Kupandishwa ada ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo ni kikwazo kwa Elimu; Haikubaliki!

Kupandishwa ada ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo ni kikwazo kwa Elimu; Haikubaliki!

Utangulizi

Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo (Law School of Tanzania) imepandisha gharama za mafunzo ya uanasheria kwa vitendo kutoka Shilingi 1,570,000/ hadi Shilingi 2,950,000/= ambayo ni sawa na 88% inayotakiwa kulipwa ndani ya muda wa mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa utaratibu uliopo malipo hayo yanapaswa kufanywa kwa mkupuo ili mwanafunzi aweze kukidhi vigezo vya kusajiliwa na kuendelea na masomo hayo.

ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa sekta ya Katiba na Sheria tunaungana na wadau wengine kupinga kwa nguvu zote uamuzi huu. Tunaupinga kwa sababu zifuatazo;

Moja, ongezeko hili la ada kwa wanafunzi wa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo linaenda kuongeza mzigo mzito kwao na kuwa kikwazo cha kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu kwa ustawi wa vyombo vya kutoa haki nchini. Wakati uhalisia unatuonyesha kuwa gharama za elimu zinapoachwa kwenye mabega ya wananchi, zinategeneza matabaka ya upatikanaji wake kati ya wenye nacho na wasio nacho.

Pili, uamuzi huu ni kufanya elimu hii ya vitendo kuwa ni kitega uchumi cha biashara na siyo huduma. Kwa hiyo wenye uwezo ndio wataweza kununua na wasio na uwezo wataikosa. Uamuzi huu unapaswa kupingwa kwa kuwa unakuza ubaguzi katika kupata haki ya elimu miongoni mwa watanzania kwa kigezo cha kumudu gharama.

Tatu, tunapinga kwa kuwa hakuna sababu za msingi zilizoelezwa au zinazoweza kuhalalisha ongezeko hilo maradufu la ada.
Nne, ada inaenda kuongeza mzigo kwa kuwa hali ya sasa wanafunzi wengi wanajigharamia kila kitu kuanzia ada, vifaa vya kujifunzia, malazi, chakula na mafunzo kwa vitendo. Ongezeko la gharama za Maisha kwa kupanda kwa bei mbalimbali za bidhaa ilitegemewa Serikali kufikiria namna bora ya kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia kwa wanafunzi hao kuliko kuongeza ugumu wa mazingira hayo.

Ongezeko la ada linaacha maswali mengi; zipi sababu za msingi za kupandisha ada kiasi hiki? Je, imezingatiwa uwezo wa wanafunzi? Ongezeko linalenga kuwezesha uendeshaji au kubidhaisha elimu? Maswali haya yanaleta hisia za kudhani kuwa nia ya taasisi hiyo ni kuzuia au kuweka taratibu za kupunguza wanafunzi kupata haki yao ya kuingia kwenye chuo hicho. Uamuzi huu unabakisha wasiwasi huo kwamba miongoni mwa mbinu za kuzuia ni kupitia ada kwa kuwa ni wazi watoto wanaotoka familia maskini hawatoweza kumudu gharama hizi.

Hivyobasi, ACT Wazalendo tunapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa ili kuhakikisha mafunzo ya uenasheria kwa vitendo yanakuwa kwa wote bila vikwazo;-

1. Serikali iache kutumia mantiki za soko kwenye kutoa huduma muhimu kwa watu kama elimu. Elimu ni huduma sio bidhaa, ihakikishe kila mtu anaweza kuipata bila kikwazo chochote.

2. Ikiwa taasisi ya mafunzo kwa vitendo imepandisha ada kwa sababu za uendeshaji; tunaishauri Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itoe ruzuku ili kuiwezesha taasisi hiyo kumudu gharama za uendeshaji kuliko kuruhusu gharama hizo kubebwa na wanafunzi.

3. Ili kuleta ufanisi na kuondoa vikwazo kwa wanafunzi, Wizara iwapunguzie wanafunzi hao gharama nyingine kwa kuweka mazingira wezeshi kama vile hostel na kutanua wigo wa mikopo ya Elimu kwa wanafunzi wa sheria kwa vitendo (LST).

Imetolewa na;
Ndg. Advocate Victor Kweka
Twitter: @Advocate_Kweka
Waziri Kivuli wa Sekta ya Katiba na Sheria

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK