Mkataba wa EPA: Maoni ya ACT Wazalendo

MAONI YA ACT WAZALENDO KUHUSU MKATABA WA MASHIRIKIANO YA KIBIASHARA NA JUMUIYA YA ULAYA (EPA)


Utangulizi:

Mkataba wa Mashirikiano/Muungano wa Kiuchumi (European Partnership Agreement-EPA) ni makubaliano ya kiuchumi yanayolenga kuunda eneo huru la biashara (Free Trade Area) kati ya nchi za umoja wa Ulaya (EU) na mataifa ya Afrika.

Makubaliano haya yanajadiliwa na kuingiwa kupitia Jumuiya za kikanda za Afrika badala ya Umoja wa Afrika (AU).

Mkataba huu una lengo la kuwa na soko huru la bidhaa kati ya nchi za Afrika na nchi za Jumuiya ya Ulaya bila vikwazo vya kikodi, lakini katika kipindi cha miaka mitano mbele baada ya muungano huu wa kiuchumi kuanza wajumbe watapaswa kujadili zaidi na kukubaliana kupitia kifungu cha ‘Rendezvous Clause’ katika ibara ya 3 ya mkataba wa EPA kujadiliana katika maeneo ya uwekezaji (investment), huduma (Service), manunuzi ya Serikali (Government Procurement), biashara na maendeleo, hatimiliki (Intellectual Property) na Sera shindani (Competition Policy).

Hivyo ni mkataba utakaojumuisha maeneo mbalimbali ya kiuchumi hapo baadaye ambayo yana athari kubwa kwa nchi masikini kama Tanzania, tusipochukua hatua stahiki.

Tanzania tuliamua kujadili suala la EPA kupitia Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuridhia EPA tarehe 16 Oktoba 2014 baaada ya majadiliano ya muda mrefu takribani miaka kumi.

Hatua hiyo ilitoa fursa kwa nchi wanachama ikiwemo nchi yetu Tanzania kuanza majadiliano ya ndani ili kufikia hatua ya kusainiwa na serikali na kuidhinishwa na Bunge. Hata hivyo, hadi sasa Tanzania hatujasaini wala Bunge halijaidhinisha mkataba huo kutokana na sababu mbalimbali na kuna Azimio la Bunge la Novemba 8, 2016 linalozuia Serikali kusaini Mkataba wa EPA.

Kufuatia taarifa iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alipokutana na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel mara baada ya kuwasili katika Makao Makuu ya Baraza hilo mjini Brussels, Ubelgiji tarehe 15 Februari, 2022 kuhusu utayari wa Tanzania kufanya mkutano wa maridhiano mwanzoni mwa mwezi Machi 2022 na kupitia upya makubaliano ya mkataba wa EPA (European Partnership Agreement) kati ya nchi za Afrika Mashariki na Umoja wa nchi za Ulaya, tunaona kuna haja na umuhimu wa kutoa maoni na mapendekezo yetu katika suala hili.

Hii ni kwa sababu ACT Wazalendo tunaamini katika ‘biashara shindani zenye tija na endelevu kwa maslahi ya nchi yetu na wananchi wa Tanzania.’ Jambo hili limebainishwa katika ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2020, ukurasa wa 30 kifungu cha 4.1(vi). Tumeahidi kupanua na kujenga biashara shindani, zenye tija na zilizo endelevu.

ACT Wazalendo tunaamini katika kutumia diplomasia na mahusiano ya kimkakati na nchi nyingine ili kupanua soko/biashara ya nje kwa mazao na bidhaa nyingine zinazozalishwa hapa nchini. Biashara au masoko hayo lazima yawe shindani, yenye tija na endelevu, yenye maslahi mapana kwa taifa letu na watu wake.

Maoni na mapendekezo yetu ni kama ifuatavyo;-

1. Mkataba huu unaruhusu upotevu mkubwa wa Mapato.

Kwa hesabu zilizofanywa awali na umoja wa nchi za Ulaya, kupitia mkataba huu Tanzania peke yake itapoteza dola milioni 853. Ni muhimu, kabla ya kusainiwa mkataba huu, serikali ihakikishe kuna mfumo wa kufidia upotevu wa mapato hayo yatokanayo na kupunguzwa au kuondoshwa kwa ushuru wa uingizaji na utoaji wa bidhaa (Export -Import tariffs/tariff barriers) kwani kwa makubaliano ya sasa Umoja wa nchi za Ulaya ulikataa kulipa fidia za upotevu huo wa mapato.

Iwapo Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea na msimamo wa kutolipa fidia (Compensation Mechanism) ni ushauri wetu nchi yetu sikubali kusaini EPA.

2. Mkataba usainiwe na Afrika (AU) nzima kwa umoja wetu.

Tunashauri Mkataba huu usainiwe na nchi za Afrika chini ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Ulaya kupitia Soko Huru la Afrika (African Continental Free Trade Agreement -AfcFTA) ambayo sasa Tanzania ni mwanachama wake. Hii itawezesha kuwa na eneo pana la uhuru wa biashara ndani ya Afrika na Tanzania kuwa na mahusiano na nchi hizo.

Pia, kupitia njia hiyo Afrika itakuwa na sauti zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo Afrika imegawanywa gawanywa katika kambi 7 kupitia jumuiya za kikanda ili kujiunga na EPA.

3. Serikali ije na Mkakati Unaoeleweka wa Kufidia Mapato ya moja kwa moja yatakayopotea kutokana na kuingia makubaliano ya EPA.

Mkataba huu kwa kiasi kikubwa utafunga au kuminya uhuru wa biashara kati ya nchi yetu na nchi nyingine kwa baadhi ya bidhaa ili kutoa kipaumbele kwa EPA na kufanya nchi yetu isiweze kuagiza bidhaa kutoka katika nchi hizo jambo ambalo ni wazi litaikosesha Serikali mapato.

Athari za jambo hili zinakwenda moja kwa moja na kugusa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu vya ndani kutokana na udhaifu wa ushindani wa viwanda vyetu dhidi ya bidhaa zinazozalishwa Ulaya.

Athari kubwa itakuwa kwenye bidhaa za kilimo, upotevu wa mapato, viwanda vidogo kuathirika, na kuporomoka kwa soko la ndani.

Kwa mujibu wa mkataba huo, bidhaa za Jumuiya ya Ulaya zitaingizwa katika nchi zetu kwa kiwango cha 82.6% katika kipindi cha miaka 25. Ni sharti Serikali ije na mpango utakaofidia athari na upotevu huo wa mapato hayo.

4. Kanuni ya 'Variable Geometry' itumike kupunguza athari hasi za Mkataba huu.

Tunashauri Serikali ifanye majadiliano na Umoja wa Ulaya (EU) ili nchi yetu au nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ziwe na fursa ya kutumia kanuni ya "Variable Geometry" yaani kuwa na uhuru wa kuchagua vifungu vya kutekeleza na kuacha vile ambavyo vinaonekana kuhatarisha maslahi ya nchi kibiashara na kiuchumi hadi pindi vitakapofanyiwa maboresho au marekebisho.

EU haipaswi kulazimisha nchi zote za Jumuiya kuridhia kwa pamoja kwani kila Taifa lina maslahi yake tofauti.

5. Fursa ya Ukanda wa Soko Huru la Afrika (AfcFTA) haijatumika ipasavyo.

Tunaishauri Serikali kuelekeza juhudi zaidi katika kuchangamkia fursa ya nchi yetu kunufaika zaidi na fursa ya AfcFTA ambayo Tanzania ni mwanachama wake.

Pamoja na masoko yanayopatikana kupitia Jumuiya zetu za kikanda EAC na SADC, bado tumeonesha kulegalega katika kuitumia fursa hiyo.

Ni maoni yetu kuwa, tunaweza kushindana ipasavyo na nchi ambazo angalau tuna mlingano wa kiuchumi (at least equal level of economy) kuliko nchi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ambazo zimetuzidi kwa viwango vikubwa.

Mathalani, takwimu zilizotolewa na taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya tarehe 31 Disemba 2021 ilionesha kuwa uuzaji wetu wa bidhaa ndani ya soko la Afrika Mashariki kutoka Tanzania umepanda kutoka Tsh 1.56 trilioni kwa mwaka 2019 hadi kufikia thamani ya 1.86 trilioni.

Hii inaonyesha tuna fursa kubwa za kutumia soko huru la Bara la Afrika na Jumuiya zetu za Afrika Mashariki EAC na SADC.

Mwisho, tunaishauri Serikali, ikiwa ni mjadili mkuu wa masuala ya kibiashara yaani (Chief Trade Negotiator for EU-EAC EPA) ambaye kazi yake maalum itakuwa ni kusimamia Majadiliano ya Mkataba huu kwa niaba ya Watanzania, ikumbuke uwepo wa Azimio la Bunge la Novemba 8, 2016 linalozuia Serikali kusaini Mkataba wa EPA.

Kabla ya Serikali kuanza majadiliano na EU ni muhimu suala hili lirejeshwe Bungeni kupata idhini ya Bunge na wananchi waelimishwe vya kutosha faida na athari za mkataba huo.


Imetolewa na:

Halima Nabalang'anya
Msemaji wa Kisekta
Wizara ya Viwanda na Maendeleo ya Biashara.
19 Februari, 2022.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK