MAHINDI YA TANZANIA NI SALAMA. Tanzania na Kenya Zimalize Mzozo Kidiplomasia - Zitto Kabwe

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Ndg. Zitto Kabwe ameitaka Serikali ya Tanzania kukaa mezani na Serikali ya Kenya kumaliza mzozo wa Soko la Mahindi ya Tanzania nchini Kenya. Ndugu Zitto amesema;

“Mwaka 2017 Serikali ya Tanzania ilizuia mahindi kuuzwa nje. Maumivu waliyopata wakulima hayamithiliki. Kilo ya Mahindi ilishuka mpaka shs 100. Nilipotembelea Wilaya ya Namtumbo nilikuta Wananchi wanafanya ‘barter trade’ ya mahindi na mazao mengine kwa sababu mahindi hayakuwa na soko. Wakulima wengi walitumbukia kwenye umasikini wa kutisha, wafanyabiashara walifilisika na msimu uliofuata mavuno yalishuka sana. Sitaki kuona mkulima wa Tanzania akirudi kwenye maumivu yale kwa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.

Serikali ya Tanzania ilifanya makosa makubwa na tulilaani sana uamuzi ule wa hatari kabisa kuzuia mauzo ya mahindi nje ya nchi. Wizara ya Mambo ya Nje itimize wajibu wake kwa kuzungumza na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya kwa kuzingatia Mkataba wa Afrika Mashariki.

Sisi kama Viongozi wa Kisiasa wajibu wetu ni kwa Watanzania. Wajibu wetu sio kwa wengine zaidi ya raia wetu. Mahindi ya Tanzania ni salama. Watanzania hawalimi Mahindi yenye sumu. Watanzania wanakula mahindi haya haya yanayouzwa Kenya. Ni lazima kuwalinda wakulima wa Tanzania. Ni muhimu kulinda soko la bidhaa za Tanzania. Tusirudie makosa ya Mbaazi na Korosho ambayo yaliumiza sana watu wetu.

Ni wajibu wetu kulinda wakulima wetu wa Tanzania na wafanyabiashara wa Mahindi. Tunalazimika kuisukuma Serikali ya Tanzania imalize tatizo hili kwa kuzungumza KIDIPLOMASIA na Serikali ya Kenya. Hili ni jambo la kidiplomasia sio sumu. Sumu imetumika tu kama sababu. Ni Biashara hii.

Kwenye hili la Mahindi ninaamini kuwa hoja sio aflatoxin (sumukuvu). Nchi zetu zimekuwa zikifanya juhudi za pamoja kukabiliana na aflatoxin na ushahidi ni Sheria pendekezwa EAC. Hili ni jambo la Diplomasia. Tanzania na Kenya wakae wazungumze.

Kuna taratibu za kisheria za kufuata kukagua Ubora wa mahindi. Zifuatwe hizo. Mahindi ya Tanzania ni salama na yana kiwango cha aflatoxins kinachokubalika. Kenya na Tanzania wamekuwa wakichukua hatua kukabiliana na aflatoxins kupitia EAC na kuna muswada wa Sheria ya EALA juu ya hilo.

Hiyo amri (ya kuzuia mahindi ya Tanzania kuingia Kenya) haipaswi kuwa Juu ya Mkataba wa EAC na Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Kila mwanachama wa EAC lazima aheshimu Mkataba na Itifaki. Aflatoxin imetumika kama sababu tu lakini sio hoja. Hoja ni biashara.

Kwa mujibu wa utafiti, Mahindi ya mikoa miwili tu ndio yana kiwango kikubwa cha aflatoxin, Manyara na Dodoma. Mahindi ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Ruvuma, Kigoma etc hayana kabisa aflatoxin. Kenya hawawezi KISHERIA/KIMKATABA kuzuia Mahindi yote ya Tanzania!

Idara ya Nje ya Usalama wa Taifa (TISS) ifanye uchunguzi kama ni kweli Jamhuri ya Kenya imezuia Mahindi ya Tanzania kwa sababu kuna meli yenye shehena ya Mahindi kutoka Mexico Bandari ya Mombasa. Kama ni kweli Tanzania iishitaki Kenya EAC kwa kukiuka Mkataba wa EAC kwani EAC ni Soko Moja. Hizi ndio kazi za Usalama wa Taifa badala ya kuhangaika na kuteka wanasiasa wa upinzani. Soko la bidhaa za Tanzania nje ni Sera ya Mambo ya nje na ni wajibu wa kitengo cha nje cha Usalama wa Taifa. Watanzania wanalipa kodi ili wafanye kazi hiyo.

Sifa kubwa ya Mahindi ya Mexico ni kuwa na pumba nyingi na hivyo kuleta hasara kwa wasagishaji (Millers). Inawezekana kabisa kuwa Mahindi ya Tanzania yanazuiwa ili kulazimisha Millers nchini Kenya kupokea Mahindi ya Mexico. Serikali ya Tanzania ina Wajibu wa kufanyia kazi Haya.

Mwaka 2020 Tanzania ilivuna mahindi Tani Milioni 6 ilihali matumizi yake ni Tani Milioni 4.8 tu. Tani Milioni 1.2 za ziada zinauzwa Nje na Kenya ni soko muhimu la Mahindi ya Tanzania. Takwimu zinaonyesha kuwa Kenya hununua Mahindi ya Tanzania yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani Milioni 250 sawa na Shilingi Bilioni 600 za Kitanzania.

Kiongozi wa Chama ndugu Zitto ameitaka Serikali kulinda soko hili kwa wivu mkubwa na amekemea tabia ya viongozi wa Serikali kuchukua maamuzi dhidi ya Kenya ambayo madhara yake ndio haya tunayoona sasa. Kenya na Tanzania ni ndugu na wanachama wa EAC hivyo mgogoro wowote utatuliwe kwa kutumia Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC, alisisitiza.


Imetolewa na:
Idara ya Habari na Uenezi,
ACT Wazalendo,
08 Machi, 2021.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK