HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MADINI ACT WAZALENDO NDG. EDGAR MKOSAMALI KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2022-2023

HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MADINI ACT WAZALENDO
NDG. EDGAR MKOSAMALI KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2022-2023

Utangulizi
Ndugu Waandishi wa Habari, kama mnavyofahamu kwamba hivi sasa tupo katika Bunge la Bajeti, macho ya watanzania yanaangaza kwa kiasi gani bunge litaenda kugusa maisha yao na ya taifa kwa ujumla. ACT Wazalendo imeweka utaratibu wa kuzipitia bajeti za kila wizara kupitia kamati ya kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta iliyoundwa na chama. Leo bunge linajadili mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini. ACT Wazalendo kupitia msemaji wa sekta ya madini tumeangalia maeneo nane (8) kutoka kwenye bajeti na kutoa mtazamo mbadala.
Yafuatayo ni maeneo ambayo tumeyachambua kwa kina na kutoa maoni ya Chama cha ACT Wazalendo kupitia wasilisho la bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

1. Upotevu wa mapato na utoroshwaji wa madini bado ni tatizo sugu:
Tanzania kama taifa limekuwa likipoteza fedha nyingi sana kutokana na mikataba mibovu na mianya mingi ya wizi na utoroshwaji wa madini.
Licha ya kuwa na takwimu za mwenendo wa makusanyo ya Serikali kwenye sekta ya madini kuonekana kuongezeka na mchango wa sekta kwenye pato la taifa kufikia wastani wa 7.7% mwaka 2021 kutoka 3.4% kwa mwaka wa fedha 2014/15. yetu.
Kwa taarifa za wizara katika mwaka wa fedha 2021/2022, zinaonyesha Tume ya Madini imeokoa kiasi cha shilingi milioni 501.23 baada ya kukamata madini yaliyokuwa yakitoroshwa. Hakuna taarifa ya wazi ya madini kiasi gani yalifanikiwa kutoroshwa.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabau za Serikali (CAG) 2020/21 inathibitisha upotevu kutokana na serikali kutotekeleza matakwa ya sheria ya madini. Sheria ya Madini, Sura 123 (marekebisho ya mwaka 2019) kinataka, katika kila shughuli ya uchimbaji chini ya leseni ya uchimbaji madini au leseni maalumu, Serikali iwe na hisa isiyopungua 16% katika mtaji wa kampuni ya uchimbaji wa madini kulingana. Hii ni kulingana na aina ya madini na kiwango cha uwekezaji ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali madini. Lakini hadi kufikia mwaka 2021, CAG anaonyesha kuwa serikali haitekelezi matakwa haya ya sheria kuwa kati ya leseni 62 zilizotolewa na Tume ya Madini kwa makamapuni 62 yaliyosajiiwa katika ya tarehe 1 Agosti 2017 hadi tarehe 30 Juni 2021 hayana hati za kuthibitisha umiliki wa 16% ya Hisa kwa serikali. Hakuna uthibitisho wala taarifa kuonyesha umiliki wa 16% za Serikali kutoka kwenye taasisi zote zinazohusika yaani Tume ya Madini, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni na Ofisi ya Msajili . Watanzania wana haki ya kufaidi rasilimali za madini katika kujenga uchumi wao.
ACT Wazalendo tunatoa wito kwa Wizara ya Madini na Serikali kwa ujumla kuendelea kuzuia mianya ya utoroshwaji wa madini na kuchukua hatua kali kwa wahusika wa vitendo hivyo. Na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ya madini na kanuni zake zinaipa serikali 16% ya umiliki kwenye makampuni ya madini.

2. Serikali imetelekeza Mradi wa kufua chuma wa Liganga na makaa ya Mawe Mchuchuma.
Imepita miaka 10 tangu tusikie Serikali kupitia shirika la maendeleo hakuna Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Company Limited kusaini mkataba wa ubia na kuunda kampuni ya ubia inayoitwa Tanzania China International Mineral Resources LTD (TCIMRL) ili kutekeleza mradi huu wa chuma.

Umuhimu na mchango wa mradi huu una tija kubwa kwa taifa letu lakini tunashangaa sana kuona serikali haiweki kipaumbele kwenye mradi makakati. Ni wazi kuwa kupitia uwekezaji kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma taifa lingeweza kunufaika kwa kuzalisha bidhaa za chuma, madini ya vanadium na madini mengine, umeme wa makaa ya mawe na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

CAG katika ripoti ya mwaka 2020/21 ameonyesha kuwa hadi sasa serikali imeshindwa kusimamia kulipwa kwa fidia kwa wakazi ambao mradi unatarajiwa kutekelezwa. Pia anasema “Nilibaini kuwa Kampuni ya TCIMRL na Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji walitia saini mkataba wa utendaji kazi tarehe 21 Septemba 2021 kuhusu vivutio kadhaa vilivyoidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Vivutio vya Uwekezaji. Hata hivyo, utekelezaji wa mradi bado haujaanza kwa sababu tangazo la serikali bado halijatoka ambalo lingehalalisha utoaji wa vivutio vya uwekezaji vilivyoainishwa.”
Ucheleweshwaji wa mradi ni kurudisha taifa nyuma na tumeona katika bajeti ya mwaka huu wa fedha bado haujapewa kipaumbele. Sisi ACT Wazalendo kupitia ilani ya uchaguzi 2020 (4.10) tuliuweka mradi kwenye miradi mikakati. Tulisema kwamba Serikali ya ACT Wazaledno itaweka mkazo kwenye miradi ya uchimbaji madini ambayo ina faida kubwa ya fungamanisho, miradi mikubwa miwili ya kipaumbele itakuwa ni Mradi wa Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa, mkoani Njombe, na mradi wa Kabanga Nickel wilayani Ngara, mkoani Kagera.

3. Wachimbaji wadogo na mchango wao katika pato la taifa:
Sekta ya madini Tanzania imeajiri wachimbaji, wachenjuaji, wanunuzi na wauzaji wa madini wengi sana. Hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2021, Tume ya Madini ilikuwa imetoa zaidi ya leseni 6,300 kwa wachimbaji wadogo ikilinganishwa na leseni 6 za migodi mikubwa na leseni 12 za migodi ya kati. Wachimbaji wadogo mbali na kutoa ajira nyingi zisizo rasmi kwa watanzania wanao jishughukisha na shughuli za madini, wanachangia wastani wa 30% ya mapato yote ya madini kwenye pato la taifa. Hii ina maana wastani wa shilingi bilioni 584 zilizokusanywa na wizara na kuchangia 7.7% ya pato la taifa mwaka 2020/2021, wastani wa shilingi bilioni 175 zilitokana na wachimbaji wadogo.
Kwa bahati mbaya Serikali bado haiwajali wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo ni yatima walioachwa wajitafutie madini bila msaada au uwezeshaji wowote wa kifedha, vifaa na mafunzo. Sera ya madini yam waka 2009 imetamka bayana kwamba serikali itawaendeleza na kuwawezesha wachimbaji wadogo ili wakue na waweze kuchangia kwenye uchumi wa nchi lakini ni kinyume chake. Serikali inafurahia kuvuna matunda ya kodi na tozo kutoka kwa wachimbaji wadogo pasipo kuwekeza katika kuwainua kimtaji na zana za kufanyia kazi. Badala yake wizara ya madini imetoa elimu kwa benki 4 za NMB, CRDB, TIB na NBC ili benki zianze kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo pasipo kuingiza fedha yoyoye kwenye benki hizo.

ACT Wazalendo inaitaka serikali kuanza kutenga pesa katika bajeti yake kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wa Tanzania kama tunavyoshauri kwenye mapendekezo yetu hapo chini, na sii kuishia kuwapa semina, mafunzo na maelekezo pekee.
Pia, Serikali ianzishe benki ya madini kwa ajili ya kusimamia mikopo na amana za wanachi wanaojihusisha na tasnia ya madini. Risk ni kubwa katika biashara ya madini. Ni vigumu sana kwa benki za kawaida kutoa huduma kwa wachimbaji wadogo.
Tatu, serikali itenge walau asilimia 5 ya mapato yote yatokanayo na madini kwa ajili ya kuwawezesha kupata vifaa vya msingi vya uchimbaji, kuwakopesha na kuwaendeleza ili hatimaye wakue na kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye wakubwa.
4. Usiri katika Mikataba ya madini na ushirikishwaji hafifu wa wananchi katika umiliki wa rasilimali madini.

Serikali ilifanya marekebisho ya sheria ya madini na kanuni zake mwaka 2017 na 2019 mtawalia ilimkuhakikisha kuwa watanzania wananufaika na rasilimali hiyo ambayo kwa muda mrefu tumekuwa tukinyonywa au zikitumika kuwanufaisha watu wachache wa ndani ya nchi na wawekezaji pekee. Pamoja na kuwepo kwa marekebisho haya bado wananchi wapo gizani juu ya mikataba ambayo serikali inaingia na wachimbaji wa madini. Usiri wa mikataba unofanywa na serikali inaitia hasara taifa.
Pia, mikataba ambayo Tanzania itaingia na wawekezaji kwa kutumia mfumo wa Production Sharing Agreement, lakini bado aina hii ya mikataba inamwondoa mwanachi mkazi katika kunufaika na rasilimali madini yanayopatikana katika makazi yake. Sera ya madini (2009), inataka tu kwamba kunapotokea shughuli ya madini, serikali itafanya mchakato wa kumuhamisha kwa uwazi na kumpatia mwanachi makazi mapya ikiwa ni pamoja na fidia kwa ardhi yake itakayochukuliwa.
ACT Wazalendo tunaona hatua ya kuwahamisha wananchi na kuwapatia fidia tu ili kupisha shughuli za uchimbaji madini haitoshi. Wananchi, vijiji na maeneo yanakopatikana madini wanapaswa kushirikishwa na kupewa sehemu ya umiliki wa shughuli za madini yanayopatikana katika maeneo yao. Mwekezaji anapaswa kupata kibali na kukubaliana na wanachi wa maeneo husika kwa uwazi juu ya thamani ya madini yatakayopatikana na kukubaliana ni asilimia ngapi wanachi watakuwa wanapata kama mgao wao kutokana na faida itakayopatikana (free prior informed consent)

Mikataba itakayofungwa baina ya serikali na mwekezaji kwa utaratibu huu utapeleka maendeleo kwa wananchi kwa haraka na kuondoa umasikini wa maeneo ambako shughuli za madini zinafanyika kuliko kutegemea hisani ya mwekezaji, yaani Corprate Social Responsibility (CSR)
ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza kuwa Mfumo wa uchimbaji wa maliasili hizi ubadilike kutoka mfumo wa sasa wa kutoa leseni na kukusanya kodi na mrahaba kwenda mfumo wa umiliki na ukandarasi. Mwekezaji awe mkandarasi, arejeshe gharama zake na faida iliyobakia kugawana na Serikali kwa makubaliano maalumu. Haki (Mineral Rights) iwe ya Shirika la Umma linalomilikiwa na Serikali na wananchi kwa asilimia 100.

5. Uwezo wa serikali kusimamia na kuratibu shughuli za madini nchini
Pamoja na jitihada zilizochukuliwa na serikali za kuajiri maafisa wakazi 13 kwenye migodi mikubwa na ya kati na kuajiri wakaguzi wasaidizi 182 wa madini ya ujenzi nchi nzima, lakini bado serikali haijafanikiwa kusimamia (governance) na kuratibu vizuri shughuli za uchimbaji na mnyooro mzima wa biashara ya madini.
Kwa mujibu wa taasisi ya usimamizi wa rasilimali asili (Natural Resource Governance Institute – NRGI), Tanzania haijafanya vizuri sana katika eneo hili tangu mwaka 2017 kwa kupata alama 58/100. Katika eneo la kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya madini Tanzania iko chini kwa kupata alama 53/100 na ina alama 60/100 katika kigezo cha utambuzi wa thamani ya madini na manejiment ya mapato yanayopatikana kwenye madini (Value Realization and Revenue Management.


6. Fungamanisho la sekta ya madini na sekta zingine za kiuchumi
Ili sekta ya madini iwe na tija na iguse maisha ya wananchi moja kwa moja, hakuna budi sekta hii ifungamanishwe na sekta zingine za kiuchumi kama vile kilimo, usafirishaji, biashara na sekta ya huduma.
Lakini ni ukweli kuwa bado sekta ya madini hajafungamanishwa na sekta zingine. Kwenye ripoti ya CAG anasema kuwa migodi 25 iliomba kuunganishwa kwenye gridi ya taifa ili kupunguza gharama za uendeshaji. Hata hivyo, nilibaini kuwa TANESCO haikuunganisha migodi hii kwenye gridi ya taifa. “Kitendo cha TANESCO kutounganishwa na migodi mitatu tu ya Geita kunaikosesha wastani Mapato ya dola za kimarekani milioni 3 kila Mwezi (TZS 80 bilioni/Mwaka).

ACT Wazalendo tunatambua baadhi ya jitihada zilizofanyika katika kuunganisha sekta ya madini na sekta zingine kwa kuzitaka kampuni kubwa za uchimbaji wa madini kutoa zabuni kwa makapuni ya watanzania katika kutoa zabuni za kuuza bidhaa na kutoa huduma kwenye migodi hiyo. Hata hivyo, tunaona bado idadi ya wageni wanaotoa huduma kwenye migodi hapa nchini ni kubwa na wanachukua sehemu kubwa ya mapato ambayo yangeenda kwa watoa huduma wa kitanzania. Kufikia mwaka 2021, idadi ya watoa huduma wa ndani ilikuwa 961 na idadi ya watoa huduma wa kigeni ilikuwa 506.
Japo idadi ya watoa huduma wa ndani ni kubwa lakini pia watoa huduma 506 kutoka nje ya nchi ni kubwa sana.
Tunaishauri serikali izitake kampuni za madini zitoe takwimu za aina ya huduma na viwango vya pesa zinazolipwa kwa makampuni yote yanayotoa huduma ili kuwe na uwazi na tuweze kufanya ulinganifu na kujua aina ya bidhaa ambazo kiuhalisia haziwezi kutolewa na watanzania. Lengo ni kuhakikisha kwamba mapato mengi yanayotokana na huduma katika migodi yetu yanabaki hapa nchini na kuongeza mzunguuko wa pesa na kukuza ajira na uchumi wa nchi.
7. Serikali ituambie trilioni 5.5 zinazoshikiliwa na Mahaka ya rufaa ya kodi
Katika ripoti ya CAG ya mwaka 2020/21 anasema kuna Miongoni kesi 45 zenye thamani shilingi 5,594,675,387,242.40 ambazo zipo katika mazungumzo kati ya Serikali na kampuni za madini ambayo ni North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limited, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration.
Wakati kesi Na.189 ya mwaka 2017 inayomhusu Bulyanhulu Gold Mine imepinga maamuzi ya kulipa kiwango pungufu cha shilingi 21,395,712,853,964 ili kusajili pingamizi la kodi kwa tathmini ya kodi kutokana na kutokuwa na taarifa za walipakodi (Jeopardy assessment) kwa mwaka 2000-2017 kati ya jumla ya deni la shilingi trilioni 343.5. Kesi hii imetolewa kutoka mahakama za rufani za kikodi na kurejeshwa kusikilizwa na Mamlaka ya Mapato.
Serikali itueleza kiundani kuhusu madai haya ya watanzania.

8. Mabadiliko ya tabia nchi na uchimbaji endelevu wa madini
Mabadiliko ya tabia nchi ni tazizo la kidunia linalotokana na kuongezeka kwa joto kwenye uso wa dunia kutoana na kupungua kwa ozone layer. Hii inatokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kama viwanda, magari, kilimo na uchimbaji wa madini.
Uchimbaji wa madini huchangia katika uharibifu wa mazingira kama hakuna jitihada za maskudi za kusimamia vizuri shughuli za uchimbaji. Wachimbaji kwenye migodi mikubwa hutumia jenerata kuzalisha umeme na kemikali ambazo ni hatari kwa mazingira. Wachimbaji wadogo kwa upande mwingine hutumia magogo ya miti katika kujengea maduara yao chini ya ardhi ili kuzuia ardhi isiporomoke. Aidha wachimbaji wadogo hutegemea miti na mkaa kama nishati ya kupikia kwenye migodi yao na mashine zinzozalisha gesi ya ukaa kwa shughuli zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi ya kemikali ya zebaki katika kunasa madini.
ACT Wazalendo haina uhakika kama serikali ina taarifa rasmi za idadi ya magogo ya miti inayokatwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini nchini. Tunaishauri serikali kufanya tathmini ya kina ya athari za mazingira na kuja na njia mbadala wa namna ya kuhami mazingira yetu kutokana na shughuli za uchimbaji madini.


Mapendekezo ya Jumla Kuhusu sekta ya Madini:

i. Sera ya madini ya mwaka 2009

Sera ya madini ya mwaka 2009 ni sera nzuri isipokuwa serikali haijaitekeleza kama sera inavyotaka. Serikali iko kwenye mchakato wa kuipitia nap engine kuiandika upya. ACT Wazalendo tunaishauri serikali ifanye tathmini ni kwanini haijaweza kuitekeleza sera iliyopo walau hata kwa 40% kabla ya kuandika sera mpya. Ni muhimu sana kwa serikali kujiuliza ni kwanini imeshindwa kutekeleza sera yake? Kuandika sera mpya bila mpango sahihi wa kuitekeleza ni kazi bure.

ii. Madini ya kimkakati

Moja kati ya mapungufu kati ya serikali katika sekta ya madini ni kutokuwa na mpango mahsusi wauvunaji wa madini yetu. Tunakwenda jumla jumla. Tunaishauri serikali kuwa na mkakati na kipaumbele. Ni lazima serikali ijiulize tunataka kuchimba madini gani na kwasababu gani? Dunia inahitaji madini gani kwa sasa na yana bei gani katika soko la dunia. ACT Wazalendo katika ilani yake ya 2020, ilieleza kwamba madini ya mkakati ni uwekezaji mkubwa katika miradi ya chuma ya Liganga na Mchuchuma. Pia uwekezaji katika mradi wa Kabanga Nickel. Tunaamini kwamba chuma peke yake kitazaa mara mbili ya mapato ya madini tunayopata sasa. Serikali ifikirie na iharakishe kwa umakini uwekezaji kwenye miradi hiyo.

iii. Uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Katika kukabiliana na uhaibifu na mazingira katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini tunaishauri serikali kufanya mambo yafuatayo;
(a) Ni lazima wizara ya madini ishirikiane na wizara zinazoshughulika na mazingira, nishati, maji, ujenzi na afya katika kushughulikia changamoto za miundombinu katika maendo ya machimbo hasa ya wachimbaji wadogo na kuja na njia ya kutatua changamoto hizo.
(b) Tunaishauri wizara ya madini kushirikiana na sekta binafsi ya kupata suluhisho ya changamoto ya nishati katika migodi ili kuachana na matumizi ya diesel katika kuendesha mitambo migodini. Serikali iwekeze katika nishati jadidifu kupitia sekta binafsi. Aidha serikali iangalie namna ya kuweka kipengele cha matumizi ya nishati jadidifu katika mikataba yake ya uwekezaji kwenye migodi. Kwa eneo letu la kijiografia, kuna uwezekano kila mgodi ukaendeshwa kwa chanzo chake cha nishati jadidifu (renewable energy) hasa kwa kutimia umeme jua (Stand Alone Solar system) yenye ukubwa wa megawatts zozote zinazotakiwa kuendesha mitambo.
(c) Wizara ya madini iwekeze na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika Emergency Mobile Power Plants kwa ajili ya wachimbaji wadogo wanao hamahama katika maendeo yasiyokuwa na umeme wa gridi ya taifa. Kwa mfano, kuna maduara 105 katika kijiji cha Nyamalimbe mkoani Geita. Kila mchimbaji mwenye duara ana jenereta lake dogo kwa ajili ya uchimbaji na kuzunguusha krasha la kusagia mawe. Kwa ujumla kuna madogo madogo majenereta 105 kwa ajili ya shughuli hizo. Wamiliki wa maduara hayo wana uwezo wa kulipia umeme kwasababu kwa hali ya sasa wana uwezo wa kununua mafuta ya kuendesha jenereta zao kwa masaa 20 kila siku ili maduara yao yasijae maji.


V. Uchumi shirikishi
Kutokana na mabadiliko ya kisheria serikali inamiliki 16% ya hisa kwenye migodi mikubwa na ya kati kupitia kampuni zake za ubia za Twiga Minerals Corporation Ltd na Tembo Nickel Corporation. Tunaishauri serikali iwauzie wanachi/sekta binafsi walau 6% ya hisa zake na serikali ibakie na 10%. Hatua hii mbali na kuwafanya wanachi wawe wamiliki wa uchumi wa madini yao moja kwa moja lakini pia hatua hii itaongeza udhibiti, uwazi, uwajibikaji na ufanisi kwenye mnyororo mzima wa biashara ya madini. Kwa kuwashirikisha wanachi katika umiliki, wanahisa watakuza mitaji yao, watatengeneza miradi, ajira na kulipa kodi kwa serikali.


Vi. Taasisi zilizo chini ya wizara ya madini
Tunaishauri serikali kuziwesha taasisi zilizo chini ya wizara ya madini (Tume ya Madini, GST, STAMICO na TEITI) ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kuendana na ukuaji wa sekta ya madini na kasi ya mabadiliko ya teknolojia inayotumika katika duniani.

Vii. Matumizi ya makaa ya mawe
Tanzania ina makaa ya mawe mengi yanayofikia tani za ujazo milioni 480 (480milion metric tons) katika maeneo ya Ngaka, Kiwira, Kabula, Mchuchuma na Liganga. Wakati uelekeo wa dunia ni kupunguza kasi ya matumizi ya makaa ya mawe ni fursa kwetu kutumia makaa ya mawe kwa matumizi ya majumbani sambamba na gesi asilia. Tunaishauri wizara ya madini kupitia STAMICO kuongeza kasi ya kukamilisha mradi wa matumizi ya makaa ya mawe majumbani, ili kwanza kuongeza mapato ya serikali, pili, kupunguza gharama za watumiaji wa nishati mbadala majumbani na tatu, kupunguza ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa na hivyo kuhifadhi misitu na mazingira yetu.

Ahsante sana.

Imetolewa na:
Ndugu Edgar Francis Mkosamali
[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Madini
ACT Wazalendo

29.04.2022

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK