HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA TAMISEMI NA MAENDELEO VIJIJINI NDG. KULTHUM J. MCHUCHULI

19.04.2022

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA TAMISEMI NA MAENDELEO VIJIJINI NDG. KULTHUM J. MCHUCHULI
Tupo katika kipindi ambacho Bunge linaendelea kujadili bajeti za wizara mbalimbali, tarehe 14 April 2022, tuliona Ofisi ya Rais TAMISEMI ikiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23. ACT Wazalendo katika mwendelezo wake wa kuisimamia serikali, kupitia msemaji wa sekta ya TAMISEMI na Maendeleo vijijini imefuatilia, imeisoma na kuichambua hotuba hiyo kwa lengo la kumulika na kutazama kwa kiasi gani inakidhi matarajio na matamanio ya wananchi katika kupata huduma na usimamizi wa rasilimali zao. Kupitia uchambuzi huu tumeonyesha maoni yetu kwenye maeneo nane (8) yenye mtazamo mbadala wa ACT Wazalendo kuhusu hotuba ya bajeti ya Tamisemi, ambayo tunaona ni muhimu kwa mustakabali wa taifa letu na wananchi walio wengi.
1. Uhaba wa miundombinu katika Elimu ya msingi na sekondari
Inaeleweka kwamba ubora wa elimu unategemea sana uwekezaji kwenye rasilimali watu yaani walimu na watumishi wengi, pamoja na miundombinu na vifaa katika shule zetu.
Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa bado kuna uhaba mkubwa wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari za umma, hususani linapokuja suala la vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, madawati, vitabu vya kiada na vyoo. Uhaba huu unafanya kuwe na mazingira magumu ya kufundishia na kujifunzia na hivyo kushusha viwango vya ubora wa Elimu.
Hali ya upungufu wa miundombinu kwenye shule za umma inathibitishwa pia na tafiti, kwa mujibu wa takwimu za elimu (BEST), 2019; ni kwamba, kulikuwa na jumla ya matundu ya vyoo 175,732 kwa shule za msingi nchini. Kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo, wavulana 60 wanalazimika kutumia tundu moja la choo (1:60), uwiano unaotakiwa ni wavula 25 kwa tundu moja la choo (1:25). Wakati wasichana 56 wanatumia tundu moja la choo (1:52) uwiano unaotakiwa ni wasichana 20 kwa tundu moja la choo (1:20). Ingawa kwa wastani tuliouna hapa, zipo shule zenye upungufu zaidi hadi wanafunzi 141 wanatumia tundu moja la choo. Pia, kuna upungufu wa vyumba vya madarasa takribani 95,557 kwa shule za msingi, vyumba vya madarasa kwa shule za msingi vilikuwa 121,022 na kufanya darasa moja kuwa na wanafunzi 84, ingawa zipo shule uwiano wa chumba kimoja cha darasa ni kwa wanafunzi 175 (1:175).
Vilevile, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2020/21 uhaba wa madarasa kwa shule za msingi unafanya upungufu wa aslimia 60, upungufu wa nyumba za walimu asilimia 85.2 (198,439), upungufu wa ofisi za walimu asilimia 52, upungufu wa maktaba asilimia 94.6 (15,888), upungufu wa vyumba vya huduma ya kwanza ni asilimia 97.0 (17,677) upungufu wa viti na meza ni asilimia 44 (693,010) na upungufu wa vyoo ni asilimia 63.
Bajeti iliyotengwa na wizara kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari haifiki bilioni 200 huu ni mzaha kwenye elimu yetu.
ACT Wazalendo kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 tuliweka namna ya kukabiliana na changamoto hizi, mathalani tuliahidi kujenga madarasa 24,000 kila mwaka ambapo bajeti yake wastani wa bilioni 384.
Pia, kuna uhaba mkubwa wa vitabu kwenye shule za sekondari na msingi, serikali kutoa fedha pungufu kwa ajili ya ada ya ruzuku ya elimu bila malipo. Viwango vilivyowekwa na serikali vya shilingi 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kama ruzuku vimepitwa na wakati kutokana na uhalisia wa Maisha na mabadiliko ya thamani ya shilingi kwa dola. Upungufu wa fedha katika utekelezaji wa bajeti na ufinyu wake unaathiri kiwango cha elimu na taaluma kwenye shule nyingi kutokana na kukosa uwezo wa kutimiza mahitaji muhimu ya kutoa elimu bora kama vile ukarabati wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na nyenzo za kujifunzia.

2. Upungufu uliokithiri wa walimu na watumishi wa afya katika Mamlaka za Serikali za mitaa.
Ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hususani kwenye sekta ya elimu na afya umeathirika kutokana na Watumishi waliopo kuzidiwa na majukumu.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, mwenendo wa uchambuzi wa upungufu wa watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa miaka 6 unaonesha kuongezeka kwa asilimia ya upungufu kutoka asilimia 22 mwaka 2014/2015 hadi asilimia 41 mwaka 2020/2021 licha ya mapendekezo ya kila mwaka ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kwa OR-TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma (OR-MUU) ya kupunguza asilimia ya upungufu wa watumishi
2.1 Upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari
Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa kuna uhaba mkubwa sana wa walimu katika shule za msingi na sekondari jambo ambalo linaathiri ubora wa utoaji wa elimu kwa Watoto wetu. Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya taifa ya takwimu (2021), inaonesha idadi ya walimu katika shule za msingi imeshuka kutoka walimu 191,772 mwaka 2016 hadi kufikia 170,569 sawa na ongezeko la asilimia -6.3 kwa mwaka. Idadi ya walimu katika shule za sekondari nayo imeporomoka kutoka walimu 89,554 mwaka 2016 hadi walimu 84,614 mwaka 2020 sawa na anguko la asilimia -5.5.
Pamoja na takwimu hizi, katika hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 Waziri- Ofisi ya Rais Tamisemi Ndg. Innocent Lugha Bashungwa alisema kuwa upungufu wa walimu wa shule za msingi ni 100,958 sawa na asimilia 36.77 ya mahitaji ambayo ni walimu 274,549 huku walimu waliopo ni 173,591. Pia, mahitaji ya walimu kwa Shule za Sekondari ni 159,443 waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 74,743 sawa na asilimia 46.87. Upungufu huu ni kwa uwiano wa mwalimu mmoja wanafunzi sitini (1:60) ambao ni tofauti na uwiano tuliojiwekea kupitia sera ya elimu ya mwaka 2014 ambayo inasema lengo kwa mwaka 2022 ni kufikia uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi 1:45 (mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45).
Lakini, inashangaza sana licha ya kuwa na mahitaji makubwa ya walimu serikali kupitia hotuba ya bajeti ya wizara ya TAMISEMI mwaka huu imeweka mkakati wa kuajiri walimu 9,800 tu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari. Kwa uelekeo huu serikali inatuambia kuwa itachukua miaka 17 kumaliza tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari.

ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuongeza idadi ya ajira za walimu kutoka idadi ya ajira 10,000 kwa mwaka hadi kufika walimu 30,000. Pia, serikali irudishe utaratibu wa kutoa ajira za moja kwa moja za walimu kila mwaka bila kutegemea hisani ya viongozi, kuna vijana wengi sana takribani 123000 waliohitimu ngazi mbalimbali waliosomea ualimu hatupaswi kusumbukia tena na tatizo la upungufu wa walimu katika shule zetu.

2.2 Upungufu wa watumishi wa Afya katika mamlaka za serikali za Mitaa
Halmashauri za Wilaya hazina watumishi wa kutosha kulingana na ikama ya watumishi wa Sekta ya Afya (Staffing Levels Guideline 2014-2019). Idadi ya chini kabisa ya watumishi wa afya inayohitajika katika kutoa huduma bora katika sekta ya afya ni watumishi 145,454 lakini waliopo sasa hawazidi 70,244; na hivyo kuna upungufu wa watumishi 75,211 sawa na asilimia 52. Upungufu huu wa watumishi wa afya unaonekana zaidi katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri na hospitali za mikoa iliyopo maeneo ya pembezoni mwa nchi, yenye uhitaji zaidi na katika kada za ngazi ya kati (mid-level cadres) ya watumishi wa afya. Kwa miaka takribani 5 kasi utoaji wa ajira kwenye sekta hii muhimu ni ndogo sana.
Tunamtaka Waziri ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha ajira za afya nazo zinapewa kipaumbele na kubebwa kwa uzito mkubwa.

3. Ukiukwaji wa sheria na taratibu za ununuzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wenye jumla ya thamani za shilingi bilioni 57.18

Moja ya majukumu ya wizara ni kusimamia rasilimali kwa manufaa ya taifa. Katika kuichambua hotuba ya Waziri wa Nchi- Ofisi ya Rais Tamisemi. Tumegundua ukiukwaji mkubwa sana unaofanya na watumishi na maafisa katika mamlaka za serikali za mitaa katika suala la ununuzi.

Ripoti ya CAG ya mwaka 2020/21 imebainisha kuwepo kwa ukiukwaji huo, ununuzi uliofanyika bila kufuata idhini ya bodi za zabuni wa shilingi bilioni 10.34 katika halmashauri 47 hazikupata idhini ya bodi na halmashauri 17 hazikutoa ripoti ya ununuzi kwa bodi. Pia, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu alibaini ununuzi wenye thamani ya shilingi bilioni 3.84 uliofanyika nje ya mpango wa mwaka wa halmashauri, ununuzi wenye thamani ya shilingi bilioni 5.37 uliofanyika bila kushindanisha wazabuni. Ununuzi uliofanywa bila kuzingatia hati za kuagiza vifaa shilingi bilioni 1.24, malipo ya shilingi bilioni 2.02 kwa wazabuni wa bidhaa na huduma bila taarifa za ukaguzi.


4. Kilio cha wafanyabiashara na watoa huduma wadogo (Wamachinga) hakijasikilizwa.
Sekta ya biashara na huduma imekaliwa kwenye sehemu kubwa na wafanyabishara wadogo maarufu kama wamachinga, kutokana na umuhimu wake katika kuajiri vijana wengi ilipaswa kupewa kipaumbele na kuwekewa mazingira mazuri ili iweze kuku ana kuimarika. Lakini, tangu mwezi julai 2021, tumeshuhudia kadhia kubwa inaowakumba wafanyabishara wadogo kufukuzwa maeneo ya miji, kubolewa kwa vibanda vyao, kuchomwa moto kwa vibanda na kuungua kwa masoko. Aidha, serikali imesitisha kabisa mpango wa kuwatambua wamachinga kama ilivyoahidi kupitia Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Tamisemi katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2021/22.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara wafanyabiashara wadogo waliopatiwa vitambulisho mpaka mwezi Machi 2021 walikuwa 2,335,711 badala ya kuboreshewa mzazingira yao ya biashara kama ambavy serikali iliahidi walijikuta kwenye ya kadhia bomoa bomoa na vitendo vya chuki dhidi yao vimewafanya kuishi kwa hofu, kupoteza uhuru wao wa kufanya biashara kabisa.
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuandaa sera ya wamachinga itakayozingatia maslahi yao na ustawi wa jamii kwa ujumla.
5. Kucheleweshwa na kutelekezwa kwa miradi ya ujenzi wa vituo vya afya kuna litia hasara taifa na kuumiza wananchi.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, alibaini mamlaka za serikali za mitaa 54 zilizochelewesha ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati vyenye thamani ya bilioni 32.1. Ucheleweshaji huu ni kati ya miezi mitatu hadi miaka mitatu, kwa hakika ili ni jambo la kusikitisha kweli ikizingatiwa umuhimu wa huduma ya afya kwa wananchi. Katika Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nchi TAMISEMI haijaweka mkazo juu ya uzembe huu na hatua zilizochukuliwa kwa ucheleweshwaji. Kulegalega kwa serikali kwenye kusimamia kikamilifu miradi inayowagusa watu inatuma ujumbe kuwa serikali haijali ustawi wa maisha ya watu wake na inakumbatia wazembe na wabadhirifu.
Aidha, katika kufuatlia tumebaini pia kutelekezwa kwa miradi ya afya yenye thamani bilioni 3.98 ambayo tayari imekamilika. CAG anasema “Nilibaini miradi ya majengo ya afya iliyokamilika yenye thamani ya shilingi bilioni 3.98 katika mamlaka 20 za serikali za mitaa ambayo haikuwa ikitumika kama ilivyokusudiwa. Miradi hii inajumuisha vyumba vya upasuaji, vyumba vya kuhifadhi maiti, wodi, zahanati, na vituo vya afya.”
Kuchelewesha na kutelekeza miradi hii ni kuwarudisha nyumba na kuwatupa wananchi. ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuchukua hatua stahiki kwa watumishi waliohusika kufanya uzembe huu.
6. Ufinyu wa bajeti kwa wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA)
Kwa kuzingatia majukumu ya TARURA ambayo kwa sehemu kubwa yanahitaji fedha za kutosha kutekeleza wajibu huo kutokana na hali halisi ya barabara zetu. Kwa miaka mitatu mfululizo yaani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20, 2020/21 na mwaka 2021/22 kiwango kilichoidhinishwa na kile kilichotolewa ni asilimia ndogo imekuwa ikishuka kutoka aslimia 68, 63 na 51 kwa miaka mfululizo. Mathalani mwaka 2021/22 iliidhinishiwa kiasi cha sh. Bilioni 900. Mpaka februari 2022 ilipokea kiasi cha bilioni 461.75 sawa na asilimia 51. Mwaka huu TARURA imetengewa shilingi bilioni 802.29 kiasi pungufu zaidi, licha ya kuongezewa majukumu.
Ili kuchochea maendeleo vijijini na mamlaka za serikali za mitaa ni muhimu kuwekeza vyema kwenye miradi ya maendeleo vijiji kwa kusimamia vizuri TARURA.

7. Utegemezi wa bajeti ya miradi na maendeleo kwa fedha za nje.
Tumepitia mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2022/23, kwa sehemu kubwa bajeti ya maendeleo ni tegemezi kwa fedha za nje jambo ambalo linahatarisha ufanisi wa utekelezaji wake. Ambapo bajeti iliyotengwa kwa ajili miradi na maendeleo ni shilingi trilioni 3.267 fedha kutoka vyanzo vya ndani ni shilingi trilioni 2.147 sawa na asilimia 65.71 na fedha kutoka nje ni shilingi trilioni 1.120 sawa na asilimia 34.28.
8. Upendeleo katika utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwenye Halmashauri zetu, tunapoteza fedha.
Mwenendo wa urejeshaji wa mikopo ya hamashauri kwa makundi maalum ni mbaya sana. Ripoti ya CAG inaonyesha takwimu za miaka mitano mfululizo 2016/17 mpaka 2020/2021, mwaka 2020/21 katika halmashauri 155 kiasi cha bilioni 47 sawa na asilimia 70 ya mikopo yote haijarejeshwa.
Hali hii imekuwa ni ya kawaida sana ambapo marejesho ya mikopo hii ya chini ya asilimia 30. Vilevile, katika ripoti ya CAG ya mwaka 2020/21 amebainisha kuwa baadhi ya halmashauri zinashindwa kufuata sheria kutotenga mikopo hii (mamlaka 83- kiasi bilioni 6.68), na mamlaka 11 kushindwa kuhamisha bilioni 1.24 kwenda kwenye akaunti maalum kwa ajili ya mikopo hii kama kanuni zinavyoelekeza. Kwa ujumla utaratibu wa utoaji, udhibiti na usimizi wa mikopo ni hafifu mno.
Sisi tunafahamu mikopo hii imekuwa ikitolewa kwa upendeleo wa kisiasa na kukosa mfumo wa uwazi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuomba na kupata. Lengo kuu la Mfuko wa fedha wa Maendeleo kwa Wanawake na Vijana ili kuwainua wanawake na vijana wasiojiweza kiuchumi ambapo wengi wao hawakidhi vigezo vya mikopo inayotolewa na taasisi za fedha kutokana na ukosefu wa dhamana. Katika hotuba ya Waziri wa TAMISEMI, haijaeleza changamoto zote hizi wala mkakati wa kumaliza kabisa.
ACT Wazalendo tunamtaka waziri mwenye dhamana aje na maelezo na mkakati toshelevu kuhakikisha mfuko huu unafanya kazi yake tarajiwa
Hitimisho
Kwa ufupi kwa namna hotuba ya bajeti ya wizara ya TAMISEMI hata ikitekelezwa kwa asilimia mia moja, haitotoa matokeo makubwa kwa wananchi ni muhimu kuwekeza kwenye maeneo ambayo yataimarisha na kuboresha maisha ya watu. Tunaitaka serikali kuzingatia mapendekezo haya ili kuondokana na changamoto za miongo kadhaa nyuma. Kama taifa hatuwezi kuendelea kuzungumzia matundu ya vyoo katika shule zetu, vyumba vya madarasa, madawati, kukosekana kwa vitabu, barabara za udongo, changamoto ya maji vijijini na ubovu wa huduma za afya.

 

Ndugu Kulthum J Mchuchuli
Msemaji wa Sekta
TAMISEMI na Maendeleo ya Vijijini – ACT Wazalendo.
[email protected]
19.04.2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK