Katiba Mpya ni Sasa!: Muhtasari wa Maoni ya ACT Wazalendo

MUHTASARI WA MAONI YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO MBELE YA KIKOSI KAZI CHA MH. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA LEO, JUMATATU, TAREHE 23 MEI, 2022.

A. UTANGULIZI.

Jana tarehe 22 Mei 2022, Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo iliketi kwenye kikao chake cha kawaida katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.
Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilijadili na kuazimia juu ya maoni ya ACT Wazalendo kwa Kikosi Kazi cha Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Demokrasia nchini.

Maoni hayo yamewasilishwa mbele ya Kikosi Kazi leo tarehe 23 Mei, 2022. Ujumbe wa ACT Wazalendo mbele ya Kikosi Kazi uliongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara Ndugu Dorothy Semu. Wajumbe wengine ni Ndugu Joran Bashange (Naibu Katibu Mkuu Bara), Ndugu Salim Bimani (Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma) na Ndugu Pavu Abdallah (Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Makundi Maalum).

Maoni ya Chama cha ACT Wazalendo yalijikita kwenye maeneo yote tisa yaliyoainishwa na Kikosi Kazi ambayo ni;

i) Mikutano ya Hadhara na Mikutano ya ndani ya Vyama vya Siasa;

ii) Masuala yanayohusu uchaguzi;

iii) Mfumo wa Maridhiano ili kudumisha Haki, Amani na Utulivu;

iv) Ushiriki wa Wanawake na Makundi Maalum katika Siasa na Demokrasia ya vyama vingi;

v) Elimu ya uraia;

vi) Rushwa na maadili katika siasa;

vii) Ruzuku ya Serikali kwa Vyama vya Siasa;
viii) Uhusiano wa Siasa na Mawasiliano kwa Umma; na

ix) Katiba Mpya.
Katika muhtasari huu, tunawasilisha maoni ya ACT Wazalendo kwenye baadhi ya maeneo. Uchambuzi wa kina wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo kwenye kila eneo yanapatikana kwenye tovuti ya Chama (www.actwazalendo.or.tz).


B. KATIBA MPYA

Kamati Kuu imeendelea kusisitiza msimamo wa Chama kuwa Tanzania inahitaji Katiba Mpya na mchakato wa kuipata uanze SASA! Kamati Kuu imekwenda mbali zaidi na kuainisha hatua za kupitia hadi kufikia kupatikana kwa Katiba Mpya.

Kuna hoja inajengwa kwamba mchakato wa Katiba Mpya unapaswa kuendelezwa kwa kupeleka Katiba Pendekezwa kwa wananchi ili kupigiwa Kura ya Maoni na kuanza kutumika. Sisi katika ACT Wazalendo hatukubaliani na hoja hiyo kwa sababu Katiba Pendekezwa ilipitishwa kwa hila na ujanja na upande mmoja na haikutokana na Muafaka wa Kitaifa ambao ndiyo unapaswa kuwa msingi wa Katiba Mpya.

Hoja yetu ni kwamba Katiba Pendekezwa ilitengenezwa na CCM kupitia vikao vyake na ikapenyezwa vipande vipande katika Bunge Maalum la Katiba kupitia Wajumbe wa Chama hicho bila ya kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kazi ya kutafsiri maoni ya wananchi na kutengeneza Rasimu ya Katiba ilitolewa kwa chombo kimoja tu ambacho ni Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.

Tume hiyo ilifanya kazi hiyo na kutoa Rasimu ya Awali na kisha Rasimu ya Mwisho ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo iliwasilishwa mbele ya Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kuiweka sawa (refine) na kisha kuipitisha. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haikutoa fursa kwa chombo kingine (na kwa hapa tunazungumzia CCM iliyotengeneza Rasimu yake na kuipenyeza kwenye Bunge Maalum la Katiba) kubadilisha maoni ya wananchi.

Kwa mujibu wa baadhi ya waliokuwa Wajumbe wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum la Katiba, CCM ilitengeneza Kikosi chake kilichoundwa na Andrew Chenge, Asha Rose Migiro na Prof. Costa Ricky Mahalu na wakaandaa Rasimu yao ambayo ndiyo iliyopenyezwa kwenye Bunge Maalum la Katiba na kuchakachua na kubadilisha maoni ya wananchi waliyoyatoa mbele ya Tume ya Jaji Warioba.

Mbali na hoja hizo, Katiba Pendekezwa haiwezi kukubalika Zanzibar kwa sababu inaifanya Zanzibar kuwa kama ni Serikali ya Jimbo au Manispaa (Municipal Government). Hilo halitakubalika kwa namna yoyote ile kwa Wazanzibari.

Kutokana na hoja hizo zote, pahala pa kuanzia katika kuipata Katiba Mpya ni kurudi kwenye Rasimu ya Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi kama yalivyotafsiriwa na kuratibiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.
Mapendekezo ya ACT Wazalendo katika kuliendea eneo hili ni kama ifuatavyo:

 Mchakato wa kupata Katiba Mpya uanzishwe sasa sambamba na hatua za kufanya mabadiliko ya msingi (minimum reforms) yatakayokidhi mahitaji ya muda mfupi na muda wa kati kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025. Mchakato wa kupata Katiba Mpya unaweza kuanzishwa tena kati ya Oktoba 2022 hadi Agosti 2024 na kuona hatua itakayofikiwa (kulingana na mapendekezo yetu yanayofuata hapa chini). Iwapo mchakato huo utakamilika na kuweza kutupatia Katiba Mpya katika kipindi hicho litakuwa jambo jema. Lakini iwapo mchakato huo hautoweza kukamilika ifikapo Agosti 2024, basi usimamishwe katika hatua itakayokuwa imefikiwa katika muda huo na kuendelezwa tena mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 hadi kukamilika kwake. Ili kuipa uhalali unaotokana na watu (legitimacy) na wananchi wa Tanzania kujiona wana wajibu wa kuiheshimu, kuitii, kuitekeleza, kuilinda na kuitetea Katiba hiyo tunapendekeza mchakato uanzie katika Rasimu ya Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.

1. Hatua ya mwanzo tunayopendekeza ifanyike ni kupitiwa upya na kufanya marekebisho/mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Constitutional Review Act) na Sheria ya Kura ya Maoni (Referendum Act) ili kukidhi matakwa ya sasa ya muda (tarehe zilizoainishwa mle zimeshapitwa na wakati), kuamua mchakato wa kupata Katiba Mpya uendelezwe kuanzia hatua ipi, na pia kutambua maeneo yaliyosababisha mkwamo katika mchakato wa 2011–2014 na kuyafanyia marekebisho ili kuepuka mkwamo mwingine (ikiwemo muundo wa Wajumbe wa Bunge la Katiba au kama kuna haja ya kuja na mfumo mwingine wa chombo kingine cha kupitisha Katiba Mpya na namna ya kusuluhisha tofauti kubwa zinapojitokeza miongoni mwa Wajumbe).

Tunapendekeza kuitisha Mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa (National Consultative Conference) utakaojumuisha Serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, asasi za kidini, wasomi wabobezi wa sheria hasa katika maeneo ya Katiba na Utawala (Constitutional and Administrative Law), na makundi mbali mbali ya kijamii ili kukubaliana juu ya marekebisho/mabadiliko ya Sheria hizo mbili na namna ya kuuendea mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya. Makubaliano ya Mkutano huo ndiyo yaongoze utayarishaji wa Miswada ya Sheria ya marekebisho/mabadiliko ya sheria hizo itakayowasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupitishwa.

2. Hatua ya pili tunayopendekeza iwe ni kujenga Muafaka wa Kitaifa kuhusiana na maeneo makubwa na muhimu yanayogusa mfumo wa kikatiba wa Jamhuri ya Muungano ambayo yamekuwa ndiyo chanzo na sababu ya mivutano katika maudhui ya Katiba Mpya. Maeneo hayo ni pamoja na Muungano na muundo wake, madaraka ya Rais, mgawanyo wa madaraka kati ya Bunge (Legislature), Serikali (Executive) na Mahakama (Judiciary) na mfumo wa uchaguzi na uendeshaji wake.

Tunapendekeza utaratibu ule ule wa kuwa na Mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa (National Consultative Conference) utakaojumuisha Serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, asasi za kidini, wasomi wabobezi wa sheria hasa katika maeneo ya Katiba na Utawala (Constitutional and Administrative Law), na makundi mbali mbali ya kijamii utumike katika hatua hii kujenga na kupata Muafaka wa Kitaifa kuhusiana na maudhui ya Katiba Mpya. Muafaka wa Kitaifa ukishajengwa katika hatua hii na kukubaliwa kwa dhati, kazi ya kupitisha Katiba Mpya katika chombo chochote kitakachopewa dhamana hiyo itakuwa si ngumu.

3. Hatua ya tatu tunayopendekeza itakuwa ni kuunda Timu ya Wataalamu Wabobezi (Constitutional Experts Commission), kutoka ndani na nje ya nchi kadiri itakavyoonekana inafaa, ambao watayaweka yaliyokubaliwa kwenye Muafaka wa Kitaifa kupitia Mkutano wa Majadiliano ya Kitaifa (National Consultative Conference) tulioutaja kwenye kifungu nambari 2 hapo juu katika Rasimu ya Katiba (Draft Constitution).

Ifahamike hapa kuwa Rasimu inayozungumziwa ni ile ya Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba. Rasimu hiyo ya Katiba itawasilishwa kwenye chombo kitakachopewa dhamana ya kutunga Katiba Mpya (Enactment of the New Constitution) kama ilivyokubaliwa kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (rejea maelezo ya kifungu nambari 1 hapo juu) kwa ajili ya kupitishwa.

4. Hatua ya nne ni Katiba Mpya hiyo kufikishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa KURA YA MAONI (referendum) ambapo iwapo itaungwa mkono na wananchi walio wengi (simple majority) wa upande wa Tanganyika na wananchi walio Wengi (simple majority) wa upande wa Zanzibar basi itakuwa imeridhiwa na kuidhinishwa rasmi.

5. Iwapo katika hatua yoyote kutatokezea mkwamo au kutokubaliana, tunapendekeza kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba izingatie namna ya kukwamua au kusuluhisha mkwamo au tofauti hizo kwa namna kama ile tulioitaja kwenye kifungu nambari 1 hapo juu kuhusiana na tofauti zinazoweza kujitokeza katika chombo chochote kitakachopewa dhamana au Bunge Maalum la Katiba (endapo itaamuliwa liendelee kuwepo).

C: MIKUTANO YA HADHARA YA VYAMA VYA SIASA

Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imependekeza mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa kama ifuatavyo;

1. ACT Wazalendo inapendekeza kufutwa kwa kifungu 11(2) kinachotoa mamlaka ya matumizi ya vifungu vya 43 – 46 vya sheria ya jeshi la polisi (Police Force and Auxilliary service Act Cap 322 of 1973) katika mchakato wa uitishwaji wa mikutano ya vyama vya siasa. Kwa maudhui ya vifungu 43 – 46 vya sehria ya jeshi la polisi, taarifa kwa jeshi la polisi inatafsirika kana kwamba ni kuomba kibali na kama kibali hakijatolewa basi kwa utashi wa jeshi la polisi, wakati wowote mkutano unaweza kuvunjwa hata kama utakuwa umeanza na unaendelea.

Aidha pamoja na kwamba taarifa ni kwa ajili ya mikutano ya hadhara, jeshi la polisi; kwa utashi wao tu, limekuwa likitumia kifungu hiki kuingilia vikao/mikutano ya ndani ya vyama vya siasa vya upinzani kwa kuiita mkusanyiko haramu. Hayo ndiyo yamekuwa mazoea; hususan, katika kipindi cha miaka sita (6) ya serikali ya awamu ya tano.

Ifahamike kuwa vifungu 43 – 46 vya jeshi la polisi vilitungwa kukidhi mahitaji ya mikutano na mikusanyiko mingine (maandamano, mikutano ya kidini, mikutano ya wafanyakazi n.k.) kwani wakati huo (1973) nchi ilikuwa na chama kimoja na hivyo jeshi la polisi halikuhusika kabisa na mikutano ya kisiasa.
Sheria ya vyama vya siasa (mwaka 1992 Toleo la 2019) imevipa haki vyama vya siasa kufanya mikutano kwa kutoa taarifa polisi ili kupata ulinzi. Haiwezekani sheria ya vyama vya siasa ikatoa haki halafu, ndani mwake kukawa na vifungu vinavyo ondoa haki hiyo.

2. Aidha kukifanyia marekebisho kifungu cha 11(8) kutoa muda (saa 12) ambao ndani yake ofisa wa jeshi la polisi aliyepewa taarifa ya mkutano wa chama cha siasa atapaswa kujibu kuzuia mkutano usifanyike kama kuna sababu za msingi kufanya hivyo. Kujibiwa ndani ya saa 12 kunalenga kukifanya chama kilichotoa taarifa kutoendelea na maandalizi na hivyo kuepusha kuingia gharama.

3. Kifungu cha 8E kinachohusu makundi ya ulinzi kwa vyama vya siasa kifutwe na kiandikwe upya kuzingatia uamuzi wa mahakama ya Afrika Mashariki ambayo ilitamka kuwa kinakinzana na mkataba wa Afrika Mashariki ambao Tanzania ni mwanachama na imeuridhia. Vyama viruhusiwe kuwa na Ulinzi wake kulinda viongozi na mali za Chama.

D: RUZUKU YA VYAMA VYA SIASA.

ACT Wazalendo inapendekeza Sehemu ya V ya Sheria ya Vyama vya Siasa inayohusu fedha kwa vyama vya siasa ifanyiwe maboresho kama ifuatavyo;

1. Kifungu cha 16(1) kiboreshwe kwa kuongezewa sharti la tengo la ruzuku kwa vyama vya siasa kuwa kati ya asilimia moja na mbili ya bajeti ya mwaka wa serikali.

Maboresho hayo yanalenga kulinda tengo la ruzuku kwa vyama vya siasa kwani bila kufanya hivyo, serikali inaweza kutenga 0.3% ya bajeti yake kiwango ambacho ni pungufu ya 2%.

2. Kifungu cha 16(3) kinachoainisha sifa za chama kustahiki ruzuku kiboreshwe kwa kuongeza fasili mpya tano (5) zinazoshajihisha vyama vyote vya siasa kushiriki uchaguzi, kuzingatia uwiano wa jinsia na kuwa na matumizi mazuri ya fedha za umma zitakazotolewa kama ruzuku.

Pamoja na mambo mengine, Vyama vipewe masharti ya kushiriki chaguzi; kupata uwakilishi (angalau Mbunge au Mwenyekiti mmoja wa Kijiji au Mtaa kwenye chaguzi hizo; angalau 30% ya viongozi wake wa Kitaifa wawe Wanawake; kutopata hati chafu kwenye ukaguzi wa CAG.


3. Kifungu cha 17(2) kinachohusu mgao wa ruzuku kiboreshwe kuwezesha vyama vyote vyenye usajili wa kudumu na vinavyokidhi matakwa ya kifungu cha 16(3) kupata ruzuku ya serikali kwa mgawanyo ufuatao;

i) Asilimia 10 (10%) ya ruzuku igawanywe sawa kwa Vyama vyote vya Siasa vilivyokidhi masharti ya Kifungu hicho.

ii) Asiimia 40 (40%) ya ruzuku igawanywe kwa Vyama kwa uwiano wa viti vya Wabunge wa Kuchaguliwa.

iii) Asilimia 25 (25%) ya ruzuku igawanywe kwa Vyama vya Siasa kwa kuzingatia kura za Wabunge.

iv) Asilimia 25 (25%) ya ruzuku igawanywe kwa kuzingatia kura za Madiwani.

E: MASUALA YANAYOHUSU UCHAGUZI

Kamati Kuu ya ACT Wazalendo imependekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania na Tume Huru ya Uchaguzi ya Zanzibar. Mapendekezo ya kina ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na Sheria zinazosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yatawasilishwa kwa umma kupitia uchambuzi wa kina utakaowekwa kwenye tovuti ya Chama.

Imetolewa na:

Salim A. Bimani,
Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
ACT Wazalendo.
23 Mei, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK