Mchakato wa Katiba Mpya Uzalishe Muungano Unaokubalika na Pande zote za Nchi Washirika
TAARIFA YA MIAKA 58 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR.
Utangulizi:
Ni Fahari katika historia kwa taifa letu kuadhimisha miaka 58 ya Muungano ambapo nchi mbili huru, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ziliungana rasmi siku ya tarehe 26-04-1964 kufanya Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wa Tanzania, kama ulivyozoelekea kuitwa, umesimama na kutembea kwa kuchechemea na kuyumba huku busara zikitawala zaidi kuliko sheria na hati yenyewe ya Muungano. Bila shaka, kila awamu ya uongozi wa Taifa hili inastahili pongezi na lawama kwa kiwango sawa!
Miaka hii 58 ya Muungano wa Tanzania haijaweza kufanikisha mambo makubwa, yanayopimika ya kusifiwa wala kujidai. Kuanzia awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kufuatiwa na ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi na ya Tatu ya Hayati Rais Benjamin William Mkapa hakuna iliyotengeneza wala kuboresha mapungufu makubwa ya Muungano. Ni Katika awamu hizi ambapo makubaliano ya Muungano yalianza kukhalifiwa kinyemela na kisirisiri huku ikiwanyima wananchi wa nchi zote mbili - Tanganyika na Zanzibar uhuru wa kuamua mambo yanayo husu nchi zao. Kila mara Serikali imetoa visingizio vya kuulinda Muungano. Muungano ambao, hauna sauti za wananchi na hivyo miaka imezidi kusogeam Muungano huu ukipoteza ladha na uhalali wake kwa umma.
Awamu ya nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Awamu ya tano ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ziliendeleza na kuongeza kasi ya kuubomoa Muungano kwa kuzidi kuyapuuza makubaliano yake. Awamu ya Nne ilitekeleza hilo kidiplomasia na awamu ya tano ilitumia ubabe. Mchakato wa Katiba Mpya wa 2014/2015 ni ushahidi wa kuyabeza matakwa ya wamiliki wa Muungano wa Tanzania – wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunaadhimisha miaka 58 ya Muungano tukiwa na Kitendawili Mtegoni. Ni mwongozo upi wa Muungano wenye haki na unaokubalika kwa wamiliki wake kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Katiba ya Zanzibar au Hati Halali ya Muungano? Suala ni Je, iko wapi Katiba ya Tanganyika ilhali Tanganyika ni Mshirika sawa wa Muungano? Muungano umekuwa ukiingizwa dosari kwa kisingizio cha kutumia busara kuliko matakwa ya mambo hayo matatu au manne.
Hali halisi ya sasa ya muungano:
Tunaadhimisha miaka 58 ya Muungano tukiwa katika Awamu ya 6 ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.Tukisema tusahau yaliyopita, iwe na maana ya kuyasoma makosa yetu na kuyarekebisha bila kunyoosheana vidole. Kwenye awamu hii, ni Wakati mzuri wa kutafakari sababu za uchechemeaji na kuyumba kwa Muungano. Kuelekea mwaka wa 59 wa Muungano, sisi wananchi tuliorithi na kumiliki Muungano huu tunao Wajibu wa kujifunza na kurekebisha katika maeneo yafuatayo:
Kukosekana kwa uzalendo na utengamano wa jamii:
Mfumo wa sasa umethibitisha kuwa na mapungufu katika utekelezaji wa maswala ya Muungano. Matokeo yake yamekuwa kukosekana kwa uzalendo na utengano katika jamii. Kwa miaka 58 sasa Muungano umeshindwa kuwaunganisha Watanzania wote, kujenga utamaduni wa kusameheana kwa mambo yaliyopita ili kuwafanya Watanzania wawe wamoja bila kuipoteza historia na asili ya ukweli kwamba sisi ni Watanzania tuliotoka Tanganyika na Zanzibar na tuna haki na wajibu sawa Katika Muungano huu.
Kukosekana kwa haki sawa za misingi imara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii:
Tunaadhimisha miaka 58 tukiwa na pande mbili za Muungano zinazohitaji mfumo bora wa kuweza kuzinasua pande hizi kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa kupitia mamlaka zake kamili kama washirika sawa wa Muungano wa haki ili kila upande uweze kutumia rasilimali ilizonazo kikamilifu kwa manufaa ya wananchi wote wa pande hizi mbili.
Miaka 58 itoshe kuanza mchakato wa kujenga misingi imara ya kiuchumi itakayoleta mabadiliko makubwa katika maisha ya Watanzania wote kwa kuanzisha na kutekeleza sera madhubuti zinazojitegeea za fedha (fiscal policies) na mipango-mikakati ya muda mrefu ya uwekezaji wa ndani na nje, ili kuzifanya pande mbili za Muungano kuwa na uwezo wa kusafirisha bidhaa na kupanua huduma zake za kiuchumi na kibiashara nje yanchi zao, lakini pia kukuza uwezo wa kutengeneza ajira zaidi kwa wananchi wengi wa pande zote mbili za Muungano wa Tanzania.
Umefika wakati sasa wa kuona ulazima wa kuwa na mfumo utakaowezesha kila upande wa Muungano kujenga uchumi imara kwa kuzingatia nafasi yake kijiografia na kuzitumia rasilimali zilizopo Katika kila upande vikiwemo bahari, fukwe, urithi wa kale, mafuta na gesi asilia ili wananchi wa kila upande wa Muungano waweze kufaidika kutokana na tija ya mazao na uwekezaji huo Katika nchi yao.
Kukosekana kwa fursa sawa za matumizi ya sayansi na teknolojia:
Miaka 58 ya Muungano imeshuhudia mfumo usio bora unaozinyima pande mbili za Muungano kukosa fursa sawa za kuiingia kikamilifu katika ulimwengu wa sayansi na teknologia ili kurahisisha maisha ya watu wake na Watanzania kwa ujumla. Ipo haja sasa, kuelekea miaka 59 ya Muungano wetu, kuzipa fursa sawa pande mbili za Muungano ili ziweze kutumia vyema faida za sayansi na teknologia ya kileo.
Mapungufu ya Uongozi kushindwa kuleta matokeo ya uwajibikaji:
Mfumo wa sasa, kwa miaka 58, umezinyima pande mbili za Muungano uwezo wa kusimamia suala zima la uongozi mwema unaolenga matokeo (results focused) na uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali. Kuelekea miaka 59 ya Muungano huu, iwe wakati wa kuwa na mfumo bora wa kuziruhusu pande mbili za Muungano kuweza kuanzisha sera kali na bora kuhusu rushwa ili wananchi kila upande waweze kufaidi matunda ya nchi zao na serikali zao.
Kukosekana kwa amani na usalama na kuendelea kwa vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa haki za binadamu:
Miaka 58 ya Muungano wetu tumeshuhudia mfumo wa ulinzi na usalama ambao bado juhudi za kila upande wa Muungano za kuweza kuandaa mikakati madhubuti itakayo pelekea kila upande kuwa sehemu salama, yenye amani ya kweli na bila uhalifu. Pamoja na kwamba tumechelewa, lakini kuelekea miaka 59 ya Muungano iwe wakati muafaka wa kuwa na mfumo unaoruhusu pande mbili za Muungano kuwa na mikakati bora ya kudumisha amani ya kweli na bila uhalifu. Ni miaka ya kuwa na mfumo bora wa Muungano unaoziwezesha pande mbili za Muungano kuweza kusimamia utekelezwaji wa haki za binadamu zikiwemo haki ya misngi ya kuchagua na kuchaguliwa na haki ya raia ya kutoa na kupokea habari ili sauti ya kila mwananchi wa kila upande iweze kusikika na iweze kuwa na maana inayostahili.
Kudumaa kwa utamaduni, mila na michezo:
Kwa miaka 58, mfumo wa Muungano umedumaza mambo ya utamaduni, mila na michezona haikutoa fursa sawa Katika kuyakuza. Kuelekea miaka 59, Muungano wa Tanzania uelekee Katika kutoa fursa kwa pande mbili za Muungano kuweza kufufua utajiri uliomo katika utamaduni na mila za kila upande ili kujenga urithi imara kwa vizazi vijavyo Katika kila upande sambamba na kuimarisha sekta ya michezo kwa kujenga mazingira yatakayo pelekea ufanisi mkubwa zaidi, lakini pia kuingiza michezo mipya ili kila upande wa Muungano uweze kurejesha heshma yake kimichezo kama hapo kabla.
Mamlaka kamili ya Zanzibar, Tanganyika na Muungano:
Miaka 58 ya Muungano wetu itukumbushe kwamba, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kama ilivyorekebishwa, Zanzibar ni moja ya nchi mbili zilizounda Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Hati ya Muungano na hatimaye kuratibiwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Katiba ya Zanzibar imefafanua mipaka ya Zanzibar. Aidha, imefafanua itikadi yake ya kuwa nchi ya kidemokrasia ya vyama vingi inayoheshimu utawala wa sheria, haki za binaadamu, usawa, amani, haki, uadilifu na mgawanyo wa madaraka. Katiba ya Zanzibar imetandika pia mfumo wa utawala na utekelezaji wa majukumu kuanzia Utendaji [Executive], Baraza la Wawakilishi [Legislature] na Mahakama [Judiciary].
Msingi huu wa Mamlaka ya Zanzibar unatokana na Hati ya Muungano ambayo ndiyo ilikuwa msingi wa Zanzibar kutoa baadhi ya madaraka yake na kuipa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kuyaendesha kimuungano. Hati ya Muungano chini ya ibara (iii) (a) imeeleza bayana kuwa kwa mambo ambayo si ya Muungano, Zanzibar itakuwa na Mamlaka yake Kamili juu ya mambo hayo. Ni dhahiri kuwa mamlaka ya Zanzibar hayatokani na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali Hati ya Muungano.
Utekelezaji na usimamizi wa Mamlaka ya Zanzibar umekuwa na changamoto kadhaa. Changamoto hizo zimezaliwa kutokana na sababu kadhaa zikiwemo za kukosa uongozi thabiti unaojali kulinda katiba, mfumo mbovu wa Muungano na vitendo vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kumega mamlaka ya Zanzibar katika mambo yasiyo ya Muungano na kuyafanya ya Muungano. Mfano mzuri ni kudai hata sehemu ya Zanzibar ya kisiwa cha Fungu Mbaraka [Latham Island] kuwa ni cha Tanzania Bara ilhali kilitangazwa rasmi kuwa sehemu ya Zanzibar tokea 19 Oktoba, 1898 na kimeendelea kuwa chini ya Zanzibar kwa miaka yote. Aidha, baadhi ya watuhumiwa wanaotuhumiwa kutenda makosa ya jinai Zanzibar kusafirishwa na kushtakiwa Tanzania Bara kinyume na Katiba na Sheria za Zanzibar, za Tanzania Bara na za Jamhuri ya Muungano.
Kuelekea miaka 59 ya Muungano wa Tanzania, kunahitajika mfumo bora wa haki wa kuyatambua na kuyaheshimu mamlaka kamili ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano. Kufikia hayo, ipo haja ya kufanya yafuatayo: -
i. Kufanya tathimini ya kitaalamu juu ya hali ya Katiba za Zanzibar, Tanganyika na Muungano, na mapungufu ya kila moja na uwezo wake wa kutimiza malengo ya kujenga Muungano wa Tanzania mpya wenye kupiga hatua za kiuchumi endelevu na unaojali misingi ya itikadi ya watu wa kila upande wa Muungano ya haki, usawa, uongozi bora, amani na maendeleo kwa msalahi mapanda ya watu wa pande mbili za Muungano bila kudhulumiana. Kuelekea miaka 59 ya Muungano, iwe wakati muafaka wa kuziwezesha pande mbili za Muungano kuweza kutengeneza utaratibu wa kuratibu maoni ya wananchi wa kila upande juu ya Katiba na haja ya kufanya marekebisho au kutunga Katiba mpya ya kila upande kuelekea Katiba mpya ya Muungano. Sambamba na hilo, miaka 59 ielekeze kwenye kuziwezesha pande mbili za Muungano kuweza kushajiisha wananchi wa kila upande na taasisi zisizo za kiserikali kuendelea kutoa elimu ya uraia juu ya ufahamu wa Katiba, haki za raia, na uwajibikaji wa taasisi za umma kwa maslahi ya kila upande na kwa Muungano wenyewe.
ii. Katika kulinda Mamlaka ya Zanzibar, Tanganyika na Muungano, kuelekea miaka 59, iwe wakati muafaka wa kuchukua hatua ya kuondoa kasoro zote zinazopelekea Serikali ya Muungano kumega na kuingilia Mamlaka ya Zanzibar kwa mambo ambayo si ya Muungano na kuweka sheria na taratibu zitazokinga hayo yasitokee. Hii ni pamoja na kuchukua hatua ya kumaliza mzozo wa umiliki wa kisiwa cha Fungu Mbaraka kwa ajili ya maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano na kuepusha athari kwa vizazi vijavyo. Pia kuelekea miaka 59, iwe wakati wa kuchukua hatua ya kuwezesha kila upande kulinda rasilimali zake zikiwemo za maliasili ya nchi kavu na baharini. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, baada ya miaka hii 58, itathmini haja ya Zanzibar kushiriki katika mifumo na mashirikiano ya kimataifa inayolinda nchi za visiwa vidogo kutokana na athari ya mazingira, mabadiliko ya tabia nchi na uchumi, Pamoja na kuongeza kasi katika mchakato wa utekelezaji wa uchumi wa bahari.
Dalili za kuifuta zanzibar kama mshirika sawa wa muungano:
Miaka 58 ya Muungano tunayoiadhimisha itukumbushe kwamba, Waasisi waJamhuri ya Watu wa Zanzibar na waasisi wa Jamhuri ya Tanganyika waliingia katika Muungano wa mwaka 1964 baina ya Jamhuri hizi mbili kwa nia njema ya kuendeleza umoja na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano. Hotuba za viongozi wakuu wa pande mbili, Hayati Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walizotoa baada ya Muungano zinaeleza bayana malengo hayo.
Hata hivyo, miaka kadhaa ya Muungano hadi sasa miaka 58, imeshuhudia hali hiyo kubadilika sana. Ushirika huu wa Nchi mbili umekuwa ukibadilika hatua baada ya hatua hadi kufikia hali ya kujenga khofu yenye msingi na ushahidi wa kwamba Muungano huu unaelekea katika upande mmoja kufuta mshirika mmoja wa Muungano ama kuudhibiti kwa kiwango cha kuutawala na kubaki upande mmoja tu kwa jina la Muungano. Jambo hili sio tu linainyima fursa Zanzibar ya kupiga hatua za kiuchumi, lakini pia linapalilia mfarakano wa kijamii kwa kupandikizwa chuki za kiitikadi na kibaguzi uliopindukia na kuondoa misingi ya amani na utulivu. Hali hii pia imechangia kuondoka uwajibikaji na ufanisi kwa taasisi za umma kutokana na viongozi wa ngazi za kisiasa na kiutendaji kuwekwa kwa misingi ya kiitikadi na sio kwa uwezo na hatimaye kujengwa mtandao wa kulindana. Mfumo wa Muungano na wa kikatiba, kuelekea kuadhimisha miaka 58, umeifanya Zanzibar ijikute katika Muungano ambao umekosa sifa za kuwa Muungano kutokana na mapungufu makubwa na ya msingi yafuatayo: -
Zanzibar Kutokuwa na Sauti Katika Uendeshaji wa Muungano:
Miaka 58 ya Muungano itukumbushe kwamba, Zanzibar kama mshirika wa Muungano ilitegemewa iwe na sauti au ishiriki katika usimamizi wa mambo ya Muungano kwa vile ilitoa mamlaka yake ya dola [sovereignty] na kuyakabidhi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Katika hali ya sasa wananchi wa Zanzibar hawana sauti katika kumchagua Rais wa Muungano kwa vile anapigiwa kura kwa wingi wa kura tu, bila ya uwiano wa washirika wawili sawa wa Muugano ambao ni Zanzibar na Tanganyika. Aidha, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si Rais wa Zanzibar wala Makamu wa Rais wa Muungano anayeshiriki Kikatiba katika kuunda Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano. Huu ni mwanya mkubwa sana unaopelekea upande mmoja kutumia vibaya sana mamlaka ya pamoja ya Muungano dhidi ya Zanzibar. Kuelekea miaka 59 ya Muungano wetu, iwe wakati muafaka wakuirejeshea Zanzibar Sauti yake stahili katika uendeshaji wa Serikali ya Muungano.
i. Zanzibar Kutokuwa na Sauti Katika Kutunga Sera za Mambo ya Muungano:
Kwa mujibu wa Katiba na Sheria ziliopo, kazi ya kutunga sera za Mambo ya Muungano ni ya Baraza la Mawaziri na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambamo Zanzibar haina ama ina uwakilishi ambao haukidhi kuwa na sauti ya maamuzi. Hali hii imepelekea sera za Mambo ya Muungano kutungwa kwa kuzingatiwa mahitaji na maslahi ya upande mmoja wa Muungano.
Wakati tunaadhimisha miaka 58 ya Muungano, ipo haja ya kuwa na utaratibu wa kuiwezesha Zanzibar kuwa na sauti katika kutunga sera za mambo ya Muungano kama mshirika sawa wa Muungano.
ii. Zanzibar Kutokuwa na Sauti Katika Kutunga Sheria za Mambo ya Muungano:
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano [ibara ya 98], sheria zote zinazohusu mambo ya Muungano zinatungwa na Bunge kwa kupitishwa kwa utaratibu wa kupitishwa na Bunge kwa wingi wa kura. Kutokana na uchache wa wabunge wa Zanzibar katika Bunge, sheria hizo zinapitishwa hata kama wabunge wote wa Zanzibar watapinga. Hakuna usawa wala haki [equality or equity] katika kupitisha maamuzi hayo muhimu. Ni wakati sasa, baada ya miaka 58, Zanzibar iweze kuwa na sauti katika kutunga Sheria za mambo ya Muungano.
iii. Kukosekana usawa na haki katika matumizi ya fursa na rasilimali za Muungano:
Miaka 58 ya Muungano imeshuhudia uwekezaji wa rasilimali za Muungano ukifanywa bila kuwepo haki wala uwiano na hivyo upande mmoja kufaidika zaidi au peke yake na rasilimali za Muungano. Aidha, fursa zinazotokana na dola kitaifa na kimataifa hazikuwa zikigaiwa kwa haki wala usawa. Ni wakati sasa wa kuwa na mfumo unaolenga katika usawa na haki katika matumizi ya fursa na rasilimali za Muungano
iv. Zanzibar kukosa haki zake halali ndani ya Muungano
Chini ya mfumo uliopo wa Muungano kwa miaka 58, Zanzibar imekuwa inakosa haki zake halali ndani ya Muungano. Miongoni mwa haki hizo ni pamoja na athari kali za kisiasa na kiuchumi kwa Zanzibar zilizodumu baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa mfano, Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na Mashirika kadhaa yalichukuliwa na upande mmoja wa Muungano au kubinafsishwa bila fidia wala kuweka bayana haki za Zanzibar katika mashirika hayo katika mfumo wa sasa. Mfano mzuri ni Benki Kuu, Benki ya NBC, Kampuni ya Simu, Shirika la Ndege la Tanzania na mengine mengi. Kuelekea miaka 59 ya Muungano, iwe wakati wa sasa wa kuhakiksha kwamba Zanzibar haikosi haki zake halali ndani ya Muungano.
v. Mafao ya Zanzibar katika mapato ya Muungano kama yalivyofanyiwa uchambuzi na Tume ya pamoja ya fedha:
Ikumbukwe kwamba, Tume ya Pamoja ya Fedha iliasisiwa chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muunganowa Tanzania tokea mwaka 1984. Sheria yake ilitungwa mwaka 1996.Miaka 12 baada ya kuanzishwa! Hata hivyo, ilianzishwa rasmi mwaka 2003.Takriban miaka 20 baada ya kuasisiwa na Katiba! Miongoni mwa kazi za Tume ni kuzishauri Serikali mbili juu ya kugharamia shughuli za Muungano. Katika uchambuzi uliofanywa na Tume imebainika wazi kwamba mapato ya shughuli za Muungano ni makubwa kuliko matumizi yake.
Hivyo, ili kuwezesha mgawanyo rasmi wa mafao hayo ya ziada Tume ilizishauri Serikali mbili juu ya mfumo [formula] wa kukokotoa na kugawana mapato hayo tokea mwaka 2006 lakini hadi leo, zaidi ya miaka 16 baada ya kushauriwa, Serikali mbili hazijatekeleza ushauri huo wala kupendekeza mfumo mbadala. Matokeo yake Zanzibar imeendelea kukosa mapato hayo halali na makubwa huku ikiendelea kudaiwa na Serikali ya Muungano madeni kama vile ya umeme.
Aidha, Tume imeshauri tokea mwaka huo wa 2006 kuanzishwa kwa Akaunti ya Pamoja ya Fedha kama ilivyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo itaweka uwazi juu ya matumizi halali na stahili ya Muungano, lakini hadi leo haijaanzishwa na hivyo kupelekea Serikali ya Muungano kuendelea kuchanganya matumizi ya Muungano na yasiyokuwa ya Muungano kinyume na matakwa ya Katiba na kwa kuinyima Zanzibar haki zake ndani ya Muungano. Miaka 58 itoshe kuanza kuipatia mafao yake Zanzibar yatokanayo namapato ya Muungano kama yalivyofanyiwa uchambuzi na Tume ya Pamoja ya Fedha, ikiwemo na malimbikizo ya mafao hayo.
Hitimisho na mapendekezo:
Tukiadhimisha miaka 58 ya Muungano, pamoja na juhudi kubwa na maarifa mengi ya viongozi wa Taifa hili katika kuudumisha Muungano wetu, ni wazi kwamba, Muungano tulionao sasa unachechemea na unayumba. Muungano wetu katika mfumo wa sasa ni Kitendawili Mtegoni unaochangiwa na kuzidharau Katiba zetu, yaJamhuri na ya Zanzibar pamoja na Hati ya Muungano.
Ili kuondokana na mkwamo huo na ili kuwa na Muungano wa haki, wa kuheshimiana, na wa furaha, Chama cha ACT Wazalendo, kinapendekeza kufanyika kwa mambo yafuatayo: -
i. Mchakato wa haraka wa kupata katiba mpya kuelekea mfumo imara wa Muungano:
Baada ya kuwa na Tume Huru za Uchaguzi za Tanzania na Zanzibar, kufufua suala zima la mchakato wa kuandaa katiba mpya ya Muungano itakayoendana na Mfumo bora wa serikali tatu utakaoleta mahitaji ya misingi ya haki, heshima na usawa kama nchi mbili huru zilizoungana kwa hiari yao ili tuweze kuwa na Muungano wa haki, uwazi na usawa kwa kufaidisha kila upande wa Muungano.
ii. Utekelezaji wa haraka wa mapendekezo ya Tume ya pamoja ya fedha:
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ihakikishe kwamba Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha yanatekelezwa ikiwemo kuanzishwa kwake na kufanya kazi ipasavyo na kwa haraka Akaunti ya Pamoja ya Fedha. Aidha, irejeshe malimbikizo yote ya haki za mapato ya Zanzibar kutokana na mapato ya ziada ya Muungano kama ilivyochambuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha.
iii. Kurejesha Mamlaka stahiki kwa Zanzibar (Kodi, Fedha, na Ushirikiano wa Kimataifa):
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibari anzishe mchakato kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya kurejesha mamlaka kwa Zanzibar katika nyenzo muhimu za uchumi ikiwemo kodi, fedha, naushirikiano wa kimataifa, ili Zanzibar iweze kujenga uchumi imara unaoendana na mazingira na mahitaji ya uchumi wa visiwa na pia kuamua kuhusu mustakbali wake.
Sambamba na hilo, Zanzibar irejeshewe hadhi yake ya kuwa na dhamana na jukumu la kuamua juu ya masuala ya sera za fedha ikiwemo kuratibu masuala ya mitaji ya uwekezaji badala ya kufanya jukumu la mweka hazina kama iliyo sasa. Hii itaifanya Zanzibar kuwa na mipango ya uhakika ya kiuchumi, kifedha na uwekezaji. Juhudi maalum na halisi zifanywe juu ya kuifanya Zanzibar iwe na uwezo wa kuingia katika mashirikiano na taaasisi za kimataifa ili iweze kufaidika katika nyanja za kiuchumi, biashara na kiutamaduni.
iv. Serikali ya Muungano kuipatia Zanzibar mgao wake wa kifedha wa Asilimia 11.02 Kama Ilivyowekeza katika mtaji wa uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania:
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iipatie Zanzibar mgao wake wa kifedha wa asilimia 11.02 kama ilivyowekeza katika mtaji wa uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzaniaihakikishe kwamba hisa zote za Zanzibar katika mashirika stahiki ya Muungano ambayo yamebinafsishwa au kuchukuliwa na Serikali ya Muungano pekee, zinalipwa au kugawiwa Zanzibar kwa mujibu wa kiwango chake stahiki cha hisa.
Mwisho, ni imani ya wananchi wa Tanzania wapenda haki, kupitia Chama cha ACT Wazalendo, kwamba tunaadhimisha miak 58 ya Muungano wa Tanzania tukiwa na uongozi imara na salama wa Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameonyesha dalili za kuheshimu Sheria, kujali na kutenda haki kwa umma. Tuna kila sababu ya kutotilia mashaka uwezekano wa utatuzi wa dhati wa kero za Muungano yakiwemo mapendekezo yaliyotolewa na Chama cha ACT-Wazalendo!
Imetolewa na:
Ndg. PAVU ABDALLA
[email protected]
Msemaji wa Sekta ya Utumishi wa Umma, utawala bora na Muungano
Showing 1 reaction
Sign in with
Facebook Twitter