Maoni ya ACT Wazalendo kuhusu Muswada wa Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii kwa Wote.

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

Maoni ya ACT Wazalendo kuhusu Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote na Mapendekezo mbadala ya Hifadhi ya Jamii kwa Wote.

1. Utangulizi:

Mnamo tarehe 23, Septemba 2022 Serikali iliwasilisha kwa mara ya kwanza Muswada wa Bima ya Afya kwa wote kwenye Bunge la Jamuhuri ya Muungano kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anajumuishwa katika mfumo wa Bima ya Afya kupitia Mifuko ya Bima ya Afya ya Umma iliyopo au kampuni binafsi za bima ya afya zilizopo.
Wasilisho hili liliibua mijadala miongoni mwa wananchi, asasi za kiraia, vyama vya kijamii na vyama vya siasa ambao tuliupitia na kuujadili.

Sisi, ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Wasemaji wa Kisekta tumetumia wasaa huo kupitia muswada huo na hatimaye tumepata mapendekezo mbadala kwa ajili ya kuboresha nia ya kuhakikisha Tanzania kama jamii inakuwa na mfumo bora wa afya kwa watu wote.

Kihistoria, tangu Serikali ilipoanza kufanya utekelezaji wa sera ya uchangiaji wa huduma muhimu kama vile Afya na Elimu kutokana na sera ya urekebishaji wa uchumi na soko huria, mwanzoni mwa miaka 1990, kumeongeza pengo kubwa la wananchi wenye nacho na wasio nacho katika kupata huduma za afya. Tangu hapo, upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa umekuwa ukitegemea uwezo wa kifedha wa mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa wenyewe.

Mfumo wa sasa wa ugharamiaji wa huduma za afya umeachwa kwenye mabega ya mwananchi aidha kwa kutumia pesa taslimu au kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya. Jitihada za Serikali katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa usawa zinazuiwa na gharama kubwa na mifumo mibovu ya kuunganisha nguvu za wananchi zenye uwezo wa kupanua wigo na uwezo wa Serikali kugharamia huduma hii muhimu.

Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa zilizotolewa mwezi Juni mwaka huu (2022), zinaonyesha kuwa mwaka 2021 jumla ya Watanzania milioni 41 (41,448,117) walikuwa wagonjwa wa nje kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati Nchi nzima. Hii ina maana kuwa 71.8% ya Watanzania waliumwa mwaka 2021.

Katika nchi ambayo raia wake wanaumwa kwa kiwango hiki suala la Afya linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa sana. Kitendo cha Serikali kujiondoa kwenye kuhudumia raia wake kwenye afya kwa namna yoyote ni kuwaumiza Wananchi.

2. Uchambuzi wetu:

Matarajio yetu na ya Wananchi wote, ni kuwa muswada huu wa Bima ya Afya kwa Wote unapaswa kwenda kutatua kiini cha kukosekana kwa upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa wote nchini, mijini na vijijini. Katika hali hii ACT Wazalendo tumeutazama kwa makini muswada huu, tumeuchambua na kuja na mapendekezo ili kuhakikisha huduma ya afya inaboreshwa kwa maslahi ya Wananchi wote bila kuwabagua kijiografia na kiuchumi. Sehemu ifuatayo tumeainisha mapungufu ya Muswada wa Serikali wa Bima ya Afya kwa Wote:

I: Njia (mfumo) wa kugharamia huduma ya afya:

Muswada wa Serikali unapendekeza njia ya kugharamia afya ni kila Mwananchi kulipia bima yake ya afya kwa kila mwaka. Changamoto ya pendekezo hili ni kwamba, kutumia michango ya Wananchi ambao ni wanachama wa bima kulipia bima zao wenyewe kwa asilimia yote haitoi uhakika na uendelevu wa utaratibu huu wa uchangiaji kwa Wananchi walio katika sekta isiyo rasmi. Hii inatokana na uhalisia uliopo nchini ambapo Wananchi wanaojighulisha na shughuli za sekta isiyo rasmi hawana uhakika wa kipato kitakachowawezesha kulipia bima zao za afya kila mwaka.

II: Huduma za afya zinazopatikana (Kitita cha mafao):

Muswada huu haujaenda kuondoa kabisa matabaka yanayoletwa na vifurushi (vitita vya mafao). Muswada unataja kuwepo kwa kitita cha mafao ya msingi na mafao ya ziada.
Hivyo, muswada huu unaimarisha mfumo mbovu unaoendelea wa utoaji wa huduma ya afya nchini, mfumo unao weka na kuimarisha matabaka kwenye jamii kwa kuifanya huduma ya afya iwe bidhaa, na kuongeza ugumu wa hali ya uchumi kwa Mwananchi.

III: Viwango vya uchangiaji:

Serikali inapendekeza viwango vipya vya uchangiaji kwa kila kaya yenye watu sita ni shilingi 340,000 na kwa mtu atakayejiunga nje ya mfumo wa kaya atalipia Shilingi za kitanzania 84,000.

Mwaka 2021 taarifa zinaonyesha kuwa asilimia 70 za Wananchi walikuwa wangonjwa wa nje ingawa waliolazwa walikuwa milioni 1.6. Kwa hali ya kupanda kwa gharama za maisha na uwezo wa kiuchumi, Wananchi hawatakuwa na mwendelezo wa kulipia malipo haya kila mwaka bila kupata misukosuko.

IV: Uwezo na Utendaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF):

Muswada wa Serikali unalenga kuongeza idadi ya wanachama wa mfuko wa Bima ya Afya kwa Umma kabla ya kutatua matatizo yaliyokwamisha NHIF. Mfuko wa Bima ya Afya kwa Umma unarithi matatizo ya upotevu wa fedha yaliyoielemea NHIF.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) ya 2020/2021 inaonyesha kuna malimbikizo ya makusanyo yanayofikia shilingi bilioni 8.7 kutoka kwa taasisi za umma na Wizara. Pia kuna upotevu wa fedha unaotokana mikopo ya shilingi bilioni 98.5 iliyoiva iliyotolewa kwa taasisi za Serikali ambayo haijalipwa na mkopo wa shilingi bilioni 129 uliotolewa kwa Serikali bila mkataba. Mkopo huu pia bado haujalipwa. Zaidi ya hayo kuna uwekezaji mkubwa kwenye kiwanda cha bidhaa za tiba cha Simiyu ambao bado haujazaa faida.

Aidha, muswada umeeleza adhabu mbalimbali kwa watumiaji na watoa huduma wataokiuka sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, lakini haujaelezea udhibiti wa ubadhirifu wa fedha za Mfuko wa Bima kupitia mamlaka za Serikali.

V: Utaratibu wa kujiunga na Bima ya Afya:

Mosi, muswada wa Serikali unaweka vigezo vya Mwananchi kuwa na leseni, pasi ya kusafiria, kitambulisho cha NIDA, laini za simu ndipo apate kadi ya Bima ya Afya. Tumejiuliza, na tunadhani kuwa Serikali hawajajipanga vizuri. Hivi haki ya NIDA na Bima kipi kinaanza?

Utaratibu huu unamnyima Mwananchi uhuru na haki yake ya msingi ya kupata huduma ya afya ambazo tayari anazilipia kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Serikali haijajiandaa. Sheria hii haitekelezeki. Serikali irudi tena mezani.

Sisi ACT Wazalendo tuko tayari kushirikiana na Wizara ili kuja na mpango bora unaotekelezeka kuendana na uhalisia wa maisha ya kila mtanzania. Lengo letu ni kupata Bima ya Afya kwa kila Mwananchi.

Pili, utambuzi wa watu wasio na uwezo, katika maelezo yake Waziri wa Afya ameeleza kwamba watu wasio na uwezo watatambuliwa kupitia taarifa za uanachama wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa mwaka 2021 zinaonyesha jumla ya watu milioni 6.3 sawa na 11% ya Wananchi wote walinufaika na mfuko wa TASAF. Idadi hii ni ndogo kulinganisha na hali halisi ya umaskini nchini ambapo idadi ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi ya dola moja kwa siku ni karibia asilimia 26.4 ya Wananchi wote. Utaratibu huu hautajumuisha Wananchi wengi zaidi wenye vipato vidogo kwenye sekta isiyo rasmi wasio na vigezo vya kunufaika na TASAF.

VI: Gharama za dawa na vifaa tiba:

Kwa mujibu wa Takwimu za taifa za afya (National Health Accounts) 2019 jumla ya matumizi halisi ya kwenye sekta ya afya ni wastani wa shilingi trilioni 5.42 kwa mwaka. Kuwepo kwa gharama kubwa zinazoenda kwenye sekta ya afya kunachangiwa na bei za dawa, tiba na vifaa tiba kutoratibiwa vizuri. Muswada huu wa Serikali haujagusa kichocheo cha ongezeko la gharama za dawa, vifaa tiba na vipimo ambao unaamuliwa na soko la dawa.

3. Mapendekezo ya ACT Wazalendo ni yepi?

Hifadhi Ya Jamii Kwa Wote Itayohakikisha Kila Mtanzania Anakuwa Na Bima Ya Afya:

Yafuatoyo ni mapendekezo ya ACT Wazalendo kuhusu mfumo endelevu wa Hifadhi ya Jamii utakaohakikisha kama taifa, tunakuwa na Bima ya Afya kwa Wananchi wote:

1. Mfumo Unavyopaswa kuwa:

I. Kila Mwananchi ambaye ana ajira rasmi na kukatwa michango ya Hifadhi ya Jamii atapata Fao la Matibabu. Mfuko wa NSSF au PSSSF ambao mwajiriwa ana mchango wake utapeleka 1/5 ya mchango wa mwajiriwa kwa Skimu ya Bima ya Afya.

II. Kila Mtu ambaye amejiajiri kwenye sekta ya Kilimo, Biashara au shughuli nyingine yoyote na ni mwanachama wa hiyari katika mfuko wa Hifadhi ya Jamii anayechangia kiwango cha chini cha mchango wa Mwezi (kwa sasa ni Shs 30,000) atachangiwa na Serikali theluthi ya mchango kila mwezi, hii itakuwa pia ni juhudi ya makusudi kuvutia Wananchi walio kwenye sekta isiyo rasmi kujiunga kwenye mfuko wa Hifadhi ya Jamii na kupata Bima ya Afya. Mfuko wa NSSF utawasilisha kwa Skimu ya Bima ya Afya 1/5 ya mchango huu kila Mwezi kwa ajili ya Fao la Matibabu la mwanachama wake. Tofauti na sasa mwanachama atatakiwa kuchangia 340,000 kwa mwaka kwenye mfuko wa afya kwa ajili ya matibabu pekee.

Kwa hiyo, kila mwenye kadi ya NSSF au PSSSF moja kwa moja anakuwa ana kadi ya Skimu ya Bima ya Afya. Bima ya Afya inakuwa ni fao tu katika moja ya mafao ya Hifadhi ya Jamii lakini uendeshaji wake unafanywa na Skimu ya Bima ya Afya.

III. Mwananchi yeyote ambaye ni mnufaika wa TASAF atalipiwa mchango wake na Serikali moja kwa moja kwenye Hifadhi ya Jamii kwa 100%. Hata hivyo mfuko wa Hifadhi ya Jamii utakuwa na Fao maalumu la kuwawezesha kuzalisha kipato ili kufikia kundi la kuchangiwa theluthi tu.

IV. Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) isimamie na kudhibiti Skimu ya Bima ya Afya badala ya Mamlaka ya usimamizi wa Bima (TIRA) kama ilivyo sasa.

2. Utekelezaji Wake:
Hali halisi iliyopo hivi sasa:

- Ni Watanzania milioni 9 tu ndio wanaohudumiwa na bima ya afya. Hiyo inafanya kuwa 15% tu ya Watanzania wote,

- Watanzania milioni 14 wanaishi chini ya mstari wa umaskini uliokithiri kwa viwango vya kimataifa huku wengi wao wakiwa juu kidogo na chini ya mstari wa umaskini,

- Kiwango cha kuwa kwenye mazingira hatarishi ni kikubwa: kwa kila Watanzania wanne waliotoka kwenye umaskini, watatu walirudi tena kwenye umaskini.

- Idadi kubwa ya watu wasio maskini wanaoishi juu kidogo ya mstari wa umaskini wako katika hatari ya kuteleza chini yake na kurudi kwenye umasikini.

- Akiba kama sehemu ya Pato la Taifa ni ndogo sana kwa 16%

- Upatikanaji wa mikopo upo chini sana miongoni mwa Wananchi maskini.

Mapendekezo yetu:

I. ACT Wazalendo tunatambulisha mpango wa Hifadhi ya Jamii ambao utaenda kuwalinda Wananchi walioko katika kundi la umaskini kwa njia tatu zifuatazo;

a) Wananchi walio na kipato kidogo: watie motisha ya kuweka akiba, kwa kuoanisha mpango huo, kupitia mfumo wa Hifadhi ya Jamii ambapo faida ni pamoja na:
• Kupata mikopo (ujumuisho wa kifedha),
• Bima ya afya na
• Pensheni ya uzeeni.

b) Wananchi ambao ni maskini wa kupindukia: wanatoa msaada kwa ajili ya kuzalisha mapato huku wakichangia kwa ajili hiyohiyo akiba katika mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa muda mfupi hadi wahitimu kwenye mpango unaolingana, na;

c) Kulenga uwekezaji wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii katika shughuli za kiuchumi zinazowawezesha maskini na vyanzo vya nishati rafiki kwa hali ya hewa kwa maskini.

II. Wananchi walioko katika sekta isiyo rasmi watajiandikisha katika mpango wa hiari chini ya NSSF. Kiwango cha chini cha mchango kwa NSSF na mwanachama ni 20,000. Serikali inapaswa kuchangia shilingi 10,000 kwa kila mwanachama.

Kwa bima ya afya:

I. NSSF italazimika kutoa Bima ya Afya kama fao la muda mfupi kwa wanachama wake chini ya SHIB (faida ya bima ya afya ya jamii)
• Wanachama wote wa sasa wa NSSF na wanachama wapya kutoka kwa mpango wa hiari watapata faida ya bima ya kijamii. Mfuko utapeleka kwenye mfuko wa bima ya afya jumla ya 20% ya michango ya wanachama;

• Wanachama wote wa sasa wa PSSSF pia watapokea faida ya bima ya kijamii na mfuko kupeleka kwenye mpango wa bima ya afya 20% ya michango yote ya wanachama.

III. Kwa wanachama milioni 1.5 wa sasa wa mifuko ya hifadhi ya jamii, mpango wa bima ya afya utapata karibu TZS 530 bilioni. Wanachama wapya wa mifuko ya hifadhi ya jamii wataongeza michango katika mpango wa bima ya afya zaidi. Tutaona nambari hapa chini.

Makiso ya watu watakaojiunga na Skimu ya hiyari ya Hifadhi ya Jamii:
- Watanzania Milioni 13.7, kati yao 60% ni Wanawake wanaoishi maeneo vijijini ambao wanajihusisha na shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara ndogo ndogo pamoja na watu milioni 6.3 ambao kwa sasa wapo katika mpango wa kusaidia kaya maskini wa TASAF.

Uwekezaji na Mapato ya Michango:
- Trilioni 1.03 kila mwaka kwa miaka mitano ya kwanza. Kiasi hiki ni mchango wa Serikali ambayo itaoanisha na michango ya wanachama Milioni 7.4 watakaojiunga na skimu ya hiyari itakayokuwa inasimamiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

- NSSF itakusanya Shilingi trilioni 2.06 kila mwaka kwa makadirio ya wanachama milioni 7.4 wa skimu hii.
- NSSF itapokea kutoka Serikalini jumla ya shilingi trilioni 2.56 kwa ajili ya wanufaika wa TASAF.

Jumla ya michango ya mwaka kwenda NSSF kutokana na skimu hii itakuwa jumla ya shilingi Trilioni 5.5

20% ya michango itapelekwa kwenye skimu ya bima ya afya kwa wote. Hii itakuwa kiasi cha shilingi bilioni 620.7 kwa kila mwaka kutoka kwa wachangiaji wengine na Shilingi bilioni 477.6 kutoka kwa wanufaika wa TASAF

Muhimu:
- Skimu hii itabuniwa kupitia skimu ndogondogo lama vile Skimu ya Wamachinga, Skimu ya wavuvi, Skimu ya Wafugaji n.k. Wananchi watajiunga na skimu kupitia vyama vyao vya ushirika
- Uwekezaji wa matumizi ya Teknolojia ya kidijitali.
- Uwekaji huu wa akiba utawezesha upatikanaji wa mikopo, fao la bima ya afya na mafao mengine ya muda mfupi kama vile fao la bei kwa wakulima/wavuvi na pensheni ya wazee ili kukabiliana na umaskini wa wazee.
Kitakwimu skimu hii ina maana ifuatayo:

1. Jumla ya Watanzania watu wazima Milioni 9.9 watakuwa wanachama wa Hifadhi ya Jamii na moja kwa moja watanufaika na fao la skimu ya bima ya afya.

2. Jumla ya watu Milioni 59.4 watapatiwa ‘bima ya afya kwa wote’ kwa kanuni ya kawaida ya mchangiaji mmoja na wategemezi watano (Mwenza na wanufaika 4).

3. Watu Milioni 6.3 waliopo chini ya TASAF watachangiwa na Serikali kiasi chote cha hifadhi ya jamii na kupata fao la bima ya afya.

4. Serikali itaweza kutangaza bima ya afya kwa wote.

5. Skimu ya Bima ya afya itakusanya michango ya:
• Shilingi Trilioni 1.6 trillion kwa mwaka,
• TZS 530B kutoka kwa wanachama wa sasa wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii,
• TZS 680B kutoka kwa wanachama wachangia,
• Mchango wa Serikali na
• TZS 464B kutona na wanufaika wa TASAF kuhudumia huduma afya ya watanzania.

6. NSSF itakuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii mkubwa zaidi kwa Afrika Mashariki kama sio Afrika nzima kwa kuwa na michango ya kila mwaka wastani wa Shilingi trilioni 7.2.

Ugharamiaji wa bima ya afya kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wote Mapendekezo ya ACT Wazalendo:

I. Michango ya Serikali:
• Tsh. Trilioni 1.03 kila mwaka kwa miaka mitano ya kwanza.
• Kiasi hiki ni mchango wa Serikali kuoanishwa na michango ya Wanachama Milioni 7.4 watakaojiunga kwa skimu ya hiyari itayosimamiwa na NSSF.
• Tsh. Trilioni 2.56 kila mwaka
- Kiasi hiki kitalipwa na Serikali kwa wanufaika wa TASAF ( ambao ni Wananchi wanaotoka kwenye kundi maskini zaidi)
• Jumla kuu ya fedha zitakazotolewa na Serikali kwa mwaka inapaswa kuwa Shilingi Trilioni 3.49.

II. Michango ya Wananchi:
• Tsh. Trilioni 2.1 kila mwaka ni kiasi kinachopaswa kulipwa na Wanachama Milioni 7.4 watakajiunga na Skimu ya hiari inayochangiwa na Serikali.
• Tsh. 2.56 kila mwaka kutoka kwa mtaji wa Wanachama wa sasa ambao ni milioni 1.5 kutoka Sekta rasmi.
• Jumla ya mapato yanayotokana na michango kwenda hifadhi ya jamii inakadiriwa kuwa Trilioni 8.38
• Gawio litakalopelekwa kwenye fao la bima ya afya itakuwa Trilioni 1.66

III. Taasisi zinazohusika na usimamizi:

- Benki Kuu ya Tanzania:
Itasimamia Akaunti ya Serikali ya skimu ya hifadhi ya jamii. Itasimamia bajeti iliyoidhinishwa kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina na gawio la kila mwezi kwenda NSSF fedha za kuchangia baada ya kuthibitisha michango ya wanachama. Gawio kwa NSSF ya jumla ya michango kutoka kwa watu maskini zaidi.

- NSSF:
Kusimamia skimu ya hifadhi ya jamii kwa Sekta binafsi rasmi na sekta isiyorasmi inayopendekezwa Sasa.

-PSSF:
Kusimamia wafanyakazi ambao ni wanachama wa kwenye mifuko ya hifadhi, kusimamia akaunti za wanachama wa NHIF na kuhakikisha uwekezeji wa makusanyo.

-NHIF:
Kusimamia mfuko wa bima ya afya na madai kutoka kwa watoa huduma ya afya.

-SSRA:
Itahusika na kufanya udhibiti kwenye sekta ya hifadhi ya jamii na mfumo mzima wa bima ya afya.

-MSD:
Itasimamia upatikanaji wa nyenzo, madawa na vifaa vya kutoa huduma ya afya. NSSF itatoa uwezeshaji wa muda mrefu kwa MSD kwa kiasi cha Tsh. 500B kama mtaji wa upatikanaji wa vifaa vya tiba. Malipo haya yatafanywa kwa uhakika wa miaka kumi.

-Taasisi zinazotoa huduma ya afya kama hospitali, vituo vya afya, zahanati n.k ambazo zitahusika na kutoa huduma za afya kwa Wananchi na kudai malipo yao kutoka NHIF.

-Wizara ya Afya:
Itasimamia maswala ya sera, miundombinu ya afya, kufanya uhamasishaji na uchechemuzi wa afya ya kinga kwa kushirikiana na mifuko ya hifadhi ya jamii, wafanyakazi katika mashirika ya afya.

-Tunapendekeza kaunzishwa kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais ya Uchumi, Hifadhi ya Jamii na Mashirika ya Umma:
Itakayosimamia utengenezwaji na uendelezaji wa sera ya hifadhi ya Jamii, kusimamia uendeshaji wa mfumo wake na usajili wa wananchi.

• Umuhimu wa kuoanisha Michango, Uwekezaji na Mafao katika Mfumo wa Bima ya Afya?

Kazi tatu za mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii ni kama zifuatazo;
i. Michango
ii. Uwekezaji
iii. Mafao

Maskini hawaweki akiba na wale wanaoweka akiba wanahitaji ulinzi wa akiba zao kutokana na mshtuko mkubwa ambao ni matumizi makubwa ya afya. Madhumuni ya kuwawezesha watu kulipwa bima ya afya (kama faida ya kuwa katika mpango wa hifadhi ya jamii), kupata mikopo ya kufungua/kuendesha/kupanua shughuli zao za kiuchumi na kuweka fedha mifukoni ili kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi ulioathirika pakubwa na UVIKO-19 kupitia kuwekeza tena kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa watu wanaoathiri miradi ili kuongeza shughuli zao za kiuchumi. Wazo hilo litapanua huduma ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi na kuongeza kwa kiasi kikubwa akiba na uwekezaji.


• Uhalisia na Utekelezaji wake:

- Kuwepo kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wenye uzoefu wa kusimamia mpango kama huu. Lakini inahitaji uboreshaji wa miundo ya utawala wake ikiwa ni pamoja na kuwa na walengwa kuwakilishwa kwenye bodi ili kusimamia mpango huo.

- Kaya maskini tayari zimetambuliwa na zingine zitatiwa moyo kupitia mpango mkubwa wa elimu uliojengwa ndani ya wazo hilo.
- Teknolojia ya kidijitali kupitia akaunti za simu za mkononi, kuwepo kwa mikopo inayotolewa kwa njia ya simu na uwezo wa kuangalia taarifa mbalimbali kidigitali itakuwa ni faida nzuri kutumiwa ili kutekeleza wazo hili ni rahisi na inawezekana na hatari ndogo za matumizi mabaya na kuvuja.


Imeandaliwa na:


Baraza la Wasemaji wa Kisekta,
ACT Wazalendo.
18 Oktoba, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK