaji wa mashahidi, idadi ndogo ya watumishi wa Mahakama kama vile Majaji na Mahakimu, waendesha mashtaka na kadhalika. Vilevile, Mifumo ya utoaji haki ni pamoja na kuwa na sheria bora, miundombinu thabiti ya utoaji haki (uwepo wa mahakama na nyumba za mahakimu kwa maeneo yenye umbali mrefu) ajira kwa mahakimu na majaji, urahishishaji wa usikilizwaji wa mashauri.
Kwa zaidi ya kipindi cha miaka 61 ya uhuru wa nchi yetu bado tuna maeneo mengi ambayo yanahitaji ujenzi wa Majengo ya mahakama. Watu wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za utoaji haki ikiwemo uwepo wa vituo vya polisi ambavyo vinakuwa mbali na makazi ya wananchi katika maeneo ya nchi yetu hasa vijijini.
Katika mpango wa fedha wa mwaka 2022/23 haujawekwa kuendena na kasi ya changamoto hizi ili kuzimaliza kabisa. Hivyo basi, katika mwaka huu wa fedha serikali inapaswa kuweka fungu la fedha kuhakikisha mfumo wa kielektroniki wa uendeshaji wa mashauri unaboreshwa katika Mahakama za ngazi ya Wilaya hadi Mahakama ya Rufaa.
ACT Wazalendo tunasisitaza matumizi ya adhabu mbadala kama inavyobainishwa katika kifungu 3 (1) cha Sheria: The Community Services Act (Cap. 291 R.E. 2019) ili kupunguza msongamano. Ambapo inampa Afisa Ustawi wa Jamii mamlaka ya kupendekeza adhabu mbadala kwa watuhumiwa waliotiwa hatiani kwa makosa ambayo adhabu husika ni chini ya miaka 3.
Pia, waendesha mashtaka na mahakama kusimamia sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai hususani vifungu
Tatu, tunaitaka wizara ifanye maboresho ya mfumo wa upelelezi wa mashauri kwa kusimamia ukomo wa muda wa upelelezi na kuweka ukomo kwa makosa ambayo hayawekewa ukomo ili kupunguza mlindikano wa kesi zinazochagizwa na upelelezi kutokamilika.
Mwisho, tunapendekeza kuwepo kwa dhamana kwa makosa yote na kuboresha utaratibu wa udhibiti wa dhamana kwa baadhi ya makosa. Ruhusa hii itaimarisha mfumo wetu wa haki jinai kwa kuondosha hila za kubimbikiza kesi zisizo na dhamana ili kuwatesa na kuwakomoa wananchi.

5. Kutafsiri Sheria na Mikataba
Licha ya Serikali kubadili sheria na kufanya lugha ya mahakama kuwa Kiswahili bado sheria zetu nyingi zipo katika lugha ya kiingereza. Licha ya uwepo wa jitihada za Mahakama kupitia Jaji Mkuu kutengeneza kanuni za matumizi ya lugha katika mashauri mbali mbali, bado jitihada hizo hajizakidhi. Kuna umuhimu wa sheria zetu kuwa katika lugha ya Kiswahili kitumike ili kuwawezesha wananchi kuwa na uelewa na sheria za nchi yetu. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inapaswa kufanya utafsiri wa sheria kuu na sheria ndogo kuwa kwenye lugha ya Kiswahili ili kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi. Hii ni pamoja na kufanya urekebu wa zaidi ya Sheria 375 ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa ya jamii.
ACT Wazalendo inaisihi Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatakiwa kuendelea kushiriki na kutoa ushauri wa kisheria katika kupitia mijadala mbalimbali ya mikataba ya kibishara, mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa sambamba na kuweka wazi mikataba ya kitaifa na kimataifa kwa lugha ya Kiswahili ili kukuza uelewa wa wananchi katika mikataba inayoinufaisha nchi yetu.

6. Haki za binadamu na utawala bora
Kwa kipindi cha miaka 5 sasa, kumekuwa na uhaba wa fungu katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Ili kuhakikisha utawala bora katika nchi yetu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapaswa kufanya uchunguzi wa malalamiko yanayohusu uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora nchini. Kufikia mwaka 2020, Tume ilipokea malalamiko 2,420 na kufanya jumla ya malalamiko 9,754 (Mapya na ya Zamani) kati ya malalamiko hayo 5,398 yalichunguzwa na kuhitimishwa na 4,356 yanaendelea kufanyiwa uchunguzi. Hii inaonesha kwamba bado kuna kiwango kikubwa cha malalamiko hayajafanyiwa kazi na kufanya wananchi kuendelea kuumia kwa kukosa haki zao.

7. Mapitio ya mifumo ya sheria mbalimbali
Mifumo yetu ya utoaji wa haki nchi ina kabiliwa na changamoto kadhaa kutokana na asili ya sheria zilizopo. Jitihada zinazofanywa na wizara katika kufanya maboresho bado hazikidhi matarajio na matamanio ya wananchi walio wengi. Sheria ambazo zinahitaji kufanyiwa mabadiliko na maboresho ya haraka ni kama zifuatazo;
• Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2016
• Sheria ya vyombo vya Habari
• Sheria ya Jeshi la Polisin Tanzania (sura ya 322- 2002) kifungu cha 43(2),(4) na (6)
• Sheria ya utakatishaji fedha
• Marekebisho ya sheria ya kuzuia ugaidi (sura ya 19)

Wizara kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inapaswa kutenga fungu la fedha kufanya mapito ya sheria mbalimbali kwa ajili ya kuboresha sheria ili ziendanae na wakati kwa kuakisi mahitaji ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni, kisayansi na teknolojia.

Hitimisho
Ni muhimu kufahamika kwamba, mapboresho yote ya kiutawala na usimamizi wa demokrasia nchini kwetu, unapaswa kuonekana na kutafsiriwa kwenye mipango na vipaumbe vya wizara ya katiba na sheria. Mpango wa bajeti kwa mwaka huu wa fedha haujabeba uzito huu mkubwa wa mageuzi muhimu ya kimifumo katika nchi yetu. Ni rai yetu kuwa wizara itayabeba haya kwa uzito huo ili kuifanya nchi yetu ni sehemu salama na kurejesha umoja kitaifa.


Imetolewa na;
Ndg. Victor Kweka [email protected]
Msemaji wa sekta ya Sheria na Katiba
ACT Wazalendo
28.04.2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK